Mamilioni yatakayotumiwa na serikali kwenye mbio za Kip Keino Classic

Na AYUMBA AYODI

Serikali itatumia Sh250 milioni kuhakikisha makala ya pili duru ya Riadha za Dunia za Continental Tour ya Kip Keino Classic yanakuwa ya kufana ugani Kasarani.

Katibu katika Wizara ya Michezo, Joe Okudo alisema hayo jana akikaribisha wanariadha 265 na maafisa watakaowania mataji Septemba 18.

Baadhi ya nyota wa kigeni wanaokuja ni Soufiane El Bakkali (Morocco), Peruth Chemutai (Uganda), Justin Gatlin (Amerika), Christine Mboma (Namibia), Isaac Makwala (Botswana) na Sinesipho Dambile (Afrika Kusini).

Aidha, rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jack Tuwei amefichua kutoka idadi ya washiriki 265, wanariadha 185 watashiriki mashindano ya washiriki wote na waliosalia yale yaliyotengewa watu maalum ugani Kasarani.

Tuwei alisema kuwa AK imealika wanariadha 80 wa humu nchini kushiriki mashindano ya kitaifa ya makala hayo ya pili yaliyohamishwa kutoka uwanja wa Nyayo hadi Kasarani kwa lengo la kuwapa washiriki vifaa bora zaidi.

Alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo ya siku moja yanakaribia kukamilika na yatazinduliwa rasmi Septemba 13 katika hoteli ya Ole Sereni jijini Nairobi.

Afisa huyo pia alifichua kuwa kwa mwaka wa pili mfululizo, mashabiki hawataruhusiwa uwanjani kutokana na masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Covid-19.

Baadhi ya majina makubwa ya humu nchini yatakayoshiriki ni pamoja na bingwa wa Olimpiki Faith Chepng’etich (mbio za mita 1,500), mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki Ferguson Rotich (mita 800) na mshikilizi wa rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

Kiprotich aapa kumaliza utawala wa Julius Yego

Na GEOFFREY ANENE

“Hapa ni nyumbani kwetu na ilikuwa lazima tulinde.” Huo ndio ujumbe wa mrushaji mkuki Alexander Toroitich Kiprotich baada ya kushindia Kenya medali ya dhahabu katika fani ya uwanjani ya kurusha mkuki kwenye riadha za Kip Keino Classic uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Jumamosi.

Kiprotich, ambaye mtupo wake bora ni mita 78.84 alioandikisha mjini Eldoret mwaka 2015, alibeba taji baada ya kurusha mkuki umbali wa mita 76.71.

“Nimejawa na ari ya kujiondoa kutoka kivuli cha bingwa wa dunia wa mwaka 2015 Julius Yego baada ya kumaliza nyuma yake kwa muda mrefu sana. Kwa kushinda makala ya kwanza ya Kip Keino Classic ni kitu cha kihistoria na ninatumai kutetea taji langu katika makala ya pili mwezi Mei 2021,” aliongeza Kiprotich, ambaye atagonga umri wa miaka 26 hapo Oktoba 10.

Kiprotich alifuatwa katika nafasi ya pili na Hubert Chmielak kutoka Poland (mita 75.47) na Timothy Herman kutoka Ubelgiji (75.18).

Warushaji mkuki kutoka Kenya, Poland, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech na Ufaransa walishiriki kitengo hiki. Yego, ambaye anashikilia rekodi ya Kenya na Bara Afrika baada ya kurusha mkuki mita 92.72 akishinda taji la dunia mwaka 2015 nchini Uchina, hakushiriki.

Muethiopia Lemlem aonyesha kinadada Wakenya kivumbi mbio za mita 1,500

Na GEOFFREY ANENE

Lemlem Hailu amezidia maarifa wenyeji Kenya katika mbio za mita 1,500 za wanawake kwenye makala ya kwanza ya Kip Keino Classis uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Jumamosi.

