• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Kuku maridadi wa kienyeji walimaliza kiu yake ya kusaka ajira

Kuku maridadi wa kienyeji walimaliza kiu yake ya kusaka ajira

Na SAMMY WAWERU

RUTH Wanjiru ni mwanadada mwenye furaha kufuatia hatua alizopiga mbele kimaendeleo kupitia ufugaji wa kuku.

Ni mfugaji wa kuku wa kienyeji walioimarishwa, eneo la Githunguri, Kaunti pana ya Kiambu.

Tunampata akikagua wanavyoendelea ndege hao wa nyumbani na ambao wamegeuka kuwa chanjo cha mapato yake.

Wakiwa kwenye vizimba tofauti na kugawanywa kwa mujibu wa umri, sauti za muwiko zinatulaki na kutukaribisha.

Wanjiru anasema ana kila sababu ya kutabasamu kutokana na manufaa anuwai ya mradi wake wa kuku wa mayai na nyama.

“Ufugaji wa kuku ndio afisi yangu ya kila siku,” adokeza.

Aidha, anafichua aliingilia shughuli hiyo 2018, baada ya jaribio lake kutafuta kazi tangia 2013 bila mafanikio.

Ana Stashahada ya Masuala ya Huduma za Mikahawa na Usimamizi.

“Nilifanya vibarua vya hapa na pale kwenye hoteli na supamaketi, ila ajira ya muda mfupi,” Wanjiru asema.

Sawa na mamia na maelfu ya vijana wanaotafuta ajira baada ya kuhitimu vyuoni, kijana huyu anasema jitihada zake zilikuwa mithili ya kukwea mlima kwa kutumia kandambili miguuni badala ya viatu.

Aliamua liwe liwalo hataendelea kuwa mtumwa wa kusafiri kutoka hoteli au kampuni moja hadi nyingine akisaka kazi.

“Mwaka wa 2018 nilichukua mkopo wa Sh100, 000 kutoka chama kimoja cha ushirika, nikautumia kuanzisha mradi wa kuku,” asema.

Anafichua, alianza na vifaranga 150 wa kuku wa kienyeji walioimarishwa, kifaranga wa siku moja akiuziwa Sh100.

Sehemu ya mtaji huo pia alitumia kujenga vizimba, kuwapa chanjo na matibabu, chakula na mahitaji mengine ibuka.

Wanjiru hata hivyo anasema ni kuku 75 pekee waliofanikiwa kuendelea kuishi.

“Wengi walikufa kwa sababu sikufahamu malezi, kama vile ratiba ya chakula, chanjo na pia kudumisha usafi,” afafanua, akikadiria hasara aliyopata.

Waliosalia, walimpa mapato ya Sh24,000 pekee.

Ni kutokana na pigo hilo, alijipa breki ya miezi mitano, ambapo alijituma kufanya utafiti kuhusu malezi na ufugaji bora wa kuku.

“Nilitembelea wafugaji waliofanikisha miradi ya kuku, nikajifunza vigezo nilivyofeli.”

Wanjiru ambaye ni mama wa mtoto mmoja, sasa ni guru katika ufugaji wa kuku.

Ruth Wanjiru hufuga kuku walioimarishwa wa kienyeji Githunguri, Kiambu. PICHA | SAMMY WAWERU

Anafichua kwamba yeye ni kati ya vijana walionufaika kupitia ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO – UN), Kaunti ya Kiambu.

FAO imekuwa ikiendeleza mpango wa kuhamasisha na kupiga jeki vijana kuingilia shughuli za kilimo-ufagaji-biashara katika kaunti mbalimbali nchini.

Mwaka uliopita, mwezi Aprili Wanjiru alishiriki mafunzo ya ufugaji bora wa kuku, yaliyofadhiliwa na FAO kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Kiambu.

“Baada ya mafunzo, nilipewa vifaranga 55 kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), wa kuku wa kienyeji walioimarishwa, kama mfugaji binafsi, na wengine 20 kupitia kikundi,” afafanua.

Wanjiru ni mwanachama wa kikundi cha Pillars of Shakinah, chenye jumla ya wanachama 25.

Chini ya mpango wa Rural Youth Migration, Social Protection & Agriculture, Joy Nkoitoi, mratibu wa mradi wa ajira kwa vijana FAO, anasema programu hiyo inalenga kubuni nafasi nyingi za kazi katika sekta ya kilimo-biashara mashinani.

Joy anasema mpango huo ulianza 2017, na kufikia sasa vijana waliofaidika wamepata mafunzo bora kuendeleza kilimo-ufugaji-biashara.

“Huwapa mbegu, fatalaiza, mifugo hasa kuku na nguruwe, chanjo na vifaa kuwawezesha kuendeleza kilimo,” Joy adokeza.

Anasema unalenga walio kati ya miaka 18 – 35, mayatima, wasiojiweza katika jamii, kati ya makundi mengineyo, wenye mahitaji mbalimbali ya kimsingi.

Wanjiru pia ananufaika kupitia mikopo ya serikali kwa vijana na ile ya Uwezo Funds.

“Fedha hizo hazitozwi riba, na zimenisaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha ufugaji wa kuku,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano.

Tulimpata akiwa na kuku maridadi wapatao 300, wa madoadoa meupe na meusi, waliojumuisha vifaranga na wanaotaga mayai.

“Mradi wangu ni wa uuzaji wa vifaranga, mayai ya kienyeji na wa nyama,” akasema.

Safari ya mfugaji huyo hata hivyo haijakuwa rahisi. Anataja ongezeko la bei ya chakula cha mifugo kama mojawapo ya changamoto kuu zinazomzingira.

Wafugaji wa kuku ndio wameathirika kwa kiasi kikubwa.

“Chakula cha kuku bei imeongezeka kwa kiwango kikuu, wengi wakiishia kuacha ufugaji,” asema David Njoroge, mmiliki wa duka la kuuza bidhaa za mifugo eneo la Ruiru Kiambu.

Mhudumu huyo anasema amepoteza zaidi ya asilimia 30 ya wafugaji wa kuku.

“Watengenezaji wa chakula cha mifugo wanalalamikia gharama ya malighafi kupanda, hivyo basi hawana budi ila kuwekelea mfugaji mzigo,” Njoroge afafanua, akihimiza serikali kutathmini suala la bei ya chakula cha mifugo nchini.

Anaonya endapo hatua mahususi hazitachukuliwa, huenda hali ikawa mbaya zaidi na taifa kuishia kukosa mazao ya kuku; mayai na kuku.

Licha ya pandashuka hizo, Wanjiru, 36, ambaye pia hukuza ndizi na kufuga mbuzi, kilimo-ufugaji-biashara ni sekta ambayo inaweza kuinua vijana kwa kiwango kikuu.

“Awali, nilitegemea kazi za ofisi na ambazo hazipatikani kwa haraka ila sasa nimetulizwa na ufugaji wa kuku. Vijana wamakinike, wakumbatie kilimo na ufugaji kwani ni sekta yenye mapato,” ahimiza mwanadada huyo.

Huku kikwazo kwa vijana wengi kikiwa ukosefu wa mtaji, anawahimiza kujiunga na vyama vya ushirika (Sacco) ili kupata mikopo.

Isitoshe, serikali inaendeleza mpango wa utoaji mikopo kwa vijana na kina mama isiyotozwa riba, na Wanjiru anawashauri kuikumbatia.

  • Tags

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Kuna maisha baada ya sherehe za kukaribisha...

Umeme nafuu utaimarisha sekta ya viwanda na kupanua nafasi...

T L