DPP ataka kesi za Kimwarer, Arror ziunganishwe

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji sasa anataka kesi za ufisadi wa Sh63 bilioni zinazowakabili aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich na mkurugenzi mkuu wa zamani Shirika la Ustawi wa Kerio Valley (KVDA), David Kimosop ziunganishwe.

Kesi hizo mbili zinahusu kufujwa kwa pesa katika ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.

Katika ombi hilo, DPP amepunguza idadi ya washtakiwa kutoka 18 hadi tisa.

Pia amepunguza mashtaka kutoka 40 hadi 30.

Akiwasilisha ombi hilo, kiongozi maalum wa mashtaka, Bw Taib Ali Taib na naibu wa DPP, Bw Alexander Muteti, walimweleza Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani, Bw Lawrence Mugambi, kuwa idadi ya mashahidi imepunguzwa kutoka 104 hadi 52.

“Lengo la kuwasilisha ombi hili la kuunganishwa kwa kesi hizi mbili dhidi ya Bw Rotich na Bw Kimosop ni kuhakikisha imekamilishwa kwa haraka,” alisema Bw Muteti.

Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 26.

Yatani akiri alikabiliwa na kibarua kigumu kusawazisha bajeti

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Ukur Yatani ameungama kuwa bajeti aliyowasilisha kwa Wakenya bungeni Alhamisi jioni ilitokana na maamuzi magumu ambayo yeye na maafisa wake walifikia kwa lengo la kuendeleza taifa hili wakati huu mgumu.

Akiongea na wanahabari muda mfupi baada ya kusoma bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021, Yatani alipongeza wadau wote walioshiriki katika mchakato wa utayarishaji wa bajeti.

“Katika mazingira ya uhaba wa rasilimali huku changamoto kama vile Covid-19, mafuriko na uvamizi wa nzige zikiathiri uchumi, haikuwa kazi rahisi kuandaa bajeti inayoshirikisha vipengele vyote muhimu kwa usawa,” akasema, akiongeza ameisoma bajeti hii wakati maalum.

Kwa muda wa saa moja na dakika 40, Bw Yatani alisoma bajeti akiangazia masuala ya afya, usalama, ajenda nne za maendeleo za serikali, kati ya mengine muhimu kwa taifa hili.

Kwa mfano, Waziri alitenga Sh1.2 bilioni za kutumika kuajiri wahudumu 5,000 wa afya watakaopiga jeki vita dhidi ya janga la Covid-19.

Alisema wahudumu hao watafanya kazi chini ya kandarasi ya mwaka mmoja hasa katika maeneo ya mashinani yanayokabiliwa na uhaba mkubwa wa wahudumu hao.

Vilevile, alitenga Sh500 milioni kufadhili mpango wa ununuzi wa vitanda 20,000 vilivyotengenezwa humu nchini na vitakavyosambazwa katika hospitali za umma.

Na Sh25 milioni zimetengwa kupiga jeki mpango wa ujenzi wa mitambo ya kisasa ya sanitaiza katika vituo vya mipakani na hospitali kuu kote nchini.

Katika sekta ya Nyumba, serikali imetenga Sh15.5 bilioni kugharimia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama ya chini.

Vilevile, katika bajeti hii ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia Julai 1, 2020, Waziri Yatani ametenga Sh3.6 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), Sh7.5 bilioni kutoka Mpango wa Ustawishaji Miji na Sh1.1 bilioni kugharimia ujenzi wa masoko katika maeneo ya Gikomba, Githuria, Chaka, Kamukunji na Githurai.

Na kuhusiana na mpango wa kufufua uchumi ulioathiriwa na janga la Covid-19, Bw Yatani alisema wizara yake itahakikisha kuwa Sh10 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mpango wa “Kazi Mitaani” zinawafaidi vijana wanaostahili.

“Serikali inalenga kuwafaidi zaidi ya vijana 200,000 katika mitaa ya miji mikubwa kama Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru, Eldoret, miongoni mwa mingine katika kaunti nane. Vijana hawa watakuwa wanazibua mitaro ya majitaka na kuzoa taka katika mitaa kadha,” akasema Bw Yatani.

Pesa hizo, Sh10 bilioni ni sehemu ya Sh53.8 ambazo serikali imetanga kwa ajili ya kufadhili mipango mbalimbali chini ya nguzo nane za kuchochea ufufuzi wa uchumi ulioyumbishwa na makali ya Covid-19.

WASONGA: Bajeti inayosomwa leo haijali athari za corona

Na CHARLES WASONGA

BAJETI ya kitaifa inaposomwa leo bungeni kuna maswali mengi ibuka kuhusiana na viwango vya fedha zilizotengewa mipango muhimu na sekta kuu, ambazo zinatarajiwa kupiga jeki uchumi wakati huu wa janga la Covid-19.

Inasikitisha kuwa ingawa Mei Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliweka wazi kwamba kwa wastani, uchumi wa Kenya utakuwa ukipoteza Sh60 bilioni kila mwezi kutokana na janga hili, mipango wa kukabiliana na makali yake imetengewa Sh53.7 bilioni pekee.

