FAUSTINE NGILA: Serikali isikimye gharama ya intaneti ikizidi kupanda

NA FAUSTINE NGILA

IWEJE Kenya, taifa linalotambuka Afrika kwa mpenyo wa juu wa intaneti, inaburuta mkia katika orodha ya mwaka huu ya gharama ya vifurushi vya data Afrika Mashariki?

Binafsi ninaishangaa serikali kukubalia kampuni za mawasiliano kuwapunja Wakenya katika kipindi ambapo uchumi wa nchi umezorota kutokana na athari za janga la Covid-19.

Kama hauna habari, basi ng’amua kwamba kwa wastani, unalipa Sh244 kwa kila 1GB ya intaneti ya simu kulingana na takwimu zilizotolewa majuzi na kampuni ya utafiti ya Cable ya Uingereza.

Hii ni maradufu ya Sh112 ambazo wananchi walikuwa wanalipa mwaka uliopita, na hii sasa imefanya Kenya kuwa nyuma ya Tanzania, Rwanda, Uganda na Burundi hapa Afrika Mashariki.

Watanzania wanalipa Sh81 tu na hata taifa linaloongoza barani Afrika, Sudan, linalipisha Sh29. Yamaanisha inawezekana kupunguza bei ya data bila kuathiri sekta zingine, ila serikali imeziachia Safaricom, Airtel na Telkom fursa ya kuongeza bei badala ya kupunguza.

Najua wajiuliza imekuwaje kuwa data hii ni ghali ilhali unalipa Sh1,000 kupata 60GB za Telkom au 75GB za Airtel.

Ukweli ni kwamba kampuni hizi zinatumia teknolojia za kisasa kuchanganua watumizi wa intaneti ya simu. Zimetambua kuwa wananchi wanaotumia chini ya Sh50 kununua intaneti ndio wengi na hivyo kuifanya kuwa ghali na kuisha haraka.

Kwa Sh20, utapata 70MBs tu kwenye Safaricom na zitaisha haraka usivyotarajia, kumaanisha umeuWakenziwa data ya 40Mbs ila arafa inaonyesha 70Mbs.

Kwa wanaolipa Sh1,000 kwenda juu, wanapewa intaneti ya kasi na unayoweza kutegemea, ila ni watu wachache tu wanaweza kumudu bei hiyo. Wanalenga walio chini ndipo waunde mamilioni kwa kuhakikisha data inaisha haraka.

Sababu nyingine ni kuwa Safaricom ndiyo inaongoza kwa mtandao wa mawimbi nchini, hivyo watu wengi hutumia data ya kampuni hiyo ambayo ni ghali. Telkom na Airtel, kwa upande wao, bado wanakabiliwa na upungufu wa mawimbi katika sehemu za mashinani. Ikiwa ulikuwa umenunua intaneti yao na ukasafiri Samburu, basi itabidi ugeukie Safaricom ununue intaneti tena.

Ni mtindo huu ambao umepandisha bei ya data bila kujali kuwa Wakenya wana majukumu mengine ambayo tayari ni ghali. Wengi wamepoteza ajira kutokana na janga la corona na kupata hela za lishe, kodi ya nyumba, matibabu au karo imekuwa changamoto kuu.

Ni wakati wa serikali kugundua kuwa ingawa Wakenya wamefinywa na hali ngumu ya maisha, bado wanahitaji kupata taarifa zinazowahusu kwenye mitandao na bei ya huduma hiyo inafaa kupunguzwa.

Sudan au Somalia ni mataifa yenye uwezo mdogo wa kiuchumi kuliko Kenya, lakini wananchi wake wanafurahia intaneti kwa bei nafuu zaidi. Hii inaaamisha gharama ya kufanya utafiti au kuwekeza kwa huduma za mitandaoni iko chini. Ni nini mataifa hayo yamefanya ambacho Kenya haiwezi kutekeleza?

Hapa Kenya, inaonekana bei ya kila kitu imepanda tangu janga hili lianza kututafuna. Bei ya mkate, unga, mafuta, huduma na sasa intaneti imepanda bila serikali kufanya chochote.

Iwapo serikali itaendelea kuziacha kampuni hizi kunyanyasa Wakenya, basi hata mwaka ujao tutalipa zaidi ya Sh300 kwa kila 1GB ya data. Ni jukumu la serikali kutumia ushuru inaokata wananchi kuwalinda dhidi ya dhuluma hizi.

