• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
IEBC: 5,800 kuwania viti bila vyama

IEBC: 5,800 kuwania viti bila vyama

NA LEONARD ONYANGO

JUMLA ya watu 5,801 wamejitokeza kuwania viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 kama wagombea huru.

Kulingana na orodha iliyochapishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika Gazeti Rasmi la Serikali, watu 38 – wakiwemo wanawake sita – wanalenga kuwania urais kwa tiketi huru.

Wanawake hao wanaomezea mate urais ni Nazlin Omar Fazaldin, Faith Wairimu Ngigi, Esther Waringa Kihuha, Kemunto Dorothy Nyangori, Grita Muthoni Koue na June Juliet Munyeki.

Bi Omar aliwania urais 2007 na kuibuka nafasi ya sita kwa kura 8,624.

Katika uchaguzi wa 2013, alizuiwa kuwania kwa kukosa cheti cha maadili mema kutoka kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu wa Jinai (DCI).Mnamo 2017, Bi Omar hakuwania baada ya IEBC kubaini kuwa jina lake halikuwa katika sajili rasmi ya wapigakura.

Iwapo wawaniaji hao wote wa kujitegemea wataidhinishwa na IEBC kati ya Mei 29 na Juni 6 kuwania urais, huenda wapigakura wakashuhudia kwa mara ya kwanza karatasi ndefu ya wawaniaji urais.

Kwa mujibu wa IEBC, watu 74 wametuma maombi ya kusaka kiti cha ugavana, ubunge (748), uwakilishi wa wanawake katika kaunti (95), useneta (108) na udiwani (4,738).

Kaunti ya Nandi, ambayo ni ngome ya Naibu wa Rais William Ruto, inaongoza kwa idadi kubwa ya watu wanaomezea mate ugavana kupitia tiketi ya kujitegemea.

Kaunti hiyo ina wawaniaji huru saba wa ugavana, kisha inafuata Nairobi (6) huku Kisumu na Nakuru zikiwa na wawaniaji wanne kila moja.

Katika Kaunti ya Mombasa, Bw Daniel Munga Kitsao ametuma maombi ya kuwania ugavana kwa tiketi ya kujitegemea; katika kivumbi kitakachoshirikisha Abdulswamad Sheriff Nassir wa ODM, Hassan Omar wa UDA na Mike Sonko wa Wiper kati ya wawaniaji wengine.

Kaunti za Kilifi na Lamu hazina mwaniaji huru wa ugavana.

Wanaomezea mate ugavana wa Nairobi kwa kujitegemea ni Leonard Kipkori Ngetich, Agnes Kagure Kariuki, Esther Waringa Thairu, Peter Churchil Watua Wanyonyi, Wilson Mauti Ogonda na Ayieko Timothy Olingo.

Sita hao watamenyana na Polycarp Igathe wa Jubilee (Azimio) na Johnson Sakaja wa United Democratic Alliance (UDA).

Katika uchaguzi wa 2017, watu 4,002 waliwania viti mbalimbali kupitia tiketi ya kujitegemea. Wawaniaji urais walikuwa watatu, useneta (44), ugavana (48), uwakilishi wanawake (55), ubunge (513) na udiwani (3,339).

Kati ya 44 waliokuwa wakiwania useneta, ni mmoja tu aliyeshinda. Wawaniaji wawili wa kujitegemea walishinda ugavana 2017 huku 13 wakishinda ubunge, mmoja uwakilishi wa wanawake na 109 udiwani.

Gavana wa zamani wa Nairobi Evans Kidero ndiye mwaniaji wa pekee wa kujitegemea aliyejitolea kumenyana na mbunge wa Homa Bay Gladys Wanga katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay.

Katika uchaguzi wa 2017, watu 4,002 waliwania viti mbalimbali kupitia tiketi ya kujitegemea.

Wawaniaji wa urais wa kujitegemea walikuwa watatu, useneta (44), ugavana (48), uwakilishi wa wanawake (55), ubunge (513) na udiwani (3,339).

Kati ya 44 waliokuwa wakiwania useneta, ni mmoja tu aliyeshinda. Wawaniaji wawili wa kujitegemea walishinda ugavana 2017 huku 13 wakishinda ubunge, mmoja uwakilishi wa wanawake na 109 udiwani.

Katika ripoti yake ya baada ya uchaguzi wa 2017, IEBC ilisema kuwa idadi kubwa ya wawaniaji wa kujitegemea ilitokana na kusambaa kwa udanganyifu katika kura mchujo za vyama vya kisiasa.

Inaonekana idadi kubwa ya wawaniaji wa kujitegemea imetokana na hatua ya vyama vya kisiasa kutoa tiketi za moja kwa moja na michujo iliyokumbwa na madai ya udanganyifu.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Idara nyingine za serikali ziipe umuhimu lugha ya...

Sifa hasi ya kiongozi asiye na msimamo yaandama Kalonzo

T L