IEBC imeainisha wazi mazingira ya kituo cha kura – Chebukati

Na SAMMY WAWERU

MACHIFU na manaibu wao hawapaswi kuwa katika kituo au vituo vya kura.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati alisema Alhamisi, wakati uchaguzi mdogo kuchagua mbunge Kiambaa na diwani Muguga ukiendelea, maafisa hao wa serikali hawaruhusiwi kuwa kwenye vituo vya kura.

Hii ni baada ya wafuasi na viongozi wa mgombea wa United Democratic Alliance (UDA) John Njuguna Wanjiku kutoa malalamiko yao kwamba machifu wanatumika kisiasa.

“Nilitaja makundi sita yanayopaswa kuwa kwenye kituo cha kupiga kura na machifu si miongoni mwao. Hawaruhusiwi kuwa humo,” akasema.

Alisema hayo kufuatia kisa cha chifu mmoja Kiambaa aliyefukuzwa, akisisitiza kuingia kituoni kusimamia shughuli za kupiga kura.

Baadhi ya wagombea kiti cha ubunge Kiambaa walizua hofu kuhusu machifu na manaibu wao kuonekana vituoni.

“Mazingira ya kituo cha kura ni hadi mita 400 kutoka jengo linaloendeshewa shughuli, hivyo basi yeyote asiyepaswa kuwa humo awe nje kipimo kilichopendekezwa,” Bw Chebukati akasema.

Zimesalia saa chache vituo vya kupiga kura vifungwe ili shughuli za kuhesabu kura zianze.

Mgombea wa ubunge Kiambaa kwa tiketi ya UDA alia serikali kumhangaisha

Na SAMMY WAWERU

MWANIAJI wa kiti cha ubunge Kiambaa anayepeperusha bendera ya United Democratic Alliance (UDA) John Njuguna Wanjiku ameishtumu serikali kwa kile anadai ni kulemaza jitihada zake kusaka kura.

Bw Njuguna amesema mikutano yake ya hadhara inadhalilishwa na serikali, huku mgombea wa Jubilee, Kariri Njama akiruhusiwa kuendesha kampeni bila vikwazo.

“Jumapili tulipangia kudaandaa mechi ya soka ya ‘mahastla’, ila tulizuiwa kuingia uwanjani,” Njuguna akalalamika.

Kulingana na mgombea huyu, UDA, chama kinachohusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, mchuano kati ya Karuri United na Simba FC ulipaswa kugaragazwa katika uga wa Shule ya Msingi ya Karuri, iliyoko Kiambaa, Kaunti ya Kiambu.

“Tulikatazwa kuleta wafuasi wetu pamoja. Maafisa wa polisi walimwagwa tukazuiwa kuingia,” akasema, akieleza kushangazwa kwake na Jubilee kuandaa mechi bila vikwazo.

“Tuliona Jubilee iliandaa mechi yake chini ya ulinzi. Serikali inatumia raslimali zake kufanyia kampeni mwaniaji wa Jubilee, ni kinyume cha sheria za uchaguzi,” akasema.

Bw Njuguna aidha amelalamikia hatua ya serikali kutumia wazee wa kijiji na machifu kung’oa vibango vyake vya kampeni.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeratibu uchaguzi mdogo wa Kiambaa kufanyika mnamo Alhamisi, Julai 15.

Kiti hicho kilisalia wazi Machi 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge, Bw Paul Koinange.