Hii ni licha ya kwamba bajeti itakayosomwa leo ni ya Sh2.73 trilioni ambapo fedha nyingi zimetengewa miradi na sekta ambazo, kwa hakika, hazina dharura na umuhimu mkubwa nyakati hizi.

Sh53.7 bilioni ni pesa zile zile ambazo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Mei alipoweka wazi mpango wa kuchochea uchumi ili kupunguza makali ya janga la corona.

Inaonekana kwamba maafisa katika Hazina ya Kitaifa na wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti walipuuza kabisa ushauri wa wataalamu kwamba mpango wa kupambana na janga hili ulipasa kutengewa takriban Sh200 bilioni ili uweze kufaidi watu wengi.

PESA ZISIZOFAA

Mataifa mengi barani Afrika na mabara mengine, yametenga kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa mpango wa kukabiliana athari za Covid-19; mfano ikiwa Rwanda ambayo limetenga Sh280 bilioni kwa mpango huo.

Inakera hata zaidi kwamba licha kwamba Wizara ya Afya ndiyo iko mstari wa mbele katika vita dhidi janga la corona, imetengewa Sh111.7 bilioni pekee. Hii ni baada ya wabunge wanachama kamati ya bajeti kupunguza Sh3 bilioni kutoka mgao wa awali wa Sh114.7 bilioni.

Ukweli ni kwamba, wakati huu ambapo maambukizi ya virusi vya corona yanashuhudiwa katika ngazi za jamii, wizara hii inayoongozwa na Bw Mutahi Kagwe inahitaji bajeti kubwa zaidi ili iweze kukabiliana na hali hiyo.

Inahitaji fedha za kununua vifaa vya kupima corona katika maeneo ya mashinani, ikizingatiwa kuwa serikali za kaunti zimeonekana kulemewa na mzigo huo.

Pia kuna mpango wa kuajiri na kutoa mafunzo maalum kwa wahudumu wa afya wa kijamii (CHW) ili waweze kuendeleza mpango wa upimaji na utengaji wa watu waliopatikana na virusi vya corona.

Kimsingi, hakuna mantiki yoyote ya Wizara kama ya Ulinzi kutengewa Sh115 bilioni ilhali taifa hili halikabiliwa na tishio lolote la kushambuliwa na mataifa ya kigeni. Vile vile, haieleweki ni kwa nini kando na mgao huo, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) limetengewa Sh39 bilioni ilhali Wizara ya Usalama wa Ndani tayari imetengewa Sh131 bilioni.

Vile vile, mbona Afisi ya Rais imetengewa kiasi kikubwa cha Sh36.6 bilioni ilhali wakati huu ambapo Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto hawafanyi ziara nyingi za humu nchini na kimataifa kama ilivyokuwa zamani Kwa mfano siku hizi Rais Kenyatta huendesha mikutano ya kimataifa kupitia mitandao ya Zoom au Skype.

Na sio jambo la busara kwa serikali kutenga jumla ya Sh904.7 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni ya humu nchini na kimataifa badala ya serikali kujadiliana na wadeni wake ili kuahirisha ulipaji wa baadhi ya madeni.

Kushtakiwa kwake Rotich kulimuanika Ruto na wafuasi wake

Na BENSON MATHEKA

Kushtakiwa kwa aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich, maafisa wa wizara hiyo na wale wa mamlaka ya maendeleo ya bonde la Kerio (KVDA), kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwerer, kumemuabisha Naibu Rais William Ruto ambaye aliwatetea vikali akidai hakuna pesa zilizopotea.

Uchunguzi ulipokuwa ukiendelea, Dkt Ruto aliutaja kama feki na kumlaumu Mkurugenzi wa upelelezi wa jinai (DCI) George Kinoti na mwenzake wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji kwa kutumiwa kisiasa kulemaza ujenzi wa mabwawa hayo.

Zaidi ya mara mbili, akiwa mbele ya Rais Kenyatta na hata Jaji Mkuu David Maraga, Bw Kinoti na Bw Haji, Dkt Ruto alidai pesa zilizokuwa zimelipwa mwanakandarasi aliyeshinda zabuni ya kujenga mabwawa hayo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet zilikuwa Sh7 bilioni tu na sio Sh21 bilioni alivyodai Bw Kinoti.

Alisisitiza kuwa pesa hizo hazingepotea kwa sababu zilikuwa zimewekewa dhamana ya benki.

Dkt Ruto aliapa kwamba mabwawa hayo yangejengwa na kukamilika licha ya kubainika kuwa kampuni ya CMC di Ravenna iliyopatiwa kandarasi hiyo ilikuwa imefilisika.

Licha ya miito ya kumtaka asubiri uchunguzi ukamilike, Dkt Ruto aliendelea kumkashifu Bw Kinoti na wakati mmoja wandani wake walimtaka mkurugenzi huyo aachie Tume ya Maadili na kupambana na ufisadi (EACC) uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kiuchumi.

Wadadisi wanasema kwamba kushtakiwa kwa Bw Rotich na maafisa wa KVDA kuhusiana na sakata hiyo ni sawa na kumpiga kofi Dkt Ruto usoni machoni mwa umma.

