• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Magavana 10 Mlima Kenya waanza kujitenga na Ruto

Magavana 10 Mlima Kenya waanza kujitenga na Ruto

 Na WAIKWA MAINA 

MAGAVANA 10 ambao ni wanachama wa Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Kati (CEKEB), wameanza kususia hafla za Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo.

Kwa muda wa miezi mitano iliyopita, magavana hao hawajakuwa wakionekana katika hafla zake, kinyume na ilivyokuwa awali.

Isipokuwa Gavana Francis Kimemia wa Nyandarua na mwenzake Mutahi Kahiga wa Nyeri, wengine wamepunguza kabisa ushirikiano wao na Dkt Ruto.

Awali, wote walikuwa wakiungana naye, huku wakimshinikiza kuwasaidia kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo. Vile vile, walimhakikishia kumuunga mkono.

Baadhi yao ni Gavana Ferninard Waititu wa Kiambu, ambaye amekuwa akionekana kama mshirika wa karibu wa Dkt Ruto katika eneo hilo.

Mnamo Alhamisi, Bw Waititu alikosa kuungana naye kwenye hafla ya ibada katika kanisa la AIPCA, Muthua-ini katika Kaunti ya Nyeri.

Mabw Waititu na Kahiga ndio walikuwa magavana pekee kutoka ukanda huo ambao walihudhuria hafla ya ukumbusho wa aliyekuwa Gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua mnamo Februari.

Mkondo huo ulianza baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kama mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kusimamia Miradi ya Serikali.

Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, ambaye pia alikuwa mshirika wa karibu wa Dkt Ruto pia amebadili mwelekeo wake wa kisiasa.

Bw Wa Iria alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakiandamana naye katika ziara mbalimbali nchini, hali iliyoibua dhana kuwa huenda akateuliwa kama mgombea-mwenza kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kiongozi wa Walio Wengi katika Kaunti ya Nyandarua, Bw King’ori Wambugu anasema kuwa hatua ya viongozi wengi kujitenga na Dkt Ruto inatokana na ahadi nyingi alizotoa lakini hazijatimizwa hadi sasa.

Bw Wambugu pia alisema kuwa mikutano ya siri kati ya madiwani na Dkt Ruto pia ilichangia pakubwa uhasama kati ya Bunge na mawaziri.

“Eneo hili limebaini kuwa Dkt Ruto anatumia njia ya kuwatenga baadhi ya watu ili kuweza kupenyeza kisiasa. Wakati anaizuru Kati, huwa anatoa ahadi nyingi ambazo huwa hatimizi. Hili ni kinyume na maeneo mengine,” akasema Bw King’ori.

Alisema kuwa miongoni mwa ahadi alizotoa ni Sh3 milioni ili kusaidia katika ujenzi wa bweni katika Shule ya Msingi ya AC mjini Ol Kalou. Alisema kuwa Dkt Ruto hajatimiza ahadi hiyo kwa miezi mitano kufikia sasa.

Dkt Ruto alitoa ahadi hiyo wakati aliongoza harambee shuleni humo kununua madawati ya shule zote za msingi katika eneobunge la Ol Kalou, ambapo alitoa mchango wa Sh3 milioni.

Siku iyo hiyo, alizindua ujenzi wa barabara ya Captain ambao bado haujaanza. Bango lililowekwa baada ya uzinduzi huo pia lishaondolewa. Mwanakandarasi aliondoka dakika chache baada ya Dkt Ruto kuondoka.

You can share this post!

Askofu aanza msako wa kuwatimua mashoga na wasagaji kanisani

Polisi wazidisha doria Salgaa kuepusha ajali

adminleo