Kioja abiria jini akipotelea hewani!

Na Charles Ongadi

MAGANYAKULO, KWALE

BODABODA wa hapa alilazimika kuacha pikipiki yake kwenye steji na kutimka mbio za mguu niponye baada ya abiria wa kike aliyembeba kutoweka ghafla.

Kulingana na bodaboda mwenzake aliyekuwa akimfuata hatua chache nyuma, alimuona mwenzake akimbeba abiria wa kike.

Wote walikuwa wameanza safari pamoja kuwafikisha abiria wao walikokuwa wakienda. Alisema hata yeye alijipata amechanganyikiwa muda mchache baadaye alipomwona mwenzake akiendesha pikipiki bila abiria ilhali hakuwa amesimama kumshusha.

“Kweli kapanda yule abiria wa kike lakini alivyotoweka ghafla akiwa kabebwa na mwenzangu ingali kitendawili kwangu,” alisimulia jamaa huyo huku akionekana kuchanganyikiwa.

Jamaa alipogundua abiria wake alikuwa ametoweka, alisimamisha pikipiki na akatimua mbio kama aliyepandwa na mzuka.

Lakini hatua ya haraka iliyochukuliwa na wasamaria wema na bodaboda wa eneo hili ilifanikiwa kumzuia bodaboda huyo kuendelea kutimka mbio.

Bodaboda huyu aliishia kupoteza fahamu kwa muda ila alirudia hali yake ya kawaida na kusimulia wenzake yaliyomsibu.

“Ama kwa kweli nilimkuta binti yule mrembo katika steji akichat na akaniomba nimfikishe beach lakini muda mfupi baada ya kuanza safari yetu nilipomwangalia na side mirrow sikumwona na ndipo nikajipata nimechanganyikiwa,” alisimulia bodaboda huyo huku akiwaomba wenzake kumsindikiza hadi kwao.

Alipofika mbele ya wazazi wake, bodaboda huyo aliapa kutofanya tena kazi ya bodaboda huku akiwaomba wazazi wake kumtafutia kazi nyingine ya kufanya.

Siku mbili baadaye, alionekana akielekea shule ya karibu ya kiufundi na ikasemekana aliamua kujifunza kazi ya useremala.

 

Matapeli ‘mapepo’ wanavyohangaisha wakazi Limuru

NA MARY WANGARI

Huku gharama ya maisha ikizidi kupanda na changamoto za kupata riziki zikigeuka kitendawili kigumu, baadhi ya Wakenya wako radhi kufanya chochote kile ilmradi tu wajikimu kimaisha.

Wahalifu pia hawajaachwa nyuma katika msafara huu huku wakibuni mbinu anuai za kutekeleza uhalifu wao kuanzia matumizi ya dijitali na mbinu nyinginezo ambazo zinafanana tu na ngano za mizimwi.

Utapeli si jambo geni. Lakini utapeli huo unapofanywa kwa kutumia hirizi, mapepo au njia za kishetani, basi hapo linakuwa suala la kuhofisha mno.

Huu ndio uhalisia ambao wakazi mjini Limuru, Kaunti ya Kiambu, wanakumbana nao.

Ninapokutana na Kagendo, 24, taswira ya kwanza inayonijia kumhusu ni kwamba ni msichana mpole, mwenye heshima na mnyamavu.

Bila shaka, angali ametishika kutokana na tukio lililomsibu majuzi, jambo linalojidhihirisha wazi kutokana na jinsi machozi yanavyomlengalenga, mara tu anapoanza kunisumulia masaibu yaliyompata.

Anakumbuka kana kwamba ni jana tu Jumamosi hiyo alipotumwa na mwajiri wake kununua bidhaa za chakula sokoni.

Haikuwa mara ya kwanza kutumwa sokoni, hivyo basi Kagendo anayefanya kazi kama mjakazi Limuru, hakuwa na wasiwasi wowote maadamu alijua alichohitajika kufanya.

Mwajiri wake alimkabidhi Sh3000 pamoja na orodha ya vitu viliyohitajika na hapo akafululiza moja kwa moja hadi sokoni, akiwa na nia moja tu. Kununua bidhaa na kurejea nyumbani na kuendelea na majukumu mengine.

