Radi yaua 60 wakiwemo 11 waliokuwa wakipiga ‘selfie’

Na MASHIRIKA

NEW DELHI, India

WATU 60, wakiwemo 11 waliokuwa wakipiga picha za ‘selfie’ kwenye mvua, walifariki baada ya kupigwa na radi katika wilaya 16 nchini India.

Watu 20 walijeruhiwa vibaya huku mifugo 250 wakiuawa katika mkasa huo.

Miongoni mwa waliouawa kwenye mkasa huo uliotokea Jumapili, 14 walikuwa wakazi wa wilaya ya Prayagraj, jimbo la Uttar Pradesh.

Waziri Mkuu Narendra Modi alisema kuwa, kila familia iliyopoteza jamaa itapewa Sh185,300 za kufutia machozi. Waliojeruhiwa watalipwa fidia ya Sh46,300 na waliopoteza mifugo na mazao yao pia watalipwa fidia. Serikali za majimbo pia zimetangaza kutoa msaada wa kifedha kwa waathiriwa.

Wengi wa waliokufa walikuwa watoto na wanawake.

Jumamosi, watu wengine 20 waliuawa na radi katika majimbo ya Uttar Pradesh na Rajasthan.

Afisa Mkuu wa Polisi Anand Srivastava alisema miongoni mwa waliokufa, 11 walikuwa wakipiga picha za selfie katika mnara wa kitaifa wa Amber Fort mjini Jaipur, kabla ya kupigwa na radi, Jumapili. Watu sita walipigwa na radi katika eneo la Soraon na wawili waliangamia kijijini Koraon.

Maeneo mengine yaliyoshuhudia vifo kwenye mkasa huo wa radi ni Prayagraj na Firozabad.

Wakulima wawili waliuawa na radi walipokuwa wakifanya kazi kwenye mashamba yao katika eneo la Ramsevak. Mvua ilipoanza kunyesha, wawili hao, walienda kujikinga chini ya mti kabla ya radi kutokea na kuwaua papo hapo.

Mwanamume mmoja alifanikiwa kuokoa familia yake kwa kuwakimbiza watoto wake ndani ya nyumba na radi ilipotokea iliua mifugo wake 42.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa watu 2,876 na 2,357 walifariki kwa kupigwa na radi nchini India mnamo 2019 na 2018 mtawalia.

Visa vya watu kuuawa kwa radi nchini India huwa vingi kati ya Juni na Septemba kila mwaka ambao ni msimu wa upepo mkali unaovuma kutoka baharini na huandamana na mvua.

Mnamo 2019, watu 400 waliuawa kwa radi jimboni Bihar (400), Madhya Pradesh (400), Jharkhand (334) ana Uttar Pradesh (321).

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya India (NWS) iliwashauri raia wa nchi hiyo kuhakikisha kuwa wanaingia ndani ya nyumba mvua inapoanza kunyesha.

Idara hiyo ilisema kuwa, japo radi haina kinga, kuingia ndani ya nyumba kunaweza kusaidia pakubwa kupunguza vifo.

“Mvua inapoanza kunyesha, ingia ndani ya nyumba. Nyumba zilizojengwa kwa mawe au matofali zinazuia makali ya radi. Ukiwa ndani ya gari, hakikisha kuwa unafunga mlango na madirisha,” ikashauri idara ya NWS.

Mafuriko yaua 18, wengine 200 hawajulikani walipo

Na AFP

RISHIKESH, India

WATU 18 wamethibitishwa kufariki na wengine 200 hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokea baada ya jiwe la barafu kuporomoka kutoka katika safu ya milima ya Himalaya.

Jiwe hilo la barafu liliporomoka Jumapili asubuhi na kuharibu madaraja, barabara na mabwawa mawili ya kuzalishia umeme.

“Kulikuwa na kishindo kikubwa sawa na tetemeko la ardhi wakati wa kuporomoka kwa jiwe hilo la barafu,” mkazi wa eneo la Omo Agarwal alinukuliwa akisema.

