KINA CHA FIKIRA: Ujeuri wa mpapai hujeruhi na udhalili wa unyasi huokoa

Na WALLAH BIN WALLAH

KILA mwanadamu ana hulka au tabia tofauti.

Wapo wenye tabia za upole, unyenyekevu na heshima.

Pia wapo wenye tabia za ujeuri, ukali, hasira na kiburi!

Watu wenye sifa za ujeuri na kiburi hujisifu wakidhani ati ujeuri ni ushujaa!

Wanasahau kwamba kujisifu au kusifiwa kwa kufanya vitendo vya ujeuri, ukatili na kiburi ni kashfa wala si sifa njema!

Hawakumbuki methali zisemazo, ‘Kwa shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko; na kiburi si maungwana?’

Unyenyekevu na heshima huambatana na woga! Mtu mtiifu mwenye nidhamu huwa mwoga!

Kamwe hajipigi kifua hadharani na kujigamba au kujionyesha kiburi chake kama sokwe dume!

Chunguza nukuu za vitabu vya dini zote wanasema, ‘Ogopa Mungu wako!’

Yaani uwe mnyenyekevu na mtiifu kwa Mungu wako! Woga ni heshima! Hapo ndipo nilipopata ari na hamasa ya kuandika kauli ya leo katika Kina cha Fikira!

Babu yangu Mzee Majuto alikuwa mkulima na mfugaji maarufu.

Shambani kwake kulikuwa na mpapai mkubwa uliozaa mapapai mengi makubwa! Karibu na mpapai huo kulikuwa na nyasi ndefu zilizostawi kuwa chakula cha ng’ombe wake!

Siku moja jioni mawingu mazito meusi yalitanda ghafla angani! Mara upepo mkali ukaanza kuvuma na ngurumo za radi kurindima kuashiria mvua kubwa!

Hatimaye mvua kubwa ya theluji ikaanza kumwagika! Watu wote wakajifungia ndani ya nyumba zao. Nyasi zile ndefu zilizokuwa karibu na mpapai zikalala chini ardhini kwa kuogopa hasira za upepo na kani za mvua kubwa! Lakini mpapai ule mkubwa ulisimama tu kwa kiburi na ujeuri bila kuogopa wala kuinama kuepuka dhoruba ya mvua!

Mvua ilipozidi kumwagika na upepo kuvuma zaidi, mpapai ulivunjika matunda yake yote yakapukutika chini!

Asubuhi kulipokucha kulikuwa shwari baada ya mvua kupusa. Nyasi zile zilianza kunyanyuka taratibu na kusimama kuendelea kuishi kama kawaida!

Mpapai uliovunjika ulipoona nyasi zikisimama tena, mpapai ukafoka, “Mbona nyinyi nyasi na unyonge wenu hamkuvunjika kama mimi mpapai ilhali nina nguvu na thamani zaidi yenu?”

Nyasi zilijibu kwa upole, “Wewe mpapai umeanguka ukavunjika kwa sababu ya ujeuri wako na kiburi chako! Sisi nyasi na unyonge wetu tuliogopa upepo mkali na mvua kubwa tukanyenyekea tukalala chini kwa heshima mpaka tufani ilipoisha! Tumenusurika!”

Ndugu wapenzi, tuwe watu wanyenyekevu wenye nidhamu ili tuepuke majanga tuishi maisha marefu!

Ujeuri hujeruhi na unyenyekevu huokoa maisha! Unyenyekevu wa unyasi ndio usalama wa unyasi! Nimewaambia!!!!!

KAULI YA WALLAH: Ni busara kufikiri badala ya kupapia kusema au kujibu

NA WALLAH BIN WALLAH

KUFIKIRI ni kazi. Ubongo wako hauwezi kukupa majibu sahihi ya maswali unayoulizwa bila ya ubongo kufanya kazi ya kufikiri vizuri! Kuelewa swali vyema ndiko kupata jibu au majibu sahihi.

Kusema au kujibu kwa papara tu kunasababisha kutoa majibu batili yasiyoeleweka ama yasiyowiana na swali lililoulizwa au maswali yaliyoulizwa!

Wanafunzi wengi shuleni hula mwande, hubunda au hufeli siyo kwa kuwa ni wajinga! La hasha! Kushindwa kwao hutokana na kujibu haraka haraka kabla ya kuchambua na kutambua kiini cha swali.

Ili kuelewa kiini cha swali lazima mtu afanye kazi ya kufikiria dhamira ya swali kabla hajalijibu. Majibu sahihi ni kuelewa maswali kwa usahihi! Hakuna mwanafunzi wa kushindwa kuyajibu vizuri maswali anayoyaelewa barabara!

Chunguza uone!!Usijibu haraka haraka kabla ya kufikiria na kuelewa unachotaka kujibu na unavyotaka kujibu! Katika maswali kuna kufikiri na katika kufikiri kuna kutaka kujua madhumuni ya muulizaji maswali ndipo utoe jibu au majibu! Maswali hufikirisha!

Fikiri kabla hujatamka au kujibu!Maswali yanapoingia kichwani mwa binadamu, yanaupa ubongo msukumo wa kufanya udadisi na kutafiti zaidi ili afikie kina kamili cha kupata majibu yanayofaa! Kadri mtu anavyokumbana na maswali mazito ya kujiuliza au anayoulizwa ndivyo anavyojifunza mambo ambayo hakuwa ameyaelewa!

Maswali hujulisha, huerevusha na kutanabahisha!Ninashangaa watu wengine wanapotoa majibu haraka haraka tu punde wanapoulizwa maswali! Hawajui kwamba majibu ya papara ni hatari? Tena yanapotosha?

Watu wenye hasira, ukali na majivuno rohoni huwa wepesi wa kutoa majibu mengi upesi upesi kuonesha ubabe wao waulizwapo maswali! Mbona?Leo tufahamishane kwamba mtu anapokuwa na majibu mengi ya haraka haraka kichwani, anadhani na kujiona kuwa anajua kila kitu!

Kumbe ajuaye kila kitu ni Mola tu! Kujibu haraka haraka bila kukuna kichwa ni kutangaza udhaifu na kudhihirisha tu kwamba mtu hajui anavyojibu kwa mujibu wa majibu mujarabu yaliyotarajiwa kuyatosheleza maswali yaliyoulizwa!

Huku kujibu kwa papara tumeshuhudia sana mara nyingi katika matukio mbalimbali ya mahojiano na mihadhara hapa na pale! Ni hatari! Tufikiri kabla ya kujibu!

Ndugu wapenzi, mtu akiulizwa swali au maswali yoyote, ni bora zaidi kufikiri na kulielewa swali ndipo ajue atakavyojibu! Kujibu swali kwa kulielewa, kwa heshima na adabu ni utu! Majibu mazuri huonesha busara aliyo nayo mtu!

Chonde chonde! Fikiri kabla hujasema na ufikiri zaidi kabla hujajibu haraka haraka! Kufikiri ni kazi!!!

WALLAH: Usimtukane mamba kabla hujauvuka mto

NA WALLAH BIN WALLAH

JUZI nilimsikia Mzee Shikaadabu akimkanya mjukuu wake aitwaye Kichwamraba akome kabisa ujeuri! Akamwambia, ‘Mjukuu wangu, ujeuri hujeruhi! Usiwe mjeuri wala usiwe mkaidi! Kumbuka mkaidi hafaidi hadi siku ya Idi!’

Nilijikuna kichwa nusura ning’oke nywele zote! Nikawaza kuhusu maafa ya mtu aliye mjeuri au mkaidi maishani! Nikajiambia kwamba, ‘Mkulima anapolima shambani, hupanda mbegu ziote!

Mimea ikishastawi avune mazao mazuri ayatumie kujikimu maishani! Lakini huyu mtu mjeuri au mkaidi, anapofanya ujeuri wake, anatarajia kupata faida au mavuno gani?

‘Baada ya kudadisi zaidi niliambiwa kwamba yule Kichwamraba mjukuu wa Mzee Shikaadabu alikuwa mjeuri mkosa adabu nyumbani kwa wazazi wake waliomlea, wanaomlisha na kumlipia karo ya masomo shuleni!

Licha ya hivyo, Kichwamraba aliupeleka ujeuri wake na ukaidi wake mpaka shuleni kwa walimu aliotarajia wangemsaidia kumfunza hadi afuzu apate elimu bora ya kumfaa kuja kuishi maisha mema duniani!!!

Tunapaswa kujua kwamba wazazi wana majukumu muhimu sana katika kuwalea na kuwatimizia watoto mahitaji yao maishani jinsi walivyo walimu shuleni!

Bila ya juhudi za walimu na kujitolea kwao kuwafunza na kuwaelekeza wanafunzi wao shuleni, amini usiamini, kufanikiwa kwa wanafunzi hao kungekuwa finyu sana!

Walimu ni nguzo muhimu sana masomoni!Kwa hakika mtoto akikorofishana na mzazi wake wakati ambapo hajafikia umri wa kujimudu kujitegemea maishani, ni msiba mkubwa sana!

Hata kama amefikia umri wa utu uzima lakini hana uwezo wa kujikimu mwenyewe maishani, atateseka tu! Mzazi aheshimiwe!!

Kule shuleni nako mtoto au mwanafunzi akimletea mwalimu wake ukorofi kabla hajasoma akahitimu elimu yake, anatarajia kupata nini?

Je, akitimuliwa kutoka shuleni au walimu wakisusia kumsaidia masomoni, atafanyaje baada ya kutelekezwa? Fikiri sana!!Ndugu wapenzi, hata kama unajua kuogelea mithili ya samaki, usimtukane mamba aliye majini kabla hujavuka mto!

Mamba ndiye mfalme mtoni! Mpe heshima zake ili uvuke uende ng’ambo salama salmini bila kung’atwa! Nawe mfanyakazi, usishindane na mkubwa wako kazini. Nyenyekea ufanye kazi upate ujira wako uishi uishie!

Tabia hii ya kumtukana mamba pia wanayo sana wanasiasa wakorofi wenye hulka za kumcharuracharura kiongozi wa nchi ambaye ndiye amirijeshi! Chonde chonde! Chuja kauli zako! Usimtukane mamba kabla hujauvuka mto! Usiseme hatukukwambia!!!!!

KINA CHA FIKIRA: Epuka kujipaka uchafu ndipo nzi wasikusumbue

Na WALLAH BIN WALLAH

BABU yangu Mzee Majuto bin Kengemeka aliniambia zamani nilipokuwa kijana mchanga kwamba watu humchukia nzi -mdudu mdogo tu- na kumlaumu kuwa anaambukiza magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, ugonjwa wa macho na mengineyo.

Huo ni ukweli kabisa! Nzi ni mdudu hatari sana kwa afya ya wanadamu na wanyama! Lakini tujiulize nzi humfuata mtu au mnyama mwenye sifa na hulka gani?

Kwa hakika nzi hatui wala haendi mahali bila kuwapo na kitu au vitu vinavyomvutia kuenda kutua pale kama vile uchafu na uvundo!

Ukitaka kuwaepuka nzi ili wasikusumbue, uondoe uchafu! Ama uondoke mahali penye uvundo!

Ni kazi bure kupigana na nzi hata ukitumia marungu, mishale, nyundo, bunduki au mawe endapo umejipakaza uvundo au umekaa palipo na uchafu! Nzi watang’ang’ania pale pale! Watakusumbua tu mpaka ujisafishe uondoshe uchafu ubakie ukiwa safi!

Wahenga walisema kwamba, ‘Mwenye kidonda ndiye amwogopaye nzi.’ Mtu asiye na kidonda hashtuki hata akimwona nzi akitua mwilini pake kwa sababu hana jeraha ambalo nzi ataanza kung’ong’ona!

Kasoro zetu na uchafu wetu hutuletea matatizo makubwa maishani kisha tunaparamia kulalamika!

