Joho awalaumu viongozi wa Pwani kumtelekeza Kamto baada ya mauti

Na SAMUEL BAYA

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Joho Jumatano alisema kuwa baadhi ya wanasiasa katika eneo la Pwani walimtenga aliyekuwa naibu wa gavana wa Kilifi Bw Kenneth Kamto.

Akiongea wakati wa misa ya marehemu katika Shule ya Msingi ya Lugwe, Rabai, Joho alisema lilikuwa jambo la kushangaza kwamba baadhi ya wale ambao walikuwa wakimsifu marehemu aidha walimtenga wakati akikabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha.

“Marehemu Kamto alikumbana na changamoto nyingi sana katika maisha baada ya kutoka uongozini. Na baadhi yenu hapa mlikataa hata kupokea simu zake kila alipohitaji msaada kutoka kwenu. Ajabu leo mko hapa na maneno ya kumpongeza. Lakini kwangu mimi, hili ni somo ambalo lazima tujifunze. Najua kuna wanasiasa ambao kila walipoona simu zake walizipuuza, na labda hata mimi ni mmoja wao, lakini huo ndio ukweli, lazima tubadilike na tushikane mikono ndani na hata nje ya siasa,” akasema Gavana Joho.

Wakati uo huo, Naibu wa Rais William Ruto ambaye pia alihudhuria mazishi hayo aliwahakikishia Wakenya kwamba waliomuua marehemu watakamatwa.

Akiwahutubia waombolezaji wakati wa misa ya marehemu katika Shule ya Msingi ya Lugwe, Rabai, Bw Ruto alisema kuwa tayari uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwansaisa huyo unaendelea.

“Niliposikia kuhusu habari za kifo cha Bw Kamto kutoka kwa rafiki yetu Bw Gedion Mung’aro, nilimpigia simu mkewe na kumuuliza kilichofanyika.

Aliponieleza kila kitu, mara moja nilimpigia simu Inspekta Mkuu wa polisi Bw Joseph Boinnet na kumwambia atume kikosi maalumu kutoka Nairobi kuja kukichuguza kifo hicho,” akasema naibu huyo wa Rais.

“Kile ambacho ninaweza kuwahakikishia ni kuwa kifo cha ndugu yetu Kamto hakitabakia hivi tu. Lazima kitachunguzwa kikamilifu mpaka mwisho,” akasema Bw Ruto katika misa ambayo ilihudhuriwa na viongozi wengi wa kisaisa na kijamii kutoka eneo la Pwani.

Hakikisho hilo la naibu wa Rais lilitokana na shinikizo kutoka kwa viongozi wa Pwani kwamba polisi wamezembea katika kuwatafuta wale ambao walihusika na mauaji ya Bw Kamto.

Magavana ambao walihudhuria mazishi hayo walikuwa ni Bw Salim Mvurya (Kwale), Bw Amason Kingi(Kilifi) na Bw Hassan Joho (Mombasa).

Vilevile, Seneta Christine Zawadi (Seneta Maalum), Mohamed Faki (Mombasa) na Issa Boy (Kwale) pia walihudhuria mazishi hayo.

Baadhi ya wabunge ambao walihudhuria mazishi hayo ni pamoja na Bw William Kamoti (Rabai), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Paul Katana (Kaloleni), Teddy Mwambire (Ganze), Aisha Jumwa (Malindi), Naomi Shaban (Taveta), Badi Twalib (Jomvu), Charles Njagua (Starehe) Gertrude Mbeyu (Mwakilishi Maalum-Kilifi), Zulekha Juma (Mwakilishi – Kwale) na Benjamin Tayari (Kinango).

“Tunasikitika kwamba marehemu Kamto ambaye alihudumu kama naibu wa kwanza wa gavana katika Kaunti ya Kilifi alifariki katika kifo cha namna hii. Naibu wa Rais, hali ya usalama katika Mombasa na Pwani yote kwa ujumla imezorota.

Mimi niliwahi kuvamiwa ila Mungu akanisaidia wezi walinikosa. Lakini tujuliulize mawali kwamba ikiwa kiongozi anavamiwa, je kwa raia kule mashinani hali iko vipi,” akahoji Bw Kingi.

Kifo cha marehemu Kamto lazima kichunguzwe kikamilifu na tujue ni akina nani ambao walihusika na kwa sababu gani hasa,” akasema Gavana Kingi.

Aidha Bw Kingi alisema kuwa serikali ya kaunti iliamua kugharamia mazishi ya Bw Kamto kwa sabau aliwahi kuhudumu kama naibu wa kwanza wa gavana wa Kilifi.

“Wengi labda wanajiuliza kama ni kwa sababu gani serikali ya kaunti ya Kilifi imegharamia mazishi ya Bw Kamto. Jibu ni kuwa ile heshima ya kwamba alihudumu kama naibu wa gavana. Kwa hivyo ni kwa uchungu kwamba tunamzika kama kaunti,” akasema Gavana Kingi.

Aidha Bw Kingi alitangaza kwamba yeye pamoja na gavana mwenzake wa Mombasa Bw Hassan Joho wataipatia familia hiyo Sh2millioni ilikugharamia maisha na elimu ya watoto wa marehemu.