Serikali ya jimbo la Uttarakhand ilisema Jumatatu kuwa miili ya watu 18 tayari imepatikana na waziri mkuu wa jimbo hilo, Trivendra Singh Rawat alithibitisha kuwa zaidi ya watu 200 hawajulikani waliko.

Wengi wa waliotoweka ni wafanyakazi wa vituo viwili vya kuzalisha umeme. Inasadikiwa kuwa baadhi ya waathiriwa wangali wamefunikwa kwa matope na mawe yaliyokuwa yakibingirishwa na mafuriko hayo.

“Maafa yaliyosababishwa na mafuriko hayo yangepungua kwa kiasi kikubwa iwapo maporomoko hayo yangetokea jioni baada ya watu kutoka kazini,” akasema Rawat.

Watu 12 waliokolewa kutoka kwenye moja ya mitaro Jumapili. Lakini watu wengine kati ya 25 na 35 walikuwa wangali wamekwama katika mtaro wa pili, kulingana na mkuu wa masuala wa mikasa wa jimbo hilo, Piyoosh Rautela.

Shughuli ya kuokoa waathiriwa ilipata pigo kutokana na barabara kuharibiwa na tukio hilo, huku wanajeshi wakilazimika kutumia kamba kupanda juu ya mlima kufikia lango za vituo vya kuzalisha umeme.

Wanajeshi na maafisa wa mikasa ya dharura kufikia jana walikuwa wakitumia trekta na vifaa vinginevyo kuondoa tope, miamba na takataka ili kufikia vituo hivyo vya kuzalishia umeme.

Kulingana na maafisa wa uokoaji, kelele za waathiriwa zimekuwa zikisikika; kumaanisha kuwa kuna watu wengi ambao wangali hai.

Serikali ilisema kuwa mafuriko hayo yalitokea baada ya jiwe hilo la barafu kuanguka ndani ya mto.

Barafu nchini India imekuwa ikiyeyuka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ongezeko la joto duniani. Lakini wataalamu wanasema kuwa ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme katika eneo hilo pia huenda kulichangia mawe ya barafu kuwa dhaifu na kuishia kuporomoka.

Mkasa sawa na huo ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 6,000 mnamo 2013 – hali iliyosababisha wataalamu kutaka mradi huo wa mabwawa ya kuzalisha umeme ulio katika jimbo la Uttarakhand lililoko katika mpaka wa Tibet na Nepal, ufutiliwe mbali.

Matokeo ya utafiti uliofanywa 2019 yalionyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya barafu katika safu ya milima ya Himalaya itayeyuka kufikia 2100.

MbS atarajiwa kutanzua mkwamo baina ya India na Pakistan

Na AFP

KASHMIR, INDIA

MAJESHI ya India yalipata pigo Jumatatu katika vita ambavyo yanashiriki na wapiganaji wa Kashmir, baada ya tisa wao kuuawa.

Uvamizi huo unakuja siku chache baada ya shambulio jingine la muuaji wa kujitoa mhanga, wakati joto linazidi kupanda kati ya India na nchi jirani ya Pakistan.

Leo Jumatano Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, maarufu kama MbS inatarajiwa kwamba akiwa jijini New Delhi katika ziara yale ya kibiashara hasa, atazungumzia uhusiano baina ya India na Pakistan kujaribu kutanzua mkwamo uliopo.

India ililaumu Pakistan kwa shambulio hilo la Alhamisi wiki iliyopita dhidi ya msafara wa magari ya kijeshi, ambapo wanajeshi 14 waliangamia.

Katika vamizi hilo la Jumatatu, makabiliano makali ya bunduki yalichacha kwa zaidi ya saa nne katika wilaya ya Pulwama, kusini mwa Jiji kuu la Kashmir, Srinagar, wakati maafisa wa serikali walitangaza kuwa wanajeshi wanne, afisa wa polisi, wanamgambo watatu na raia mmoja waliuawa.

Kati ya waliouawa ni afisa wa kijeshi wa ngazi ya Meja. Aidha, wapiganaji watatu wa upande wa Jaish-e-Mohammed (JeM) wa Pakistan, kundi ambalo lilijigamba kutekeleza vamizi la wiki iliyopita, maafisa wa polisi na jeshi wakasema.

