• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KAA Gent anayochezea Okumu yachangisha Sh5.7 milioni kusaidia waathiriwa wa mafuriko Ubelgiji

KAA Gent anayochezea Okumu yachangisha Sh5.7 milioni kusaidia waathiriwa wa mafuriko Ubelgiji

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya KAA Gent anayochezea beki Mkenya Joseph Okumu imechangisha Sh5,746,535 chini ya saa 24 zilizopita kusaidia waathiriwa wa mafuriko kusini mwa Ubelgiji.

Klabu hiyo maarufu “The Buffalos” imesema Julai 17 kuwa iliamua kuanzisha uchangishaji huo wa fedha kutoka kwa umma kwa sababu “sote tumeathiriwa kwa njia moja ama nyingine na tatizo la mafuriko”.

“Watu wengi kutoka mji wa Ghent wanataka kuchangia. Hiyo ndiyo sababu mji wa Ghent umeanzisha kampeni ya kukusanya fedha kusaidia walioathirika,” klabu hiyo imesema kwenye tovuti yake.

Mkenya Joseph Okumu wakati akiichezea klabu ya Elfsborg ya Uswidi. Picha/ Hisani

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Ubelgiji, taifa hilo limetangaza kutenga siku moja ya kuomboleza juma lijalo baada ya mafuriko hayo kuua watu 20 kusini na magharibi mwa Ubelgiji kufikia Julai 16, huku wengine 20 wakiwa hawajulikani waliko.

Mvua kubwa imenyesha nchini humo kwa juma moja na kusababisha mafuriko ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 200.

Taarifa zaidi zinasema kuwa zaidi ya watu 21,000 katika eneo la Wallonia nchini Ubelgiji, ambako wakazi wake wengi wanazungumza Kifaransa, hawana stima.

KAA Gent, ambayo ilinunua Okumu kutoka Elfsborg nchini Uswidi kwa Sh448.4 milioni wiki tatu zilizopita, imeratibiwa kuanza kampeni yake ya Ligi Kuu mnamo Julai 25 dhidi ya Sint-Truidense V.V.

  • Tags

You can share this post!

Ujerumani watoka uwanjani dhidi ya Honduras baada ya Jordan...

Mfumaji Lukas Nmecha ajiunga na Wolfsburg ya Ujerumani