“Ruto hana pa kujificha kwa kutetea ufisadi. Ukiangalia matukio ya hivi majuzi na hasa kuhusu sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwerer utagundua kwamba alikuwa akifahamu kilichotendeka na ndio sababu alikuwa akiwatetea washukiwa,” alisema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anataja matamshi ya Dkt Ruto alipohutubia kongamano la ugatuzi kaunti ya Kirinyaga kwamba alikuwa mhusika katika mabwawa hayo kama yaliyomuanika zaidi.

“Dkt Ruto alikosea kwa kupiga vita idara ya upelelezi ilipokuwa ikichunguza sakata hiyo. Alijaribu kuwalinda washukiwa lakini hakufaulu na hii imemuacha pabaya,” asema.

Kwenye kongamano hilo, Dkt Ruto alipuuza waliomlaumu kwa kutetea mradi huo akisema ni sawa na kuuliza fisi sababu ya kutaka kuvamia kundi la mifugo.

Wandani wake, akiwemo seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, mwenzake wa Kericho Aaron Cheruiyot na wabunge Oscar Sudi na David Rono wamekuwa wakimtetea na kumlaumu Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kumpiga vita naibu rais ili kuzima azima yake ya kuwa rais 2022.

Bw Kamwanah anasema Dkt Ruto anafaa kujiandaa kwa mashambulio makali zaidi kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa.

“Watatumia sakata hiyo kuendelea kumsawiri kama kiongozi anayewatetea wafisadi. Atakuwa na wakati mgumu sana. Makosa aliyofanya ni kukashifu idara huru za uchunguzi, kukaidi mkubwa wake (Rais Kenyatta) ambaye ametangaza vita dhidi ya ufisadi,” alieleza.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha ODM, John Mbadi, Dkt Ruto na Bw Murkomen ambaye ni kiongozi wa wengi katika seneti anafaa kujiuzulu kufuatia kushtakiwa kwa Bw Rotich na maafisa wa KVDA kuhusiana na sakata ya ujenzi wa mabwawa hayo.

“Naibu Rais Ruto na vibaraka wake akiwemo Murkomen walijitokeza hadharani kusema hakuna pesa zilizopotea. Hatua ya DPP ya kuwafungulia mashtaka washukiwa imemuanika Dkt Ruto na seneta huyo. Wanafaa kuomba msamaha kwa kuwapotosha Wakenya,” Bw Mbadi alisema.

Wadadisi wanasema kushtakiwa kwa washukiwa hao kutazidisha malumbano kati ya mirengo ya Kieleweke na Tangatanga ya chama cha Jubilee. Tangatanga inamuunga Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022 na Kieleweke unampinga vikali.

Mmoja wa wanachama wa Kieleweke mbunge wa Cheragany, Joshua Kutuny alisema kushtakiwa kwa washukiwa kuhusiana na sakata hiyo ni pigo kwa wanaotetea ufisadi.

“Hatua ya DPP inafaa kukumbusha wale wanaotetea ufisadi kwamba wataanikwa. Uchunguzi ulipokuwa ukiendelea, walimkashifu DPP na DCI lakini ushahidi umewaanika. Hawafai kupotosha watu kwa kudai jamii fulani inalengwa. Hivi ni vita dhidi ya ufisadi,” alisema Bw Kutuny.

Mwanachama mwingine wa mrengo wa Kieleweke Ngunjiri Wambugu alisema uchunguzi ulibainisha kuwa Bw Kinoti hakuwa akitumiwa kisiasa Dkt Ruto alivyodai kwa sababu ilibainika pesa zilipotea.

Mbunge huyo wa Nyeri mjini alisema madai ya Dkt Ruto na wandani wake yalilenga kutisha wapelelezi wakomeshe uchunguzi ambao uliwapeleka ng’ambo kufuatilia jinsi pesa zilivyolipwa, zabuni ilivyotolewa na waliohusika.

Wadadisi wanasema kwamba kauli za wandani wa Dkt Ruto baada ya kushtakiwa kwa washukiwa wa sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer zinaweza kumwanika zaidi.

Mnamo Jumatano, mbunge wa Kapsaret, Oscar Sudi alimshambulia Rais Kenyatta kufuatia kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Rotich na kumtaka ajiuzulu.

Kulingana na Bw Ben Makali, mdadasi wa siasa, Dkt Ruto na wandani wake wanajiharibia kwa kuendelea kupinga vita dhidi ya ufisadi.

“Dkt Ruto anafaa kuwazima wandani wake waache kupinga vita dhidi ya ufisadi. Hii inamfanya aendelee kutengwa serikalini. Anafaa kunyenyekea kwa mkubwa wake Rais Kenyatta na kukumbatia handisheki. Hauwezi ukashindana na serikali unayohudumia,” aeleza.

Bw Sudi mwenyewe alikiri kuwa hali ni mbaya kwa Dkt Ruto. “Hii inaudhi sana. Niliuliza Rais kama kuna mahali wamekosana na William wasuluhishe mambo yao lakini mambo yanaelekea kuwa mabaya,” Bw Sudi alisema alipohutubia wanahabari nyumbani wake Jumatano.

UFISADI: Rotich atumbukia bwawani

Na VALENTINE OBARA

SAKATA ya mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Jumatatu ilimtumbukiza Waziri wa Fedha, Henry Rotich kwenye hatari ya kupoteza kazi na kufungwa gerezani.

