Wanaume wawili wakamatwa Mombasa kwa kujifanya maafisa wa polisi

Na MISHI GONGO

WANAUME wawili wanazuiwa katika kituo cha polisi cha Chaani eneobunge la Changamwe, Kaunti ya Mombasa kwa kosa la kujifanya maafisa wa polisi.

Wawili hao Stephen Obonyo na Mathew Onduru walikamatwa Jumanne, wakiwa wanawahangaisha wakazi eneo la Mlolongo.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi eneo la Changamwe Ali Ndiema amesema maafisa wa polisi walifaulu kuwakamata wawili hao baada ya kudokezwa na wakazi.

“Tulipokea habari kutoka kwa wakazi kuwa kumetokea kundi la watu ambao wanavalia makoti yaliyoandikwa ‘Shofco’ ambao wanasema kuwa ni maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Mikindani,” akasema kamanda huyo.

 

Stephen Obonyo (kushoto) na mwenzake Mathew Onduru wakiwa katika kituo cha polisi cha Chaani ambako wanazuiliwa. Picha/ Mishi Gongo

Amesema alituma maafisa wake mwendo wa saa kumi na mbili jioni ambao waliwatia mbaroni watu hao wakiwa katika shughuli ya kuhangaisha watu.

Aidha alisema watu hao wanatembea na mipira ambayo walitumia kuwachapa wakazi.

Amesema kwa sasa washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Chaani wakisubiri kufikishwa mahakamani Alhamisi.

Bw Ndiema amesema wawili hao watashtakiwa kwa kosa la kujifanya maafisa wa polisi na kujitayarisha kutekeleza uhalifu.

Mwanamume ashtakiwa kujifanya Jaji Ibrahim

Na RICHARD MUNGUTI na PHYLIS MUSASIA

MWANAUME alishtakiwa Ijumaa kwa kujifanya Jaji Mohammed Ibrahim wa Mahakama ya Juu.

Henry Antony Wasike alikanusha shtaka la kuandikisha laini ya simu katika kampuni ya Safaricom akijifanya kuwa Jaji Ibrahim.

Shtaka dhidi ya Bw Wasike lilisema mnamo Februari 26, 2019, mwendo wa saa tatu na dakika 14 asubuhi alisajili laini ya simu ya kampuni ya Safaricom akitumia jina la Jaji Mohammed Ibrahim wa Mahakama ya Juu.

Ilidaiwa kwamba mshtakiwa alifanya hivyo akiwa na nia ya kutumia laini hiyo kutenda uhalifu.

Bw Wasike ambaye hakuwa amewakilishwa na wakili aliomba Hakimu Mkuu Bw Francis Andayi amwachilie kwa dhamana.

“Ninaomba mahakama iniachilie kwa dhamana wa sababu hadi sasa sina hatia na niko hapa kwa madai tu,” mshtakiwa alimsihi Bw Andayi.

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi hakupinga kuachiliwa kwa mshtakiwa kwa dhamana.

“Dhamana ni haki ya kila mshukiwa kwa mujibu wa kifungu nambari 49 cha katiba,” alisema Bi Kirimi.

Bw Andayi aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh50,000 pesa tasilimu hadi Mei 6, 2019.

Watu watatu wameorodheshwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Mahakama iliamuru kiongozi wa mashtaka ampe mshtakiwa nakala za ushahidi ndipo aandae ushahidi wake.

Nakala za ushahidi

Mahakama iliamuru kiongozi wa mashtaka ampe mshtakiwa nakala za ushahidi ndipo aandae ushahidi wake.

Kesi itatajwa Mei 29 ili upande wa mashtaka uthibitishe ikiwa umempa mshtakiwa nakala za mashahidi kisha maagizo zaidi yatolewe ikiwa ni pamoja na kutengewa tarehe ya kusikilizwa.

Kwingineko mjini Nakuru, mwanamume mwenye umri wa miaka 70 alikanusha kulaghai mfanyabiashara Sh680,000 akidai angemuuzia ploti.

Micheal Ndungu Muriuki alidaiwa kumtapeli Bi Priscilla Wambugu pesa hizo eneo la Kabatini Kaunti ya Nakuru.

Kesi itasikilizwa Mei 24, 2019.