Agizo wanafunzi waliokosa kujiunga na sekondari wasakwe

MAUREEN ONGALA na STANLEY NGOTHO

MAELFU ya wanafunzi hawajajiunga na Kidato cha Kwanza katika kaunti mbalimbali nchini, wiki nne tangu wenzao kuripoti.

Katika Kaunti ya Kilifi, Kamishna wa Ukanda wa Pwani, John Elung’ata, alisema kuwa wanafunzi 12,000 hawajajiunga na Kidato cha Kwanza.

Bw Elung’ata alitoa amri kwa machifu na naibu wao kaunti hiyo kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amejiunga na kidato cha kwanza kabla ya mwezi wa Oktoba.

Bw Elung’ata aliwaomba wasimamizi husika kuwasaka watoto wote ambao hawajaweza kujiunga na Kidato cha Kwanza kutokana na sababu mbalimbali ili wasaidiwe.

Akizungumza na wadau katika shule ya sekondari ya wasichana ya Wakala, Kaunti ndogo ya Magarini, Bw Elung’ata alisema wasimamizi wahusika wanafaa kusimama kidete kuhusiana na masuala ya masomo.

“Machifu wanafaa kuisaidia wizara ya Elimu kutimiza lengo lake la kuhakikisha kuwa kila mtahiniwa wa KCPE amejiunga na sekondari,” akasema Bw Elung’ata.

Aliwahimiza machifu kuhakikisha kuwa watoto wote wanajiunga na kidato cha kwanza bila kujali hali ya kiuchumi ya wazazi wao.Hata hivyo, kamishna wa Kaunti ya Kilifi alisema kuwa tayari machifu wameanza kutimiza jukumu lao.

“Tunaamini ifikapo wiki ijayo, idadi ya watahiniwa watakaojiunga na sekondari itapanda kutoka asilimia 64 hadi asilimia 80,” akasema Bw Olaka.

Katika Kaunti ya Kajiado, zaidi ya wanafunzi 4,000 hawajaripoti katika shule za sekondari.

Wizara ya Elimu katika Kaunti ya Kajiado ilisema kati ya watahiniwa 21,000 waliofanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) ni 17,000 pekee waliojiunga na shule za sekondari.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti hiyo Luka Kangogo, alisema huenda wazazi walikosa kupeleka watoto wao shuleni kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na hatua ya machifu kulegeza kamba.

Polisi wasaka mshukiwa wa ugaidi aliyekwepa mtego wao

SIAGO CECE na FARHIYA HUSSEIN

MAAFISA wa polisi wanamtafuta mshukiwa wa ugaidi anayeaminika alikwepa mtego wao Jumatatu, wakati walipokamata wengine wawili katika kivukio cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Duru zimefichua kuwa, kulikuwa na mpango wa kutekeleza shambulio katika maeneo tofauti Mombasa mnamo Agosti 27, 2021 kuadhimisha siku ambapo Sheikh Aboud Rogo aliuawa baada ya kuhusishwa na itikadi kali ikidaiwa zinazochochea ugaidi.

Washukiwa wawili waliokamatwa hawakufikishwa mahakamani Jumanne jinsi ilivyotarajiwa, polisi wakisema wanataka kuomba waendelee kukaa kizuizini kwa muda ambao watakuwa wanaendeleza msako kutafuta wenzao.

Mshukiwa mmoja aliyekamatwa ni raia wa Kenya na mwenzake ni wa Tanzania, wana umri kati ya miaka 30 na 35, na wote walikuwa wamerudishwa nchini baada ya kukubali kuasi kikundi cha magaidi cha al-Shabaab.

Imefichuka kuwa, msako umepangiwa kufanywa katika mitaa ya Mombasa inayoaminika kuwa maficho ya washukiwa wa ugaidi na wasaidizi wao.

Mshukiwa wa tatu anayetafutwa amesemekana alikuwa amebaki Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale, wakati wenzake wawili walipokuwa wakielekea Mombasa wakiwa na silaha kama vile bunduki na vifaa vya kutengeneza mabomu.

Salim Rashid Mohammed almaarufu kama Chotara, 28, amedaiwa aliwahi kuhusika katika kikundi cha kigaidi cha ISIS, na kupanga mashambulio mbalimbali maeneo ya Kusini mwa Pwani.