Gavana Mvurya alimsifu Bw Kamto kama rafiki ambaye walifanya kazi na yeye akiwa katika upinzani(ODM) kisha baadaye alipotoka katika chama hicho na kujiunga na Jubilee.

Mbunge wa Rabai Bw William Kamoti alitaka manaibu wa magavana n ahata magavana ambao wanatoka katika afisi za umma kuendelea kupatiwa ulinzi na serikali.

MAUAJI YA KAMTO: Wito uchunguzi wa kina ufanywe

Na SAMUEL BAYA

VIONGOZI wa eneo la Pwani wamewataka polisi kuchunguza kwa kina mauaji ya aliyekuwa Naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi, Bw Kenneth Kamto.

Bw Kamto alifariki baada ya kupigwa risasi tatu nyumbani kwake eneo la Nyali, Mombasa jana asubuhi.

Marehemu ambaye hadi kifo chake alikuwa mfanyabiashara jijini Mombasa alipigwa risasi hizo mbele ya mkewe sebuleni kabla ya kuaga dunia.

Maafisa wa polisi wakiongozwa na kamanda wa polisi eneo la Pwani, Bw Noah Mwivanda walithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi umeanzishwa.

Kufuatia kisa hicho, Gavana wa kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi aliagiza bendera zote za serikali ya kaunti kuwekwa nusu mlingoti ili kumuomboleza Bw Kamto.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba tumempoteza Bw Kamto na kama wakazi wa Kilifi, tumepoteza rafiki, ndugu na jamaa. Kwa sasa tunaitakia familia yake afueni wakati wakiendelea kuomboleza,” alisema Bw Kingi baada ya kuongoza viongozi wengine kutazama mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya mkoa wa Pwani

Aliongeza, “Na kwa sababu Bw Kamto alikuwa naibu wa kwanza wa Gavana wa kaunti ya Kilifi, pia nimeagiza bendera zote za serikali ya kaunti zipeperushwe nusu mlingoti kwa kumuenzi marehemu.”

Mkewe marehemu Bi Fauzia Kamto alieleza wanahabari kwamba mumewe aliingia mbio nyumbani mwendo wa tisa asubuhi.

“Jumanne jioni, mume wangu alikuja kunichukua kazini hadi nyumbani. Mimi ilipofika saa mbili jioni, nilienda hafla nyingine sio mbali sana na nyumbani na nilimuacha akiwa nyumbani bila tashwishi yoyote,” akasema.

Hata hivyo, aliporudi nyumbani mwendo wa saa tano usiku hakumkuta mumewe.

“Mimi niliangalia runinga lakini baadaye usingizi ulinizidi na nikalala kwa kiti. Hata hivyo, mwendo wa saa tisa asubuhi, mume wangu alifungua milango mbio akikimbilia jikoni. Wakati huo wote alikuwa akipiga kelele akisema niite askari mara moja,” akasema Bi Kamto.

Alisema muda mchache, majambazi watatu waliingia ndani hadi sebuleni. Mmoja wao aliichukua familia yote mateka huku mwengine akimfuata marehemu karibu na jikoni.

“Mume wangu alitoka tena jikoni lakini akikaribia sebuleni akapigwa risasi tatu.Muda huo wote, tulikuwa tumezuiliwa mateka na jambazi mmoja. Ninasikitika sana,” akasema mjane kabla ya kuanza kuangua kilio.

Viongozi wa eneo hilo waliendelea kutuma risala zao za rambirambi.

Wakiongozwa na naibu wa sasa wa gavana, Bw Gideon Saburi, walisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa kaunti ya Kilifi.

Seneta wa Kwale Bw Issa Juma Boy,alitaka polisi wachunguze kifo hicho na kuwakamata washukiwa.

Aliyekuwa mbunge wa Kaloleni , Bw Gunga Mwinga pia alitaka chanzo cha mauaji hayo kichunguzwe.

Waliokuwa wabunge Gunga Mwinga(Kaloleni) na Anaina Mwaboza(Kisauni) pia waliomboleza kifo hicho cha Bw Kamto.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba Bw Kamto alifariki katika kifo hiki. Hata hivyo ninaamini kwamba maafisa wa usalama watachunguza kiini hasa cha kifo hiki,” akasema Bw Gunga.

Seneta wa Kwale Bw Issa Juma Boy,ambaye ana uhusiano na familia hiyo alitaka polisi wachunguze kifo hicho na kuwakamamata wale ambao walihusika na uhalifu huo.

Mashirika ya kutetea haki za kibindamu ya MUHURI, Haki Africa na Tihuri pia yalitaka polisi wafanye uchunguzi wa haraka kuwakamata wale wote ambao wlaihusika na uhalifu huo.

“Ni wazi kabisa kwamba polisi wameshindwa na kukabiliana na ongezeko la utovu wa usalama katika kaunti ya Mombasa,” akasema Bw Francis Auma kutoka shirika la MUHURI.

“Mauaji haya sasa yanazidi kuthibitisha ukweli kwamba visa vya mauaji vinazidi kuwa kero katika kaunti ya Mombasa,” akasema Bw Husein Khalidi wa Haki Africa.

“Maafisa wa usalama lazima waanzishe mara moja uchunguzi kuhusu kifo cha Bw Kamto na kuwakamata wale wote ambao walihusika na uhalifu huo,” akasema Bw Eric Mgoja wa shirika la Tihuri.