Maafisa sita wa ngazi za juu katika jeshi na polisi walijeruhiwa katika makabiliano ya bunduki yaliyofuata.

Mamia ya wanajeshi walivamia vijiji na kuvamia kwa risasi katika eneo lililoshukiwa kuwa maficho ya wanamgambo hao.

Wahindi wakejeli utumizi wa mafuta ya ng’ombe kutengeneza pesa

MASHIRIKA Na PETER MBURU

JAMII ya Hindu inaitaka benki ya Reserve kutoka Australia kuanza kuchapisha sarafu za noti zisizoundwa kutumia sehemu za wanyama, baada ya kubainika kuwa mafuta ya ng’ombe hutumika kuzichapisha.

Noti mpya ambazo zimeundwa na tayari kuanza kutumiwa katika nchi hiyo, sarafu za noti za $5, $10 na $50. Sarafu za $20 na $100 zitaanza kutumiwa 2019 na 2020 mtawalia.

Wiki hii, Rais wa jamii ya Kihindi duniani Rajan Zed aliitaka benki ya RBA “kuonyesha heshima kwa hisia za Wahindi na kutengeneza noti zisizotumia nyama ya ng’ombe kama kiungo cha kutengeneza.”

Kiwango kidogo cha ‘tallow’, ambayo hupatikana kutoka kwa mafuta ya nyama ya mbuzi ama ng’ombe, kinatumika kutengenezea sarafu hizo ili kuzipa ubora fulani.

Hata hivyo, ng’ombe ni myama takatifu katika dini ya Kihindi na ulaji wake unakinzana na imani zao. Aidha, umepigwa marufuku huko.

Bw Zed sasa anamtaka gavana wa RBA Philip Lowe kuchukulia suala hilo kwa uzito na kurekebisha.

“RBA ingekuwa na busara na kusoma vya kutosha kufahamu mahitaji ya kidini ya wateja wake kabla ya kuwekeza kiwango kikubwa cha pesa hivyo kutengeneza sarafu hizo,” akasema.

Watu wasiokula nyama aidha wameeleza ghadhabu zao kuhusiana na suala hilo.

Ufichuzi kuwa ‘tallow’ hutumiwa katika utengenezaji wa noti ulitolewa Novemba 2016 wakati benki ya Uingereza ilikiri kwenye twitter kuwa kuna kiwango kidogo chake kinachotumika.

Kupitia ujumbe, kampuni hiyo ilisema kuwa inajaribu kukoma kutumia bidhaa hiyo, japo ikisema kuwa “lakini ni hatua ngumu sana.”

Hii si mara ya kwanza kwa kiungo hicho kwenye sarafu kusababisha mzozo, kwani mnamo 2002 ilibainika kuwa kampuni ya vyakula McDonald’s ilikuwa ikitumia tallow kupika chakula cha French Fries. Hata hivyo, baadaye, kampuni hiyo ilianza kutumia mafuta ya nafaka na mimea mingine.

Kuna zaidi ya Wahindi 440,000 nchini Australia kulingana na sense iliyotekelezwa mnamo 2016 na dini hiyo ni ya nne kwa wingi wa wafuasi, baada ya zile za Kikristo, Kiislamu na Wabuddha.

UTAMADUNI: Watu milioni 15 kukongamana katika mito mitakatifu

MASHIRIKA Na PETER MBURU

TAYARI watu milioni 4 wameanza kushiriki utamaduni wa kukongamana majini nchini India, baada yao kwenda katika mito mitakatifu ya Ganges na Yamuna, kuadhimisha hafla ya Kumbh Mela, ambayo ndiyo huwa mkutano mkubwa zaidi wa watu duniani.

Angalau watu milioni 15 wanatarajiwa kuhudhuria katika siku yake ya kwanza pekee, huku katika kipindi kizima cha hafla hiyo ambacho kitakuwa siku 49 kikitarajiwa kuvuta watu milioni 120.

Jamii ya Hindu ina Imani kuwa kuoga katika mito hiyo kutawasaidia kuosha thambi zao na kupata wokovu.