Waganda washerehekea kurejeshwa kwa intaneti

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA 

RAIA wa Uganda wamesherehekea kurejeshwa kwa huduma za mawasiliano ya intaneti ambazo zilizimwa siku chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 14, 2021.

Hata hivyo, mitandao mbalimbali ya kijamii ilisalia kufungwa na ingefikia tu kupitia mtandao wa siri (VPN).

Rais Yoweri Museveni ambaye aliibuka mshindwa na hivyo kupata nafasi ya kuendelea kuongoza Uganda kwa muhula wa sita, aliishutumu mitandao hiyo kwa kupendelea upande wa upinzani na “kutumiwa vibaya kuendeleza ajenda za wageni.”

Hata hivyo, Robert Kyangulanyi, almaarufu Bobi Wine, ambaye alikuwa wa pili katika matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, alidai kuwa serikali ya Museveni ilizima mawasiliano na intaneti na mitandao ya kijamii ili ifanikishe nia yake ya kuiba kura.

Naye Katiba Mkuu wa chama cha National Unity Platform (NUP) kilichodhamini Bw Wine, Joel Ssenyonyi alimshutumu Museveni kwa kuzima huduma za intaneti ili kuwazuia kuwasilisha ushahidi kuhudu udanganyifu katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, aliwaambia wanahabari kuwa chama hicho kinaendelea kukusanya fomu za matokeo ya uchaguzi wa urais, zilizo na ushahidi wa udanganyifu.

Tume ya uchaguzi ilimtangaza Museveni mshindi kwa kuzoa asilimia 58.64 ya kura zilizopigwa huku Wine ambaye alikuwa mpinzani wake wa karibu akipata asilimia 34 ya kura.

Ushindi huo sasa unaashiria kuwa Museveni mwenye umri wa miaka 76 ataongoza Uganda kwa miongo minne (miaka 40) ikizingatiwa kuwa aliingia mamlakani mnamo 1986.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu imeshutumu vikali serikali ya Museveni kwa kuzima mifumo ya mawasiliano.

Wakati huo huo, maafisa wa usalama wanaendelea kuzingira boma la Bobi Wine viungani mwa jiji la Kampala huku mwanasiasa huyo akilalamika kuwa familia yake inakeketwa na njaa kwa kukosa chakula.

Mshindi wa urais Uganda kujulikana kesho

NA DAILY MONITOR

TUME Huru ya Uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kumtangaza mshindi wa kiti cha Urais hapo Jumamosi baada ya kuandaa uchaguzi wake mkuu Alhamisi.

Sheria ya tume hiyo inasisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi lazima yatangazwe saa 28 baada ya upigaji kura kumalizika. Shughuli za uhesabu wa kura bado zinaendelea kote nchini na matokeo ya awali yanaanza kupokelewa leo kutoka vituo mbalimbali vya kupiga kura.

Zaidi ya wapigakura milioni 18 walimiminika katika vituo mbalimbali kumchagua Rais mpya huku ushindani mkali ukitarajiwa kuwa kati ya Rais Yoweri Museveni na Mwanasiasa mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Huduma za mitandao nazo zilisalia kuzimwa kwa siku ya pili mfululizo hatua iliyochukuliwa na serikali ili kuzuia raia kueneza habari ambazo zingezua taharuki na ghasia.

Pia kulikuwa na visa vya mashine za kielektroniki za kuwatambua wapigakura kufeli kufanya kazi katika Wilaya ya Wakiso na pia masanduku ya kupiga kura yalichelewa kufika katika baadhi ya maeneo ya mashinani na hata kwenye baadhi ya vituo jijini Kampala.

Katika kituo cha polisi Gayaza, shughuli za upigaji kura hazikuwa zimeanza kufikia saa tatu asubuhi baada ya mashine za kielektroniki za kuwatambua wapiga kura kukosa kufanya kazi.

“Nimetembelea vituo vingi vya kupiga kura na hakuna chochote kinachoendelea. Baadhi wameondoka kwa hasira huku wengine nao wakiwazomea maafisa wa uchaguzi,” akasema mmoja wa waangalizi Lydia Ainomugisha.

Katika Manispaa ya Kira, watu walisusia kupiga kura baada ya kugundua masunduku yaliyokuwa na karatasi za kupiga kura yalikuwa yamefunguliwa.