Hata hivyo, hakuwa tayari kwa tukio lililomsubiri ambalo bila shaka atalikumbuka kwa muda mrefu.

Zilisalia tu siku chache kabla ya Sikukuu ya Krismasi hivyo soko lilifurika watu katika pilkapilka za kununua vyakula na mavazi katika maandalizi ya sherehe.

Katika pitapita zake akielekea sokoni kabla ya kuanza kununua bidhaa, wanawake wawili waliojifunga kanga walimjia.

Walimsalimia Kagendo kwa upole huku wakimwomba awaelekeze katika jumba fulani mjini humo, lakini akawafahamisha hakufahamu eneo hilo vyema.

“Walinisalimia kwa mkono kisha wakaniomba niwaelekeze kwa jumba linaloitwa Metropolitan Sacco. Niliwaeleza kwamba pia mimi nilikuwa mgeni hivyo sikufahamu sehemu nyingi mjini humo,” anaeleza.

Baada ya kila mmoja kushika hamsini zake, binti huyo ghafla, kama aliyepagawa, alikumbuka kuna hela alizokuwa ameacha nyumbani na akashikwa na hamu isiyo ya kawaida kwenda kuzichukua, hata pasipo kujua ni kwa nini hasa alizihitaji.

“Nilimwita mwendeshaji pikipiki aliyekuwa karibu na nikarejea nyumbani kwa haraka. Nilipofika nilichukua pesa zangu zote nilizokuwa nimeweka kama akiba kwa takriban mwaka mmoja nilipokuwa nikifanya kazi zilikuwa karibu Sh30,000.

“Nilidhamiria kuwatumia wazazi wangu na kuwanunulia ndugu zangu zawadi nitakaporejea nyumbani,” anasimulia huku akisita kwa muda kufuta machozi huku akishindwa kujizuia.

Kisha aliabiri pikipiki iliyomleta maadamu mwendeshaji bodaboda huyo alimsubiri kwenye lango na kurejea sokoni akidhamiria kukamilisha shughuli iliyomsubiri.

Aliwasili sokoni tena na kwa njia ya kimiujiza ambayo Kagendo hajawahi kuelewa hadi hii leo, walikutana kwa mara nyingine na wanawake hao wawili.

“Kutoka hapo sikumbuki kilichotokea. Ninachokumbuka tu ni kwamba waliniitisha hela na nikawapa zote nilizokuwa nazo ikiwemo nilizotumwa kununulia bidhaa.

“Kisha waliniitisha simu na nikawapa hata bila kuwauliza chochote. Mwishowe nilijipata tu nikiwa nimeketi chini ya daraja nikiangalia tu hewani. Nilipotanabahi nilikuta wapita njia kadha wamenizingira,” alieleza.

Kulingana na Kagendo, juhudi za wasamaria wema kumsaidia ziliambulia patupu maadamu alikuwa hajijui hajitambui, hakuwa na simu na ilichukua muda kabla ya fahamu zake kumrudia.

“Nilianza kulia nikishangaa ni vipi nilivyoishia hapo. Nilimwomba mtu mmoja simu nimpigie mwajiri wangu aliyekuwa kazini na kumfahamisha kuhusu mashaka yaliyonipata. Kwa bahati nzuri alikuja na akanipeleka nyumbani,” alieleza Kagendo.

Kisa cha Kagendo ni mojawapo wa misururu ya visa vya utapeli usio wa kawaida, na ambao umewahangaisha wakazi wa Limuru.

Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba kwa sasa baadhi ya wakazi wanahofia kuwasalimu au kuwasaidia watu wasiowafahamu.

Siku chache tu baada ya Kagendo kutapeliwa Joel mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu mojawapo nchini kutoka eneo la Tigoni, Limuru, alitapeliwa kiasi cha Sh8,000 alizodhamiria kulipa nazo karo.

Sawa na Kagendo, Joel alikuwa akielekea chuoni anamosoma alipokutana na mwanamke mmoja aliyemsalimia kwa unyenyekevu na kumwomba amwelekeze katika duka mojawapo eneo hilo.

Kama mwenyeji eneo hilo na bila kushuku chochote, Joel alijitolea kumsaidia mwanamke huyo na kisha aende zake.