Video ambazo hatungeweza kuthibitisha uhalisia wao, zilimwonyesha akikata shingo ya mtu ambaye hakutambulika, na baadaye akamwamuru mvulana mdogo wa takriban umri wa miaka minane pia afanyie mwingine hivyo.

Afisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi aliambia Taifa Leo kwamba mshukiwa huyo amethibitishwa alirudi nchini majuzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupitia Tanzania.

Alikuwa amekamatwa katika mwaka wa 2016 lakini akaachiliwa kwa dhamana baada ya ushahidi wa kuendeleza kesi kukosekana.

Habari za kijasusi zilionyesha kuwa ni mshirika wa karibu wa mfanyabiashara Abdulhakim Salim Sagar, ambaye alikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi hivi majuzi.

Bw Sagar alidaiwa kufadhili shughuli za kigaidi, na ni shemejiye marehemu Sheikh Aboud Rogo.

Katika tukio la Jumatatu, polisi walipata bunduki mbili aina ya AK-47, vifaa vya kutengeneza mabomu, panga na aina nyingine za silaha katika gari aina ya Probox ambalo washukiwa wawili walikuwa wakisafiria.

Kando na hayo, polisi pia walipata ramani za vituo vya polisi vya Makupa na Central, na karatasi zilizokuwa na maelezo kuhusu duka kuu la Naivas Nyali na Kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC), ikiwemo kuhusu aina ya usalama ulioekwa katika sehemu hizo.

“Inavyoonekana, walitaka kutambua sehemu ambayo ni rahisi kushambulia. Walikuwa wanakuja Mombasa kushirikiana na wenzao,” duru zikaambia Taifa Leo.

Akithibitisha tukio hilo, Mshirikishi wa Eneo la Pwani, Bw John Elungata, alisema mmoja wa washukiwa hao alikuwa akiishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na akawasiliana na wenzake walio nchini kuhusu mipango ya shambulio hilo.

“Polisi sasa wanawatafuta wenzake ambao wanaaminika wako Mombasa. Uchunguzi bado unaendelea ili kubainisha habari zaidi kuhusu mipango ya shambulio,” akasema.

Usalama waimarishwa Rais Kenyatta akitarajiwa kupokea meli katika Bandari ya Lamu Alhamisi

Na KALUME KAZUNGU

USALAMA umeimarishwa Kaunti ya Lamu na Pwani kwa ujumla wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa rasmi katika Bandari ya Lamu wiki hii.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuzuru Lamu Alhamisi ili kupokea meli ya kwanza ya mizigo itakayotia nanga kwa mara ya kwanza bandarini Lamu kuashiria mwanzo wa bandari hiyo kutegemewa kwa shughuli muhimu za uchukuzi.

Akizungumza alipozuru Lamu Jumapili ili kujua ilipofikia mipango ya kumkaribisha Rais Kenyatta katika bandari hiyo iliyoko eneo la Kililana, Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, alisema serikali imehakikisha sehemu zote za Lamu zimelindwa vilivyo tayari kwa shughuli ya Alhamisi.

Bw Elungata alieleza kufurahishwa kwake na jinsi ujenzi wa Bandari ya Lamu ulivyotekelezwa.

Aliwahakikishia wakazi wa Lamu na watumiaji wa bandari hiyo usalama wa kutosha wakati itakapoanza shughuli zake rasmi mwezi huu wa Mei.

“Nimefurahishwa kabisa na maendeleo ya hapa, tuko tayari kumpokea Rais Uhuru Kenyatta katika Bandari ya Lamu Alhamisi,” akasema Bw Elungata.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bandari (KPA) nchini, Rashid Salim alisifu hatua zilizopigwa katika kuhakikisha mradi wa bandari ya Lamu unafaulu.

Bw Salim alisema kufunguliwa kwa bandari ya Lamu kutainua vilivyo uchumi na biashara Lamu na eneo zima la Kaskazini mwa Kenya.

Alisema KPA tayari imefikisha vifaa muhimu vya kupakua na kupakia mizigo kutoka kwa meli hadi kwa malori ya usafirishaji punde bandari ya Lamu itakapoanza shughuli zake.

“Bandari ya Lamu ina uwezo mkubwa wa kuboresha biashara na uchumi wa Lamu na kaskazini mwa Kenya,” akasema Bw Salim.