Vijana katika kituo cha Wandegeya, nao walikataa kuwapisha wazee na akina mama wajawazito kutangulia kupiga kura wakisema kuwa hata wao walikuwa na haraka ya kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

“Tumekuwa tukiwaruhusu wazee hawa na akina mama kutangulia kila mwaka wa uchaguzi kisha wanawapigia kura viongozi wakongwe wasiotusaidia kitu. Leo hatutawahurumia wazee hao kwa sababu watakufa hivi karibuni na kutuacha hapa tukiteswa na viongozi hao ilhali wao ndio waliwachagua. Tumekuwa tukiwaheshimu lakini leo wapange laini au warejee nyumbani,” akasema kijana mmoja.

Hapo Alhamisi, usalama uliimarishwa katika vituo mbalimbali vya kupiga kura hasa jiji la Kampala ambalo kwa miaka mingi imekuwa ngome ya upinzani.

Baadhi ya maafisa wa polisi walionekana wakipanda kwenye paa ya majumba marefu wakiwa wamejihami vikali kupambana na utovu wowote wa usalama.

Katika mtaa wa mabanda wa Kamwokya ambako Bobi Wine alilelewa, foleni ndefu zilishuhudiwa huku nao polisi wakiwa ange kuhakikisha kuwa raia wanasimama umbali wa mita moja unusu kuzuia maambukizi ya corona.

“Niko hapa kupiga kura ili kubadilisha uongozi wa nchi. Mara nyingi utawala wa sasa umekuwa ukidai utabadilisha maisha yangu lakini hali bado ni ile ile,” akasema dereva Joseph Ndung’u aliyekuwa kati ya watu wa kwanza kupiga kura.

Mwaniaji huru Henry Tumukunde ambaye alipiga kura yake katika kituo cha Kisementi, jijini Kampala naye alisema hatukubali matokeo hata kabla ya kura kuhesabiwa akisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu.

“Angalia nimepiga kura lakini baada ya kutumia sanitaiza, mkono umekuwa safi na wino umefutika. Watu wanaweza kupiga kura hata zaidi ya mara moja hasa ikizingatiwa mashine nazo zinafeli. Sitakubali matokeo hayo,” akasema.Rais Yoweri Museveni, Wine na wawaniaji wote walipiga kura kwenye uchaguzi huo ambao ulishirikisha nyadhifa za ubunge na udiwani.

TAFSIRI NA CECIL ODONGO

Masharti ya kuzima wazee yazua kizuizi kwa ufunguzi wa makanisa

TITUS OMINDE, DIANA MUTHEU na MAUREEN ONGALA

IBADA ndani ya makanisa na misikiti huenda zikaathirika, baada ya viongozi wa kidini kusema mojawapo ya masharti ya ufunguzi inawazuia wao kushiriki.

Kwenye kikao na wanahabari mjini Eldoret, Jumapili, viongozi hao walisema sharti la kuzuia watu wa zaidi ya miaka 58 linawazuia wengi wao kushiriki ibada hizo.

“Sharti la kuzuia wazee wa umri wa miaka zaidi ya 58 kuhudhuria ibada ni pigo kwa kanisa. Makanisa yetu mengi yanaongozwa na wazee. Vijana wamepotelea katika pombe na hawana ufahamu wa mambo ya dini,” akasema kiongozi wa muungano huo wa waumini, Askofu Wilson Kirui.

Walidai vikwazo vilivyowekwa vina nia fiche ya kulemaza kanisa, hivyo basi hawakubaliani na kamati iliyohusika kutoa mapendekezo hayo kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Kuzuia wazee kuhudhuria ibada ni sawa na kuacha kondoo bila mchungaji,” akasema Askofu Kirui.

Naye Kasisi Boniface Simani wa kanisa la Bread Of Life, aliitaka serikali iondoe vikwazo hivyo, akisema hata kuzuia watoto kuhudhuria ibada ni sawa na kulemaza kanisa la siku za usoni.

Naye mhubiri maarufu Askofu J.B. Masinde wa kanisa la Deliverance Umoja jijini Nairobi alisema kanisa hilo halitafunguliwa kwa ibada na wataendelea kutoa mahubiri kupitia intaneti.

Askofu David Oginde wa CITAM pia ametangaza kuwa hawatafungua.

Wakuu wengi wa dini nchini ni wazee wa umri wa kuanzia miaka 60.

Katika kaunti ya Mombasa, waumini wengi Jumapili walidinda kuhudhuria ibada, hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa makanisa yako huru kufunguliwa.