“Mambo yalitendeka haraka sana hadi sasa mimi huona kama ni ndoto. Baada ya kunisalimia na tukaandamana pamoja, nakumbuka tu akiniitisha pesa nami nikampa zote nilizokuwa nazo bila pingamizi lolote,”anasimulia huku akicheka kwa kutoamini.

Kwa Maryam ambaye ni mkazi wa Limuru vilevile, nyota ya jaha ilikuwa upande wake maadamu alinusurika kwa tundu ya sindano kutapeliwa kiasi cha zaidi ya Sh40,000 alipokutana na washukiwa hao.

“Ilikuwa siku ya Jumapili ambapo niliamua kupitia sokoni baada ya kuhudhuria ibada kanisani. Mshahara ulikuwa umeingia hivyo nilienda kwanza kwenye mtambo wa hela kisha nikaelekea sokoni,” anaeleza.

Mama huyo wa watoto watatu hakuwa na habari kuhusu hatari iliyokuwa ikimkondolea macho.

“Nilipokuwa nikielekea kwenye kibanda mojawapo kununua mboga, nyanya na vitunguu, wanawake wawili walinijia ghafla. Sikuwa nimewaona mbele yangu, ni kama walichipuka tu. Kwanza nilimwona mmoja aliyenisalimia na kuniomba niwaelekeze mahali ambapo wanaweza kupata viatu aina ya ‘boots’,”

“Baadaye nilimwona mwenzake kando yake. Sijui ni vipi lakini niligutuka na nikakumbuka ghafla nilikuwa nimebeba kiasi kikubwa cha hela. Pia nilijisaili kimoyomoyo, iweje katika soko lote ni mimi tu walikuwa wameona wa kuuliza. Iweje walitoka mwendo wote huo na kunijia mimi huku kukiwa kumejaa wateja na wauzaji kwenye vibanda sokoni?

“Niliwaeleza sijui na kuwaondokea haraka. Ni kama hata hao waligundua kuna jambo lilikuwa limetendeka. Waliondoka na kutoweka ghafla sawa tu na walivyoibuka,” anasimulia Maryam huku akimshukuru Maulana kwa kumnusuru siku hiyo.

Hata hivyo kuna baadhi ya wakazi wanaoamini kwamba matapeli hao si wa kawaida na kwamba wanatumia nguvu za kishetani kuwalenga na kuwapumbaza wahasiriwa wao na kisha kuwaibia mchana peupe.

“Ni kama wanatumia nguvu za mapepo kuwaongoza kwa wahasiriwa wao. Mara tu unapowagusa ama kuzungumza nao unajisahau na kufanya chochote wanachokuagiza kufanya,” anaeleza Mama Ian ambaye ni muuzaji katika soko la Limuru.

Siku za wahalifu hao hata hivyo zimehesabiwa huku wakazi wenye ghadhabu wakililia damu yao na kuapa kumpa kichapo cha mbwa yeyote atakayepatikana na bahati mbaya ya kukamatwa.

“Lakini kwa sababu kuna siku tutawakamata, hiyo ndiyo siku watajutia kwa dhati vitendo vyao. Tunaomba na tunajua Mungu halali kuna siku watafumaniwa hadharani,” anaeleza mfanyabiashara mmoja huku akiwa amejawa na machungu.

Visa vya matapeli si vipya mjini Limuru huku wahalifu hao wakitumia mbinu za kila aina ikiwemo watoto huku baadhi ya visa vikiweza hata kuwafanya watengenezaji tajika wa filamu duniani kuwaonea gere kwa ustadi wao.

Mnamo Julai 2019, wasichana wawili mmoja aliyejifanya kuugua kifafa na mwingine akisingizia kuwa dadake walikuwa wakiwalenga waendeshaji magari kwenye barabara kati ya Limuru hadi Nairobi.

“Mmoja wao alikuwa akijifanya amezirai na kulala barabarani ili kuvutia wasamaria wema. Karibu wanitapeli eti niwape hela za matibabu kabla ya dereva aliyekuwa amewaona hapo awali wakiwatapeli watu kwenye barabara ya Kiambu aliponitahadharisha kuondoa upesi kabla sijanaswa mtegoni,” anasimulia Nicholas Kareu.