Mkurugenzi Msimamizi wa Bandari ya Lamu, Abdullah Samatar alisema bandari mpya ya Lamu inatarajiwa kuvutia biashara ya uchukuzi kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Ethiopia na Sudan Kusini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Reli nchini (KRC), Omudho Awitta alisema mji wa kihistoria wa Lamu unatarajiwa kupanuka zaidi kufuatia uwepo wa bandari ya Lamu.

Onyo kwa wakazi wa Pwani wanaouza miti na makaa kiholela

Na MISHI GONGO

SERIKALI imewaonya wanaoendeleza biashara haramu ya kuuza makaa na kukata miti ovyo katika eneo la Pwani.

Akizungumza na Taifa Leo mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata alisema ukataji huo umechangia pakubwa katika kubadilika kwa hali ya hewa na uhasama kati ya binadamu na wanyama.

Mkuu huyo alisema shughuli hiyo inaendelezwa zaidi katika kaunti za Lamu, Kwale, na Kilifi.

Alisema kuwa kuendeleza biashara na shughuli za ukataji miti ovyo kutalemaza ari ya Rais Uhuru Kenyatta ya kurudisha asilimia 10 ya misitu ifikapo mwaka 2022.

“Japo serikali imekuwa ikipinga ukataji holela, kuna baadhi ya watu ambao bado wanaedeleza shughuli za ukataji miti. Tutawaandama wanaopuza onyo hili na kuwachukulia hatua,” akasema.

Alitaja maeneo ya baadhi ya sehemu za Kilifi, Lunga Lunga, Samburu na Puma kuwa maeneo sugu ya watu wanaoendeleza biashara hiyo.

“Wakazi wanaoishi katika sehemu kavu za kaunti hii ndiyo wanaendeleza biashara hii. Tutahakikisha kuwa anayekamatwa anachukuliwa hatua kali ili kudhibiti biashara hii haramu,” akasema.

Alisema kuendeleza ukataji miti misituni kunakosesha wanyama wa porini makazi na chakula hivyo kuvamia vijiji na mashamba kujitafutia chakula na hata makazi.

“Tumekuwa tukipokea visa vya watu kuharibiwa mazao yao na wanyamapori au hata kushambuliwa, hali hii inatokana na binadamu kuharibu makazi ya wanyama hawa,”akasema.

Alisema janga la ugonjwa wa Covid-19 nalo limechangia katika kunoga kwa biashara hiyo akisema kuwa wengi ya walioachishwa kazi katika hoteli wamejitosa katika biashara za makaa kujipatia riziki.

“Baada ya serikali kusimamisha kutua kwa ndege kutoka mataifa ya kigeni, sekta ya utalii ilipata pigo kubwa mno. Hoteli zililazimika kupunguza wafanyakazi ili kujimudu. Hali hiyo ilisababisha watu wengi kukosa kazi,” akasema.

Wakati huo huo aliwaonya wahudumu wa bodaboda kwa kukubali kutumika katika kuendeleza biashara hiyo.

Alisema kufuatia uwezo wake wa kupita vichochoroni wachomaji makaa hutumia boda boda hizo kusafirisha makaa yao ili kukwepa mitego ya maafisa wa serikali.

Awali wazee wa Kaya Tiwi walilalamikia kuwa ukataji wa miti umeharibu sehemu zao za matambiko.

Bw Kassim Mnyeto aliiomba serikali kuingilia kati na kuwakamata wanaohusika na ukataji huo akisema kuwa ukataji huo umekuwa tishio kwa kaya zao.

“Msitu huu unaumuhimu mkumbwa kwa jamii yetu. Ni sehemu hii ambayo tunatekeleza maombj yetu. Si sawa msitu huu kukatwa, tunaomba usaidizi wa serikali,” akasema.

Aidha alisema anahofia kuwa miti ya kale itapotea iwapo serikali haitawachukulia hatua wanaotekeleza shughuli hiyo.

Wazee sita huuawa kila wiki Pwani – Serikali

Na WACHIRA MWANGI

YAHOFIWA mkongwe mmoja huuliwa kila wiki katika kila kaunti za Pwani kwa madai ya uchawi, kwa mujibu wa Mshirikishi wa Eneo la Pwani, Bw John Elungata.

Eneo la Pwani lina kaunti sita.

Bw Elungata alisema asasi za usalama zina wasiwasi kuhusu hali hii na maafisa wanajitahidi kukabiliana na wahusika wakiwemo jamaa wa waathiriwa.