Katika kuyachunguza mambo utagundua kwamba wanyama wakubwa wote wa porini na nyumbani wana matatizo na mahangaiko makubwa bila utulivu! Chunguza uone! Kila wakati wanyama hao wanapotembea au wanapolala wana wasiwasi hawatulii kamwe! Watazame simba, nyati, ndovu, chui, ng’ombe, punda, nyumbu, pundamilia na wengineo. Kila wakati wanarusharusha na kutikisatikisa miguu yao, mikia yao na masikio yao kwa sababu wanasumbuliwa na wadudu hao wadogo waitwao nzi!

Nzi hung’ong’a na kuwang’ong’ona wanyama wakubwa hao kwa sababu wana vidonda na uchafu unaotafutwa na nzi. Wanyama hawanawi nyuso zao, hawaoshi macho yao, hawapigi miswaki baada ya kula! Hawasukutui vinywa vyao wala kusafisha masikio yao! Viungo vyao vyote hivyo vina uchafu unaowavutia nzi na kusababisha nzi kuwahujumu, kuwasumbua na kuwakera wanyama wakubwa!

Hayo ndiyo masaibu na madhila waliyo nayo wanyama wakubwa wasiojua kujisafisha kuondoa uchafu ili wasisumbuliwe na wadudu wadogo kama nzi!

Ndugu wapenzi, matatizo ya mwanadamu huletwa na mwanadamu mwenyewe! Chambilecho Profesa Ebrahim Hussein katika kitabu cha Kinjeketile kwamba, ‘Binadamu huzaa neno kisha neno likawa kubwa kumshinda binadamu aliyelizaa!’

Ni vizuri mtu ajitakase awe safi ili asije akateswa na kujutia makosa yake mwenyewe hatimaye aanze kuwalaumu nzi wadudu wadogo ambao wamefuata uchafu aliojipaka binadamu! Ondoa uchafu! Uwe safi! Ukiepuka kujipaka uchafu, nzi hawatakusumbua!

wallahbinwallah@gmail.com

KINA CHA FIKRA: Kuteka watoto nyara ni unyama na hatari kwa usalama

Na WALLAH BIN WALLAH

KILA kunapokucha kunakucha na kucha zake!

Siku hizi kila kunapokucha utasikia visa vya kuatua moyo na kuogofya kabisa kwamba mtoto wa fulani amepotea au watoto fulani wametekwa nyara!

Licha ya hayo, mara utasikia ati watekaji nyara wametuma arafa kwa wazazi kudai walipwe kitita kikubwa cha pesa wakati huu wa ukame wa kupata hela!

Msiba mkubwa zaidi ni kwamba pesa hizo za dhuluma zikichelewa kidogo tu kuwafikia hao maharamia, utasikia kwamba mtoto aliyetekwa nyara amechinjwa na kupatikana akiwa maiti!

Makubwa zaidi ni kwamba watoto wengine hupotea vivi hivi tu wanapotumwa na wazazi wao au wanapotoka nyumbani kuenda kucheza na wenzao bila kupatikana taarifa zozote kuhusu kupotea kwao! Halafu baada ya msako wa siku kadhaa ndipo mwili hupatikana ati mtoto alinyongwa au alichinjwa baada ya kutendewa unyama!!

Katika hali kama hii, tuseme nini? Kunani jamani? Usalama uko wapi? Wazazi roho mikononi!! Nao watoto vifo visogoni! Nani atakayemnusuru nani kutokana na jangamizi hili la watoto kutekwa nyara na kuuawa kinyama kwa kuchinjwa kama kuku?

Wazazi wafanyeje? Waache shughuli zao za kila siku za kuenda kutafuta riziki wakae na watoto wao majumbani?? Au watawafungia watoto ndani ya nyumba kama kuku wanavyofungiwa vizimbani? Ama waache kuwatuma watoto madukani? Au watoto waache kutoka majumbani kuenda kucheza na wenzao? Mbinu mwafaka wa kufumbua mafumbo haya na kuvitegua vitendawili hivi ni zipi? Ipi dawa mujarabu ya kuadua msiba na mizingile kama hii kuhusu maisha ya watoto wetu? Hali ni tete! Maisha ya wanetu yamo hatarini kila leo! Utekaji nyara ni hatari kubwa kwa usalama wa watoto wetu! Tufanyeje?

Kwa upande mwingine, tukichuja na kuchungulia, vyombo vya dola na asasi za usalama, kunani? Usalama wetu uko wapi? Enyi walinda usalama mliokabidhiwa dhima na dhamana za ulinzi, mnatuhakikishia nini kuhusu usalama wa raia, mwananchi na hasa hasa watoto hawa wanaotekwa nyara na kupatikana wamechinjwa? Mnasemaje wazalendo wenzangu walinda usalama? Walindwa wanaangamia na kuomboleza! Wanalia! Au ulinzi umegeuka ulizi? Chonde chonde jamani! Tafadhali! Tunaomba ulinzi na usalama ulio salama salmini!

Ndugu wapenzi, wakati mwingine mimi hutamani mwanadamu angejua wajibu wa kuwalea na kuwalinda watoto wao kama nyani ambao huwatunza kwa kuwabeba na kuwap akata watoto wao kila wakati! Lakini hapana! Binadamu tuna akili zaidi! Tuwalinde watoto wetu! Utekaji nyara ukomeshwe na ukome kabisaaa!!!

KINA CHA FIKRA: Asilan usikubali kushindwa hata kabla ya kujaribu

Na WALLAH BIN WALLAH

UNYONGE wa watu wengine ni kukata tamaa mapema hata kabla ya kujaribu kufanya shughuli au kazi fulani wanazopaswa kufanya!

Ni kasoro kubwa sana mtu kufikiria atashindwa kabla ya kupambana hadi mwisho!

Ni hatari kubwa kuanza kutoa vijisababu na visingizio vya hapa na pale kujitetea kuonyesha jinsi unavyodhania ungeshindwa kufanikiwa kuyatimiza malengo yako! Kwa kweli kushindwa kupo.

Kila mtu hutokea akashindwa! Lakini tabia ya kukata tamaa kabla ya kujaribu kupambana ni duni zaidi! Jaribu kwanza! Ukishindwa kila mtu atajua umejitahidi! Wewe pia utajua kuwa umejikakamua! Huko ndiko kushindwa kishujaa! Usikubali kushindwa kabla hujashindwa! Huo si ujasiri!

Duniani kuna mafanikio mengi! Lakini lazima yatafutwe! Yasipotafutwa hayawezi kupatikana kamwe! Tazama wadudu wadogo wadogo kama vile siafu, mchwa, vipepeo na nyuki wanavyojituma kusafiri kuenda mbali kuhemera ili wapate chakula na mahitaji yao mengine bila uzembe!

Aghalabu utawaona kwenye misafara na makundi yao wakiwa wamebeba mizigo ya vyakula bila kukata tamaa! Na wanaishi hivyo miaka yote! Kwani wadudu hao wana busara au akili gani kuliko baadhi yetu sisi wanadamu? Tusikubali kushindwa kabla ya kujaribu! Atafutaye hachoki; labda achoke akishapata!

Hebu tukumbushane kidogo! Wiki iliyopita matokeo ya mtihani wa darasa la nane yalitangazwa! Tuwapongeze zaidi wanafunzi waliofanya mtihani huo katika wakati mgumu wa janga la corona pamoja na walimu wao waandalizi! Pongezi kwenu nyote!

Licha ya matokeo mema yaliyopatikana, usidhani wanafunzi wote wa darasa la nane walifanya mtihani! La, hasha! Wengine walihepa na kujificha bila ya kufanya mtihani kwa vijisababu na visingizio mbalimbali! Wapo waliosingizia hali ngumu kutokana na corona wakiamini kwamba kufanya mtihani ni kuanguka tu! Wakaamua kushindwa hata kabla ya kujaribu! Wengine walisingizia ujauzito! Ati walichelea kuenda kwenye mtihani wakiwa wajawazito ilhali serikali ya nchi yetu iliwasihi na kuwarai wasikose mtihani kwa vyovyote vile! Wakashindwa kabla ya kujaribu!

Wanafunzi wengine waliamua kuacha kufanya mtihani kwa visingizio kwamba hata kama wangefaulu vizuri, wasingepata pesa za kulipia karo katika shule za sekondari! Na wengine waliamini mtihani ni mgumu tu kwa watu ambao hawakuenda shuleni miezi mingi! Nao wakashindwa hivyo bila kujaribu!

Ndugu wapenzi, jaribu kwanza. Usikubali kushindwa maishani kabla ya kujaribu!

KINA CHA FIKRA: Profesa Ken Walibora alikichapukia Kiswahili kwa kauli na matendo, Mola azidi kumrehemu

Na WALLAH BIN WALLAH

LEO tumeumega mwaka mzima kasoro siku tatu tangu alipoaga dunia Profesa Ken Walibora mwandishi mahiri mtajika wa vitabu vya Kiswahili aliyetuacha tarehe kumi Aprili, 2020.

Katika kitabu cha Juliasi Kaizari kilichotafsiriwa na Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Mark Antonio anasema, “Ndugu Warumi, matendo mema ya mwanadamu huishi milele baada ya mwanadamu kuondoka duniani! Kwa hivyo, mimi nimekuja hapa kumzika Kaizari wala sikuja kumsifu Kaizari, kwa sababu nyinyi nyote mnaelewa matendo mema ambayo Kaizari aliwatendea Warumi wote!”

Katika uzi huo huo, ninaunganisha kwa kusema kwamba, mimi siandiki makala haya ya leo kumsifia hayati Ken Walibora, ila nimeshika kalamu na kuupinda mgongo wangu kuandika kumkumbuka Ndugu Profesa Ken Walibora mwandishi mwenzetu aliyetuacha duniani tukigwayagwaya kwa majonzi na machozi baada ya kutuondoka ghafla tarehe kumi mwezi wa nne mwaka jana! Sina maneno mapya ya kumsifia hayati Ken Walibora katika makala haya kwa sababu kazi alizofanya katika kukuza Kiswahili pamoja na vitabu alivyoviandika matopa kwa matopa, vinatosha kutangaza sifa zake kwa matangazo ya kweli bila matilia chumvi milele na milele duniani! Ndipo kila mara tunakumbushana kwamba ukiwa hai duniani, tenda matendo mema watu wayaone!

Matendo ni muhimu kuliko maneno matupu! Matendo hayafi hata kama mtu mwenye matendo ameondoka duniani! Tenda matendo uyaache duniani! Usiishi bila matendo! Utakuwa sawa na kalamu isiyokuwa na wino iliyoandika bila kuacha maandishi!

Jitahidi uwe kama mdudu konokono ambaye huacha alama kila mahali anapopitia bila kufutika! Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno! Tenda watu wayaone matendo ili nawe ukumbukwe kwa matendo si kwa maneno matupu!

Aidha sitaki kujivisha joho la kumsifia sana hayati Profesa Ken Walibora kwa sababu watu wote waliobahatika kukutana naye, wanaelewa fika kwamba Komredi Ken Walibora alikuwa mtu wa watu, mcheshi mwenye uso wa bashasha siku zote; mwungwana mwenye roho safi asiyejua kununa anaponena maneno yake ya busara!

Alicheka na kila mtu na kumheshimu kila mja! Hatuwezi kumsahau mzalendo huyu mpenzi wa Kiswahili aliyeitetea lugha yetu adhimu kwa udi na uvumba hadi siku ya mauko yake!

Ndugu wapenzi, namalizia kauli ya leo kwa kukariri kwamba, mtu ni matendo! Ukiwa mwema utende mema duniani uache matendo mema! Bado tunamkumbuka Ndugu Profesa hayati Ken Walibora mwandishi mtajika wa Kiswahili kwa matendo yake na kazi zake bora kama jina lake Walibora! Mola aisitiri roho yake mahali pema peponi! Aamina!!!!

KINA CHA FIKRA: Daima Magufuli atakumbukwa kwa uzalendo na utetezi wake wa Kiswahili

Na WALLAH BIN WALLAH

KIONGOZI yeyote awaye mwanamapinduzi na mzalendo halisia mara nyingi hukumbatia na kuonea fahari lugha ya taifa lake!

