• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:36 PM
Kassait apendekeza Sheria ya Kulinda Data ya 2019 ifanyiwe mabadiliko

Kassait apendekeza Sheria ya Kulinda Data ya 2019 ifanyiwe mabadiliko

NA CHARLES WASONGA

KAMISHNA wa Kulinda Data Nchini Immaculate Kassait, amewataka wabunge kuifanyia mabadiliko Sheria ya Kulinda Data iliyotungwa 2019 na kanuni za kuitekeleza ili kuzuia mradi tata kama wa Worldcoin.

Akiongea Alhamisi jioni alipofika mbele ya kamati ya muda ya bunge inayochunguza shughuli za kampuni hiyo nchini, Bi Kassait pia alitaka afisi yake ipewe uwezo zaidi kifedha na wafanyakazi.

“Afisi yangu imejifunza mengi kutokana na shughuli za Worldcoin nchini. Na tumeng’amua kuwa kuna pengo kubwa katika Sheria ya Kulinda Data, 2019. Aidha imebainika kuwa afisi yangu imekabiliwa na upungufu wa kifedha na wafanyakazi wenye ujuzi kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” akasema.

“Kwa hivyo, naomba bunge kupitia kamati hii kuanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria hii kama hatua ya kwanza ya kuziba mianya iliyotumiwa kuiwezesha Worldcoin kupata nafasi ya kuvuna data kutoka kwa Wakenya kwa njia ya kutatanisha,” Bi Kassait akasema.

“Kwa mfano, tunahitaji sheria inayofafanua data za kibinafsi na jinsi data kama hizo zinavyofaa kushughulikiwa,” akaeleza kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.

Bi Kassait pia alipendekeza kuwa kampuni za kusimamia na kuchanganua data ziwe zikichapisha notisi katika vyombo vya habari kabla ya kuanza shughuli ya kukusanya data za kibinafsi kutoka kwa wananchi.

Alisema kuwa sheria kuhusu ukusanyaji data, na kanuni husika, zinafaa kutekelezwa chini ya mpango unaoshirikisha Wizara ya Usalama wa Ndani.

Aidha, Bi Kassait aliiambia Kamati hiyo kwamba kampuni za kigeni za kukusanya data sharti zitafute leseni za kibiashara na vibali vinginevyo kabla ya kuwasilisha maombi ya kutaka zisajiliwe humu nchini.

Kauli yake inajiri baada ya maafisa wa kampuni ya Worldcoin mnamo Jumatano, kuiambia kamati hiyo kuwa haikuwa imesajiliwa nchini Kenya.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tools For Humanity (TFH), iliyotumiwa na Worldcoin kuingia nchini, Alex Blania, alisema hakuna sheria iliyowalazimu kusaka usajili nchini kwanza kabla ya kuendesha shughuli za ukusanyaji data kutoka kwa Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Samboja aliyebwagwa uchaguzini...

Wanaume 3 wanaswa Bungoma kwa kuitisha hongo kwa vijana...

T L