Hii ni baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji kuagiza Bw Rotich pamoja na Katibu wa Wizara ya Fedha, Kamau Thugge na wengine akiwemo Katibu wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Susan Jemtai Koech, Meneja Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kustawisha Kerio Valley (KVDA) David Kimosop na Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Mazingira (NEMA) Geoffrey Wahungu.

Wizara ya Fedha ni kitovu cha mipango yote ya maendeleo ya kitaifa na kukamatwa kwa waziri na katibu ni pigo kubwa kwa imani ya wawekezaji wanaochangia uchumi wa nchi.

Punde baada ya tangazo la Bw Haj, dhamana ya hati zinazotumiwa na Kenya kukopa pesa kutoka masoko ya kimataifa ilianza kushuka nchini Uingereza.

Wizara hiyo ina majukumu ya kushawishi wawekezaji na wahisani, hasa kutoka mataifa ya kigeni kufadhili miradi mbalimbali.

Waziri wa Fedha akisaidiana na katibu wake huhitajika kusimamia na kuidhinisha uundaji wa sera za kifedha zinazoongoza taifa, na vile vile kuidhinisha mapendekezo kuhusu mikopo na utumizi wa pesa za umma.

Hata hivyo, Mhadhiri wa somo la Uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Samuel Nyandemo aliambia Taifa Leo kwamba ingawa athari za kifedha zitashuhudiwa kwa sasa, hali ya kawaida itarudi kwa vile serikali ina watu wanaoweza kuendeleza mbele kazi ya wizara.

“Hizo athari hazitadumu kwa muda mrefu. Kuna maafisa serikalini wanaoendelea na kazi, na usisahau pia kuna waziri kwenye baraza la mawaziri ambaye hana wizara yoyote anayoshikilia,” akasema, akimrejelea Bw Raphael Tuju.

Duru zilisema Rais Uhuru Kenyatta alikuwa anapanga kutangaza kaimu waziri wa fedha mara Bw Rotich atakaposhtakiwa mahakamani.

Kufikia jana jioni washukiwa walikuwa bado wanahojiwa katika afisi za DCI maeneo mbalimbali nchini. Kulingana na Bw Haji, maafisa aliotaja wakiongozwa na Bw Rotich wanapasa kuondoka ofisini mara watakapofunguliwa mashtaka.

“Ni lazima waondoke ofisini. Hawa si magavana. Nitamwandikia barua Mkuu wa Utumishi wa Umma mara moja. Sheria inahitaji ukishtakiwa na ujibu mashtaka sharti uondoke. Hata katika mataifa ya nje huo ndio mwelekeo,” akasema Bw Haji.

Wakati sakata ya mabwawa ilipofichuliwa, Rais Kenyatta alikwepa shinikizo la kuwasimamisha kazi mawaziri waliotajwa akisisitiza kuwa ni lazima washtakiwe kwanza ndipo achukue hatua dhidi yao.

Alipohutubu bungeni Aprili mwaka huu kuhusu hali ya taifa, Rais alisisitiza lazima waliotajwa watendewe haki bali wasiadhibiwe bila ushahidi.

“Wafisadi wataadhibiwa kwa misingi ya kisheria. Hatua tutakazochukua hazitategemea jinsi watu wanavyolaumiwa kabla wasikilizwe,” akasema Rais.

Mawaziri wengine waliokuwa wamehojiwa na DCI wakati huo ni Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Eugene Wamalwa (Ugatuzi).

“Wale tunaowashtaki leo walikuwa na majukumu ya kulinda masilahi yetu ya umma na wakakiuka imani tuliyoweka kwao,” Bw Haji alisema.

Maafisa wengi katika idara ya ununuzi ya KVDA ni miongoni mwa wanaotarajiwa kushtakiwa kuhusiana na kashfa ambapo mabilioni ya pesa yalipotea.

Rotich kung’olewa afisini baada ya kushtakiwa

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha Henry Rotich na maafisa wengine wa serikali ambao watafikishwa mahakamani Jumanne kwa tuhuma za kuhusika katika sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer watasimamishwa kazi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Jumatatu alisema Rotich na wenzake sharti wajiondoe afisini baada ya kujibu mashtaka kadhaa yanayowakabili.

“Sharti waondoke afisini kwa muda… hawa sio magavana. Nitamwandikia Mkuu wa Utumishi wa Umma. Nitafanya hivyo sasa hizi. Hii ndio sheria.

“Ikiwa umeshtakiwa na ukajibu mashtaka, lazima ukae kando kwa muda kutoa nafasi kukamilishwa kwa kesi dhidi yako,” Bw Haji akawambia wanahabari alipoulizwa ikiwa itabidi washukiwa hao kuondoka afisini.

Jumatatu asubuhi Bw Haji aliamuru kukamatwa kwa Bw Rotich, Katibu wa Wizara ya Fedha Kamau Thugge na maafisa wengine 25 wa wizara hiyo na Halmashauri ya Ustawi wa Bonde la Kerio (KVDA) na NEMA kwa tuhuma za kuhusika katika sakata hiyo.