Anajua dhahiri shahiri kwamba lugha ya taifa ndicho chombo muhimu cha kuleta umoja na mshikamano wa kweli nchini.

Katika mataifa yetu ya Afrika Mashariki, hasa Kenya na Tanzania, tunajivunia lugha ya Kiswahili kwa kutuunganisha! Hapo ndipo ninapochukua fursa hii katika kauli ya leo kumtaja kwa heshima na taadhima hayati Rais Dkt John Pombe Magufuli kwamba alisimama kidete bila kutetereka kuitetea lugha ya Kiswahili nchini Tanzania kila mahali na kila siku wakati wote wa uongozi wake hadi mauti yalipochukua roho yake iliyopenda Kiswahili kupeleka mapumzikoni mbele ya Mwenyezi Mungu!

Wakati tunapomwombea Rais mpendwa wetu Dkt John Pombe Magufuli Mwenyezi Mungu kuilaza roho yake mahali pema peponi, tumpongeze kwa dhati kwa jukumu kubwa na uzalendo wake wa kukitukuza, kukikuza na kukitumia Kiswahili katika hotuba na hafla zake zote za uongozi, kisiasa, kiuchumi, kitaifa na kimataifa! Rais mpenda watu na nchi yake, mzalendo mchapakazi, John Joseph Pombe Magufuli ametuachia mfano mwema sana ambao endapo hatukuiga alipokuwa hai, tuige sasa na tuendeleze mikakati na harakati za kumheshimu na kumuenzi daima Mwana huyu wa Afrika, mzalendo ambaye hakuyumbishwa wala kubabaishwa na kasumba za kikoloni! Tumpe heko kwa juhudi zake za kuipenyeza lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Angola, Botswana, Ethiopia na kwenye Muungano wa nchi za Afrika Kusini. Buriani mtetezi wa Kiswahili, Rais John Joseph Magufuli! Mola ailaze roho yako mahali pema pa watu wema peponi! Amina!!

Ndugu wapenzi, watu waliotenda matendo mema duniani wanapoondoka, matendo yao mema hudumu daima katika nyoyo za walio hai! Nasi tuyakumbuke mawazo mema ya kiongozi huyu ya kukikuza Kiswahili! Aidha, tuwapongeze zaidi wadau wa Kiswahili waliowahi kumtuza Rais John Magufuli tuzo adhimu ya Kiswahili katika Kongamano lililoandaliwa Chuo Kikuu cha Dodoma mwanzo wa mwaka huu.

Ni matumaini yangu kwamba Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan atakitetea na kukiendeleza Kiswahili kama hayati Rais John Magufuli! Ninavyomjua Mama Samia Suluhu pia mzalendo kindakindaki mpenda Kiswahili. Mliohudhuria Kongamano la BAKIZA mwaka 2018 katika ukumbi wa Abdul Wakil, Zanzibar, bila shaka mnakumbuka nilimtuza medali ya dhahabu ya Tuzo za Wasta kwa Ufasaha na Umilisi wa Kiswahili.

Wakati tunapomhimiza Mama Samia afuate nyayo za kukitukuza Kiswahili, kwa majonzi na simanzi tunasema, buriani Rais mpendwa Dkt John Magufuli mtetezi wa Kiswahili!!!!

WALLAH BIN WALLAH: Tumia Kiswahili kujinyanyua kimaisha, usilaze damu aisee!

NA WALLAH BIN WALLAH

KILA kitu kinatafutwa papa hapa duniani. Ukikosa kukipata unachokitaka, usiseme hakipo au hakipatikani ama kimekosekana! Aliyekosa kukipata ni wewe!

Au labda unacho lakini hujui kukitumia kikuletee faida! Kauli hiyo inanikumbusha hotuba na nasaha zilizotolewa katika Kongamano la Kiswahili lililoandaliwa na Mkurugenzi wa Nurisha Africa, Mwalimu Titus Sakwa kwa udhamini wa Shirika la Uchapishaji Vitabu la East African Educational Publishers; kwa hisani ya Meneja Mchapishaji, Ndugu Job Mokaya, jijini Nairobi siku ya Jumamosi tarehe 13, Machi 2021.

Kongamano hilo babu kubwa lilihudhuriwa na wapenzi wa Kiswahili kutoka janibu zote za Kenya. Baadhi ya mabingwa wa Kiswahili waliohudhuria ni Balozi Arthur Andambi, Mwalimu Yassin kutoka Garissa, Mwalimu K.M. Anduvate, Estrada Bin Estrada kutoka Kwale, Yusufu Sultane kutoka Kajiado, Eric Muteti wa Nairobi na wengineo.

Walumbi wakuu waliohutubia kutoa wasia na nasaha kwa waungwana wasikivu ni Dada Zubeda Koome, Ndugu Nuhu Bahari, Ndugu Hassan mwana wa Ali, Dkt Hamisi Babusa, Ndugu Job Mokaya, Mwalimu Abubakar Tsalwa, Mwalimu Titus Sakwa, Balozi Arthur Andambi, Mwalimu Wallah Bin Wallah na wengineo.

Katika ukumbi nadhifu uliopambwa ukapambika, wapenzi wa Kiswahili waliovaa nyuso changamfu zilizovishwa vitamvua au barakoa za kudhibiti virusi vya korona, awali walikaribishwa kwa burudani za mashairi na maonyesho anuai yaliyofuatiwa na kuzinduliwa rasmi vitabu viwili ambavyo ni Malenga wa Ziwa Kuu , kitabu chenye mashairi mazuri yasiyo kifani kilichoandikwa na Wallah Bin Wallah miaka mingi iliyopita.

Katika diwani hiyo Malenga wa Ziwa Kuu ndimo utakamopata mashairi kama yale: Kilio si Dawa , Nimpe Mama Zawàdi Gani ?, Kiswahili Nairobi , Kufu ya Umalenga pamoja na shairi lake lile maarufu Kiswahili Kitukuzwe alilolitunga alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha pili. Kitabu kingine kilichozinduliwa ni Picha ya Karne kilichoandikwa na Hassan mwana wa Ali.

Wawasilishaji wakuu walipokuwa wakitoa nasaha waliwahimiza na kuwakumbusha wasikilizaji wazingatie kwamba Kiswahili ni bidhaa adhimu sana inayostahili na kustahiki kuuzwa ghali zaidi. Ndugu Nuhu Bahari aliwatanabahisha wapenzi wa Kiswahili kwamba “Lugha ya Kiswahili ni utajiri, ni pesa, ni ajira, ni bidhaa adhimu na adimu kama dhahabu!

Anzeni leo kubidhaisha Kiswahili kwa kuandika makala, mashairi na vitabu mkauze! Fanyeni tafsiri na ukalimani! Tazameni wataalam ambao wameajiriwa kama vile walimu wa Kiswahili, watangazaji, wahariri na waandishi wa habari, wanalipwa pesa lukuki kwa sababu ya Kiswahili!”

Ndugu wapenzi, tumia Kiswahili upate pesa! Ukishindwa usiseme pesa hakuna! Kiswahili ni bidhaa ya kuleta pesa! Ukikosa kutumia Kiswahili umejikosesha wewe mwenyewe kupata pesa, usiseme zimekosekana! Uza Kiswahili upate pesa!!!!!

KINA CHA FIKRA: Kujiamini kama kiambata cha ufanisi maishani

Na WALLAH BIN WALLAH

WATU wengi wana uwezo wa kuyatenda mambo mazuri makubwa maishani lakini wanashindwa kwa sababu hawajiamini!

Wanadhania ati wangekuwa kama akina fulani fulani ndipo wangeyatenda matendo mazuri makubwa yenye sifa na faida mzomzo ulimwenguni!

Leo nikwambie hivi: Wewe ni wewe! Usiogope kuwa wewe! Mwenyezi Mungu alikuumba hivyo ulivyo kwa uwezo wake akakupa akili, ubora na umuhimu wako maishani!

Ukijiamini utajifanyia mambo yako yote na shughuli zako zote vizuri zaidi mpaka ufanikiwe bila ya kungojea uwe fulani au uwe kama fulani! Wewe ni wewe! Amua unachotaka na unavyotaka kuwa kwa kujiamini kwamba una uwezo! Kujiamini ndiko kutekeleza wajibu!

Mtu anapojiamini huongeza ujasiri moyoni na busara kichwani. Mfano mzuri ni wa kijana mdogo Daudi mwana wa Yesse ambaye alimshinda Goliati kwa sababu ya kujiamini na kuamini kwamba alikuwa na uwezo wa kumpiga Goliati na kumwangusha chini licha ya ukubwa wake, unene wake na urefu wake! Daudi aliamini kwamba katika mapambano usijione kwamba u mdogo! Usijidunishe na kusema ati lazima uwe jitu kubwa ndipo ushindane upate ushindi!

Katika mapambano binadamu anahitaji imani na uwezo wa akili za kupambana wala si ukubwa wa mwili na kifua kipana cha kupambana. Ukijiamini kwamba unaweza lazima utaweza! Katika imani na kujiamini kwako pia uongezee nia ya matendo ili utende kwa vitendo! Lakini kujiamini kunampa mtu msukumo, ari, ghera, motisha, kichocheo na hamasa za kutaka kuendelea kutekeleza wajibu hadi ufanikiwe! Usiwe na unyonge wa kukata tamaa! Usikubali kushindwa kabla ya kujitahidi kujaribu! Jiamini!!

Mtu anayefanya kazi kwa kujiamini siku zote kazi zake huwa njema na zenye mafanikio mazuri zaidi! Mti mwema ndio uzaao matunda mema!

Vivyo hivyo, mwanafunzi anayesoma kwa kujiamini kwa nia moja, hupata mafanikio na matokeo bora zaidi! Na siyo matokeo pekee katika mtihani, bali kuelewa kwake huwa imara na kwa kiwango cha juu sana! Kwa mfano sasa hivi tumo katika msimu wa mtihani.

Wewe mwanafunzi unapaswa kuwa na imani na kujiamini kwamba umekuwa shuleni muda wote huo ukisoma, walimu wapo, vitabu vipo, afya unayo na akili unazo kichwani! Kwa hivyo mtihani utakapoletwa, uyasome maswali uyaelewe kisha ujibu kila swali kulingana na jinsi ulivyoulizwa! Toa jibu linalotakikana linalowiana na swali! Usijibu unavyofikiria wewe! Ujiamini!

Ndugu wapenzi, leo namalizia kina cha fikra kwa kunukuu kwamba, “Katika mashindano ya mbio za masafa marefu dhidi ya Kobe na Sungura, Kobe alimshinda Sungura kwa kujiamini tu wala siyo kwamba alikuwa na mbio sana!” Amua! Ukijiamini utapata ushindi na mafanikio bora maishani! Jiamini!!!!

KINA CHA FIKIRA: Uzuri na ubaya wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe!

Na WALLAH BIN WALLAH

SIFA za upole na ujeuri zimefichamana ndani ya mtu!

Hazionekani mpaka zichokorwe na kuchokozwa ndipo zilipuke kama bomu au guruneti lililokanyagwa njiani! Kila mwanadamu ana ubora na unyonge wake. Ana wema wake na chembechembe za uovu wake ndani kwa ndani! Lakini wema na uzuri hupaliliwa na kukuzwa ili mtu awe bora kabisa! Aidha ubaya au uovu na ujeuri hudekezwa mpaka mtu akawa mjeuri sugu wa kuwaogofya wengine! Ni wajibu wetu sisi sote katika jamii kutoa miongozo ya kuwalea watoto wetu huku tukijiuliza, “Tunawaelekeza upande wa kuwa waovu au waadilifu?”

Mageugeu alikuwa kijana mdogo mwanafunzi wa gredi ya nne katika shule ya Kijiweni. Alijulikana kwa ujeuri wake tu! Wanafunzi wenzake walimkemea kila mara, “Wewe Mageugeu u mjeuri mno!” Walimu nao walimshutumu, “Wewe mtoto mbaya sana! Badilika uwe mwema na mpole! Uwe mtoto mzuri!” Lawama zote hizo zilimkera Mageugeu moyoni! Kila jioni alirudi nyumbani ameudhika na kununa! Mama yake aliona tabia hiyo siku nyingi. Jumamosi moja, alimwambia mwanawe, “Wewe Mageugeu una roho mbaya sana! Wewe mtoto mbaya zaidi! Huna furaha wala husemi na wenzako! Tabia mbaya hii umetoa wapi?”