Wanaume watakatifu ndio walikuwa wa kwanza kuwasili kwa hafla hiyo mapema Jumanne, ambapo walijipaka jivu milini na kwenda majini wakiimba, kucheza densi na kupiga picha.

Wakati wa hafla hiyo mnamo 2013, wanawake watakatifu kwa mara ya kwanza katika historia waliruhusiwa kuoga katika maji hayo. Mwaka huu, hata watu wa jinsia mbili waliruhusiwa kushiriki.

“Maandalizi ya mwisho yanaendelea, vikundi vyote vya kidini vimetengewa wakati na nafasi ya kutekeleza utamaduni huo,” akasema Rajeev Rai, afisa mkuu wa usimamizi.

Utamaduni huo umekuwa ukiendeshwa kwa karne nyingi, lakini kwa miongo miwili iliyopita imekua na kubadilika kuwa hafla inayounganisha watu wengi zaidi.

Ghasia baada ya mahakama kuamuru wanawake waruhusiwe hekaluni

BBC na PETER MBURU

KERALA, INDIA

KULIKUWA na maandamano na fujo katika hekalu moja nchini India, baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutoa uamuzi wa kutatanisha, ilipoamua kuwa wanawake wanapasa kuabudu humo, jambo ambalo halijawahi kuonekana.

Hekalu hilo la Sabarimala lililopo katika mji wa Kerala kusini mwa India limekuwa na imani ya aina yake kuwa ni wanaume tu wanaoshiriki, lakini wiki hii mahakama ikaamua kuwa hata wanawake wanapaswa kushiriki ibada.

Uamuzi huo wa korti ulisababisha maandamano makubwa ya fujo, huku zaidi ya polisi 100 wakitumwa kutuliza hali wakati wanawake wawili ambao walijaribu kuingia hekalu hilo kwa mara ya kwanza wakitupiwa mawe na waandamanaji wenye ghadhabu walioziba njia.

Polisi zaidi ya 100 waliwalinda, mwandishi Kavitha Jagdal na mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Rehana Fathima kuzuia mawe waliyokua wanatupiwa na waandamanaji walipokuwa wakitembea kilomita tano sawa na maili tatu kuelekea kwenye hekalu hilo.

Lakini iliwalazimu kurudi baada ya kusimamishwa na wafuasi wa hekalu hilo mita chache kutoka kwenye hekalu hilo.

Waandamanaji pia wamejumuisha wanawake wengi ambao wameshiriki katika migomo, kuziba barabara na kukagua magari yanayokwenda hekaluni yakiwa yamebeba mwanamke yeyote aliye kati ya umri wa miaka 10 mpaka 50.

Hekalu hilo linavutia mamilioni ya wafuasi huko India, huku baadhi ya wanawake wakichukulia hali ya kunyimwa kuingia hekaluni kuwa upendeleo.

Waandamanaji hao sasa wamepinga amri za korti wakisema zinaenda kinyume na matakwa ya Mungu, akiitwa Ayappa.

Waumini wa dini ya Kihindu wanawachukulia wanawake wanaopata hedhi kutowa watakatifu na hivyo huwazuia kushiriki shughuli za kidini.

Hekalu la Sabarimala ni moja kati ya mahekalu machache ambayo huwazuia kabisa wanawake walio katika umri wa kupata hedhi kuingia hekaluni.

Lakini wafuasi wa dini hiyo wamejitetea kuwa kuwakataza wanawake kuingia katika hekalu hilo si kwa sababu ya hedhi pekee, ila pia kwa sababu ya kutii matakwa ya Mungu wao ambaye waaamini ni taratibu zake ili awabariki.

Kila mwaka mamilioni ya wafuasi wa kiume wa dini hiyo hupanda mlima bila viatu ili kuliona kaburi, mbali na kufunga kwa siku 41 na kuepuka kuvuta sigara, pombe, nyama, ngono au kuwasiliana na wanawake walio katika hedhi kabla ya kuanza safari.

Kila mungu katika imani ya Kihindu ana haiba yake na upekee wa visa vyake mwenyewe, na mungu Ayappa hana tofauti.

