• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 1:25 PM
KPC yaagizwa kuchunguza athari za mafuta yaliyomwagika Makueni

KPC yaagizwa kuchunguza athari za mafuta yaliyomwagika Makueni

Na PIUS MAUNDU

WAZIRI wa Maji Simon Chelugui ameitaka Kampuni ya Mafuta nchini Kenya (KPC) kuongeza juhudi katika kuchunguza kiwango cha mafuta yaliyomwagika katika eneo la Kiboko, Kaunti ya Makueni.

Waziri ametaja hali hiyo kama mkasa mkubwa wa kimazingira, ikiwa hautachunguzwa na hatua zifaazo kuchukuliwa kwa haraka.

Kiwango kisichojulikana cha dizeli na petroli kilimwagika katika eneo hilo na kimekuwa kikielekea katika Mto Kiboko. Hii ni baada ya kuharibika kwa sehemu moja ya bomba jipya la kusafirishia mafuta kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Tayari kampuni hiyo imekarabati bomba hilo na imekuwa ikichimba mitaro ili kutathmini kiwango cha mafuta kilichoenea katika meneo yaliyo karibu na mto huo.

Mamlaka ya Usimamizi wa Maji (WRA) imewatahadharisha wakazi dhidi ya kutumia maji katika eneo hilo, baada ya tafiti kadhaa kuonyesha yamechanganyika na mafuta. Maji hayo ni yaliyo katika visima na chemchemi ya Kiboko, ambapo hutegemewa sana na asasi muhimu kama Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kilimo (KALR).

“KPC inapaswa kuongeza juhudi kuhakikisha mafuta hayo hayasambai zaidi,” akasema Bw Chelugui. Alikuwa amezuru eneo hilo akiandamana na maafisa wengine serikalini.

“Tumeona kuwa mafuta hayo yanaweza kuharibu eneo nzima la Kiboko na Athi,” akasema.

Gavana Kivutha Kibwana amekuwa akilalamika kuwa mafuta hayo yanahatarisha maisha ya wakazi walio katika eneo hilo.

Viongozi waliokuwa naye walitangaza kubuniwa kwa jopo maalum ambalo litachunguza athari na suluhisho kwa hali hiyo.

You can share this post!

UFISADI: Rais asiyeweza kung’ata atisha tena

Kaunti kutwaa usimamizi wa kiwanda cha Mumias Sugar

adminleo