• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
MAONI: Afrika itapiga hatua hata zaidi watu wa nje wakiacha vurugu

MAONI: Afrika itapiga hatua hata zaidi watu wa nje wakiacha vurugu

NA DOUGLAS MUTUA

MWENYEKITI wa Tume ya Muungano wa Afrika (ACU) anayeondoka, Bw Moussa Faki, ameanza kunguruma mwishoni mwa kipindi chake cha kuhudumu.

Juzi, ameyaambia mataifa tajiri yaliyo na mazoea ya kuingilia mambo ya ndani ya Afrika yakome, akasisitiza kwamba, Waafrika wana uwezo wa kujitatulia mizozo yao.

Sijui amepata makucha wapi akaweza kuyachomoa kiasi hicho muda huu, lakini kwangu haidhuru kwa kuwa ni heri mtu akayasema kuchelewa yanayofaa kusemwa, mlengwa akayajua.

Kilichoonekana kumuudhi zaidi ni mzozo unaoendelea ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya majeshi ya serikali na makundi mbalimbali ya waasi.

Mzozo huo unaaminika kuzushwa na Rwanda kwa ufadhili wa mataifa mengine tajiri duniani yanayonufaika kutokana na utajri wa madini ambao ardhi ya DRC inasheheni.

Rwanda ina maslahi yake kule: inawafuata waasi wa jamii ya Hutu wanaoipinga serikali ya Rais Paul Kagame, inadai kuwatetea Wakongomani wanaozungumza lugha ya Kitutsi na wanaoaminika kunyanyaswa na serikali ya DRC, na pia inaiba madini.

Wageni waliolengwa na Bw Faki hasa ni hao wanaotoka nje ya Afrika kwa kuwa wasingetumia Rwanda na wadau wengineo kuiba madini, basi hata na vita hivyo havingekuwepo.

DRC ni mfano bora wa mataifa yanayoendelea, ambayo huvurugiwa amani na yaliyoendelea ili yasalie katika hali hiyo ya ukata wa kutupwa huku wizi ukiendelea.

Si siri kwamba madini aina ya koltani, ambayo hutumika kuunda vifaa vingi vinavyotumia umeme zikiwemo simu, tarakilishi, runinga na kadhalika, yanaibwa huko ili kuendesha viwanda vya mataifa yaliyoendelea.

Yangepatikana kihalali na kampuni hizo ziyanunue na kuyalipia ushuru utakiwao, basi hata bei za bidhaa nilizokwisha kutajia zingekuwa ghali zaidi ya zilivyo.

Madini hayo na mengine, japo yana thamani kubwa mno, yamegeuka laana na maangamizi kwa wenyeji, wengi wakatamani ni heri yasingekuwepo kabisa. Mashariki mwa DRC hasa hakukaliki.

Mwenzako nasisitiza, ni heri wezi wenyewe wasingekuwepo ila madini yawe mengi tu ili taifa hilo litajirike.

Juzi niliposikia kuwa madini hayo yamepatikana nchini Kenya, eneo la Embu, nilijiuliza iwapo tutaingiliwa na wezi, nchi yetu igeuke DRC ya pili, hasa kwa kuwa viongozi wetu wote ni fisi walafi. Nilitia dua Mwenyezi Mungu atuepushie maafa.

Inawezekanaje anga ya DRC, taifa lililo nyuma mno kimaendeleo, ndiyo inayopaa ndege nyingi zaidi barani Afrika? Zinatua silaha na kubeba madini ya kuiba.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Jeneza la kilo 65, sawa na uzito wa Kiptum alipokuwa hai

Kisanga mwanamume akiachiwa mtoto mchanga wa siku nne na...

T L