Mungu Ayyappa hana mahusiano kwani amechukua kiapo cha useja, yaani kutoishi na mwanamke.

Kwa mujibu wa hadithi, Ayappa alizaliwa baada ya muungano kati ya miungu wawili wa kiume ambao wamempa nguvu na uwezo wa kumshinda pepo wakike ambaye alikuwa akisumbua hadi wakati huo.

Watupa mtoto kwa kukejeliwa kuzaa watoto wengi

Na MASHIRIKA na VALENTINE OBARA

KERALA, INDIA

MWANAMUME na mkewe waliyekamatwa na polisi kwa kutupa mtoto wao walisema walifanya hivyo kwa vile majirani walikuwa wakiwacheka kwa kuwa na watoto wengi.

Bitto Davis, 32, na mke wake Pravitha, 28, walinaswa kwenye kamera za CCTV walikamatwa baada ya mwanamume huyo kunaswa kwenye kamera za CCTV akimbusu mtoto wa siku tatu kisha kumtupa kanisani.

Iliripotiwa kuwa jamaa na marafiki wa wawili hao walikuwa wakiwakejeli wakati Pravitha alipokuwa mjamzito.

“Tayari wana watoto watatu wa kiume wenye umri wa miaka minane, sita na minne na huyu alikuwa ni mtoto wao wa nne,” afisa wa polisi alinukuliwa kusema. Watashtakiwa kwa kutelekeza mtoto na ukatili.

Familia yakabiliwa na mzigo wa kulipia upasuaji wa binti yao

Na PETER MBURU

Kwa Muhtasari:

  • Babake Jane Wacuka, aliamua kumgawia sehemu ya ini lake asimwone akiteseka tena
  • Familia hiyo masikini ilifanya mchango na kupata Sh3 milioni
  • Kadri anavyokua Wacuka, ini lake linazidi kuwa dogo

FAMILIA moja katika eneo la Bahati, Nakuru inatatizwa na mzigo wa kulea binti wa miaka 14, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Ingawa mzazi wa mtoto huyo, Bw Geoffrey Warui aliamua kumgawia bintiye sehemu ya ini lake, shughuli hiyo inafaa kufanywa nchini India.

“Inaniuma sana kumwona mwanangu akiteseka kila wakati, amekuwa na matatizo mengi ya afya ambayo yameishia kuathiri elimu yake. Niliamua kumgawia sehemu ya ini langu nisimwone akiteseka tena,” Bw Warui akaeleza Taifa Jumapili.

Msichana Jane Wacuka, 14, amekuwa na ugonjwa wa ini (Liver Cirrhosis) tangu akiwa na miezi sita, jambo ambalo limetatiza hali ya maisha yake na elimu.
Leo, familia hiyo itakuwa ikifanya mchango nyumbani kwao eneo la Ndundori ili kujaza pesa zilizosalia.

Matibabu hayo ambayo yatahusisha upasuaji wa baba na bintiye kwa takriban saa 15, utafanyika katika hospitali moja nchini India na yatagharimu Sh7 milioni.

Familia hiyo masikini ilifanya mchango na kupata Sh3 milioni ambapo wazazi walizuru India mnamo Januari 14 pamoja na binti yao kwa ajili ya upasuaji, wakiwaacha marafiki na familia wakichangisha pesa zilizosalia.

“Utakuwa upasuaji wa wazi baina yangu na binti yangu tukiwa katika chumba kimoja na utaendeshwa na vikosi vitatu vya madaktari watano kila kimoja, kwa saa tano,” Bw Warui akaeleza.

Serikali ya kaunti ya Nakuru imekuwa ikishirikiana na familia hiyo kutoa msaada na iliahidi kuzidi kuwashika mkono.

“Tunaamini kuwa pesa zilizosalia zitapatikana ili mtoto huyo apone na erejelee maisha ya afya bora,” Spika wa kaunti Joel Kairu akasema.

Kulingana na babake mtoto huyo, kadri anavyokua Wacuka, ini lake linakuwa dogo na hivyo inakuwa vigumu kwa mwili wake kuendesha shughuli zake kikamilifu.