Wakizungumza na Taifa Leo, walisema sheria ambazo makanisa yaliagizwa kufuata ni ngumu.

Kwa maoni yake, Bw Simon Mwaniki ambaye ni mshirika wa kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC), alisema kuwa alijihisi salama zaidi kufuatilia ibada akiwa nyumbani.

“Kwa maoni yangu, sheria hizo ni nyingi sana. Tumepewa jukumu la kujikinga wenyewe kutokana na virusi hivi na ni heri nisalie tu nyumbani ambapo bado nahubiriwa mtandaoni. Natuma sadaka kwa njia ya simu na cha muhimu zaidi, afya yangu nimeilinda,” akasema Bw Mwaniki.

Kwa upande wake, Collins Omondi ambaye ni mshirika wa kanisa la LifePoint, Mombasa alisema bado ana uwoga wa kutangamana na watu wengine.

Lakini katika Kaunti ya Kilifi, Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, alianzisha shughuli ya kunyunyuzia dawa makanisani, huku akiitaka serikali iwakumbuke wahubiri ambao wanaendelea kuathiriwa na maambukizi ya corona.

Akizungumza katika eneo la Mtepeni alipowagawia chakula cha zaidi ya wahubiri 600 Bw Chonga alisema viongozi wa kidini wameathiriwa mno na kufungwa kwa makanisa, japo wengi wao wamekataa kujitokeza kuomba misaada.

Gharama za juu za Intaneti nchini Uganda zawafungia wengi nje

Na MAGDALENE WANJA

IDADI ya wanaotumia mtandao nchini Uganda ilipungua kwa asilimia 30 mwaka 2018 baada ya serikali kuongeza kodi kwenye huduma za simu zinazotumia mtandao.

Serikali ya Uganda iliweka kodi ya asilimia moja kwa shughuli mbalimbali kama vile kutoa na kuweka pesa kwenye simu ambayo iliongeza gharama kutoka asilimia 10 had asilimia 15.

Vilevile, iliongeza kodi mpya kwa zaidi ya huduma 60 za Facebook, WhatsApp na Twitter ambayo ilichangia kuwa Sh200 za Uganda kila siku.

Kulingana na utafiti kuhusu huduma ya Regulatory Treatment of Over the Top Services; kodi ambayo inawekwa bila kuwahusisha wananchi ama kufanya upelelezi kuhusu madhara yake, hali hii imechangia katika watu wengi kuachana na matumizi ya mtandao.

Utafiti huo ulifanywa katika baadhi ya mataifa ya Afrika likiwemo lile la Uganda.

Matokeo ya utafiti huo yalitolewa na kampuni ya Mozilla ikishirikiana na Tume ya Umoja wa Afrika yaani African Union Commission (AUC).

“Hizi ni baadhi ya hatua ambazo serikali inachukua ambazo zinapunguza idadi ya watu wanaotumia mtandao badala ya kuiongeza idadi hiyo,” alisema mshauri wa sera wa Mozilla barani Afrika Bi Alice Munyua.

Watafiti sasa wameshauri nchi za Afrika kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kukuza uchumi wa nchi.

Banglandesh yazima tovuti 20,000 za ngono

MASHIRIKA Na PETER MBURU

SERIKALI ya Bangladesh imezima takriban tovuti 20,000 ambazo zimekuwa zikipeperusha mambo ya ngono na michezo ya kamari, kama sehemu ya operesheni ya kumaliza biashara hiyo, waziri amedhibitisha.

Watoaji wa huduma za intaneti wiki iliyopita waliondoa tovuti zote ambazo zinatoa huduma za Kamari ama kanda za ngono, baada ya kuamrishwa na mamlaka ya kudhibiti mitandao ya mawasiliano nchini humo.

“Nataka kuwe na intaneti salama na safi kwa raia wote wa Bangladesh, ikiwemo watoto. Na hivi ni vita vyangu dhidi ya mitandao ya ngono na vitakuwa vita visivyoisha,” akasema Mustafa Jabbar, waziri wa mawasiliano.

Mitandao ya kijamii kama TikTok na Bigo ambayo ina umaarufu mkubwa nchini humo- na ambayo serikali inaamini imekuwa ikitumiwa vibaya- aidha ilizimwa, Bw Jabbar akadhibitisha.

Mitandao mingi iliyozimwa imekuwa ikiendeshwa kutoka nje ya nchi hiyo, japo mingine pamoja na ile ya kijamii imekuwa ikiendeshwa kutoka ndani ya mipaka yake.