Mageugeu alimjibu mama kwa hasira, “Watu hawanitaki wala hawanipendi! Shuleni kila mtu ananiita mtoto mbaya! Tena nyumbani hapa mamangu unaniita mtoto mbaya!? Basi mimi sina hamu ya kuishi! Heri nikajinyonge!!” Akachukua kamba akaenda kwenye mabonde ya milima ya kwao! Akalia kwa kelele, “Mimi mbaya!! Mimi mbaya aa!!” Alishtuka aliposikia sauti kubwa ikisema kutoka milimani, “Mi-mi mba-mbaya!!” Mi-mi mba-mbayaa-aa-aa!!” Mageugeu alitoka mbio na kamba mkononi kurudi nyumbani kumwomba mama msamaha! Akasema, “Mama unisamehe! Leo nimeamini mimi mbaya! Milima na watu wote wa mabonde huko wamesema kwa sauti, “Mimi mbaya!!” Kumbe siyo chuki! Mimi ni mbaya kweli! Sasa naenda kujinyonga kwa sababu ya ubaya wangu! Nimemsamehe kila mtu!”

Mama alijua kwamba Mageugeu alisikia mwangwi! Akamshauri kwa upole, “Kabla hujajinyonga huko, uende upige kelele useme, “Mimi mzuriiiiiiiiiii!!” Mageugeu alifika mabondeni akapiga kelele, “Mimi mzuriiiiiiiiiii!!!” Sauti ilirejelea, “Mimi mzuriiiiiiiiiii iii iii!!!” Alishangaa akarudi nyumbani kumwambia mama, “Sasa wamesema mimi mzuri!” Mama alimjibu, “Naam, mwanangu, umekuwa mzuri! Watu wa milimani wamekubali wewe mzuri! Na uwe mzuri sana kuanzia leo! Usiwe mbaya tena!”

Ndugu wapenzi, Mageugeu alibadilika akawa mtoto mwema sana! Uzuri na ubaya wa mtu umo ndani ya mtu! Ukikubali kuwa mwema utakuwa mwema tu! Uamuzi ni wako!!!!

KINA CHA FIKIRA: Ukijiamini kwa lolote utafanikiwa hivyo hivyo ulivyo

Na WALLAH BIN WALLAH

MAFANIKIO hupatikana kwa bidii pamoja na jinsi mtu anavyojiamini katika shughuli au kazi anazofanya maishani.

Usidhani mtu hufanikiwa au hufaulu kwa kuwa ameumbwa tofauti ama anavyo viungomwili vya ziada kuliko wewe!

Usidhani mwenzako ana vichwa viwili, mikono mitano, macho sita, masikio manne ama miguu zaidi ya miwili! La hasha! Wengine ni wadogo, wembamba na wafupi zaidi yako! Lakini wanafanya mambo makubwa, matendo bora na kazi njema zaidi kwa kujiamini na kuamini kwamba hakuna kisichowezekana kwa mtu mwenye nia anayejituma!

Kijana mdogo aitwaye Karatasi alipokuwa na umri wa miaka kumi, aliamua kujifunza michezo ya judo na karate. Lakini balaa ilitokea! Kijana Karatasi alipata ajali kwenye gari. Mkono wake wa kushoto ulivunjika kenyekenye!

Alipolazwa hospitalini, madaktari waliamua kuukata. Karatasi akabaki na mkono mmoja tu wa kulia! Ajali ilimkata mkono lakini haikumkatisha tamaa ya kujifunza karate na judo! Baada ya kutoka hospitalini alipopona kabisa, alienda kwa Mwalimu wa judo na karate akamwambia, “Mwalimu, nimekuja unifundishe!” Mwalimu Yaimoto alimtazama na kumchuja kwa macho ya maswali. Akajibu, “Sawa Karatasi! Nitakufundisha! Tuanze lini?”

Karatasi alimwambia Mwalimu, “Ninaomba tuanze kesho ili leo nikanunue sare pamoja na vifaa vinavyohitajika!” Kesho yake Karatasi alienda kuanza kujifunza baada ya kulipia ada! Alianzia mafunzo ya judo. Kwa muda wa miezi mitatu aligundua kuwa Mwalimu alikuwa akimfunza mtindo mmoja tu wa kuutumia mkono wake mmoja wa kulia pamoja na miguu. Alielewa kuutumia na kujikinga vizuri zaidi.

Walipofanya mazoezi na majaribio ya kupigana na Mwalimu wake, Mwalimu alitokwa jasho! Siku moja Karatasi alimuuliza Mwalimu wake, “Mbona unanifunza mtindo mmoja tu wa kupambana na kujihami?” Mwalimu Yaimoto alimjibu, “Heri mtu anayejua mbinu moja anayoamini na kujiamini kwamba anaweza kuitumia vizuri kuliko ajuaye mambo mengi yasiyomsaidia! Muhimu ni kujiamini!”

Baada ya siku kadhaa Karatasi alihitimu kozi za judo na karate. Mwalimu Yaimoto alimpeleka kwenye mashindano makubwa ya kitaifa katika ukumbi Mkuu jijini Kumbuko. Zamu yake ilipofika na akapanda jukwaani, kila mtu alishtuka kumwona kijana mdogo mwenye mkono mmoja akirukaruka jukwaani kusubiri kipenga apambane na Nyundonyundo; jitu la miraba minne kwenye karate!

Refarii alipopuliza kipenga, Karatasi alimrarua mpinzani wake Nyundonyundo kwa kutumia mkono mmoja na mateke! Akamwangusha chini mara nyingi bila kumpa nafasi! Kwenye dakika tano za kwanza, Nyundonyundo alianguka chini tena akashindwa kunyanyuka! Refarii akatangaza, “Mchezo umekwisha!” Karatasi alishinda kwa kishindo!!

Ndugu wapenzi, mtu akijiamini katika kutenda mambo au kazi ama shughuli zake vizuri, atafaulu hivyo hivyo alivyo! Tujiamini!!!!

WALLAH BIN WALLAH: Usitumie nguvu za kifua unapofanya kazi, ni akili tu!

NA WALLAH BIN WALLAH

KATIKA maisha ukitumia akili kidogo tu vizuri utafanya kazi kubwa vizuri bila kuchoka wala kuumia. Lakini ukitumia nguvu nyingi za kifua bila kutumia akili wakati unapofanya kazi, utachoka, utaumia na kutokwa jasho chapachapa bila kufanikiwa!

Nguvu pekee za kifua hazitoshi kuleta mafanikio katika kila kazi! Kufanya kazi si vita! Lakini hata vita huhitaji akili za kukabiliana na adui! Mafanikio katika utendakazi huhitaji akili na umakinifu zaidi kuliko nguvu nyingi zinazotokana na ugali!

Kila mtu anamjua ndama mtoto wa ng’ombe. Ana ujeuri na kiburi si haba! Akiamua kusumbua wakati akishalala juani, humwamshi, humbebi wala humtikisi atikisike!

Huyo ndiye ndama kwa wanaomjua ndama kuandamana na tabia za ndama!Bwana Tutufe alimtuma mwanawe mvulana aitwaye Tuletule aende akamlete ndama wao aliyelala njiani kwenye jua umbali wa mita mia tatu kutoka nyumbani.

Tuletule kijana wa kidato cha tatu alienda kifua mbele mpaka alikolala ndama! Akajaribu kwa uwezo wake wote kumwamsha ndama lakini ndama hakunyanyuka!

Alijitahidi kwa nguvu zake zote lakini ndama alijipweteka pwetepwete bila kunyanyuka angalau sentimita moja! Alijaribu kumbeba lakini ndama hakubebeka kutokana na uzito wake! Tuletule alitokwa jasho na kuishiwa nguvu!

Alirudi nyumbani akamwambia baba yake, ‘Nimeshindwa kumleta ndama nyumbani!’Bwana Tutufe alimwambia Tuletule, ‘Unakula kama ndovu lakini huna nguvu za kumleta ndama tu nyumbani kutoka juani!!? Twende tukamlete!’ Walipofika mahali alipolala ndama, walijitahidi kumnyanyua lakini ndama alikatalia chini!

Wakaamua kutumia nguvu nyingi zaidi! Baba akamkamata ndama kwa masikio yake amvute. Naye mwana Tuletule amsukume ndama nyuma kwa nguvu zake zote! Walipojaribu hivyo ikawa kazi ngumu zaidi! Waligundua kwamba ndama alikuwa akiumia sana! Alianza kutoa sauti ya kutisha na kukoroma kana kwamba alikaribia kufa!

Walimwachilia alale chini! Wakasimama kumtazama tu huku jasho likiwatiririka baba na mwana!!Mara alifika msichana mdogo aliyetoka sokoni na kikapu chake mgongoni, jina lake Esha!

Baada ya salamu, Esha aliwauliza Baba na Mwana, ‘Ndama ana shida gani?’ Walimjibu juu juu, ‘Amekataa kuenda nyumbani!’ Esha akaomba, ‘Niwasaidie?’ Hawakumjibu, lakini Esha alimkaribia ndama akaweka kidole chake kwenye mdomo wa ndama yule!

Ndama alitoa ulimi akaramba kidole cha Esha! Akanyanyuka na kuanza safari akimfuata Esha unyounyo huku akimramba kidole mpaka nyumbani!!Ndugu wapenzi, tusidhani kazi zote lazima zifanywe kwa kutumia nguvu za kifua tu!

Ukitumia nguvu nyingi bila akili utaumia lakini kazi haitafanyika! Lakini ukitumia akili kidogo tu utafanya kazi kubwa kuliko kutumia nguvu nyingi uchoke bure!!!!

KAULI YA WALLAH: Jogoo mwoga aghalabu huwa ndiye mfalme

NA WALLAH BIN WALLAH

WAHENGA walisema kwa mwoga huenda kicheko kwa shujaa huenda kilio. Ukweli ni kwamba waoga hufa mara nyingi sana maishani kabla hawajafa kifo cha kweli!

Lakini wanaishi miaka mingi zaidi kabla hawajafa kweli! Shujaa hufa mara moja tu! Kifo cha shujaa hutokea haraka zaidi ndiyo maana mashujaa hawana maisha marefu. Kinachobakia cha kujivunia kwa shujaa ni kwamba huwa amekufa kishujaa! Lakini kifo ni kifo tu, hakuna kifo kitamu!

Licha ya hayo, ni bora kuwa mwoga, mpole na mnyenyekevu wa kupiga magoti chini kuliko kujitutumua na kujipiga kifua wakati mambo yanapokuwa moto!

Heri uwe kama nyasi usipigane na moto mkali nyikani. Tafadhali, okoa roho yako moja aliyokupa Mwenyezi Mungu kwa kuitunza vizuri isikutoke! Bora kuwa mwoga uishi kuliko kuwa shujaa uishe!Katika kijiji cha Kukupunda walikuwapo jogoo wawili waliopigania ufalme wa kutawala kijiji cha Kukupunda.

Kila jogoo alitaka kuwa mfalme wa kuwatawala kuku pamoja na vifaranga pale kijijini Kukupunda. Vita vikatokea kati ya Jogoo Mwekundu na Jogoo Kijivu! Vilikuwa vita vikali vya kuogofya! Jogoo Kijivu na Jogoo Mwekundu walipapurana kwa kucha na kudonoana kwa vidona vyao kwa hasira na hamaki!

Kuku wengine na vifaranga walitazama kwa wasiwasi kisirisiri tu!Jogoo Mwekundu ndiye aliyeonyesha ujeuri na ubabe zaidi. Jogoo Kijivu alimwambia Jogoo Mwekundu, ‘Tusipigane bure! Tutaumizana bure! Vita ni hasara, havina faida! Tusipigane!’

