• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Hatari Afrika ikipunguziwa chanjo ya corona hadi nusu

Hatari Afrika ikipunguziwa chanjo ya corona hadi nusu

Na MASHIRIKA

CAIRO, MISRI

NCHI za Afrika zimepuguziwa idadi ya chanjo ya corona na sasa zitapokea chini ya nusu ya kiasi zilichotengewa awali kupitia mpango wa Covax, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema.

Afrika ilipaswa kupokea chanjo milioni 520 kufikia mwisho wa mwaka huu wa 2021 lakini WHO inasema itapokea milioni 100 pekee kufikia Desemba.

Shirika hili linahusisha hatua hii na hatua ya nchi tajiri kuweka mikataba ya kununua chanjo kwa wingi kutoka kwa watengenezaji na kucheleweshwa kwa uidhinishaji wa chanjo.

Hatua hii inayojiri wakati nchi za Afrika zikiwa zimeongeza kasi ya kuchanja raia wake dhidi ya corona, hii ikiwa ni ishara kuwa usawa katika chanjo utabaki kuwa ndoto hasa kwa mataifa yanayoendelea.

Nchi za Afrika hasa hutegemea Covax kwa mahitaji ya chanjo lakini mpango huo umeshindwa kuzipa chanjo ambazo zinaahidiwa.

Kati ya nchi 54 za bara la Afrika ni 12 pekee ambazo zitatimiza lengo la ulimwengu la kuchanja asilimia 10 ya raia wake kufikia mwisho wa Septemba 2021.

Huku ikiibuka kuwa baadhi ya nchi zimeanza kuwapa raia wake chanjo ya tatu ili kuimarisha kinga licha ya wito zisifanye hivyo kwa wakati huu hadi mwisho wa mwaka, serikali za mataifa ya Afrika zitalazimika kutafuta mbinu tofauti za kchanja raia wake.

Kufikia sasa, ni asilimia tatu ya raia wa Afrika waliopata chanjo dhidi ya corona.

Mkurugenzi wa WHO eneo la Afrika Dkt Matshidiso Moeti, alisema hatua hii italemaza mipango ya mataifa ya Afrika kuchanja asilimia 10 ya watu kufikia mwisho wa Septemba.

Moeti aliomba nchi tajiri kusambaza chanjo zinazozihifadhi kwa usawa. Alisema kuwa mataifa ya Afrika kusini mwa Sahara yamechanja asilimia 1.7 ya raia wake.

“Nchi na kampuni zikizingatia usawa wa chanjo, janga hili litaisha haraka,” alisema na kuongeza ingawa Covax imesambaza zaidi ya chanjo milioni tano barani Afrika katika muda wa wiki moja iliyopita, zaidi ya mara tatu ya idadi hiyo imetupwa Amerika pekee’ katika muda wa miezi sita iliyopita.

Moeti alisema ingawa maambukizi yameshuka barani, bado kuna hatari kubwa kutokana na aina hatari ya virusi ya Delta.

Kulingana na WHO, aina ya Delta imegunduliwa katika asilimia 70 ya sampuli kutoka Botswana, Malawi, na Afrika Kusini na zaidi ya asilimia 90 ya sampuli kutoka Zimbabwe.

“Kuzuia hatari ya virusi hivi ni kupata chanjo,” alisema Moeti.

Mnamo Agosti, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alihimiza nchi kusitisha chanjo ya tatu. Hata hivyo, wito wake ulipuuzwa na baadhi ya mataifa, hatua inayosababisha uhaba wa chanjo katika mataifa masikini yakiwemo ya Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Mpinzani mkuu wa Kagame akamatwa kwa dai la unajisi

Waislamu wamlilia DCI akomeshe utekaji