• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kunyonyesha kuna umuhimu mkubwa, kina mama washauriwa

Kunyonyesha kuna umuhimu mkubwa, kina mama washauriwa

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kufungua vituo vya wanawake kwa ajili ya kunyonyesha watoto wao wachanga.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Kiambu Bi Mary Kamau alizindua kituo kipya Jumatano katika hospitali ya Gatundu Level Five ambacho kitawafaa wanawake walio na watoto wanaonyonya.

“Tutatilia mkazo vituo kama hivyo vifunguliwe katika hospitali zingine na hata kwenye ofisi mbalimbali,” alisema Bi Kamau.

Akaongeza: “Vituo hivyo vitakuwa na vifaa muhimu kama maji safi, viti vya kisasa, na runinga.”

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Kiambu Bi Mary Kamau (katikati) ahutubia waandishi wa habari katika hospitali ya Gatundu Level Five baada ya kuzindua kituo cha wanawake ambacho ni spesheli kwa ajili yao kunyonyesha watoto wao. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema serikali inastahili kupambana na maradhi ya saratani kwa kila hali.

Aidha, alishauri kwamba jamii ikifuata masharti muhimu ya kiafya, bila shaka itakuwa rahisi kukabiliana na Saratani.

Alisema amewasilisha mswada wa Community Health Bill unaolenga kuleta sheria ya kuihusisha jamii na walioteuliwa kushirikiana na wauguzi mashinani.

“Mpango huo ni muhimu kwa sababu watagundua maradhi mengi yanayoathiri wananchi vijijini. Watapata nafasi ya kuwahoji raia hao na kuelewa matatizo yao ya kiafya,” alisema Bi Kamau.

Kina mama walishauriwa wawe wakinyonyesha kwa angalau miaka miwili.

Kuwa mstari wa mbele

Dkt Peris Wanjiku Maina naye alitoa mwito kwa wanawake kuwa mstari wa mbele kunyonyesha watoto wao.

“Mtoto yeyote anayenyonya huepuka kupata maradhi kadhaa mwilini,” alisema Dkt Maina.

Alisema mwanamke anayenyonyesha mtoto wake huweza pia kuepuka kuambukizwa saratani ya matiti.

“Mwanamke anastahili kunyonyesha mtoto wake kwa muda wa miezi Sita mfululizo bila chakula kingine. Lakini ikibidi mtoto ana haki ya kunyonya kwa muda wa miaka miwili,” alisema Dkt Maina.

Naye Daktari mkuu wa hositali ya Gatundu Level Five Dkt Simon Gitau, alisema mama wanastahili kunyonyesha kila baada ya Masaa Matatu.

” Mwanamke mwenye mtoto mchanga an nafasi nzuri ya kukuza ubongo wake kuwa timamu.

Kila Mara ni lazima Mwanamke anawe mikono kabla ya kunyonyesha,” alisema Dkt Gitau.

Afisa mkuu wa shirika ya (Nutrition International ) Bw Elijah Mbiti, alisema shirika hilo limekuwa na ushirikiano wa karibuni na serikali kwa zaidi ya miaka kumi.

” Shirika hilo linauzia serikali vidonge vya madawa ya vitamin A ambapo kwa muda wa mwaka moja wamesambaza dawa hizo kwa gharama ya Sh10 milioni,” alisema Bw Mbiti.

You can share this post!

‘Ziara ya Rais Kenyatta eneo la Mlima Kenya italenga...

Forlan astaafu rasmi kucheza soka ya dunia

adminleo