Hapo ndipo Jogoo Mwekundu alipochachamaa na kujipiga kifua zaidi akaongeza hasira kumshambulia Jogoo Kijivu! Akamparuza na kumdonoadonoa kichwani, machoni na kwenye undu!

Jogoo Kijivu akavuja damu kichwani! Aliogopa akakimbia kuingia katika nyumba kujificha chini ya kitanda! Jogoo Mwekundu alipoona mwenzake amekimbia, alijipapatua mbawa zake akawika kwa maringo kutangaza ushindi, ‘Mimi ndiye mfalme wa kuku wote kijijini Kukupunda!’

Alitaka dunia nzima ijue kwamba alishinda. Akapanda juu kabisa kwenye paa la nyumba akawika kwa nguvu, ‘Kokoikoooo!!! Nimeshindaaaa!! Mimi mfalme wenu kuanzia sasa hivi!!’

Jogoo Mwekundu alipokuwa kwenye paa akijisifu na kujitangazia ufalme, tai mkubwa aliyekuwa kwenye mti mbali mlimani, alikuja upesi kama umeme akamnyakua chwap!!! Akaenda naye kwa watoto wake kiotani wakamla Jogoo Mwekundu bila ya kujitetea!

Yule Jogoo Kijivu mwoga alitokeza polepole akatangazwa rasmi bila wasiwasi kuwa ndiye mfalme wa Kukupunda mpaka leo!Ndugu wapenzi, piga magoti usipige kifua! Waoga hufa mara nyingi, lakini wanaishi miaka mingi duniani. Jogoo mwoga ndiye hutokea kuwa mfalme!

Kwa mwoga huenda kicheko! Kuwa mnyenyekevu katika dunia hii ya Mungu!!!!!

KINA CHA FIKIRA: Jitahidi ule jasho lako, vya wengine vitakusakama

Na WALLAH BIN WALLAH

MAISHA si mteremko.

Ni safari ngumu kama kuukwea mlima! Lakini unavyozidi kuukwea mlima ndivyo unavyosonga zaidi juu kileleni. Lazima ujitahidi na uvumilie ndipo ufanikiwe! Maisha ni magumu na kuishi si rahisi. Unapaswa kuwa mgumu! Ukaze moyo na uutumikishe ubongo ufanye kazi. Akili inayofanya kazi hailali. Akili isiyolala ndiyo inayoleta mali tunu! Mali halali hupatikana kwa akili ambayo hailali. Usitafute mali haramu kwa njia ya mkato! Njia ya mkato ikikatika huyakata maisha yakaisha! Hivyo ndivyo Mzee Bongombili alivyomuusia mjukuu wake Tekemoja!

Miaka mingi baadaye tangu Mzee Bongombili alipoaga dunia, Tekemoja alikumbwa na njaa. Akachukua upanga kuenda msituni kukata kuni akauze kijijini apate pesa anunue chakula! Jua lilikuwa kali sana! Alipokuwa akikata kuni alisikia sauti dhaifu ikimwita, “Eee, kijana, njoo!” Alipotazama kushoto alimwona mzee mkongwe mwenye nywele timtimu za mvi! Alimsogelea akamsalimia kwa huruma, “Shikamoo babu?” Mzee aliitikia kwa unyonge, “Marahaba mjukuu wangu!” Kisha mzee akamwonyesha Tekemoja unyayo wake uliokuwa umedungwa na mwiba mkubwa! Tekemoja alishika mwiba akauvuta kuutoa! Mzee alihisi uchungu sana! Mwiba ulipotoka damu ilichirizika! Tekemoja alirarua kipande cha shati lake akalifunga jeraha kuzuia damu! Babu alipata nafuu akatamka, “Asante sana mjukuu wangu lakini nina njaa na kiu! Tangu mwiba huu uliponidunga siku tano sijala chochote!”

Tekemoja alitoa kibuyu cha maji na vipande vya muhogo uliochemshwa kutoka katika mkoba wake akampa mzee akala akanywa maji! Babu alipata uhai upya! Akamwambia Tekemoja, “Hali ni ngumu na maisha ni magumu sana! Lakini binadamu asikate tamaa wala asitafute kuishi kwa kutumia njia haramu! Na muhimu zaidi ni kwamba, heri kuwe na ukame wa mazingira badala ya ukame wa wema, utu na uadilifu! Kumbuka, wema hauozi!” Baada ya kusema hivyo, Babu alimwonyesha Tekemoja ng’ombe aliyefungwa kwa kamba kwenye shina la mti kando. Akasema, “Umchukue ng’ombe yule! Utakuwa ukimkama kila siku upate maziwa mengi ya kunywa na kuuza! Lakini mwiko ni kwamba, wewe au mtu yeyote asipitie upande wa nyuma ya ng’ombe huyo!” Mzee akatoweka!

Tangu siku hiyo Tekemoja akawa muuzaji maarufu wa maziwa akapata pesa nyingi! Lakini usiku mmoja wezi walikuja wakamwiba ng’ombe wake! Alipoamka asubuhi alisikitika sana. Kumbe waliomwibia ng’ombe walikuwa rafiki zake wakubwa, Seko na Sako! Huko Sako alipopita nyuma ya ng’ombe ili amkame alipigwa teke mdomoni akang’olewa meno kumi! Seko alipojaribu kumwinua Sako amtoe nyuma ya ng’ombe, alipigwa teke kichwani akafa pale pale!

Ndugu wapenzi, hata kama maisha ni magumu, lakini ujitahidi ule jasho lako! Usithubutu kupora mali ya wengine!

wallahbinwallah@gmail.com

KINA CHA FIKIRA: Ishi ukienda mbele badala ya kurudi nyuma!

Na WALLAH BIN WALLAH

MAISHA ni safari ya kuenda mbele moja kwa moja mpaka mwisho!

Kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake wakati huu anapoishi. Mwanafunzi anaposoma shuleni asiwe mzembe wala asiwe mtoro wa kutoroka kutoka shuleni kuacha masomo! Baada ya kuzeeka hatarudi shuleni kusoma tena! Kila kitu kina wakati wake. Chochote unachostahili kufanya leo usingojee kesho.

Tafadhali, mtu yeyote au mfanyakazi yeyote asiwe mvivu! Afanye kazi zake vizuri kwa wakati unaofaa ili maendeleo na mafanikio yapatikane! Ni vyema kutimiza wajibu bila ya kutarajia ati siku moja miaka itarudi nyuma upate muda mwingine wa kufanya shughuli ambazo hukuzifanya miaka iliyopita! Maisha ni kama maji ya mto yanayoelekea baharini. Hayarudi nyuma kamwe! Yanayowezekana uyatende leo!

Bwana Tupatupa mwenye umri wa miaka sitini alipatwa na ugonjwa wa kiharusi ghafla! Viungo vya mwili wake vikapooza na kukosa nguvu kabisa! Alipelekwa hospitalini akalazwa akiwa mahututi si hayati si mamati! Kila mtu alikata tamaa na kusema, “Huyu hatapona!”

Baada ya siku kadhaa, usiku mmoja Tupatupa aliota ndoto kuwa punde angekata roho! Akaomba ndotoni, “Mungu wangu, mimi ninaaga dunia na kuwaacha wanangu bila chochote! Sikujitahidi kufanya kazi yoyote ya kuwaletea maendeleo wala mafanikio ya kuwasaidia maishani! Sasa wanabaki katika shida!!!”

Mara Tupatupa akasikia Mungu au Malaika akimwambia, “Tupatupa, hufi leo! Una miaka mingine arubaini ya kuishi duniani!” Maneno hayo yalimpa nguvu akapata fahamu akawa mzima tena! Asubuhi daktari alimpata Tupatupa akiwa amepona kabisa! Lakini moyoni alibeba siri ya kuishi miaka arubaini zaidi. Aliamini maana yake ni kurudi kuanza maisha upya ili aende akafanye kazi na majukumu ambayo hakutimiza alipokuwa kijana!

Daktari alipomhakikishia Tupatupa kuwa alipona arudi nyumbani, Tupatupa alimwomba amtume nesi wake aende akamnunulie mavazi ya vijana, suruali ya kuteremsha, shati, kofia ya chepeo, miwani ya jua na viatu vya kisasa vya ujana avae aonekane kijana anapotaka hospitalini akienda nyumbani! Tupatupa aliacha mavazi na kila kitu cha kizee hospitalini! Alitembea kwa makeke na mikogo kama kijana huku bega moja ameliinamisha chini! Alipokuwa akivuka barabara, gari la ambulensi lilimgonga akakata roho pale pale! Tupatupa alipofika mbele ya kiti cha enzi alilalamika, “Mungu wangu, uliniambia ningeishi miaka mingine arubaini! Kulikoni?” Mwenyezi Mungu akamjibu akilini, “Samahani, Malaika wangu wanaokulinda hawakukutambua kwa jinsi ulivyojibadilisha!”

Ndugu wapenzi, maisha hayarudi nyuma hata ukifanya nini! Tekeleza wajibu na majukumu yako leo leo! Liishalo haliji tena!!!

KINA CHA FIKIRA: Shirikiana na watu bora ili nawe uwe bora, visivyo utasalia bure tu!

NA WALLAH BIN WALLAH

KATIKA maisha ubora hutafutwa kwa hali na mali. Lazima ukae na watu walio bora mahali palipo na ubora ndipo ujifunze ubora ili uwe bora! Ubora ni ghali wala haupatikani bure bure bila ya kujituma na kujitahidi mpaka uzipate mbinu zitakazokusaidia kuwa bora!

Kwa mfano, ukitaka kujifunza elimu au maarifa fulani, unapaswa kukaa na wenye elimu hiyo na maarifa unayoyataka ili ujifunze au wakufunze uwe mtaalam mwenye ubora kama wao.

Huwezi kuwa mchezaji bora wa kandanda bila ya kushirikiana na wachezaji walio bora kufanya mazoezi pamoja uwanjani. Ni vigumu kuwa mkulima hodari bila ya kuenda shambani pamoja na wakulima wanaojua hali ya anga na mimea mbalimbali.Ukitaka kuwa mvuvi lazima ujue mazingira ya majini pamoja na tabia za samaki wote ukielekezwa na wavuvi wakongwe.

Kujifunza ndiko kuelewa mambo. Nako kujifunza ni kutafuta ubora kama unavyojifunza ujenzi, hisabati, sayansi, ufasaha wa lugha, uandishi wa habari na mengineyo kutoka kwa wataalam wenye ubora wakusaidie kuwa bora!

Vivyo hivyo, ukitaka kuupoteza ubora wako, enda ushirikiane na watu ambao hawana ubora wowote! Baada ya muda, utakuwa kama hao hao! Ujifunze kila wakati ili ujiboreshe kila siku.

Kinolewacho hupata! Na kikipata hukata!Bwana Tuishi alienda kutembea msituni. Akaona kiota cha ndege aitwaye tai. Kiota hicho kilikuwa na mayai! Tai ni ndege mwenye macho makali yanayoona mbali sana.

Tai ana nguvu nyingi, kidona kikali na kucha zenye ncha kali za kumrarua mnyama yeyote akaliwa nyama! Aidha tai ana mbio zaidi za kupaa angani kuenda masafa marefu!Bwana Tuishi alilichukua yai moja katika kiota cha tai akapeleka nyumbani na kuliweka pamoja na mayai ya kuku wake aliyekuwa akiyaatamia mayai kwenye oto!

Baada ya siku kadhaa, kuku wa Bwana Tuishi aliyaangua mayai yote pamoja na lile la tai! Vitoto vyote vya kuku na cha tai vilikua pamoja na kutembea pamoja vikidonoa punje za nafaka na vijitakataka vingine ardhini!Kwa hakika, Bwana Tuishi alitarajia kuona kwamba kitoto cha tai kingeruka angani siku moja kama tai wengine aende zake, lakini wapi!!

