Viongozi wa makanisa wataka bei ishuke

Na WINNIE ONYANDO

VIONGOZI wa makanisa wameomba serikali ipunguze bei za mafuta wakisema ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.

Wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana (ACK), Jackson ole Sapit, viongozi hao wanadai bei hizo zinawaathiri raia ambao tayari wanapitia wakati mgumu kutokana na corona.

Akizungumza Alhamisi katika mkutano na viongozi wa makanisa ya Anglikana nchini, uliofanyika katika Kanisa la All Saints Cathedral, Askofu Sapit alisema hatua ya kuongezwa kwa bei za dizeli, petroli na mafuta ya taa inafanya gharama ya maisha kuendelea kupanda.

“Sisi kama viongozi wa makanisa, tunaomba serikali ipunguze bei za mafuta. Hii itakuwa afueni kwa raia,” akarai Askofu Sapit.

Kadhalika, alitaka serikali ipunguze ushuru unaotozwa kwa Wakenya akisema pia ni mzigo kwa raia.

“Wengi tayari wamelemewa na majukumu nyumbani. Hii ni kwa sababu serikali inatoza ushuru wa juu huku bei za bidhaa pia zikiendelea kupanda. Tunaomba serikali izitatue shida zinazowaandama wananchi kabla ya uchaguzi wa mwaka 2022,” akasema.

Alisema kuongezeka la bei za mafuta na ushuru wa juu utafanya nchi isipige hatua hasa kimaendeleo.

“Ni wakati mwafaka kwa serikali kupambana na umaskini nchini. Tukiendelea hivi, uchumi wetu utaendelea kudidimia,” akaongeza.

Kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa hatabadili msimamo wake wa kupiga marufuku wanasiasa kuzungumza katika makanisani yote ya ACK.Alisema mimbari ni mahali patakatifu na hapafai kutumiwa na wanasiasa kujipigia debe.

Kama njia ya kuhakikisha maamuzi hayo yanatekelezwa, Askofu Sapit alisema hataruhusu harambee zifanywe katika makanisa yote ya ACK hatua inayolenga kuwazuia wanasiasa makanisani.

“Hatutaruhusu harambee zifanyiwe makanisani. Tunataka tutofautishe kanisa na hafla za kisisa,” akasema.

Aliwataka wanasiasa waheshimu maabadi huku akisisitiza kuwa mimbari ni za makasisi pekee na si wanasiasa.

Alisema makanisa ya ACK yanapanga kuzindua programu za kuwahamasisha wananchi kudumisha amani hasa nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu.Kadhalika, aliwaomba wanasiasa kuepuka maneno ya chuki na ya kueneza ukabila wakati wa kampeni.

TAHARIRI: Makanisa mengine nao waige mfano kanisa la ACK

NA MHARIRI

MSIMU wa siasa huwa muda wa wanasiasa kufanya lolote. Ndio wakati ambao utawaona masokoni, matangani, harusini, na hata makanisani.

Kutokana na kanuni za kuzuia maambukizi ya corona, serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu kwenye viwanja na kumbi mbalimbali.

Maeneo pekee ambako bado watu wanapatikana kwa wingi, ni katika makanisa.Si ajabu kwamba ghafla wanasiasa wanaomezea mate kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao, wamekuwa waumini wakuu kila Jumapili.

Jana Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga na mwenzake wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi walikuwa kanisani Butere, Kakamega.

Kanisa la Kianglikana (ACK) lilikuwa likimtawaza Askofu wa Dayosisi ya Butere, Rose Okeno.Ingawa hafla hiyo ilikuwa ya kihistoria kwa kuwa Bi Okeno ni mwanamke wa kwanza kuchukua wadhifa huo, kuhudhuria kwa wanasiasa hao kulikuwa na lengo tofauti.

Ndio maana Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alipotangaza kwamba hawangeruhusiwa kuhutubu, waliondoka mmoja baada ya mwengine.Kwa kawaida, wanasiasa huwa wanatumia mialiko katika hafla za makanisa na ibada zinazohudhuriwa na watu wengi, kuuza sera zao, hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Vigogo hao wa kisiasa huwa wanaandamana na wabunge na madiwani, na hugeuza hafla za kidini kuwa mikutano ya kampeni za kisiasa.

Bila aibu wanasiasa wanapopokea vipaza sauti, husahau kuwa wako mahali patakatifu. Hugeuza fursa ya kuzungumza kuwa nashambulizi dhidi ya wapinzani wao.

Askofu Ole Sapit aliwaambia wazi wanasiasa kote nchini kwamba wasitarajie kupatiwa nafasi ya kuzungumza wakihudhuria ibada katika makanisa ya ACK.

Kwamba kila mmoja anakaribishwa kanisani, lakini altari ni ya viongozi wa kidini pekee.Msimamo huu wa Askofu Ole Sapit kwamba kanisa la Kianglikana (ACK) hakitawapa nafasi wanasiasa kuzungumza, ni mzuri. Unafaa kuungwa mkono na Wakenya wote.

Viongozi misikitini wamekuwa na msimamo huu tangu zamani. Hata uwe nani, unaswali kwenye mikeka kama watu wengine. Swala ikiisha, unaondoka na kuendelea na shughuli zako.Lakini wanasiasa wamekuwa wakiotea majukwaa ya makanisa kuongea.

Wangekuwa wanazungumza mambo ya kuwajenga raia kiuchumi na kimaendeleo, hakungekuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi.

Wengi wakipewa nafasi ya kuzungumza, huonyesha wazi kuwa hawana sera. Badala ya kueleza ni vipi wanapanga kubadili maisha ya vijana, akina mama, wazee na watu wengine, huanza kushambulia wenzao na kuvuruga heshima ya madhabau. Tabia hii si katika makanisa pekee.