Katika duru hii ya mwisho ya Riadha za Dunia za Continental Tour, Muethiopia huyo alilazimika kukamilisha mizunguko hiyo mitatu kwa kuongeza kasi ikisalia mita 200 hivi baada ya Mkenya Winny Chebet kutisha kuvuruga mpango wake alipompita, japo kwa hatua chache tu.

Mshindi huyo wa nishani ya shaba kwenye Michezo ya Afrika mjini Rabat nchini Morocco mwaka 2019 alikuwa ameonyesha ana nguvu kwa kukimbia kama kwamba alikuwa akifanya mazoezi akifuata Silvia Chesebe kwa karibu katika mizunguko ya kwanza miwili. Chesebe alijiondoa kabla ya kufika mwisho, huku Hailu akisalia mbele.

Hata hivyo, Chebet,29, ambaye alishinda medali ya dhahabu katika Riadha za Bara Afrika mjini Asaba nchini Nigeria mwaka 2019 alimpita Hailu wakikaribia kona ya mwisho na kulazimu Muethiopia huyo kuongeza kasi na kutwaa taji kwa dakika 4:06.43.

Chebet alikamilisha kwa dakika 4:06.78 akifuatiwa na bingwa wa mbio za mita 5,000 wa michezo ya Jumuiya ya Madola 2014 Mercy Cherono, ambaye alikuwa akirejea ulingoni baada ya kuwa nje na jeraha kwa miaka miwili, aliyetumia dakika 4:0679.

Bingwa wa Olimpiki za Makinda 2018 Edinah Jebitok aliridhika katika nafasi ya nne (4:0724) katika kitengo hicho kilichovutia wakimbiaji 10.

#KipKeinoClassic: Paul Tanui ashinda mbio za mita 10,000

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Paul Tanui ndiye mshindi wa makala ya kwanza ya mbio za mita 10,000 za kitaifa kwenye Riadha za Dunia za Continental Tour za Kip Keino Classic zinazoendelea katika uwanja wa Nyayo mnamo Oktoba 3, 2020.

Tanui,29, ambaye aliridhika na medali ya fedha nyuma ya Muingereza Mo Farah katika mbio hizi za mizunguko 25 kwenye Michezo ya Olimpiki 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil, alisubiri hadi ikisalia mizunguko miwili alipochomoka kama risasi na kutwaa taji la Kip Keino Classic kwa dakika 28:06:91.

Mshindi huyu wa medali za shaba kwenye Riadha za Dunia mwaka 2013 mjini Moscow nchini Urusi, 2015 mjini Beijing nchini Uchina na 2017 mjini London nchini Uingereza, alifuatwa kwa karibu na Nathan Lagat na mshindi wa medali ya fedha ya mbio za kilomita 21 kwenye Michezo ya Bara Afrika ya Ufukweni 2019 Charles Yosei Mneria.

Rhonex Kipruto, ambaye aliweka rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 10 kwa wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 20 ya dakika 26:24 hapo Januari 12 mwaka huu mjini Valencia, alikuwa amepigiwa upatu wa kung’arA katika kitengo hiki kichovutia wakimbiaji 25. Hata hivyo, Kipruto,20, ambaye anapanga kujitosa katika mbio za kilomita 21 kwa mara ya kwanza kabisa hapo Desemba 6 mjini Valencia, alikamilisha katika nafasi ya nne.

Naye William Mbevi ameshinda mbio za mita 400 kuruka viunzi kwa sekunde 51:30 akifuatwa unyounyo na Nicholas Chirchir (51:48) na Edward Ngunjiri (51:91).

Mabingwa wanne wa dunia ni miongoni mwa wakali watakaonogesha Kip Keino Classic

Na CHRIS ADUNGO

EDRIS Muktar ni miongoni mwa mabingwa wanne wa dunia ambao wamethibitisha kunogesha riadha za kimataifa za Kip Keino Classic uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020.

Mabingwa wa dunia raia wa humu nchini ambao watashiriki pia kivumbi hicho ni Timothy Cheruiyot (mita 1,500), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji) na Hellen Obiri (mita 5,000).