Kilitembea kufuatana na vifaranga mpaka vifaranga vilipokuwa kuku wakubwa! Naye tai akawa mkubwa lakini hakuruka kabisa angani! Aliupoteza ubora wake wa kawaida ya tai kupaa angani kwa sababu aliishi na kuku wasiopaa angani!Ndugu wapenzi, usipojitambua mapema, utaupoteza ubora wako wakati wa kushirikiana na watu ambao hawana ubora unaoutamani wewe na unaopaswa kuwa nao maishani!!!

wallahbinwallah@gmail.com

KINA CHA FIKIRA: Tumia ubora ulio nao kufanyia kazi bora ili ufanikiwe

Na WALLAH BIN WALLAH

BINADAMU ana ubora wa kipekee.

Hawezi kupaa angani kama ndege wanaotumia mbawa zao kupaa angani. Lakini binadamu ana akili na ujuzi wa kutengeneza vyombo vinavyomsaidia kupaa kuenda mbali zaidi ya ndege wanaotumia mbawa!

Binadamu hawezi kuogelea au kupiga mbizi ndani ya maji kama samaki wanaotumia mapezi kuogelea na matamvua ya kuvutia hewa majini. Lakini binadamu anatumia akili na ubora wake kuunda vyombo vinavyomsafirisha katika maji baharini, maziwani na mitoni.

Binadamu hana macho makali ya kuona mbali kama ndege waitwao mwewe, kipanga na tai. Lakini ana uwezo wa kutazama na kuona vitu au mambo yanayotokea pande zote duniani kwa kutumia vyombo bora alivyovivumbua kama vile runinga, darubini na darumbili!

Binadamu hana uwezo wa kukimbia kasi kama duma, farasi, sungura na swara ardhini. Lakini ameunda magari ya kila aina yanayomsafirisha kwa mwendo kasi nchi kavu.

Binadamu amefaulu kuyatenda yote hayo kwa sababu ana uwezo wa kufikiri, kuvumbua na kubuni mbinu bora zaidi za kuishi katika mazingira yake duniani.

Masikitiko ni kwamba watu wengine hawafanyi jitihada kuutumia ubora na uwezo waliojaliwa na Mwenyezi Mungu angalau kufanya kazi au shughuli zao kubwa au ndogo zikawa bora! Aidha wapo watu wanaokubali kushindwa hata kabla hawajajaribu! Kushindwa kufanikiwa na kufaulu kufanikiwa ni uamuzi wa mtu binafsi! Ni unyonge mkubwa kutarajia kupata kitu chochote bila ya kutafuta au bila ya kutia bidii kwa matarajio kwamba Mwenyezi Mungu ataleta kila kitu!

Katika kijiji cha Jikazeni, kando ya barabara kuu inayoelekea mjini, kulikuwako mashamba mawili ya mahindi yaliyopakana. Yote yalikuwa na ukubwa sawasawa wa ekari mbili. Lakini shamba moja lilikuwa na mahindi yaliyostawi vizuri zaidi. Shamba jingine lilikuwa na mahindi hafifu yaliyosinyaa na kunyaukanyauka!

Profesa Sifatupu alikuwa akiliendesha gari lake kuelekea mjini. Alipoyaona mashamba yale, alishtuka akaliegesha gari pembezoni ili ayatazame vizuri! Akasema, “Mashamba haya yamelimwa katika mazingira yanayofanana! Lakini Mungu amelibariki shamba hili moja likastawisha mahindi vizuri sana!”

Kumbe mwenye shamba zuri, Bwana Mtukazi alikuwa shambani akilinda ndege wasimharibie mahindi! Alipoyasikia maneno ya Profesa Sifatupu, alitokeza akasema, “Naam! Ninakubali Mwenyezi Mungu amelibariki shamba langu! Ninashukuru! Lakini ujue kwamba nililima mapema, nikapanda mbegu vizuri, nikaweka mbolea na kupalilia vizuri! Angalia, wakati huu nipo hapa nikiwafukuza ndege wasile mahindi yangu!

Ndugu wapenzi, ukifanya kazi yako vizuri na kuitunza vyema, bila shaka Mwenyezi Mungu ataleta baraka!

wallahbinwallah@gmail.com

WALLAH: Umoja huwa nguvu imara kuliko nguvu za kutumia kifua

NA WALLAH BIN WALLAH

MAHALI palipo na umoja pana amani. Na palipo na amani pana nguvu na maendeleo. Umoja ndio nguvu imara kuliko nguvu za kutumia kifua na silaha.

Wanyamapori wanayamudu maisha yao ya kuishi porini kutokana na umoja wao. Wao hutembea pamoja na kutafuta malisho kwa makundi! Adui anapokuja kuwavamia, wanyama wote hukimbia pamoja kuelekea upande mmoja. Mwenzao anayejitenga kukimbia peke yake kuelekea upande tofauti ndiye huandamwa na adui hatimaye hukamatwa kwa urahisi!

Sisi binadamu na akili zetu alizotujalia Mwenyezi Mungu, tuna umoja kweli? Tunatumia nguvu nyingi za vifua ambazo wakati mwingine hazitusaidii kujilinda adui anapokuja! Kwani hatujui kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu?

Siku moja nilimsikia Mzee Pepeta akisema kwamba, “Kila mtu anajua njia lakini wote hawafuati njia!” Sasa kuna faida gani kujua njia iliyo salama bila ya kuifuata ili uende penye usalama? Kuna mantiki gani wanadamu kujua kwamba umoja ni nguvu kisha waendelee kuishi kwa kutengana kama ardhi na mbingu?

Mzee Pepeta alikuwa na watoto sita. Wasichana watatu na wavulana. Wote walisoma wakahitimu vizuri sana katika masomo yao.

Pamoja na elimu yao nzuri, kila mara Mzee Pepeta aliwakumbusha watoto wake kuishi kwa umoja na amani bila wivu wala chuki. Aliwahimiza washirikiane na kushikamana kama jembe na mpini! Alisema, “Wanangu, palipo na umoja pana amani na upendo! Umoja una nguvu kama ukuta wa zege ambao haubomoki kwa urahisi!” Mzee Pepeta alitoa nasaha!

Hatimaye Mzee Pepeta alipohisi kuwa siku zake za kuishi duniani zakaribia ukingoni, aliwaita wanawe wote sita katika ukumbi wa nyumba yake.

Baada ya salamu za heshima kwa baba yao, watoto waliketi! Mzee Pepeta alifungua shubaka akatoa vijiti sita vyembamba vilivyofungwa pamoja vyenye urefu wa sentimita ishirini hivi! Akawaambia watoto hao, “Kila mmoja ajaribu kuvunja vijiti hivyo vikiwa pamoja!” Kila mtoto alijaribu kwa nguvu zake zote lakini hakuna aliyeweza kuvivunja vijiti sita vilivyofungwa pamoja!

Mzee alivifungua vijiti vile akampa kila mtoto kijiti chake akishike mikononi! Akawaambia, “Sasa kila mmoja akivunje kijiti chake!” Kila mtoto alikivunja kijiti chake kimoja kwa urahisi na wepesi kama mchezo tu! Mzee Pepeta akawaambia wanawe, “Naam, hiyo ndiyo siri ya umoja na udhaifu wa utengano! Nyinyi pia wakati mtakapotengana, walimwengu watawavunja haraka sana kama mabua ya mahindi!” Umoja ndio nguvu za kweli kuliko nguvu za kutumia kifua!” Wazalendo wote tushikane tuwe na umoja katika nchi yetu bila kutengana! Umoja ndio nguvu!!!

KINA CHA FIKIRA: Ukiogopa kuvumilia kubeba mzigo wa mateso utateseka zaidi

Na WALLAH BIN WALLAH

UVUMILIVU huleta mafanikio katika maisha.

Mtu anayevumilia kufanya kazi kwa bidii huyavuna matunda ya uvumilivu wake.

Lakini mtu wa kukaa bure anayeogopa kufanya kazi, hujisababishia njaa, mateso na majuto maishani!

Ukiogopa kuvumilia kufanya kazi, utateseka zaidi!

Vijana watatu, Peto, Pote na Pato waliishi katika kijiji cha Walavyote. Ukame ulitokea kijijini hapo baada ya mvua kuacha kunyesha kwa muda mrefu. Mimea yote ilikauka mashambani. Chakula kiliadimika kabisa! Watu waliteseka kwa njaa! Hapo ndipo vijana hao watatu walipoamua kuondoka asubuhi kuenda kutafuta angalau matunda msituni walete wakale na jamaa zao.

Kila mmoja alibeba mkoba wake na chupa ya maji ya kunywa! Walitembea kwa muda mrefu wakafika katika msitu ulioitwa Nguvukwisha saa sita na nusu adhuhuri. Jua lilikuwa la kuchoma kama pasi! Walichoka sana kwa njaa! Msitu wote ulikuwa mkavu! Hawakuona dalili yoyote ya matunda kwenye miti iliyokauka msituni!! Walikataa taa! Wakaamua kurudi kijijini kwao Walavyote. Lakini kabla ya kuanza safari ya kurudi, waliketi chini kupumzika kidogo.

Mara walisikia sauti kutoka hewani ikisema,”Vijana rudini nyumbani! Msitu huu si salama sana! Lakini msirudi mikono mitupu hivyo! Kila mtu achukue mawe hayo mnayoyaona hapo chini abebe kadri ya uwezo wake apeleke nyumbani!” Sauti ilirudia, “Chukueni mawe myapeleke nyumbani!” Walishangaa!

Peto na Pote waliyaokota mawe machache tu wakilalamika, “Jua kali hivi na njaa, halafu mtu ajibebeshe uzito wa mawe apeleke kijijini!?” Lakini Pato alichukua mawe mengi akajaza mkoba wake pamoja na mifuko ya suruali yake ya dangrizi (jeans). Alitembea kwa shida kuelekea nyumbani lakini alivumilia uzito!

Peto aliyatupa mawe yake njiani akabaki na jiwe moja tu! Naye Pote alifika nyumbani na mawe mawili tu! Kijana Pato alifika nyumbani akiwa na mawe mengi aliyoyajaza mkobani na katika mifuko ya suruali yake!

Waliwasili kijijini Walavyote jioni jua likizama. Kila mmoja alienda nyumbani kwao. Wazazi na ndugu waliwapokea kwa hamu ya kutaka kujua walikotoka na walileta nini? Kumbe walipofika nyumbani mawe yote yaligeuka yakawa matunda mazuri matamu sana! Peto aliyefika na jiwe moja, aliwaletea watu wake tunda moja tu zuri! Naye Pote aliyebeba mawe mawili, alileta matunda mawili mazuri! Pato aliyevumilia kuyabeba mawe mengi alileta nyumbani matunda mengi mazuri matamu ambayo waliyala kwa muda wa miezi mitatu mpaka mvua iliponyesha tena chakula kikapatikana mashambani!

Ndugu wapenzi, hivyo ndivyo maisha yalivyo. Mafanikio ni siri kubwa iliyofichwa ndani ya uvumilivu na kujituma kufanya kazi kwa bidii bila uzembe wala ugoigoi. Ukivumilia utafanikiwa! Lakini ukiogopa kuvumilia kuubeba mzigo wa mateso, utateseka zaidi katika dunia! Vumilia!!

KINA CHA FIKIRA: Bahati ina sifa ya kuteleza, ikienda hairudi tena!

Na WALLAH BIN WALLAH

BAHATI haibagui haichagui!

Bahati hutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mtu ana bahati yake. Lakini hakuna anayejua siku yake ya kuipata. Anayejua na kupanga siku ya kuteremsha bahati ni Mungu pekee! Ukiwa hujaipata bahati, tulia tu usubiri! Siku yako itafika! Mungu hana choyo!

Ingawa kila mtu ana bahati yake, lakini bahati ina siri zake. Kwanza, bahati haina ahadi wala haimwambii mtu siku ya kuja! Pili, bahati hailazimishwi ila huja tu siku yako ikifika! Tatu, bahati hupatikana mara moja tu! Ikija na ukaiachia iende, huwezi kuipata tena hata ukilia! Ukibahatika kuipata bahati, uitunze usiichezee! Na uitumie vizuri sana!