Operesheni hiyo ilianzishwa baada ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo Novemba mwaka uliopita kuamrisha tovuti za ngono kupigwa marufuku na kuzimwa.

Korti ilitoa uamuzi huo baada ya shirika la kutetea haki kufika kortini, likisema kuwa mitandao mingi ilikuwa ikichapisha mambo ya kupotosha kimaadili.

“Tunachunguza kurasa za Facebook za humu nchini, mitandao ya Youtube na tovuti pia,” akasema Bw Jabbar.

“Chache zimezimwa kwa kuwa na mambo yasiyokubalika kimaadili. Tumeshauri watu wengine kutochapisha kitu chochote ambacho kinakiuka maadili yetu ya kijamii,” akasema.

Bangladesh kuna zaidi ya raia milioni 160 na asilimia 90 yao ni watumizi wa intaneti. Masuala ya ngono yamekuwa yakiongoza kitu ambacho raia wa nchi hiyo wanatumia kwenye intaneti sana.

Lindeni watoto dhidi ya hatari za intaneti – Safaricom

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Safaricom imewashauri washikadau kuwalinda watoto dhidi ya hatari inayotokana na matumizi ya intaneti.

Afisa wa uhusiano wa wateja wa Safaricom Bw Stephen Chege alisema kampuni hiyo zaidi ya kulenga kuimarika kibiashara, inalenga pia kuimarisha usalama wa wateja wake hasa watoto.

“Tunataka kila mtu kuwa na uwezo wa kusoma mambo mapya bila kutishiwa usalama wao,” alisema Bw Chege.

Aliwataka wateja wa Safaricom kutumia intaneti kwa kuwajibika na kuheshimu watu wengine.

Mnamo Novemba 2018, Safaricom ilitia saini mkataba wa kuimarisha usalama katika matumizi ya intaneti pamoja na kampuni zingine za simu nchini.

Safaricom pia ilizindua sera ya kuwalinda watoto mitandaoni na inashirikiana na Wakfu wa Internet Watch Foundation kuziba maudhui ya ngono kwa watoto wake katika mfumo wake wa intaneti.

2019: Ukosefu wa usiri wa data mitandaoni utazidi kuwaumiza Wakenya mwaka huu

Na FAUSTINE NGILA

TEKNOLOJIA ya dijitali mwaka uliopita ilituwezesha kupata taarifa tunazotaka mitandaoni kwa urahisi zaidi ila bila kujali athari za kukubalia mitandao hiyo kutuchunguza.

Tulichohitaji kufanya ni kufungua tovuti kwenye intaneti na kujipakulia huduma kadha kama ununuzi wa bidhaa, upakuaji wa video na matini ya kusoma, na kurambaza mitandao ya kijamii bila vizuizi.

Hata hivyo, kupakua taarifa hizi humaanisha kukiuka kanuni kuhusu ukusanyaji wa data, matumizi yake na ulinzi wa taarifa zetu za siri.

Yamkini kila Mkenya hubonyeza maandishi ‘Ninakubali’ bila kusoma na kuelewa masharti ya tovuti nyingi kwenye intaneti, na hivyo kuziruhusu tovuti hizi kukusanya data kumhusu bila taarifa kutokana na uzembe wake wa kusoma.

Mwaka 2019 utazidi kuwa hivi, kwa kuwa kizazi cha dijitali hakipendi kabisa kudurusu maandishi ya masharti ya tovuti, programu za simu na mitandao ya kijamii kabla ya kupokea huduma zake.

Mwaka huu data zote za siri zitakuwa wazi kwa kuwa tunapopakua programu za simu, ujumbe wa onyo huja: ‘Je, ungependa kuiruhusu apu hii kukusanya data yako ya simu kuhusu orodha ya nambari za simu, picha, video, sauti, umri, jinsia, familia, ajira, nambari ya kitambulisho na historia ya intaneti?’

Wakenya wengi hubonyeza ‘Ndiyo’, na hapo ndipo tunazikandamiza sisi wenyewe haki zetu za usiri wa data.

Hii inamaanisha kuwa tumebadilisha imani na mtazamo wetu kuhusu usiri wa data na jinsi tunajithamini, na kukubali kuwa watumwa wa mitandao.