“Wanawake hao huchanganya mtu. Unajipata wametumia kifaa cha kusaidia kupumua (inhaler) unajisahau unawapatia kila kitu,” anaonya Magecha.

Ikiwa hilo halijakushtusha basi hujasikia kisa mojawapo 2018 ambapo mwanamme mmoja aliyekuwa akijifanya kuwa kasisi kutoka Benedictine Monastery, alikuwa akiwatapeli wafanyabiashara Limuru.

Kasisi huyo feki kwa jina Kasisi Edward alikuwa vilevile akisingizia kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Katoliki ili kuwarushia chambo wahasiriwa wake ambapo alimtapeli muuzaji dawa mmoja kiasi cha Sh500,000.

Mwaka uo huo kuliripotiwa visa vya wasichana matapeli waliokuwa wakisingizia kusaka kazi za ujakazi na kisha kufagia vitu vya nyumbani na kutoweka baada ya siku chahe.

Ni hali hii ya kuongezeka kwa matapeli mjini Limuru ambayo imefanya baadhi ya watu kushangaa nini hasa kiini chake.

Jinsi wanavyotania baadhi ya watu, huenda ni hali ya anga yenye baridi shadidi, ukungu na barafu ambayo eneo hilo linalosifika kwake, ndiyo inayochangia pakubwa kwa kuwapa maficho mwafaka wahalifu hao.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

FUNGUKA: ‘Napashwa joto na jini’

Na PAULINE ONGAJI

KWA muda sasa, kumeibuka kejeli nyingi mtandaoni kuonyesha jinsi mtoto mvulana – boy child – amekuwa akihangaika mikononi mwa mabinti hasa katika masuala ya mapenzi.

Ni suala ambalo limewafanya wanaume wengi kuonyesha wazi chuki dhidi ya mabinti huku baadhi yao wakisisitiza hawana haja ya kuwachumbia.

Ousman, 33, alikata kauli hiyo akiwa na miaka 19 pekee, wakati huo akiwa katika shule ya upili.

Hata hivyo uamuzi wa jamaa huyu mkazi wa eneo la Pwani ya Kenya haukutokana na machungu kutokana na binti, bali aliamua kufanya hivyo baada ya kuonja utamu wa jini wa kike, kama anavyosimulia.

“Maishani mwangu sijawahi kuwa katika uhusiano wala kufurahia mahaba na binti mwanadamu. Huyu jini wangu tulikutana naye miaka 14 iliyopita baada ya kutambulishwa na mwenzangu ambaye kwao walikuwa wamefuga viumbe hawa.

Yeye ni mrembo ajabu ambapo tangu nimjue hajawahi kuzeeka. Umbo lake ni lile lile; tumbo bapa, kifua thabiti na kiuno cha mviringo. Uke wake ni thabiti kabisa, licha ya kuwa tumekuwa tukirushana roho kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Nilimuonja kwa mara ya kwanza nikiwa na umri wa miaka 19 nikiwa ningali kushiriki tendo lenyewe la kuonana kimwili na yeyote na hapo nikaamua kwamba ni yeye tu sitaki mwingine.

Jini wangu huja usiku wa manane akiwa uchi wa mnyama ambapo akiingia kwenye fleti ninamoishi, hakuna jirani anayemuona wala kumsikia.

Akifika, sisi hutekenyana kwa saa nzima na kuzungumza kwa muda wa saa kadha kabla yeye kurejea majini.

Uhondo anajua kunipa na ninachofurahia ni kwamba yeye ni mungwana kiasi kwamba tukishamaliza, husafisha kila mahali na kuhakikisha kwamba anaacha kila kitu alivyokipata.

Mbali na hayo, licha ya kwamba hakuna kinga tunayotumia, sina wasiwasi wa kuambukizwa maradhi ya zinaa, wala hatari ya mimba isiyotarajiwa.

Sisi hushiriki mahaba mara tatu kwa wiki; Jumanne, Ijumaa na Jumapili, na nyakati zote huwa saa tisa za usiku.