Bwana Papara aliingojea bahati yake kwa muda wa miaka mingi mpaka akakata tamaa! Akaanza kulalamika na kumlaumu Mungu akisema, “Eee! Mungu wangu! Mimi nimekosa nini? Mbona sipati bahati niwe na mali nyingi nitajirike kama watu wengine?!”

Alilia hivyo kwa miaka kumi! Halafu siku moja alipokuwa ameketi chini ya mti nyumbani kwake kwa huzuni, machozi yakimtoka machoni, mara alisikia sauti ikisema naye kutoka angani!

Bwana Papara alitega masikio akasikia sauti ikimwambia, “Bwana Papara umelia sana! Nyanyuka uende kule shambani kwako karibu na mto. Ukasimame kando ya mti mkubwa wa mpera ungojee hapo! Utamwona punda akitokea ndani ya mto! Akifika karibu nawe umshike mkia. Utajiona umebaki na mfuko uliojaa pesa nyingi kwenye mkono wako! Utakuwa tajiri kuliko matajiri wote wa hapa kaunti ya Malimoto! Amka uende!”

Baada ya kusema hayo, sauti ilitoweka hata kabla Papara hajauliza swali lolote!!

Bwana Papara aliondoka kuelekea kule shambani.

Alipofika, alisimama chini ya mpera alivyoambiwa. Zilipopita dakika kumi, punda mwenye sura mbaya ya kutisha alitokea mtoni! Bwana Papara alishtuka na kuzubaa! Kabla hajafikiria kumshika mkia, punda alipita akaenda! Papara alibaki akilia na kuomba punda mwingine atokee amshike mkia! Baada ya dakika kumi nyingine, alitokea punda mwenye sura ya kutisha kuliko wa kwanza!

Papara alipokuwa bado ameshangaa, punda alipita akaenda! Papara alilia na kujiangusha chini akaomba apate nafasi ya mwisho punda atokee!

Akaapa, “Sasa akija punda yeyote lazima nimshike mkia!”

Mara punda wa tatu akaja! Pale pale Papara alimrukia amshike mkia! Lakini alishtuka kuona kwamba punda huyo hakuwa na mkia!! Punda bila mkia!!

Ndugu wapenzi, hivyo ndivyo bahati inavyokuja na kupita! Wewe usipokuwa macho kuishika bahati yako, huwezi kuipata! Itakupita tu! Na bahati ikipita hairudi wala haipatikani tena! Ukibahatika kuipata bahati uitunze, usiichezee! Haitarudi tena!!

KINA CHA FIKIRA: Kisa cha Mlajasho mfano kwa vijana

Na WALLAH BIN WALLAH

DAWA ya umaskini ni kazi.

Umaskini utaisha tukifanya kazi kwa bidii. Katika nchi yetu, kazi ziko nyingi. Lakini wanaopenda kufanya kazi ni wachache mno!

Watu wengi hudhania ati kazi ni za kuajiriwa tu na kupokea mishahara kila mwezi!

Kazi ni shughuli yoyote unayofanya ikuletee mapato, pesa na chakula. Si lazima kila mtu aajiriwe! Unaweza kujiajiri mwenyewe ujifanyie kazi upate pesa utajirike kama wengine.

Mafanikio katika maisha huhitaji akili, bidii na uwezo wa kufanya kazi kwa kujituma. Siyo lazima mtu awe na karatasi ya kuonyesha alivyosoma kidogo au sana shuleni. Karatasi haifanyi kazi! Mtu ndiye anayefanya kazi. Anaweza kuajiriwa au kujiajiri kuwa mkulima, mfugaji, seremala, msusi, kinyozi, mfanyabiashara au kazi yoyote kulingana na akili au uwezo alio nao!

Kijijini Songambele kuna maduka madogo madogo au vibanda vinavyoitwa vioski. Huko ndiko wanakijiji wanakonunulia vitu muhimu katika maisha ya kila siku kama vile mikate, sukari, chumvi, mafuta, unga, maziwa, viberiti, sabuni na vinginevyo. Na wauzaji hujipatia pesa kwa kazi zao muhimu za kuuza bidhaa!

Kibanda au kioski kinachopendwa zaidi kijijini Songambele ni MALIMALI ambacho ni cha Bwana Keni Mlajasho! Bwana Keni Mlajasho alizoea kukifungua kioski chake mapema alfajiri saa kumi na nusu kabla ya wauzaji wengine hawajafungua.

Alifunga usiku baada ya wengine kuvifunga vioski vyao. Kwa ukweli wauzaji wengine walivifungua vibanda vyao kwenye saa mbili au tatu asubuhi na kuvifunga saa kumi na mbili au saa moja usiku!

Na walipovifungua vioski vyao saa mbili au tatu, tayari wateja waliotaka bidhaa mapema ili wajitayarishie kifunguakinywa waende kazini, watoto wao pia waende shuleni, huwa wameshanunua kutoka kwenye kioski MALIMALI kwa Bwana Keni Mlajasho. Watu wakazoea kwa Bwana Mlajasho maana alifungua mapema. Pia walipata mahitaji na bidhaa zote walizohitaji. Mlajasho akawa maarufu! Baada ya miaka kadhaa akatajirika sana!

Sasa hivi ameanza kujenga duka kubwa hapo hapo Songambele.

Majirani waliokuwa na vioski wamefilisika kutokana na uvivu, kupenda usingizi, kuchelewa kufungua, kufunga vioski mapema na kukosa kuleta bidhaa muhimu!

Juzi mwanahabari mmoja alimhoji mwenye kioski aliyekuwa jirani wa Mlajasho pale MALIMALI! Akamuuliza kwa nini alifilisika akafunga kioski chake!?

Muuzaji huyo alijibu, “Mlajasho ndiye aliyeiroga biashara yangu, ikaanguka nikafilisika!” Upuuzi mtupu huo!

Naam, leo ninaomba kumwambia huyo ndugu aliyefilisika pamoja na wazalendo wengine kwamba, “Uchawi wa kumroga mtu ni UVIVU wake mwenyewe!”

Ukifanya kazi zako vizuri kwa bidii, utafanikiwa tu!

Uvivu ni nyumba ya njaa! Dawa ya umaskini ni kazi, si uvivu! Anza leo kufanya kazi kwa bidii!! Utafanikiwa!!

wallahbinwallah@gmail.com

WALLAH BIN WALLAH: Jichunge, asilani usijigeuze ng’ombe wa kuchungwa

NA WALLAH BIN WALLAH

UNAPOAMBIWA chunga usifikirie tu kitendo cha kuwapeleka wanyama malishoni! Ama usidhanie ni kuchukua chungio au chekeche ili kuchunga unga au nafaka kuondoa chenga na takataka nyingine.

Chunga ujichunge, ujitunze, ujilinde na uyatazame mambo kwa macho ya tahadhari.  Chunga ujichunge usiwe kama ng’ombe mnyama ambaye lazima aelekezwe ndipo ajue pa kuenda kujilisha! Ujichunge sana kwa akili na maarifa!

Kaokote alikuwa na tabia aliyoijua yeye mwenyewe. Ilikuwa siri yake ambayo hakuna aliyeijua kuanzia wazazi wake, walimu wake hata mimi rafiki yake wa dhati!

Kaokote alikuwa na tabia ya kuokotaokota kila kitu alichokipata njiani au mahali popote pale! Alizoea kuokotaokota mpaka akawa na mazoea ya kuchukua vitu vya watu bila idhini!

Mtu akisahau au akiacha kitu chochote mahali, Kaokote hukiokota akaenda nacho! Kwa mujibu wa heshima zetu tu, hatupendi kumwita MWIZI!

Lakini kusema ukweli, Kaokote alikuwa MWIZI!Wazazi wa Kaokote walimshauri na kumkumbusha kila mara, ‘Mwanetu, tabia njema ndio usalama wa mtu duniani! Ujichunge! Usiwe na tamaa wala usivipende vitu vya bure, vya kupewa au vya kuchukuachukua kutoka kwa watu! Utakula sumu siku moja!

Vitu vingine vitakukwamia tumboni! Tumia akili! Fikiria sana kabla ya kuyatenda mambo! Majuto ni mjukuu! Tafadhali ujichunge!’Walimu nao huko shuleni waliwashauri wanafunzi kila mara wakisema, ‘Tabia njema ndiyo mafanikio na maendeleo ya kila mtu maishani!

Hata ukijaliwa kuwa na kila kitu maishani, lakini tabia zikiwa mbaya, ujue kila kitu ulicho nacho ni kibaya!’ Kaokote na wenzake waliyasikia hayo lakini hawakuyazingatia.Siku moja wazazi wa Kaokote waliondoka nyumbani kuenda kwenye matanga katika kijiji jirani!

Kaokote aliona amepata mwanya wa kuenda kuzurura! Alipokuwa njiani akienda alikoamua kuenda, karibu na msitu, aliona kikapu kikubwa kichafu kilichokuwa kando ya njia. Alisimama akatazama kila upande na hakumwona mtu yeyote karibu!

Kaokote akakiokota kikapu na kukibeba kichwani akapiga mbio kurudi nacho nyumbani! Alipofika nyumbani, alijifungia ndani ya chumba. A

kaanza kuyaondoa majani yaliyofunikiwa mdomo wa kikapu! Ghafla, chatu mkubwa alikiinua kichwa chake akamtemea Kaokote mate ya sumu machoni!

Kaokote akawa kipofu pale pale mpaka leo!Naam, hivyo ndivyo matendo yetu mabovu na tabia zetu mbaya za ujeuri zinavyotuletea maafa makubwa maishani!

Tujichunge na tuyachunge macho yetu ili tuyaone matendo yaletayo maafa na majuto kila uchao katika jamii na mazingira yetu ili tuyaepuke! Chunga! Ujichunge mwenyewe! Usingojee kuchungwa! Chunga uone usalama wako uko wapi?

KINA CHA FIKIRA: Heri adui mwerevu kuliko rafiki mwovu

Na WALLAH BIN WALLAH

KADANDIE alikuwa rafiki yangu.

Nasema alikuwa rafiki yangu kwa sababu hivi sasa siye rafiki yangu tena. Nimemkataa! Heri nikae peke yangu kuliko urafiki na Kadandie.

Mimi na Kadandie tunasoma katika darasa moja shuleni Kambikambo. Ningekuwa na uwezo ningehama nitoke katika darasa letu hili la pamoja na Kadandie. Lakini sina uwezo kiasi hicho! Siwezi kuyafanya mambo ambayo ni zaidi ya uwezo wangu.

Hapo mwanzo mimi na Kadandie tulipendana sana. Tusingetengana kwa dakika tano bila kuonana. Lakini baadaye, mimi Kachuji mwana wa Paki, niligundua kwamba rafiki mbaya ni hatari kuliko nyoka!

Leo ninaamini kwamba afadhali kukaa na adui mwerevu kuliko rafiki mjinga mwovu! Rafiki mwizi, mlevi na mvuta bangi ni hatari zaidi! Akiiba, watu husema nyinyi nyote mliiba pamoja! Akilewa na kuvuta bangi zake, na wewe watu hupita karibu wakikunusanusa kuthibitisha kama kweli hunuki bangi au pombe! Mtembea na muuza shombo hunuka shombo!

Kadandie hakuwa akisoma! Kila kazi alitaka nimfanyie mimi. Majibu ya maswali ya mtihani alizoea kuyanakili kutoka kwangu! Tukipewa kazi ya ziada tukafanyie nyumbani, Kadandie alinipa daftari lake nikamfanyie kazi yake ya ziada na kumjibia maswali! Kisha hunipumbaza kwa kunipa pesa kidogo, peremende, maandazi, biskuti na vijitakataka vingine ambavyo vyote nilivikataa! Samaki aliyepanua mdomo ndiye anayekamatwa kwa chambo! Samaki aliyefumba mdomo chambo kitapitia wapi? Nilikataa kupanua mdomo ili nizuie chambo cha ndoano ya Kadandie. Na wewe je? Ukimwona mamba amelala kapanua kinywa usidhani anacheka! Ametega mtego! Kiumbe kikiingia tu kinywani, hubanwa na kugeuzwa kuwa kitoweo!