Na huu ndio mwaka utawasikia Wakenya wakilalamikia baada ya data za siri kuwahusu kutumika kwa shughuli nyingine, huku wakisahau wameiruhusu Google kukusanya na kuhifadhi taarifa kuhusu maeneo wanayozuru, wanakoishi na wanaotangamana nao.

Huku teknolojia ya dijitali ikizidi kuwa nguzo muhimu ya maisha ya Wakenya, tofauti ya taarifa za umma na data za kibinafsi itazidi kuwa finyu mwaka huu, na wataalamu wengi wanakubali mjadala kuhusu usiri na ulinzi wa data haupo tena.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya ulinzi wa data za mitandaoni GreyCastle Security, Bw Reg Harnish, dhana ya usiri wa data ni ndoto.

“Katika miaka ijayo, tutakuwa tukizungumza kuhusu usiri wa data jinsi tunavyotania simu za jamii,” anasema.

Anaelezea kuwa bado kuna manufaa ya ulimwengu usio na dhana ya sasa kuhusu usiri wa taarifa.

Tofauti na Amerika ambapo data hiyo hukusanywa na serikali kuwafaa wananchi wake, hapa nchini baadhi ya kampuni hutumia data kuhusu Wakenya kujinufaisha huku mianya ya wizi wa hela ikijitokeza.

“Uwepo wa data nyingi mikono mwa watu wachache ni hatari , lakini iwapo ulimwengu ambao utatumia data hiyo pamoja utaondoa hatari hiyo, hasa katika uvumbuzi wa teknolojia mpya zinazowafaa watu kijamii,” anasema.

Huu utakuwa mwaka ambao Wakenya watakubali kabisa kuuza usiri wao ili kupata starehe za mitandaoni, lakini hatimaye watachoka na kuamua kurudishiwa usiri wao.

Lakini suluhu ni nini? Badala ya kulaani jinsi habari zinapatika na kwa urahisi, Wakenya wanafaa kubuni mbinu za kuzuia ukusanyaji wa data muhimu kuwahusu.

Licha ya Sheria ya Habari na Mawasiliano kubuniwa Kenya, huenda isiwalinde Wakenya dhidi ya ukusanyaji wa data bila taarifa, kwa kuwa Wakenya wamezoea mtindo wa kuruhusu mitandao kupakua data zao.

Kutokuwa na habari

Tatizo ni kwamba hatujui aina ya data tunayosambaza kwa mitandao ya kijamii na idadi ya data hiyo, na kwamba hatuna mamlaka tena ya kurudisha data ambayo tayari tushasambaza.

Wakati sera za Facebook kuhusu ubinafsi wa data zinasema kampuni hiyo inaweza kukusanya data unayotengeneza au kuchapisha, inamaanisha kuwa posti zote ambazo umeunda lakini ukakosa kuchapisha pia zitakusanywa.

Kwa kuwa Wakenya wamekubali kuuza usiri wao ili wapate starehe za dijitali, kile ambacho ni hatari zaidi ni kukosa kuelewa madhara ya kufanya hivyo.

Ikumbukwe kuwa ukusanyaji wa data mitandaoni ni zaidi ya kutia neno siri kwa tovuti au kupakua apu, kwani runinga za dijitali na vituo vya Wi-Fi pia ziko mbioni kukusanya taarifa kukuhusu.

Mwishoni mwa mwaka huu, utapata kwamba taarifa zote kukuhusu zimekusanywa na kuhifadhiwa. Kando na machapisho ya mitandaoni, utashangaa kuwa mawazo na maamuzi yako pia yanajulikana.

Kukabili hili, tunafaa kuanza kujali kuhusu umuhimu wa kulinda data zetu za siri, na kusoma kwa makini masharti ya kuingia kwa baadhi ya tovuti, na kuwafunza watoto wetu kuhusu hatari iliyopo ya kuruhusu kampuni za dijitali kukusanya data zao.

Kwa mfano, tatizo la usiri wa data mwaka 2018 halikuwa udukuzi bali kampuni za teknolojia zenyewe, ambazo zilivuna milima ya data na kutumia mifumo ya hila kusambaza data hiyo kujinufaisha.

Sakata ya Facebook iliyohusisha kampuni ya Cambrige Analytica ilitokana na huduma ya Facebook kwa jina Facebook Graph API. Katika hali hiyo, Facebook iliundwa kukusanya data nyingi iwezavyo, kisha kuisambaza bila kujali kwa waundaji wa programu za simu.