Maafisa hao watashtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha, njama ya kutekeleza udanganyifu kinyume cha sheria, kuanza utekelezaji wa mradi bila kufanya maandalizi yanahitajika, kutozingatia sheria ya usimamizi wa fedha za umma na ukiukaji wa Sheria kuhusu utoaji wa zabuni kwa kuipa zabuni kampuni ya CMC di Ravenna kutoka Italia.

Kampuni hiyoilipewa zabuni ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet wenye thamani ya Sh63 bilioni.

Vitimbi vya ‘Kamata Kamata’ vyarudi Rotich akibambwa

Na WAANDISHI WETU

IDARA ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) Jumatatu ilirejelea shughuli zake za kukamata washukiwa wa ufisadi, almaarufu kama ‘Kamata Kamata’ baada ya utulivu wa miezi kadhaa.

Kufuatia amri ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji, baadhi ya washukiwa wa sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer walijisalimisha kwa DCI huku wengine wakisakwa maeneo tofauti ya nchi.

Waziri wa Fedha Henry Rotich alijisalimisha katika makao makuu ya DCI jijini Nairobi huku Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira (NEMA), Bw Geoffrey Wahungu akitiwa mbaroni katika Kaunti ya Tharaka-Nithi na kusafirishwa hadi Nairobi.

Wapelelezi pia walifika katika afisi za Mamlaka ya Ustawishaji wa Kerio Valley (KVDA) na kumkamata Kaimu Afisa Mkuu Francis Kipkech pamoja na maafisa wengine.

Lakini maswali yaliibuka miongoni mwa wananchi kama ‘Kamata Kamata’ za jana ni sehemu tu ya vitimbi ambavyo vimeshuhudiwa kufikia sasa, vinavyohusu washukiwa wa ufisadi kukamatwa ilhali kesi hazionekani zikipiga hatua mahakamani.

Kuhusiana na sakata za wizi wa mamilioni ya pesa katika Taasisi ya Huduma kwa Vijana (NYS), wengi wa washukiwa waliishia kuachiliwa huru katika sakata ya 2015.

Washukiwa 23, akiwemo aliyekuwa katibu katika wizara Peter Mangiti waliachiliwa huru na aliyefungwa ni mmoja wa maafisa aliyekuwa katibu katika kamati ya tenda, Selesio Karanja pekee kwa miaka minne jela.

Kuhusiana na sakata ya pili ya NYS mwaka jana, kesi bado zinajikokota kortini zaidi ya mwaka mmoja baadaye.

Kesi nyingine inayoenda mwendo wa kobe ni sakata ya mahindi ambapo washukiwa kadhaa walikamatwa kwenye kashfa iliyohusu kupotea kwa zaidi ya Sh5 bilioni zilizonuiwa kulipwa wakulima.

Serikali kupimia wazee hewa

Na PAUL WAFULA

SERIKALI imewapimia hewa wafanyikazi wanaostaafu kabla ya kufikisha miaka 60 kwa kuwazima kupokea akiba yao yote ya pensheni.

Kulingana na kanuni mpya ya Serikali, wafanyikazi wanaostaafu sasa hawataweza kupokea mchango wa mwajiri wao kama ilivyo sasa hadi wafikishe miaka 60.

Awali, wafanyikazi wanaostaafu kabla ya kutimiza miaka 60 walipokea nusu ya mchango wa mwajiri pamoja na kiasi chao chote walichoweka kwenye akiba ya uzeeni.

Kanuni hiyo iliyotangazwa na Waziri wa Fedha, Henry Rotich, ni pigo kubwa kwa wale wanaofutwa kazi kabla ya umri wa kustaafu ama wanaotaka kuacha kazi ya kuajiriwa

“Inamaanisha kuwa sasa wafanyikazi hawataweza kupata akiba ya mwajiri wao hadi wastaafu. Sasa wataweza kupokea sehemu yao pekee ya akiba,” alisema Meneja Mkurugenzi wa kampuni ya Enwealth Financial Services, Simon Wafubwa.

Wataalamu wa masuala ya fedha wanasema hatua hii inalenga kuwezesha Serikali kupata pesa zaidi za kukopa ndani ya nchini, na hivyo kuacha kutegemea mikopo ya kigeni.

“Hatua hii itasaidia Serikali kupunguza ukopaji kutoka nchi za kigeni kwa sababu kutakuwa na pesa nyingi za kukopa katika soko la hapa nchini,” akasema Bw Wafubwa.

Uamuzi huo pia utasaidia kampuni za akiba ya malipo ya uzeeni, kwani sasa zitaweza kuendelea kuzalisha pesa hizo na kupata faida za juu kwa kipindi kirefu zaidi.

Kampuni hizo zimesifu uamuzi huo ambao wafanyikazi wanauona kama unyanyasaji.

Hatua hii inaendeleza sera za utawala wa Jubilee wa kutumia mbinu mbalimbali kufaidi mashirika makubwa makubwa na wakati huo huo kukadamiza wananchi wa tabaka la chini.

Tayari kuna kesi kortini inayopinga utozaji wa ushuru walioajiriwa kufadhili nyumba za mradi wa Serikali, licha ya kuwa wahusika wengi hawatafaidika nazo.

Pia ushuru umeendelea kupanda kila mara kwa bidhaa nyingi, hali ambayo imesababisha kupanda kwa gharama ya maisha na kuongezeka kwa umaskini ambao Jubilee iliahidi kupunguza.