Aidha, sina ajira wala mbinu yoyote ya kujitafutia riziki, lakini naishi maisha kama mfalme, nina nyumba na magari kadha ya kifahari anayoninunulia.

Sihitaji kufanya kazi kwani hunipa pesa pia. Nabadilisha simu kila mara bila wasiwasi. Kila ninapochoshwa na niliyonayo, mimi humrejeshea kisha ananiletea mpya.

Nina fanicha na vyombo vya kisasa ndani ya nyumba yangu na mali nyingi kutoka kwake na asema hufanya hivi kunizuia kuingia kwenye mtego wa mwanamke yeyote binadamu.

Pia, amenionya kwamba nikiwahi kuonja vya binadamu nitayaona matokeo ambayo hajawahi nifichulia. Lakini mwenyewe sifikirii kutafuna vya binadamu kwa sababu uhondo anaonipa umenilewesha”.

Je, ushirikina husababisha ajali za barabarani?

Na MWANGI MUIRURI

AJALI za mauti barabarani zimekuwa kero kubwa kwa familia nyingi hapa nchini ambapo nyingi hutazama makaburi ya wapendwa wao kwa macho ya huruma huku wakiwaza mbona usafiri ukawaletea majonzi.

Wengine wengi wamebakia tu kuangalia majeraha yao kwa huzuni wakijaribu kusahau masaibu yao barabarani ambako ajali iliwatunuku vilema.

Huku serikali ikihimizwa iwe na uwajibikaji wa kuwafurusha madereva na makanga watukutu barabarani ambao kwa mienendo yao isiyofaa huhatarisha maisha ya abiria na watembeao kwa miguu, baadhi ya madereva sasa wanadai ushirikina unachangia janga hili.

Wengine wanadai kuwa baadhi ya barabara za hapa nchini zimevamiwa na majini ambayo husababisha ajali hizo.

Kwa mfano, baadhi ya madereva wa magari na pia wa bodaboda ambao wamenusurika katika ajali eneo la kati wanadai kuwa katika sehemu tofauti za barabara za eneo hilo kwa mfano, huwa na nyanya wazee ambao hujitokeza ghafla barabarani wakiwa uchi na kusababisha ajali hizo.

Madai haya yalitolewa na walionusurika katika ajali iliyowaua watu wanne na kuwajeruhi vibaya wengine watatu katika eneo la Kambiti katika Kaunti ya Murang’a Kusini hivi majuzi.

Nyanya mzee akiwa uchi

Joseph Karanja ambaye alinusurika ajali hiyo iliyohusisha trela na gari la abiria aina ya Nissan aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa alimsikia dereva akipiga duru kuwa ameona nyanya mzee akiwa uchi akijitosa mbele ya gari lake.

“Alipiga duru akikemea nyanya huyo aondoke haraka ama akanyangwe lakini tukajipata tumeangukiwa na lori hilo,” akasema.

Makanisa yanaombwa yapange ibada za maeneo yanaodaiwa kusakamwa na majini hayo ili kuyatakasa ili watu wanusurike ghadhabu ya mapepo hatari ya kuwasajili walio hai kwa maisha ya kuzimu.

Aidha, wahudumu wa bodaboda katika mji wa Sabasaba waliambia Taifa Leo kuwa ni ukweli kuna nyanya mzee ambaye amekuwa akijitokeza mbele yao katika eneo la Gakarati na ambapo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, watu sita wamepoteza uhai wao katika ajali eneo hilo.

Lakini Kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anapuuzilia mbali madai hayo akisema ni ya kuudhi na pia ya kutafuta vijisababu kwa madereva watukutu kuendelea kuua watu kwa uendeshaji mbaya wa magari.

“Madereva wengi hasa wa pikipiki katika eneo hilo hujitokeza kwa barabara bila ya kuzingatia usalama wowote na ndipo huwa wakitoka kwa barabara za kuwaunganisha na barabara kuu huwa wanakumbana na magari na kuwaua papohapo,” akasema.

“Madereva waache visingizio vya kusema wanaona mazingaombwe barabarani. Ndio kuna Shida za barabara mbovu, madereva kukaidi sheria za barabara na raia nao kuwa na utovu wa kinidhamu katika shughuli zao barabarani, lakini tusiwe wa kukwepa uhalisia wa mambo kuwa ajali nyingi zinatokana na maamuzi mabovu ya madereva, ulevi na umang’aa,” akasema.