“Huwa tunapokea kisa kuhusu mzee aliyeuawa kila wiki katika kila kaunti ya Pwani. Inatia wasiwasi sana. Hata tunapolalamika kuhusu ukatili wa polisi na mizozo ya kinyumbani inayolenga wanawake, tunasahau kuna wazee wanaouliwa tu kwa sababu ya umri wao na madai ya uchawi,” akasema.

Bw Elungata alitoa changamoto kwa mashirika ya kijamii kuanzisha hamasisho kwa umma kuhusu umuhimu wa kuheshimu wazee na wakome kuwashambulia bila sababu.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Africa, Bw Hussein Khalid alisema uchawi hutumiwa kama kisingizio kuua wazee wakati watoto wao wanapokosa subira ya kurithi ardhi na mali nyingine.

“Tulifanya uchunguzi tukagundua vijana wanaona wazee wanaishi kwa muda mrefu kwa hivyo wanaibua madai ya uchawi ili wauawe,” akasema Bw Khalid. Alisema tatizo hilo ni sugu katika Kaunti ya Kilifi na wanashirikiana na Serikali Kuu kulitatua.

Mratibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) tawi la Pwani, Bi Brenda Dosio alisema inahitajika vijana watafutiwe mbinu za kupata riziki.

KURUNZI YA PWANI: Wakazi wahimizwa wajiandae hali ya kawaida ikitarajiwa

Na MISHI GONGO

ENEO la Pwani limeanza mikakati ya kujitayarisha kurejea kwa hali ya kawaida kama alivyodokeza Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata alisema ni wakati mwafaka wa sekta mbalimbali kuanza matayarisho ya kurejea kwa hali ya kawaida siku chache zijazo.

Bw Elungata aliwahimiza wamiliki wa hoteli kuanza kuandaa matayarisho ya kuwakaribisha watalii.

“Wamiliki wa hoteli wamekuwa na muda wa kutosha kurekebisha hoteli zao ili kuanza kupokea wageni pale nchi itakapofunguliwa,” akasema Bw Elungata.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta alitangaza kuwa serikali italegeza marufuku ili kufufua uchumi ambao umedorora kutokana na athari hasi za Covid-19.

Rais Kenyatta alieleza kuwa nchi haiwezi kuendelea kujifungia.

Alisema ugonjwa utakuwa nasi kwa muda kabla ya kudhibitiwa vilivyo.

Bw Elungata alisema miongoni mwa matayarisho wanayoweka ni kuchimba visima 15 katika kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa ambazo zina idadi kubwa ya maambukizi ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata maji ya kutosha.

Aidha Bw Elungata alisema vijana 18,000 wataandikwa kuhakikisha kuwa wanachunga wanyamapori.

“Vijana wasipoajiriwa katika shughuli hii, wanyamapori ambao ni kivutio kikuu cha utalii watakuwa katika hatari,” akasema.

Alisema shule zitapanuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa katika mazingira mazuri watakaporudi shuleni.

Bw Elungata pia alisema serikali inapanga kujenga daraja katika kivuko cha feri, ambalo litasaidia kupunguza msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa.

“Daraja litakuwa na uwezo wa kufunga na kufunguka ili kuwezesha meli kupita, lakini ujenzi wake utachukua muda wa miezi sita ndipo likamilike. Daraja hili litasaidia kudhibiti virusi vya corona kwani litaruhusu wakazi kuekeana nafasi,” akasema.

Hata hivyo Bw Elungata aliwatahadharisha wakazi kuwa zuio na kafyu vikishaondolewa, ni muhimu waendelee kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kudhibiti kueneo kwa ugonjwa huo hatari.

“Mikahawa na sehemu za burudani zitafunguliwa lakini tutapaswa kuendelea kuzingatia masharti yaliyowekwa kama kuvaa barakoa ili kujikinga,” akasema.

Aidha alisema magari ya usafiri wa umma yatalazimika kutobeba abiria kupita kiasi.

“Maisha yatageuka; hayatakuwa kama awali. Tutalazimika kuendelea kuvaa barakoa na kuekeana umbali baina ya mtu na mwenzake,” akasema mshirikishi huyo.

Pia alisema barabara zilizoharibika kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa katika kaunti za Taita Taveta na Tana River zitakarabatiwa.

Aliongezea kuwa vijana wanaosafisha mitaa watapata Sh3,000 kwa siku kutoka kwa serikali.