Mazoea ya Jubilee kukopa sana katika soko la humu nchini yamefanya kampuni za kifedha kupendelea kuikopesha, hali ambayo kwa upande mwingine imefanya iwe vigumu kwa wenye biashara ndogo ndogo na wananchi wa kawaida kupata mikopo ya kujiendeleza.

Bw Wafubwa alieleza kuwa wafanyikazi wanaweza kutumia mbinu zingine kunufaika na akiba hiyo kama vile kutumia pesa hizo kama dhamana ya mkopo wa kununua nyumba, ama kuhamisha baadhi ya pesa hizo kwa hazina ya matibabu baada ya kustaafu.

Hatua hiyo ya Serikali imetokea wakati ambapo inakabiliwa na mzigo mkubwa wa kulipa pensheni ya watumishi wa umma.

Kufikia Juni mwaka huu, Serikali ililipa pensheni ya jumla ya Sh50.8 bilioni kwa watumishi wa umma waliostaafu, hili likiwa ni ongezeko kubwa kutoka Sh15 bilioni mnamo 2002.

Kiasi hicho ni zaidi ya Sh42 bilioni ambazo Kenya imetumia katika sekta ya afya.

Tangu Kenya ijinyakulie uhuru, watumishi wa umma waliostaafu wamekuwa wakipokea malipo ya uzeeni kwa gharama ya walipa ushuru.

Shinikizo Rotich ang’atuke zazidi

SAMWEL OWINO na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Fedha, Henry Rotich Jumatano alirejea tena katika Makao Makuu ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhojiwa kuhusiana na sakata ya Sh21 bilioni ya mabwawa ya Arror na Kimwarer, huku shinikizo za kumtaka kujiuzulu zikiendelea kutolewa.

Jana, Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi waziri huyo ikiwa waziri huyo hatajiuzulu kwa hiari yake.

“Nataka kumhimiza Rotich kujiuzulu kutokana na sakata hii. Na jinsi nilivyomhimiza Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi Bw Rashid Echesa kama Waziri wa Michezo, nataka kumhimiza kumpiga kalamu Bw Rotich ikiwa waziri huyo hatasikiza miito ya viongozi na kujiuzulu,” Bw Atandi akasema.

Akiongea na wanahabari jana katika majengo ya bunge, Mbunge huyo alidai ana habari kwamba Bw Rotich alitumia kampuni moja kwa jina HEKIRO kununua ardhi katika bonde la Kerio kwa kutumia raia wa Italia kama wakurugenzi.

“Walinunua ardhi hiyo kwa Sh1 bilioni na baada ya miezi michache, wakauza ardhi hiyo hiyo kwa serikali kwa Sh6.3 bilioni. Baadaye, Bw Rotich alihakikisha pesa hizo zimetengwa katika bajeti. Alifahamu barabara kwamba alikuwa akiilaghai serikali ambayo anapaswa kulinda mali yake,” Bw Atandi akadai.

Kulingana na Mbunge huyo wa ODM, hatua ya Bw Rotich ya kutenga pesa za ununuzi wa ardhi ambako mabwawa hayo yangejengwa ilikuwa ni sawa na kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake.

“Sharti Bw Rotich afutwe kazi. Yeye ndiye mhusika mkuu katika sakata hii ya mabwawa. Alihusika moja kwa moja katika uporaji wa pesa za umma.

Bw Atandi alisema Wakenya waliamini madai kuwa hakuna pesa zilizopotea katika sakata hiyo. “Mabilioni ya pesa ziliibiwa na wahusika sharti waadhibiwe.”

“Huu ni uporaji wa rasilimali za kitaifa katika kiwango cha sakata za Goldenberg na Anglo Leasing,” Bw Atandi akasema.

Mbunge huyo alisema ni makoa kwa watu fulani kumshika Rais Kenyatta mateka kwa kisingizio kwamba anapaswa kuwalipa deni fulani la kisiasa.

“Rais asikubali kushikwa mateka na watu kama hawa kwa sababu alikula kiapo cha kulinda na kutetea katia pamoja na sheria zote za Kenya.

Mnamo Jumanne Bw Rotich alihojiwa kwa zaidi ya saa 10 ambapo duru zinasema alikabiliwa na wakati mgumu kujibu maswali 300 kuhusu jinsi kampuni moja ya Italia ililipwa mabilioni ya fedha, hata kabla ya kuanza kazi ya kuchimba mabwawa.

NGILA: Pesa zilizoibwa na kufichwa ughaibuni zirejeshwe na serikali

NA FAUSTINE NGILA

RIPOTI ya Shirika la Kitaifa kuhusu Utafiti wa Uchumi kutoka Amerika iliyotolewa juma lililopita kuwa Kenya ni ya pili duniani katika orodha ya mataifa yenye matajiri walioficha matrilioni ya pesa ughaibuni inasikitisha mno.

Licha ya serikali kuweka mikakati ya kutwaa fedha zilizopatikana kwa njia za ufisadi na ukwepaji wa ushuru, bado kuna Sh15 trilioni zilizochumwa nchini na kufichwa na mabwanyenye katika mataifa ya nje.

