• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kenya Police Bullets FC kutaja kikosi cha msimu mpya Ijumaa

Kenya Police Bullets FC kutaja kikosi cha msimu mpya Ijumaa

NA TOTO AREGE

KENYA Police Bullets FC mnamo Ijumaa itataja kikosi cha wachezaji 26 ambao watawakilisha timu hiyo katika msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL).

Timu hiyo ambayo awali ilijulikana kama Thika Queens, ilianza mazoezi ya kujiandaa kwa ajili ya msimu mpya Jumatatu, katika uwanja wao wa Police Sacco jijini Nairobi.

Akizungumza na Taifa Spoti, mkufunzi mkuu Beldine Odemba amesema walikuwa na mechi yao ya kwanza ya kirafiki Jumatatu na tulifanya mazoezi ya pili Jumanne asubuhi.

“Kikosi chetu cha mwisho kitakuwa na wachezaji wazoefu na chipukizi,” amesema kocha Odemba.

Mazoezi ya Bullets pia yamehudhuriwa na wachezaji wa Harambee Starlets.

Nahodha wa Starlets Dorcus Shikobe na kiungo mshambulizi Ivy Faith pia wanafanya mazoezi na Bullets kutoka Seth FC ya India.

Kiungo mzoefu zaidi Christine Nafula anajiunga na washika doria hao kutoka Kayserispor FC ya Uturuki.

“Tutawekeza kwenye soka ya wanawake huku tukijipanga kusukuma fedha kwa klabu. Kila mchezaji kwenye timu yangu atapata mshahara wa kila mwezi wa Sh25,000 na marupurupu ya Sh2,500,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Police FC Chris Oguso amesema.

Kiungo wa Nation FC Yasmin Said tayari amenaswa na timu hiyo.

Mercy Mwachi, Lydia “Ozil’ Akoth, Esther Aluoch, Drailer Adhiambo, Anita Adongo, Lavender Okeyo, Mercy Njeri, Mercy Masika na Quinter Seduda Adhiambo ni baadhi ya sura mpya katika klabu hiyo.

Klabu hiyo pia iko kwenye mazungumzo na kiungo wa Zetech Sparks Puren Alukwe. Katika msimu wa 2022/23 KWPL uliomalizika Mei, alifunga mabao 15 katika mechi 22, yakiwa ni mabao matatu nyuma ya mshindi wa Kiatu cha Dhahabu Airine Madalina wa Bunyore Starlets.

Kipa chaguo la kwanza la Gaspo Women Valentine Khwaka pia yuko kwenye rada. Alisaidia Gaspo kumaliza katika nafasi ya pili kwenye ligi msimu uliopita wakiwa na pointi 48 katika mechi 22 ambapo aliruhusu mabao 17.

Angalau wachezaji watano kati ya 16 waliokuwa na Thika Queens msimu uliopita wamesalia klabuni. Wachezaji waliosalia ni Lorna Nyarinda, Wendy Atieno, Juliet Andibo, Georgina Mulati na Nelly Sawe.

  • Tags

You can share this post!

Magenge yanayojipenyeza kwa bodaboda yaonywa

Mswada walenga kuzima waajiri kuhamisha wafanyakazi ghafla

T L