• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Jordan Pickford atia saini mkataba mpya kambini mwa Everton

Jordan Pickford atia saini mkataba mpya kambini mwa Everton

Na MASHIRIKA

KIPA wa timu ya taifa ya Uingereza, Jordan Pickford, amerefusha mkataba wake kambini mwa Everton.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa akielekea mwisho wa miezi 12 ya kandarasi yake ugani Goodison Park na alikuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kuyoyomea Tottenham Hotspur mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23.

Pickford alijiunga na Everton mnamo 2017 baada ya kuagana na Sunderland kwa kima cha Sh4.5 bilioni. Tangu wakati huo, amewajibishwa na Everton mara 222.

“Ni mchezaji mzuri ambaye ni tegemeo letu. Kwa kukubali kutia saini mkataba mpya, ameashiria kwamba anafurahia maisha yake Merseyside na anaridhishwa na kila kitu kambini mwa Everton,” akasema kocha mpya wa Everton, Sean Dyche.

“Amekuwa miongoni mwa wachezaji wenye ushawishi mkubwa uwanjani na tunatarajia kwamba ataendelea kufanya hivyo. Nazidi kujifunza kumhusu Jordan. Amekuwa akisema nami kwa uwazi mkubwa kuhusu jinsi anavyohisi kila anapovalia jezi za Everton,” akaongezea Dyche.

Everton almaarufu Toffees wameshinda mechi mbili kati ya tatu zilizopita tangu Dyche aaminiwe kujaza pengo la kocha Frank Lampard aliyetimuliwa kwa sababu ya matokeo duni.

Kufikia sasa, kikosi hicho kinakamata nafasi ya 16 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 21 sawa na Bournemouth ambao pia wametandaza jumla ya michuano 23 ligini muhula huu. Everton watakuwa wenyeji wa Aston Villa katika pambano la EPL mnamo Februari 25, 2023 ugani Goodison Park.

Pickford aliwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza kwa mara ya kwanza mnamo 2017 na anajivunia kuchezea kikosi hicho mara 50 kufikia sasa. Alikuwa sehemu ya kikosi kilichotinga fainali ya Euro 2020 ila kikazidiwa maarifa na Italia kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Seneta Khalwale hana shida magavana wa zamani wakiwa CASs

Kipngeno ashinda Tel Aviv Marathon, Njuguna apata taji la...

T L