Changamoto ya matajiri kuficha ukwasi wao kwenye mataifa ya kigeni inakumba mataifa mengi yanayoendelea, lakini hali ya Kenya kuibuka katika mstari wa mbele kwa uovu huo ni jambo hatari kwa uchumi wetu na Afrika Mashariki kwa jumla.

Wakati Waziri wa Fedha Henry Rotich kwenye Sheria ya Fedha 2016 alitoa mwanya wa kuwaongezea muda Wakenya wenye mali ughaibuni kuirudisha nchini, alifikiri angewashawishi kutoa fedha zao kutoka mataifa ya Bermuda, Switzerland, Cayman Islands, Channel Islands na Isle of Man na kuzirudisha nchini.

Hilo halikufaulu na sasa ni wakati wa kubuni mikakati mingine itakayozaa matunda hasa ikizingatiwa kwamba fedha hizo ni mara tano ya bajeti yetu ya sasa, na zikiwekezwa vizuri hapa nchini, deni la Sh5 trilioni linalotukodolea macho litakuwa historia.

Serikali ina jukumu la dharura la kuzidisha juhudi za kurudisha matrilioni hayo ya pesa humu nchini. Hili linawezekana kwa kuunda vishawishi vya kuwachochea matajiri hawa kurudisha fedha hizo humu nchini kwa hiari yao.

Hazina kuu

Ikiwa hilo litashindikana, basi Hazina Kuu haitakuwa na budi kuwalazimisha mabwanyenye hawa kurudisha mali hiyo, kwa kuwawekea vikwazo vya kifedha.

Hatua ya pili inafaa kuhusisha ushirikiano wa serikali yetu na serikali za mataifa ambako utajiri huo umefichwa kwa kutia saini mikataba ya usaidizi kuhusu fedha hizo kama ule wa Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Switzerland Alain Berse mnamo Julai.

Kukosa kuchukua hatua za dharura kuhusu utajiri wa njia za mkato utazidisha kiburi kwa matajiri wanaotambua ufisadi kama ngao, na watazidi kujitajirisha kinyume cha sheria huku Wakenya wakiumia.

Iwapo serikali itachukua hatua mapema, basi mwendendo wa baadhi ya Wakenya kujizolea mabilioni ya pesa kutokana na ufisadi, ukwepaji kulipa ushuru na wizi wa fedha za umma utakoma.

Ni kinaya kikubwa kwa watu wachache nchini kumiliki fedha ambazo ni mara tatu ya deni tunalodaiwa na mataifa ya kigeni huku serikali ikishindwa kufadhili bajeti ya Sh3 trilioni pekee.

Wabunge wa Jubilee waapa kumng’oa Rotich ofisini

Na CHARLES WANYORO

WABUNGE wawili wa chama cha Jubilee wametoa mwito kwa Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi Waziri wa Fedha Henry Rotich wakimlaumu kwa kuchangia sera mbovu za kifedha ambazo wanasema zimedunisha hali ya uchumi.

Mbunge wa Chuka Igamba Ng’ombe, Patrick Munene na mwenzake wa Runyenjes Eric Muchangi walimlaumu Bw Rotich kutokana na hali mbaya ya kiuchumi inayoshuhudiwa, ambayo imepelekea serikali kuongeza ushuru wa VAT kwa asilimia 16 kwa bidhaa za petroli.

Wakizungumza mjini Embu, viongozi hao walishikilia kwamba watashughulikia suala hilo la VAT wakati Bunge litakapoandaa vikao maalum kesho na Alhamisi, na vile vile kuhakikisha waziri huyo anatimuliwa ofisini.

“Kabla Bunge lielekee likizoni kulikuwa na mswada wa kumtimua ofisni Bw Rotich na tutaundeleza kwa sababu hajawajibikia majukumu yake ipasavyo. Si lazima tupige kura ya kumwondoa ofisini kama waziri kwa kuwa hata yeye anajua ameshindwa na kazi. Lakini tunashindwa kwa nini amekataa kujiuzulu kwa hiari?,” akauliza Bw Munene.

Mbunge huyo alimlaumu Bw Rotich kwa kumakinikia utekelezaji wa sera za Shirika la Fedha ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia kwa sababu alikuwa afisa wa zamani wa shirika hilo.

“Ukiangalia sera za kifedha anazokumbatia utaona kwamba wizara yake inaongozwa na watu waaminifu kwa shirika la IMF. Si ajabu kwamba maafisa wa ngazi za juu wa hazina hiyo walitoka shirika hilo,” akalalamika Bw Munene.

Kando na Bw Rotich aliwataja katibu wa wizara hiyo Kamau Thugge, gavana wa benki kuu Patrick Njoroge na Mkurugenzi Mkuu wa bajeti, fedha na maswala ya kiuchumi kama maafisa wa zamani wa IMF.

Bw Muchangi kwa upande wake alimtaka Bw Rotich kubeba msalaba wake kuhusiana na maswala yote ya wizara hiyo ambayo alitaja kwamba haijakuwa ikitekeleza wajibu wake vizuri.

Wakati huo huo, viongozi hao wawili vile walionya Bunge la Kitaifa dhidi ya kuandaa mkutano na kuafikia uamuzi wa kumwokoa Bw Rotich kabla ya vikao vya Jumanne na Alhamisi.

