• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
Jaguar abambwa nje ya majengo ya bunge

Jaguar abambwa nje ya majengo ya bunge

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Sterehe Charles Njagua Jumatano adhuhuri alikamatwa nje ya majengo ya bunge, Nairobi kwa madai ya kutisha kuwafurusha raia wa kigeni wanaoendesha biashara nchini Kenya.

Zaidi ya maafisa 20 wa upelelezi ambao walikuwa wamepiga kambi nje ya bunge tangu asubuhi walimkamata mbunge huyo mara tu alipotoka nje kwenda kuandikisha taarifa kwenye kituo cha polisi cha Bunge.

Hii ni baada ya Bw Njagua kupata habari kwamba alikuwa akisakwa kutokana na vitisho alivyotoa Jumatatu akihutubia wafanyabiashara katika eneo la kibiashara la Kamukunji.

Kukamatwa kwa mbunge huyo kunajiri saa kadha baada ya serikali ya Tanzania kulalamika kwamba raia wake wanaofanya biashara katika soko kuu la Gikomba pia walilengwa katika vitisho hivyo.

Soko hilo maarufu kwa biashara za nguo zilizotumika, mitumba, linapatikana katike eneo bunge hilo.

Katika video iliyosambazwa mitandaoni Jumatatu Bw Njagua, almaarufu Jaguar, anaoenekana akisema: “Juzi Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitangaza kuwa amewafuruha wafanyabiashara sita wa China. Ningependa kumwambia kwamba wale tunaowalenga sio hao pekee, bali mamia ya wageni ambao wamekufurika nchini, hasa hapa Nairobi”.

“Naipatia serikali saa 24 kuwafurusha, la sivyo tutavamia biashara zao na kuwaondoa kwa nguvu, na kuwapeleka uwanja wa ndege. Kazi ya Matiang’I na Idara ya Uhamiaji itasalia ni kuwaweka kwenye ndege na kuwarejesha makwao,” akafoka Bw Njagua ambaye alionekana mwenye hasira.

Bw Njagua alikuwa ameandamana na Mbunge wa Langata Nixon Korir na Tindi Mwale wa Butere.

Hata hivyo, msemaji wa serikali Cyrus Oguna alipuuzilia mbali vitisho hivyo kwa kusema kuwa haviwakilishi msimamo wa serikali.

“Wakenya ni watu wapenda amani ambao kwa miaka mingi wameishi kwa utulivu na watu kutoka mataifa ya kigeni. Huu ni moyo ambao tutaendeleza nyakati zote,” akasema kwenye taarifa aliyoitoa Jumanne.

“Kwa hivyo, serikali ingependa kuwahakikisha wageni wote kwamba wako salama kuendesha shughuli zao halali nchini na matamshi ya mbunge huyo ni yake kama mtu binafsi na hayawakilisha msimamo rasmi wa taifa hili,” Bw Oguna akaongeza.

You can share this post!

Bunge la Kenya limejaa watoto, asema Munya kuhusu madai ya...

Kuria ashangaa kwa nini Matiang’i hajakamatwa kwa...

adminleo