Ikumbukwe kuwa hatari hii huleta athari za kisiasa, hasa baada ya kiongozi wa chama cha ODM kudai kuwa Cambrige Analytita ilichangia katika wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Iliripotiwa 2018 kuwa Facebook na Google zilishirikiana na benki na kununua data za kifedha kuhusu wateja wa benki hizo kisiri, hali ilizyozua maswali mazito kuhusu usiri wa data muhimu ya wateja.

Kampuni kama Yahoo na Facebook huwafungia nje watumizi ambao hawako tayari kuruhusu ukusanyaji wa data kuwahusu, hali ambayo inaibua hisia kuhusu iwapo 2019 tutahitaji sheria ya kimataifa kulinda data ya watumizi.

Kenya kunufaika na mradi wa kuweka intaneti vijijini

NA AGGREY MUTAMBO

KENYA ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayotarajiwa kunufaika na mradi mpya unaolenga kupanua idadi ya maeneo ambayo raia wake wanaweza kufikia huduma za mtandao Barani Afrika.

Benki ya uwekezaji ya Bara Uropa, Jumanne ilitangaza kwamba itafadhili kampuni moja ya kibinafsi kujenga miundombinu ya kupenyeza huduma za intaneti katika vijiji vya mashambani nchini Kenya, Rwanda, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mradi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miaka miwili na utatekelezwa na kampuni ambayo jina lake bado halijatangazwa.

Lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha uwezo wa raia wa mataifa hayo kunufaika na huduma za mtandao ili kurahisisha shughuli zao za kiuchumi kupitia njia za kidigitali.

Kulingana na benki hiyo, mradi huo utagharimu Sh1.8bilioni hii ikiwa sehemu ya mabilioni ya fedha yaliyotengewa uimarishaji wa miradi mbalimbali kama uchukuzi, kawi safi na uwezo wa kufikia intaneti barani Afrika.

“Uchukuzi wa kutegemewa, kawi na mitandao ya mawasiliano ni changamoto zinazokabili mataifa ya Bara Uropa na Afrika. Tukifanya kazi pamoja tunaweza kuimarisha maisha ya mamilioni ya watu. Miradi mitatu iliyotiwa saini leo inadhihirisha hili,” akasema Dkt Werner Hoyer, Rais wa Benki ya uwekezaji wa Bara Uropa kupitia taarifa kwa wanahabari Jumanne.

Tangazo hilo lilitolewa pembeni mwa Kongamano kubwa kati ya mataifa ya Bara Afrika na Uropa linaloendelea mjini Vienna, Austria.

Mkutano huo pia unahudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Bara Afrika (AU).

Mada kuu ya Kongamano hilo ni ‘’Kufikisha ushirikiano kwa kizazi cha kidigitali’ na la mno haswa ni kutumia ubunifu na udigitali kama kichocheo cha maendeleo siku zijazo ili kunufaisha kila raia wakati dunia inapoendelea kukumbatia mwamko mpya wa utandawazi.

Wakenya wengi wanapenda simu za Tecno – Utafiti

Na CHRIS ADUNGO

KAMPUNI ya Uchina, Transsion Holdings inaongoza kwa mauzo ya simu za mkononi katika soko la Kenya kulingan na utafiti wa hivi majuzi.  

Bradi zake tatu, Tecno, Infinix na iTel ni miongoni mwa tano bora zinazoenziwa na Wakenya kote nchini, kulingana na utafiti wa Consumer Insight.

Kwenye ripoti yake, brandi hizo tatu zina jumla ya asilimia 54 ya simu zote zinazomilikiwa na Wakenya. Mwaka 2016, brandi mbili za kampuni hiyo – Tecno na iTel – zilikuwa na asilimia 34 ya soko la simu nchini.

Kwa watu waliohojiwa katika utafiti huo, asilimia 28 wanatumia simu za Tecno, asilimia 16 simu za Samsung, asilimia 12 Nokoa na asilimia 10 Infinix.

Katika ripoti tofauti, kampuni ya Jumia imeonyesha kuwa Kenya inaongoza kote ulimwenguni kwa trafiki ya intaneti kutokana na ununuzi wa simu na kuipiku Nigeria, ambayo iliongoza mwaka 2017.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa kampuni ya Transsion Holdings imechochea pakubwa kupanuka kwa utumizi wa simu za kisasa humu nchini. Kampuni hiyo kutoka Hong Kong ndiyo kubwa zaidi barani Afrika kwa mauzo.