Wanasiasa wamekuwa wakiotea matanga. Badala ya kuwafariji waliofiwa, hugeuza matanga hayo kuwa majukwaa ya matusi na fitina. Kwa hivyo Wakenya wengine yafaa waige hatua zilizochukuliwa na ACK.

Askofu amtaka Uhuru apige marufuku kampeni za 2022

Na SHABAN MAKOKHA

ASKOFU Jackson Ole Sapit wa Kanisa la Kianglikana Kenya (ACK), anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku kampeni zote za uchaguzi wa 2022 na badala yake kuwaagiza viongozi wote kuwahudumia Wakenya.

Bw Sapit alisema kuwa viongozi wa Serikali na Upinzani wanapaswa kuwadhibiti wanachama wao ambao wanaendelea kujihusisha kwenye kampeni za mapema.

Alieleza viongozi hao wanapaswa kuelekeza juhudi zao kwenye mikakati itakayoboresha maisha ya Wakenya, kama uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aliwarai viongozi kutambua haja ya kuielekeza nchi kwenye njia inayofaa, badala ya sasa, ambapo majibizano makali baina ya wanasiasa yanatishia umoja na uthabiti uliopo.

Akihutubu jana katika Kanisa la St Luke’s ACK Cathedral, Butere, Kaunti ya Kakamega, Bw Sapit alisema kuwa majibizano hayo ni hatari kwa nchi.

“Tunawaomba viongozi kwenye Serikali na katika Upinzani kuwa waangalifu wanapozungumza katika mikutano ya umma, hasa wanapowahutubia wafuasi wao. Inasikitisha kuwa baadhi ya semi wanazotoa zinaweza kuwachochea Wakenya ama kuzua rabsha zisizofaa,” akasema.

Alieleza kuna haja viongozi wote nchini kufanya kikao cha pamoja kudhibiti hali hiyo, hadi pale Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakapowaruhusu kufanya kampeni.Alieleza sikitiko lake kuwa wanasiasa nchini huendesha mikutano yao kama kila siku ni wakati wa kampeni. Alilalamika wengi huwa hawatilii maanani masuala muhimu ambayo yanamfaidi mwananchi.

“Wakati wa kampeni haujafika kwani imebaki miaka miwili. Viongozi wanapaswa kusimamisha siasa kwa sasa na kuangazia maendeleo. Si vyema wananchi kushuhudia siasa za majibizano kila wakati bila kutoa nafasi kwa utekelezaji wa masuala muhimu yanayowafaa,” akasema.

Alieleza kuwa mwelekeo wa siasa nchini kwa sasa umekitwa kwa lengo la kuwagawanya Wakenya kwenye misingi ya kitabaka.Hivyo, aliwaomba viongozi kukoma kuelekezeana matusi na badala yake kuanzisha miradi itakayowafaidi wananchi kwa muda mrefu.

Bw Sapit alieleza hofu yake kwamba vijana wengi nchini hawana ajira, ila viongozi wanaangazia siasa za 2022, badala ya kusuluhisha tatizo hilo.

“Vijana wanapaswa kupewa ajira, kwani nafasi za kufanya biashara ni chache. Janga la virusi vya corona limetuathiri vibaya, hasa uchumi wa nchi. Haya ndiyo masuala tunayopaswa kuangazia,” akasema.

Alisema mikakati ya kukabiliana na janga hilo na kubuni nafasi kwa vijana ndiyo inapaswa kupewa kipaumbele.Bw Sapit, ambaye ametangaza kuunga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI), alisema kuwa tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mazingira ya siasa yalibadilika nchini huku miradi muhimu ikipuuziliwa mbali.

Alisema ripoti ya BBI inawapa Wakenya matumaini mapya kwani inataja masuala ambayo lazima yashughulikiwe kwa dharura ili kuleta utangamano zaidi nchini.

Ole Sapit aitaka serikali isambaze PPE kwa hospitali zinazosimamiwa na makanisa

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Kanisa la Anglikana Nchini (ACK) Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ametoa wito kwa serikali kusambaza vifaa vya kujikinga (PPE) katika hospitali zinazosimamiwa na makanisa wakati huu wa janga la Covid-19.

Alisema hatua kama hiyo itahakikisha wahudumu wa afya katika hospitali hizo pia wanakingwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona wanapowahudumia wagonjwa.

“Vifaa vya kujikinga vinavyotolewa kwa serikali na wahisani au kununuliwa kwa fedha zinazokusanywa visambazwe kote nchini katika hospitali za umma na zinazosimamiwa na makanisa,” Ole Sapit akasema wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi.

Ibada hiyo ilipeperushwa kupitia runinga na mitandao kwani serikali imepiga marufuku ibada za kawaida kama sehemu ya mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Askofu Ole Sapit pia aliitaka serikali kusambaza pesa zinazotolewa na wahisani kama msaada wa kufadhili vita dhidi ya janga hilo kwa hospitali hizo ambazo zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa pesa wakati huu ambapo watu wengi hawaendi huko kwa matibabu.

“Unyanyapaa unaohusishwa na ugonjwa wa Covid-19 umechangia watu wengi kuogopa kwenda hospitalini. Hali hii imesababisha hospitali za makanisa kukosa fedha za kuwalipa wahudumu wao,” akasema.

Askofu Ole Sapit aliitaka serikali kuondoa ushuru unaotozwa vifaa vya PPE ili bei yavyo ishuke wakati huu ambapo vinahitajika kwa wingi.