Alisema tayari ameagiza misako itekelezwe dhidi ya wahudumu wa bodaboda ambao hawajatimiza masharti ya sheria za barabarani.

Majini barabarani

“Ikiwa kuna majini barabarani, hawa madereva wa matatu na bodaboda ni wao. Hawawezi kusingizia roho za kuzimu na wao ndio wanaua watu kwa kutozingatia sheria za barabarani,” akasema.

Maeneo yanayotajwa kukubwa na majini hayo ni Kiganjo-Naromoru, Kibirigwi-Sagana, Limuru-Uplands, Blue Post-daraja ya Sagana, na Nyeri-Nyahururu. Maeneo mengine Kiriaini-Murang’a, Makongeni Kuelekea Garissa kutoka Thika, Makutano-Embu na pia Kiambu-Muthaiga.

Kulingana na ripoti za Trafiki katika eneo la Kati, maeneo hayo yamekuwa kichinjio kwa watu 980 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita huku wengine 510 wakipata majeraha mabaya na mamia ya wengine kunusurika mauti na majeraha mabaya.

Aidha, aina mbalimbali za mifugo 136 wamekufa katika barabara hizo kwa kipindi hicho wakiwemo ng’ombe sita.

Lakini mbona hatari ya ushirikina ionekane kuaminiwa hivyo na wenyeji hao?

Ushirikina unaogopwa sana katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini na mara kwa mara visa vya raia wakiwafurusha washukiwa wa ushirikina zimeripotiwa.

Katika maeneo ya Kisii na Pwani, washukiwa huwa wanachomwa hadharani na kundi

lla vijana.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, kundi lingine limechipuka ambalo limeapa kutekeleza sheria kali za Sharia dhidi ya wachawi.

Kuua washirikina

Kundi hilo kwa jina Wakombozi wa Mwea limeapa kuwasaka washukiwa wa ushirikina na kuwaua hadharani kwa kuwapiga mawe huku maafisa wa polisi wakililinganisha na makundi ya kigaidi na kutangaza hali ya kutotoka nje katika maeneo yanayolengwa na kundi hili.

Wiki iliyopita, kundi hili lilimuua mzee wa miaka 52 kwa jina Githaka Kirombo kutoka kijiji cha Kirogo kwa madai kuwa amewaroga watu wanne katika kijiji hicho.

Shirika la Afya duniani (WHO) limeonya kuwa barabara za Kenya ni miongoni mwa hatari zaidi kwa uchukuzi.

Aidha, Shirika lingine la Uingereza Transport Research Laboratory (TRRL) linadai kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi tano mbaya duniani katika visa vya ajali za barabarani.

Katika ripoti yake ya kila mwaka, Shirika hili linadai kuwa kwa mwaka Wakenya 3, 000 huaga dunia kutokana na ajali hizo.

Ripoti hiyo inasema jumla ya watu 1.17 million huaga dunia kila mwaka ulimwenguni huku asilimia 70 ikiwa ni kutoka nchi zinazoendelea. Hapa Kenya, WHO inaonya kuwa, kati ya magari 100,000 ni lazima 510 yahusike katika ajali mbaya na ambazo huzua mauti.

“Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Kenya ina hatari kubwa ikilinganishwa na Afrika Kusini ambayo kati ya magari 100, 000 ni magari 260 ambayo huhusika katika ajali mbaya. Nchini Uingereza, ni magari 20 pekee kati ya 100, 000 ambayo huua watu,” ripoti hiyo yasema.

Asilimia 65 ya vifo hizo hapa Kenya zinadaiwa kuwahusisha watembeao miguu asilimia 35 ikiwa ni vifo kwa walio chini ya miaka 18.

Nyoka wavamia pasta akitimua mapepo

NA MWANDISHI WETU

Kasikeu, Makueni

Hali ya taharuki ilitanda eneo hili pasta mmoja msifika aliposhambuliwa na nyoka wawili alipokuwa akijaribu kufukuza mapepo katika boma la jirani ya muumini wa kanisa lake.