Muktar ambaye alihifadhi ufalme wa mbio za mita 5,000 katika Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar ataongoza Waethiopia wenzake katika mbio hizo za mizunguko 12 jijini Nairobi.

Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limethibitisha kwamba mbio za Kip Keino Classic zimevutia wanariadha 120 kutoka mataifa 30 tofauti kufikia sasa.

Hata hivyo, mkurugenzi wa mbio hizo, Barnaba Korir, amesema kwamba wanariadha wa haiba kubwa zaidi kutoka humu nchini wanatazamiwa kuthibitisha kushiriki kwao kufikia Septemba 25 ambayo ni siku ya makataa.

Naibu Rais wa AK, Paul Mutwii amefichua kwamba majaribio katika fani za mita 200, mita 400 na mita 800 yatafanywa mnamo Septemba 26 ili kufanyia majaribio vifaa mbalimbali katika uwanja wa Nyayo ambao umekuwa ukikarabatiwa kwa miaka mitatu iliyopita.

Kati ya watimkaji wanaotazamiwa pia kunogesha mbio za Kip Keino Classic mabingwa wa zamani wa dunia na washindi wa nishani za fedha katika Riadha za Dunia za 2019, mabingwa wa mbio za dunia za nyika, washindi wa Olimpiki na miamba wa Jumuiya ya Madola.

Fani zitakazoshindaniwa katika kivumbi hicho ni kuruka mara tatu, urushaji wa kisahani, mbio za mita 200, mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji kwa upande wa wanawake na wanaume.

Vitengo vingine ni urushaji mkuki (wanaume), mbio za mita 400, mita 800m, mita 1,500 na mita 5,000 kwa upande wa wanawake na wanaume.

Mbali na Muktar, 26, Waethiopia wengine watakaonogesha mbio za mita 5,000 ni mshindi wa nishani ya fedha duniani Selemon Barega na Hagos Gebrhiwet aliyeridhika na nishani ya fedha katika Olimpiki za Rio 2016. Hagos alitwaa pia nishani ya shaba katika Riadha za Dunia za 2015 jijini Beijing, China na akaridhika na fedha katika Riadha za Dunia za 2013 jijini Moscow, Urusi.

Mbio hizo zimevutia pia Waethiopia Haile Talahun na Berihu Aregawi watakaotoana jasho na Wakenya Jacob Krop, Nicholas Kimeli, Rhonex Kipruto na Waganda Samuel Kibet na Oscar Chelimo.

Francine Niyonsaba ambaye ni bingwa wa mita 800 nchini Burundi atashiriki kivumbi cha mita 5,000 kitakachomjumuisha Obiri na wanariadha wengine wa haiba kutoka Kenya na Ethiopia wakiemo

Margaret Chelimo, Beatrice Chebet, Agnes Tirop na Abersh Minsewo.

Kipruto atafufua uhasama wake na mshindi wa medali ya shaba dunia katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Soufiane El Bakkali wa Morocco.

Bingwa wa zamani wa kitaifa katika mbio za mita 100 na mita 200, Mike Mokamba na Steve Mwai watanogesha kitengo cha mita 200 ambacho pia kina Arthur Cisse wa Ivory Coast. Cisse aliibuka wa pili katika mbio za mita 100 (sekunde 10.04) kwenye duru ya Diamond League iliyoandaliwa jijini Roma, Italia mnamo Septemba 17, 2020.

Eunice Kadogo ndiye Mkenya wa pkee katika mbio za mita 200 kwa upande wa wanawake. Bingwa wa kitaifa katika mbio za mita 400 Alphas Kishoyian atashirikiana na Collins Omae huku Hellen Syombua, Joan Cherono Mary Moraa wakinogesha mbio hizo kwa upande wa wanawake.

Mbio za Kip Keino Classic sasa zaahirishwa kutoka Septemba 26 hadi Oktoba 3, 2020

Na CHRIS ADUNGO

MBIO za kimataifa za Kip Keino Classic zilizokuwa ziandaliwe katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo, Nairobi mnamo Septemba 26, 2020, sasa zimeahirishwa hadi Oktoba 3, 2020.