Brandi za simu za Korea Kusini kama Samsung, Huawei, LG  na Nokia zimepata ushindani mkali kutoka kwa brandi za Uchina zinazowapa Wakenya simu za kifahari kwa bei nafuu.

Orion yajitosa kwa biashara ya mtandaoni

Na CHRIS ADUNGO

MADUKA ya Orion yanayofanya biashara ya mtandaoni humu nchini yamejiunga na shirika la ununuzi na uuzaji wa mitandaoni  humu nchini, Kenya Online Shopping Space, ambalo hivi karibuni limedhidhirisha kuwa mazingira ni shwari.

Biashara kupitia kwa intaneti (E-Commerce) huwezesha ununuzi na uuzaji wa bidhaa mbalimbali katika mitandao zikiwemo elektroniki, vyakula na mboga.

‘’Tunataka kutoa njia nyepesi inayowezesha  wateja kuagiza bidhaa na huduma kupitia mitandao,’’ akasema Peter Wangai,  mwasisi wa maduka ya mtandaoni ya Orion .

Sekta ya E-Commerce barani Afrika imekua kwa kasi na inatarajiwa kufika dola milioni 28,942 kufikia mwaka wa 2022 kulingana na ripoti  ya 2017 kuhusu mtazamo wa masoko ya dijitali.

‘’Tutatumia pia trafiki ya tovuti yetu kutangaza mapato tunayopata kutoka kwa washirika na watangazaji. Mwanzoni, Orion itafanya biashara kutokana na bidhaa zake ikishirikiana na wauzaji wa rejareja kwenye tovuti watakaolipwa kulingana na idadi ya bidhaa watakazouza.”

Kulingana na waujazi wa  mitandaoni, uuzaji wa rejareja wa mitandaoni umechukua asilimia 10 ya biashara hiyo kote duniani ambayo ina thamani ya dola trillion 290 kulingana na takwimu za mwaka wa 2017

Mwaka 2017,  kampuni ya Safaricom ya Kenya ilizindua biashara kwa njia ya intaneti iliyokuwa na bidhaa elfu ishirini kutoka kwa wachuuzi 160.

 

Kisura ataka picha zake mtandaoni ili ajue polo anampenda

Na LEAH MAKENA

KILELESHWA, NAIROBI

Mzozo mkali uliibuka kati ya wapenzi wa hapa pale kidosho alipojaribu kumlazimisha jamaa kuanika picha zake kwenye mtandao kama thibitisho kuwa alimpenda. Yasemekana jamaa alikutana na kipusa wiki moja baada ya kutengana na mpenzi wake wa awali.

“Kabla ya wawili hao kukutana, polo alikuwa na mchumba aliyekuwa amemtandaza kwenye mitandao yake yote ya kijamii,” alisema mdokezi.

Inasemekana jamaa alidinda kuziondoa picha hizo baada ya kutengana na mwanadada huyo akidai kuwa zilikuwa za kumbukumbu.

Licha ya kidosho kumsihi jamaa kuondoa picha hizo ili aweke zake, polo alisita na kusema kuwa mapenzi yake kwa mrembo yalikuwa rohoni na wala sio mtandaoni, jibu ambalo halikumridhisha kipusa.

Siku ya kioja, kidosho alikuwa amemtembelea  polo na alipopata simu yake, akavamia picha zilizokuwa kwenye mtandao na kuzifuta zote kwa matarajio kuwa jamaa angeweka zake.

Inasemekana kuwa polo alipandwa na mori kwa kitendo cha kidosho na hapo ndipo alimhakikishia kuwa kamwe hangetumia picha zingine kwenye mtandao.

“Mara ngapi nimekwambia sidhamini mapenzi ya mtandao? Unafaa kuelewa kuwa huwezi kunilazimisha kufanya jambo ambalo sitaki. Iwapo huna imani nami nimekupa uhuru wa kutafuta utakaowaamini,” polo aliteta.

Wadokezi wetu walisema kuwa, kidosho alitulia ila hatua ya kutoweka picha zake mtandaoni ilisalia kitendawili huku akishuku kuwa huenda polo alikuwa akiendeleza mazungumzo na mpenzi wake wa awali kwa lengo la kuzika tofauti zao na kurudiana.

Inasemekana demu ameanza kuchunguza mienendo ya jamaa kisiri kujua iwapo huwa anawasiliana na mpenzi wake wa zamani.

…WAZO BONZO…