• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Hydroponic: Mfumo bora wa kilimo kukwepa kero ya magonjwa

Hydroponic: Mfumo bora wa kilimo kukwepa kero ya magonjwa

Na SAMMY WAWERU

KERO ya magonjwa ni miongoni mwa changamoto zinazozima ari ya mkulima, hasa endapo anaendeleza kilimo-biashara.

Ikiwa hatadhibiti magonjwa, mimea na mazao yataathirika, kilele kikiwa kukosa kuafikia malengo yake.

Ufanisi katika kilimo, pia hutokana na msingi bora wa mbegu na miche.

Athari nyingi za magonjwa huanza kwenye kitalu na miche inapohamishiwa shambani.

Aidha, kuna magonjwa yanayokolea kwenye mimea na udongoni.

Kiini cha magonjwa mengi hata hivyo hutokana na udongo, kufuatia yanayosalia humo hasa baada ya mavuno.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema changamoto za magonjwa zinapaswa kuangaziwa kuanzia udongoni.

“Changamoto nyingi za magonjwa ya mimea na mazao husababishwa na udongo ulioathirika,” anasema Caroline Njeri, mtaalamu wa kibinafsi.

Njeri anaeleza, athari hizo zinaweza kudhibitiwa upesi endapo hali ya udongo itaangaziwa.

Matumizi ya mara kwa mara ya dawa zenye kemikali, yametajwa kuchangia udongo kuharibika.

“Dawa zenye kemikali huusababisha kudhoofika, na rutuba kupungua,” anaonya mdau huyo.

Isitoshe, dawa za aina hiyo pia ni kichocheo cha magonjwa yanayohusishwa na mazao ya shambani.

Ugonjwa wa Saratani, na ambao ni kero kuu nchini na ulimwenguni, unatajwa kusababishwa na chakula, hususan kilichokuzwa kwa kutumia dawa ma mbolea zenye kemikali.

Ili kukwepa changamoto za magonjwa ya mimea na mazao, katika kilimo cha mvungulio maarufu kama greenhouse, baadhi ya wakulima wamekumbatia matumizi ya malighafi asilia mahala pa udongo.

Mfumo wa kisasa almaarufu Hydroponic System, unajumuisha malighafi hayo hai.

Aidha, ni mfumo usiotumia udongo kupanda mimea, na badala yake kutumia malighafi kama vile; Pumice pia Pumicite, ungaunga unaotokana na mawe ya Volkeno.

Malighafi mengine ni pamoja na maganda ya mpunga, maganda ya nazi yaliyosagwa au kupondwapondwa na peat moss – Sphagnum aina ya mmea wenye karibu spishi 380.

Miriam Karuitha akionyesha malighafi asilia anayotumia kukabiliana na magonjwa ya udongo, kwenye kivungulio chake eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Mmea huo pia husagwa au kupondwapondwa.

“Malighafi hayo huchanganywa na kutumika badala ya udongo,” anasema Miriam Karuitha, mkulima wa eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu anayeyatumia mfumo huo wa Hydroponic System.

Miriam amekumbatia kilimo cha mvungulio, ambapo mfano wa vitanda virefu vinavyositiri malighafi hayo vimeundwa.

Vilevile, kwenye mashina ya mimea amesindika mifereji ya kunyunyizia maji.

“Baada ya kugundua siri ya malighafi asilia, kero ya magonjwa imepungua kwa kiasi kikubwa. Ninayopambana nayo ni ya kusambazwa, kutoka nje kupitia wanaoingia kivungulioni,” Miriam anaelezea, akiongeza kuwa hudhibiti wanaoingia.

Langoni, kuna maji yaliyotibiwa, ambapo kila anayeingia sharti makanyagio yake ya viatu yaloweshwe ili kuua viini virusi visababishi vya magonjwa.

Mkulima huyu anasifia mfumo huo wa kisasa kumsaidia kuafikia kigezo cha kilimohai, mazao yaliyokuzwa kwa kudhibiti matumizi ya dawa na mbolea zenye kemikali.

Mbali na kuzalisha mazao salama, Miriam anasema amepunguza gharama ya kuendeleza kilimo.

Kukabiliana na wadudu waharibifu, hutumia pilipili mboga zilizosagwa, sabuni ya majimaji, mkojo wa sungura na mmea asilia aina ya akapulko.

Ni matumizi ya malighafi asilia na hai anayosifia, akisema ikiwa wakulima watayakumbatia kero ya magonjwa na wadudu, watakuwa wameiangazia pakubwa.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya Brian Mandela asherehekea kushinda Ligi Kuu ya...

JAMVI: Ruto kupokelewa kishujaa Kisumu kunaashiria nini?