• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Kazi kwa Vijana: Kibicho achemkia Ruto, Gachagua

Kazi kwa Vijana: Kibicho achemkia Ruto, Gachagua

NA MWANGI MUIRURI

KATIBU katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho ameyataja matamshi ya baadhi ya viongozi wa Muungano wa Kenya Kwanza kuhusu mradi wa Kazi kwa Vijana kama ya uongo na ya kuhadaa Wakenya.

Bw Kibicho amesema madai ya viongozi wa Kenya Kwanza kwamba mpango huo umesambaratika kutokana na kugubikwa na ufisadi ni uongo na unalenga kuzima Kazi kwa Vijana ambayo itawavunia vijana 534,000 kiasi cha Sh5 bilioni kwa muda wa miezi miwili inayokuja.

Katibu huyo alikashifu Kenya Kwanza akisema viongozi wake wamekuwa na mazoea ya kueneza propaganda dhidi ya miradi ya serikali ili kuvutia kura ilhali wanaharibu maisha ya vijana wanaotegemea mradi huo.

Alisema vijana ambao wamekuwa wakifanya kazi kupitia mradi huo tangu 2020 wamelipwa jumla ya Sh16 bilioni.

Mradi huo ulikumbatiwa mwaka huo ili kuwakwamua vijana kutokana na athari za virusi vya corona ambavyo vilisababisha wengi wao kupoteza ajira.

Walioajiriwa wamekuwa wakijihusisha na kazi ya kusafisha miji mbalimbali, kufungua mitaro ya maji na kazi nyingine za mikono kwa siku tisa kila mwezi.

Mpango huo ulisimamishwa wiki jana baada ya Naibu Rais Dkt William Ruto kusema kuwa ulikuwa unatumiwa kuwapa vijana ajira ili wamuunge mkono kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto pia alisema kuwa mradi huo ulikuwa ukitumika kuendeleza ufisadi na japo kila kijana anastahili kulipwa Sh1,000 kila siku, walikuwa wakipokea Sh434.

Akizungumza kwenye mahojino na runinga ya NTV, Dkt Ruto alisema kuwa ufisadi uligubika Kazi Mtaani kwa sababu serikali ilikuwa ikilenga kupata pesa za kufadhili kampeni za Bw Odinga.

Kauli ya Dkt Ruto iliungwa mkono na mgombeaji mwenza wake Rigathi Gachagua ambaye hata alidai kuwa Bw Kibicho alikuwa akiuza chakula cha msaada kwa walioathirika na janga la corona katika Kaunti ya Kirinyaga ili kuvutia kura kwa mrengo wa Azimio la Umoja kinyume na maadili ya kazi ya mtumishi ya umma.

Hata hivyo, Bw Kibicho amekanusha madai hayo akisema kuwa Kaunti ya Kirinyaga haikutengewa chakula chochote cha msaada na familia maskini zilikuwa zikitumiwa Sh1,000 kila siku ili kuwakimu mpango ambao uligharimu Sh10 bilioni kwa muda wa miezi tisa kwa kutekelezwa kwake.

“Badala ya kusema ni niliuza chakula cha msaada, wanafaa waseme sikuwatumia pesa hizo ili waziibe. Gachagua amekuwa na mazoea ya kueneza propaganda kuhusu miradi ya serikali na hajali,,” akasema Bw Kibicho.

“Hata kama wanamchukia Rais Uhuru Kenyatta na wanaohudumu katika serikali yake, wanafaa wahurumie vijana ambao wananufaika kiajira kutokana na miradi ya serikali kama Kazi kwa Vijana,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

NMG yasema waziwazi haiegemei mrengo wowote wa kisiasa

Sakaja aponyoka, Sonko akihema

T L