Niite nikufundishe jinsi ya kukabili madeni, Raila amwambia Rotich

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga sasa amemwitisha kikao cha dharura Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich, amfundishe jinsi serikali inaweza kuimarisha mapato na kulipa madeni bila kuwapandishia Wakenya gharama ya maisha.

Bw Raila amemmtaka Bw Rotich amwite mezani wajadiliane kuhusu suluhu mwafaka za kukabiliana na deni la Sh5 trilioni ambalo limeisukuma serikali kuongeza ushuru kwa bidhaa za mafuta kwa asilimia 16.

“Tunajua kwamba tunaweza kupata suluhu tosha kwa masaibu yetu. Tulifanya hivyo wakati wa serikali ya muungano na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, tunajua jinsi tunaweza kupata suluhu. Nitampa Rotich ushauri bila malipo jinsi atasaidia nchi hii,” akasema kiongozi huyo.

Alielezea jinsi ongezeko la ushuru limefanya maisha kuwa mlima kwa wananchi wengi ambao sasa hawawezi kumudu bei ya petroli, dizeli na mafuta taa hali ambayo imechangia bidhaa za viwandani kupanda bei.

Alisema kuwa changamoto hizi hazifai kuzuia maendeleo ya taifa hili, kwa kuwa suluhu zinaweza kupatikana bila kuwasukumia wananchi gharama kubwa ya ushuru.

“Tunajua kwamba taifa letu linaumia kwa sasa. Ndiyo maana tunafaa kufanya mazungumzo kuhusu jinsi tutakavyomudu madeni yanayotukabili ambayo yanalazimisha serikali kuongeza ushuru,” akasema.

Akihutubu nyumbani kwake eneo la Opoda, Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema kwamba mazungumzo hayo yanafaa kuleta mbinu mbadala kwa serikali kuhusu kuongeza pato la nchi, bila kuwaadhibu Wakenya kwa makosa ambayo hawakufanya.

Alitoa wito kwa mashauriano kuanzishwa haraka ili suluhu ya dharura ipatikane na kupunguza gharama ya maisha ambayo sasa imeleta taswira ya uchumi ambao uko tayari kuporomoka.

Mwanasiasa huyo kigogo alisema kuwa ana imani kwamba viongozi wa nchi hii wana uwezo wa kusaka suluhu kwa mzigo wa kiuchumi unaolikodolea macho taifa.

Kulingana naye, serikali inafaa kuzidisha vita dhidi ya ufisadi, akieleza kuwa iwapo zimwi la ufisadi litazimwa, basi serikali inaweza kupata fedha bila kupandisha ushuru kwa wananchi.

“Maoni yangu ni kwamba lazima tumalize ufisadi kwanza. Pesa nyingi ambazo serikali hii hupata hupotelea kwa mifuko ya wafisadi. Tukikusanya ushuru wetu bila kuibwa na yeyote, tutaweza kujitegemea na uchumi kumfaa kila Mkenya,” akasema.

Licha ya Mahakama Kuu ya Bungoma kusitisha kwa muda utekelezwaji wa ushuru wa asilimia 16, bei ya mafuta vituoni haijashuka, na wanachokishuhudia wananchi ni kukauka kwa mafuta vituoni huku bei ya lita moja ya petroli ikigonga Sh150 kwa vituo vichache vyenye bidhaa hiyo.

Awali, Bunge la Kitaifa lilikuwa limedinda kupitisha mswada wa kuongezea ushuru kwa bidhaa za mafuta, likitaka hatua hiyo icheleweshwe kwa miaka miwili, lakini Wizara ya Fedha ikapuuza uamuzi wake na kupandisha ushuru.

Kwa sasa ili gharama ya maisha irudi kwa viwangi vya wastani, Kenya inahitaji Sh8 trilioni, Sh3 trilioni za kufadhili bajeti ya mwaka huu wa kifedha na zingine Sh5 trilioni za kulipa madeni ambayo inadaiwa na mataifa ya kigeni pamoja na mashirika ya fedha duniani.

Kenya kupokea mkopo mwingine wa Eurobond wa Sh200 bilioni

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI imetangaza kuwa imefanikiwa kupata mkopo mpya wa Sh203 bilioni wa Eurobond.

Waziri wa Fedha Henry Rotich alisema fedha hizo zitatumiwa katika miradi ya ujenzi wa miundomsingi na kulipa madeni mengineyo.

“Tutaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundomsingi na miradi mingineyo ya maendeleo,” akasema Waziri Rotich kupitia taarifa yake kwa wanahabari.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mafanikio ya mkopo huo ni ishara kuwa wawekezaji wa kimataifa wana imani na uchumi wa Kenya.

Mkopo wa Eurobond mnamo 2016, uliibua mjadala mkali kuhusiana na matumizi yake huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akidai kuwa fedha hizo ziliibwa na baadhi ya maafisa wakuu serikalini.

Mnamo Mei 2016, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Keriako Tobiko alisema kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuonyesha kuwa fedha hizo ziliporwa.

Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko kufikia sasa imeshindwa kutegua kitendawili kuhusiana na fedha hizo.