“Pesa hivi tunatumai kuwa zitawasaidia katika kujiendeleza kiuchumi na pia kusafisha mazingira. Haya yote ni kuhakikisha kuwa uchumi wetu unarudi pale ulipokuwa kabla kuzuka kwa ugonjwa huu,” akasema.

KURUNZI YA PWANI: Elungata aelezea Wapwani haja ya kushirikiana na maafisa maeneo mpakani yasalie salama

Na WINNIE ATIENO

MSHIRIKISHI wa eneo la Pwani Bw John Elungata na afisa wa uhamiaji Bi Jane Nyandoro wamewaonya wakazi wanaoishi mipakani dhidi ya kuwaruhusu raia wa kigeni kuingia humu nchini kiharamu.

Aidha wamewataka wakazi hasa wa Kwale kuwataarifu maafisa wa usalama kila wanapoona raia wa kigeni wakiingia nchini kwa njia za mkato.

Bw Elungata alisema yeyote anayeingia humu nchini atatakiwa kuwekwa kwenye karantini.

Akiongea huko Kwale, Bw Elungata alisema mtu yeyote anayeingia humu nchini atapimwa ibainike hali yake kiafya hasa ikiwa ana virusi vya corona au la.

“Lakini tunachosema ni kwamba kama unatoka Tanzania, Msumbiji au nchi yoyote ile na unakuja Kenya, lazima upitie sehemu fulani upimwe na ukipatikana una ugonjwa wa Covid-19 unaweza kurudi kwenu. Lakini kama unaingia kwetu lazima uwekwe karantini ukimaliza muda wako unaendelea na shughuli zako,” alisema Bw Elungata.

Hata hivyo, alibainisha kwamba Kenya na Tanzania hazina mgogoro.

Bw Elungata alisema wageni 66 walitiwa mbaroni na polisi walipokuwa wakijaribu kuingia humu nchini wakitumia njia za mpenyo – panya routes – na kuwekwa kwenye karantini.

“Walipomaliza waliachiliwa na kurudi makwao. Tunajua wazee wa mitaa Lunga Lunga wanafanya kazi nzuri sana. Kama kuna ndugu zetu wengine ambao wanashawishika kuwavusha watu, tusiwakubalie kwa sababu ni hatari,” akasema.

Imefichuka kwamba baadhi ya raia wa Tanzania wanaingia humu nchini kupitia Bahari Hindi wakivuka kwa kutumia ngalawa au maboti.

Hata hivyo, Bw Elungata alisema maafisa wa polisi wakishirikiana na wale wa kuchunga bahari – Kenya Coast Guard – wataendelea kushika doria kuhakikisha hakuna raia wa kigeni wanaingia nchini kiharamu.

Aliwaonya wakazi wa Kwale dhidi ya kuwavukisha raia wa Tanzania hadi nchini akisema ni hatari.

“Kuna mtu ambaye anafanya kazi ya kuwaleta Watanzania, usiku wa manane anawatoa, nitamwambia kamishna wa kaunti amkamate na ampeleke karantini. Labda hata kwake kuna mtu amepata ugonjwa,” alisema

Bw Elungata alisema yeyote anayetoroka katika kituo cha karantini katika kaunti za Mombasa, Kwale ua Kilifi, aliyekaa na mgeni ambaye hajamtambulisha na yule aliyekataa kwenda karantini wote watatiwa mbaroni.

“Hatuna shida na hatung’ang’anii mpaka bali tunapigana na ugonjwa pekee. Mtu kama anakuja Kenya na anatoka Tanzania, hatuna shida na yeye sisi ni watu wa Afrika Mashariki tuna mikataba, tunafanya mikakati yetu pamoja hatuna matatizo,” akasema.

Amewataka maafisa wanaolinda mipaka ya Kenya kuwa makini na kuhakikisha watu wanaopita ni wale wanaotakiwa au wanaingia kihalali.

Lakini akasema wazi katika kipindi hiki kigumu ni mizigo pekee ndiyo inayotakiwa kuingia nchini kuepusha watu kutangamana kwa wingi.

Naye afisa wa uhamiaji Bi Nyandoro akasisitiza haja ya kuwakamata wanaotumia njia za kujifichaficha.

“Mkiona watu wanatumia njia za konakona kuingia Kenya tafadhali tujulishe. Tumekwua tukishirikiana na vyombo kadhaa vya usalama kuwakamata wale wanaoingia Kenya kwa njia za mpenyo. Lazima tujilinde,” akasema Bi Nyandoro.