Ripoti za mtaa zinaarifu kuwa, pasta huyo alitimua mbio za kufa kupona huku akipiga kamsa, nao nyoka hao wakapotea kimiujiza, tena kwa njia ya ajabu sana!

Kulingana na mdokezi wetu, mwenye boma hilo alimwendea jirani yake aliyekuwa ameokoka na kumsihi amsaidie kwa vyovyote vile kuyatoa mapepo yaliyokuwa yakisumbua familia yake kila siku.

Aliahidi kumletea Mtumishi wa Mungu aliyekuwa gwiji wa kuyakomoa mapepo ya kila sampuli.

Inasemekana kwamba, muumini huyo alimuarifu pasta masaibu na madhila ya jirani yake na siku ya kufukuza mapepo ikapangwa. Mwenye boma alitakiwa atafute sadaka nono .

Siku ilipowadia, pasta alifika katika boma hilo huku akiwa ameezeka Biblia kwapani na akaitisha sadaka kwanza ili aanze ‘kazi’ yake bila wasiwasi wowote.

Alikabidhiwa Sh5000 na akaanza kuomba kwa ndimi huku akizunguka boma hilo.

Tunaarifiwa kwamba, wakati pasta alipokuwa nyuma ya nyumba ya mwenyeji wake, nyoka wawili walichomoka kama swara kutoka kusikojulikana na kumshambulia.

Hata hivyo, alinusurika kiajabu na akachana mbuga huku akipiga nduru kwa hofu.

Hata hivyo, nyoka hao walitoweka kimiujiza na kuwaacha wengi vinywa wazi huku mwenye boma akijifungia ndani ya nyummba akiogopa kushambuliwa na umati huo uliokuwa umejaa mori.

”Hiki ni kisa cha ajabu mno eneo hili,” mkazi mmoja alisikika akisema.

 

Madereva wasimulia kukutana na jini jike

Na VICTORIA NDUVA

Kyumbi, Machakos

Madereva wanaotumia barabara kuu ya Nairobi kwenda Mombasa wanataka viongozi wa kanisa kuwaokoa kutokana na jinamizi la mazingaombwe wanayodai yanahatarisha maisha ya wengi eneo hili.

Kulingana na mdokezi ambaye ni dereva wa lori, wanapofika eneo hili usiku wa manane huwa wanashuhudia kioja cha mwanamke mrembo anayesimamisha gari.

Alidai kwamba mwanamke huyo huwa mrembo wa ajabu kiasi kwamba madereva hulazimika kusimamisha magari yao kumsikiliza.

Kulingana na mdokezi, dereva akikataa kusimamisha gari huwa anakumbana na mkosi mkubwa na hafanikishi shughuli zake za siku hiyo.

Inasemekana kuwa wakati mwingine, mwanamke huyo hubadilika kuwa chatu mkubwa ambaye huvuka barabara kwa mwendo wa kinyonga jambo ambalo huwafanya madereva kusimamisha magari barabarani ili kumpisha.

“Unamuona mwanamke upande mmoja wa barabara akisimamisha gari, ghafla bin vuu, anageuka chatu na kuanza kuvuka barabara na unasimamisha gari kwa mwendo wa hata saa moja,” alisema mdokezi.

Dereva mmoja alisimulia kwa machozi masaibu yake aliposimamishwa na mwanadada huyo akidhani alikuwa safarini.

Alisema baada ya dakika kumi, malkia alichukua usukani wa kuliendesha gari lile bila idhini yake.

“Sikujua kilichofanyika. Nilijipata kando huku mwanadada akidhibiti gari bila kuchoka,” alieleza. Alieleza kuwa mwanamke huyo huwaonya dhidi ya kusimulia masaibu anayowasababishia.

Kwa sasa madereva hao wanataka maombi maalum kufanywa na ikibidi wazee wafanye tambiko ili kutakasa eneo hili.

Baadhi yao wamelazimika kutumia njia mbadala ili kufanikisha shughuli zao za usafiri iwapo watalazimika kusafiri usiku. Kwa sasa hawajui kile ambacho kitawapata kwani tayari wametoboa siri ile. Wanahofia kuwa labda ghadhabu ya jini jike huyo zitakuwa juu yao.