Mwanzo mwanzo huko nilimsaidia sana Kadandie. Nilidhani angeamka na kutia bidii! Kumbe aliyeonja asali huchonga mzinga! Nilipogundua kuwa Kadandie habadiliki wala hataki kuamsha ubongo wake, nilimkataa na kuuvunja urafiki wetu ili ajitahidi kujitegemea asonge mbele kwa bidii zake.

Ni vizuri mtu kujikaza na kujifanyia kazi!

Simtaki tena rafiki mzembe, mlevi, mwizi anayeiba vitu vidogo vidogo vya wazazi wake kuniletea rushwa au hongo za kunipumbaza akili ili nimfanyie kazi zake kwa raha zake huku akinitumia kama bwege! Hapana!!

Katika maisha usipoerevuka na kujanjaruka mapema kama Kachuji mwana wa Paki na kuwaepuka akina Kadandie, utatumiwa vibaya ujute! Hatari kwa maisha yako.

Uwachunguze sana rafiki zako uwajue tabia zao na nia zao katika uhusiano wenu! Usikubali kusukumwa tu kama mkokoteni au toroli kuenda kufanya matendo mabaya kana kwamba huna akili! Hao wanaokusukuma si marafiki wema!

Heri ukae na adui mwerevu kuliko kukaa na rafiki mjinga mwovu! Erevuka!!

KINA CHA FIKIRA: Usijipalie makaa kwa kuyachezea maisha yako mwenyewe

Na WALLAH BIN WALLAH

KITENDO chochote anachokitenda mwanadamu maishani, kikiwa kizuri au kibaya, ni kwa ajili yake yeye mwenyewe!

Kila mkulima huvuna alichokipanda. Bidii za mtu ndiyo mafanikio yake. Na uzembe wa mtu ndiyo majuto yake maishani! Kadhalika, kufaulu na kutofaulu kwa mwanafunzi masomoni hutegemea kazi na bidii zake mwenyewe. Lakini masikitiko ni kwamba wanafunzi wengine hawajui kuwa wanasoma kwa maslahi yao wenyewe wala si kwa faida za walimu na wazazi wao! Ole wao wanafunzi kama hao!

Sakubimbi, mwanafunzi wa shule ya Sirimoyoni. Alikuwa mwenye machachari na kiherehere shuleni Sirimoyoni. Alitaka kila mtu amtambue. Alikuwa mchangamfu darasani lakini mtoro aliyetoroka mara nyingi kutoka shuleni! Kwa jumla Sakubimbi alikuwa mwenye tabia na sifa zisizoridhisha. Alizoea kuenda shuleni akiwa amebeba maandazi, chapati na pesa za kununulia peremende katika kantini ya shule. Kilichomkera kila mtu shuleni hapo ni kwamba Sakubimbi alipenda sana kupigana na wanafunzi wenzake!

Walimu waliamua kuwaita wazazi wa Sakubimbi ili waelezwe kuhusu tabia na mwenendo wa mtoto wao! Wazazi walishtuka na kushangaa sana walipoambiwa kila kitu! Walisema kwa kuapa kwamba, “Sakubimbi mtoto wetu ni mwema, mpole na mwenye heshima sana kwa watu wote nyumbani na majirani!” Walimfananisha na Malaika watumishi wa Mwenyezi Mungu! Wazazi hawakuyaamini maneno ya walimu! Wanafunzi wenzake Sakubimbi waliitwa kutoa ushahidi na maoni yao. Kisha Sakubimbi mwenyewe alikiri kwamba maneno yote yaliyosemwa dhidi yake yalikuwa ukweli kabisa! Hapo ndipo wazazi waliposhawishika kuamini walivyoambiwa!

Kwa hakika, watoto wabaya au watu wabaya huwa wana sura nyingi na tabia nyingi. Kila sura na tabia hizo hutumiwa mahali fulani maalum! Akina Sakubimbi wakiwa mitaani huonyesha sura na tabia za mitaani. Wakiwa shuleni, hutumia tabia na sura tofauti! Wanapokuwa nyumbani hutumia sura na tabia nyingine tofauti kabisa ili kuwaziba macho wazazi, ndugu na jamaa! Lakini zote hizo ni mbio za sakafuni ambazo huishia ukingoni! Wahenga walisema, “Ukiuficha motO, moshi utakufichua!”

Ndugu mlezi au mzazi, unapomlea mwana usiangalie upande mmoja tu wa malezi kwamba, “Mtoto anaenda shuleni na kusoma vizuri!” Chunguza pande zote za tabia na vitendo kwa undani zaidi! Tangu janga la virusi vya korona lilipotangazwa na shule zote kufungwa ili wazazi wakae na watoto wao majumbani, wamejionea sura mpya na tabia mpya ambazo hawakuzijua kwa watoto wao! Hilo ni fundisho kubwa kwetu sisi sote! Lakini muhimu zaidi ni wasia na onyo kwa kila mtoto, mvulana na msichana, “Wewe mwana, uache kabisa kuyachezea Maisha yako! Unapoyachezea Maisha yako, unajichezea wewe mwenyewe!” Zingatia!!

KINA CHA FIKIRA: Ubora wa mtu daima huwa ni mtu mwenyewe

Na WALLAH BIN WALLAH

KATIKA maisha ubora wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe.

Mtu akitaka kuwa bora au akitaka kuwa mtaalamu katika kazi au taaluma yoyote ama katika lugha ya Kiswahili, anapaswa kujitolea kwa ari na nia kujifunza mpaka awe mtaalamu kamili.

Mtu hawezi kutaalamika kwa kudhania tu au kwa kutamani tu kuwa mtaalamu; kwa kuwaigaiga watu fulani waliobobea! La, hasha! Fulani ni fulani!

Kila mtu ana ubora wake na kipawa chake asilia ambacho akikikuza na kukilea vyema, anaweza akawa bora zaidi ya wengine wengi.

Nimeamua kuleta kauli hii kuhusu kujiboresha kwenye ukurasa huu wa gazeti letu tulipendalo la Taifa Leo baada ya kushuhudia minong’ono mingi kuwa ni kwa nini baadhi ya wataalamu na wapenzi wa Kiswahili hutumia lugha bila ya kuzingatia kanuni za sarufi na ufasaha?

Mbona wengine hupotoka mpaka wakayatumia maneno ya Kiswahili Ndivyo Sivyo chambilecho Ndugu Enock Nyariki katika makala yake ya Taifa Leo kila Jumatano?

Katika udadisi wangu, nimewasikia wengine wanaokitumia Kiswahili upogoupogo wakijitetea kwa kutoa vijisababu vyao vingi tu! Wapo wanaosema ati nia yao ni kuifanya lugha ya Kiswahili iwe nyepesi ili kwamba waelewane kwa urahisi na watu ambao wanalenga kuwasiliana nao!

Wengine hudai kwamba walipokuwa shuleni au chuoni hawakufundishwa vizuri! Ati waling’ang’ana kujifunza Kiswahili wenyewe kwa wenyewe tu bila walimu! Wapo wanaotoa hoja kwa ukakamavu kabisa kwamba hivyo wanavyoitumia lugha ya Kiswahili ndivyo walivyofunzwa walipokuwa masomoni! Walilelewa hivyo wakaelewa hivyo!

Pia wapo wanaojitetea kwamba wanayatumia maneno ya Kiswahili jinsi walivyowasikia wazungumzaji wengine wakiyatumia. Nao wakawaiga hivyo hivyo wakidhani ni lugha sahihi! Hao ni miongoni mwa wale waliozoea kutamka *panguza, guza, masaa, masiku, manyumbani, vuruta badala ya vuta, mazingara badala ya mazingira. Ndio hao hao wanaotumia kivumishi mingi kuvumisha nomino zote za kila ngeli wakisema: chakula mingi, siku mingi, pesa mingi, vitu mingi, mambo mingi, ugali mingi, maneno mingi; kila kitu kwao ni mingi tu!

Wapo wanaoyatumia maneno kwa makosa bila kujua kuwa wanakosea! Hapo ndipo pana umuhimu wa kujifunza ili mtu awe na hakika ya jinsi ya kuyatumia maneno kwa usahihi na mantiki katika lugha yoyote.

Vitabu vya kujifunzia Kiswahili vipo tele! Kamusi za kumwongoza mtu kujua matumizi sahihi ya kila neno kuhusu maana na kubainisha nomino katika ngeli sahihi zipo nyingi! Ubora wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe! Kujifunza ndiko kuelewa!!

KINA CHA FIKIRA: Kusomasoma ni hazina kuu ya maarifa maishani

Na WALLAH BIN WALLAH

KATIKA maisha ukitaka uwe na maarifa mengi, busara, elimu na ujuzi mpevu kichwani kuhusu mambo mengi, soma sana vitabu, magazeti, majarida na machapisho mengineyo ainati.

Kusoma mara kwa mara kunamsaidia mtu kujiboresha, kujielimisha, kujifurahisha na kujifanyia utafiti ili ayafahamu mambo mengi maishani.

Mtu yeyote asipojisomea kwa mapana na marefu anapokuwa shuleni au baada ya kutoka shuleni ama chuoni atabakia hivyo hivyo na maarifa aliyoyapata katika nyakati hizo alipokuwa masomoni. Kisichonolewa huwa butu.

Masikitiko ni kwamba watu wengi wanataka kuwa wenye elimu bora na maarifa mengi lakini wanaogopa kusomasoma vitabu, magazeti na majarida ili kujiongezea maarifa! Mathalani, wapo wanafunzi waliosoma wakiwa shuleni au vyuoni kwa ajili ya kupita mtihani tu! Tena walivisoma vitabu vile vile vilivyoidhinishwa na kupendekezwa kutahiniwa masomoni tu basi! Ni kama waligombana na vitabu au walitalikiana! Hasara iliyoje?

Hali ni hiyo hiyo kwa wazazi, wafanyakazi na ndugu zetu wengine waliokamilisha masomo zama zao hizo! Baada ya masomo yao, hawakusoma na hawasomi tena chochote cha kuwaongezea maarifa!

Kutosomasoma ni kujinyima fursa na uwezo wa kujiongezea maarifa, elimu, busara, ujuzi, burudani na mambo mengi yanayosaidia kujenga ubongo na akili za mwanadamu kuimarika na kupevuka zaidi. Hapo tuwapongeze sana nyinyi nyote mnaopenda kusomasoma ili muerevuke na kuburudika maishani! Heko kwenu!

Tabia na desturi ya kusomasoma ndiyo mbinu muhimu ya kumwezesha mtu kujielimisha na kujifahamisha mambo na masuala yanayoibuka katika jamii ili kuenda na wakati.

Mfano, mwanafunzi mwenye mazoea ya kusomasoma vitabu vingi, majarida, magazeti na machapisho mengineyo huwa mwerevu sana na mwepesi wa kuyajibu maswali mbalimbali darasani. Naye mwalimu anayesomasoma kwa mapana na marefu hapa na pale huwa bora na mahiri zaidi katika kufundisha darasani.

Tija

Vivyo hivyo, mtu yeyote aliye na mazoea ya kusomasoma vitabu, majarida au magazeti ya Kiswahili ama ya Kiingereza kama Taifa Leo, Taifa Jumapili, Daily Nation, Sunday Nation na kadhalika, hujipatia mambo mengi yanayohusu elimu, ufundi, ujuzi, kilimo, ufugaji, uvuvi, lugha, ujasiriamali, michezo, chemshabongo, burudani na mawaidha mengi ya busara maishani. Kwa hakika kusoma kwingi ni kujifunza mengi!

Ndugu wapenzi tusome! Vijana someni! Shime wananchi wote, someni! Tusome kila mara tujiongezee maarifa na kujiburidisha ili kupunguza misongo ya mioyo wakati huu wa gonjwa la Korona! Usikubali kubakia hivyo hivyo ulivyo! Kusomasoma ni hazina kuu ya maarifa katika maisha! Soma!!