Kuratibiwa upya kwa mbio hizo kunachochewa na

mabadiliko kwenye ratiba ya mashindano mbalimbali ya riadha.

Kivumbi cha Diamond League kilichokuwa kifanyike jijini Doha, Qatar mnamo Oktoba sasa kitatifuliwa Septemba 26, siku ambapo mbio za Kip Keino Classic zilikuwa zimepangiwa pia kunogeshwa.

Riadha za Kip Keino Classic zitaandaliwa sasa siku moja kabla ya Mkenya Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele wa Ethiopia kunogesha mbio za London Marathon.

Kipchoge na Bekele ni miongoni mwa wanariadha 40 wa haiba kubwa zaidi duniani watakaoshiriki kivumbi cha London Marathon ambacho kwa kawaida huvutia zaidi ya watimkaji 40,000.

Kip Keino Classic ni miongoni mwa duru za kivumbi cha World Athletics Continental Tour kilichofunguliwa rasmi jijini Turku, Finland mnamo Agosti 11, 2020.

Kipute cha Turku kilipewa jina Paavo Nurmi kwa heshima ya aliyekuwa mwanariadha nguli wa taifa hilo, Nurmi ambaye alijinyakulia medali tisa za dhahabu na tatu za fedha katika fani mbalimbali za Olimpiki zilizoandaliwa 1920 (Antwerp, Ubelgiji), 1924 (Paris, Ufaransa) na 1928 (Amsterdam, Uholanzi).

Mbio za Continental Tour zitashirikisha nyingi za fani ambazo zimeondolewa kwenye kivumbi cha Diamond League msimu huu wa 2020 zikiwemo mbio za mita 200 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Makala ya kwanza ya Continental Tour yalikuwa yafanyike humu nchini mnamo Mei 2, 2020 ila yakaahirishwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Licha ya duru nzima kuitwa Kip Keino Classic kwa heshima ya mwanariadha veterani Kipchoge Keino, kivumbi cha fani ya mbio za mita 10,000 wakati wa mashindano hayo kitaitwa “Naftali Temu 10,000m Classic”.

Kipchoge alijizolea nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Olimpiki za 1968 nchini Mexico kabla ya kutwaa medali nyingine ya dhahabu katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki za 1972 jijini Munich, Ujerumani.

Kwa upande wake, Temu alitwalia Kenya nishani ya kwanza na ya mwisho katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico. Kipchoge, Temu na Amos Biwott (mita 3,000 kuruka viunzi na maji), ndio Wakenya wa kwanza kunyakua medali za dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki mnamo 1968 nchini Mexico.

“Kipchoge ndiye baba wa Riadha za Kenya na dunia nzima inamfahamu zaidi kuliko Mkenya yeyote mwingine katika ulingo wa riadha,” akasema Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) tawi la Nairobi, Barnaba Korir kwa kusisitiza kwamba kuita mbio za mita 10,000 ‘Naftali Temu’ kutachochea zaidi Wakenya kutamba katika fani hiyo wakati wa Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan.

Mwingereza Mo Farah na Waethiopia ndio wamekuwa wakitawala mbio za mita 10,000 duniani kwa kipindi kirefu kilichopita.

RATIBA YA CONTINENTAL TOUR:

• Paavo Nurmi Games (Turku, Finland, Agosti 11);

• Istvan Gyulai Memorial (Szekesfehervar, Hungary, Agosti 19);

• Seiko Golden Grand Prix (Tokyo, Japan, Agosti 23);

• Kamila Skolimowska Memorial (Silesia, Poland, Septemba 6);

• Ostrava Golden Spike (Ostrava, Czech, Septemba 8);

• Memorial Borisa Hanzekivica (Zagreb, Croatia, Septemba 15);

• Kip Keino Classic (Nairobi, Kenya, Oktoba 3)

• Nanjing Continental Tour (Nanjing, China, tarehe bado haijathibitishwa).