Atakubali mistari ya Raila?

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga anapojiandaa kutangaza rasmi azma yake ya kugombea urais mwaka 2022, imeibuka kuna juhudi za kumshawishi Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua kuwa mgomnea mwenza wake.

Ingawa wawili hao wamekuwa wakitofautiana kisiasa hasa kuhusiana na mchakato wa BBI uliozimwa na mahakama, duru zinasema mipango ya kujaribu kumvuta mbunge huyo wa zamani wa Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga upande wa Bw Odinga.

Bi Karua amekuwa mstari wa mbele kuunganisha eneo la Mlima Kenya kabla ya uchaguzi mkuu ujao, na ndiye msemaji wa kundi linalojiita Jukwaa la Umoja wa Mlima Kenya (MUF) linaloleta pamoja vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi eneo hilo.

Kundi hilo lilimtwika jukumu la kuzungumza na wagombeaji urais kuhusu maslahi ya eneo la Mlima Kenya kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kwa wakati huu, Bi Karua anasisitiza kuwa atagombea kiti cha ugavana wa Kirinyaga, japo duru zinadokeza kuwa mikakati inaendelea kisiri kumshawishi abadilishe nia na kukubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga, ambaye ndiye anapendelewa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wadokezi wetu wanaeleza kuwa mabwanyenye kutoka Mlima Kenya, ambao wameashiria kuwa watamuunga mkono Bw Odinga, wameonyesha nia ya kukubali mipango ya Bi Karua na kundi lake la MUF kuandaa kongamano la tatu Limuru ili kutoa mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo mwaka ujao wa 2022.

Mikakati ya Bi Karua na kundi lake ndiyo ilitumiwa na mabwanyenye hao waliokutana na Bw Odinga pamoja na vinara wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kudadisi mipango waliyo nayo kuhusu eneo la Mlima Kenya iwapo watapata ushindi wa kiti cha urais.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kila mgombea urais kueleza mipango yake ya kuinua uchumi wa eneo la Mlima Kenya, kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Rais Kenyatta na kuinua na kulinda sekta za kilimo na biashara zinazotegemewa na wakazi wengi wa eneo hilo.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa msemaji wa MUF mjini Naivasha mwezi Septemba, Bi Karua alisema kuwa wagombeaji urais wote wanafaa kueleza mipango yao kuhusu eneo lao.

Wadadisi wa siasa wanasema ikiwa Bw Odinga anataka kumshinda mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi ujao, Naibu Rais William Ruto, atakuwa na nafasi bora iwapo atamteua mgombea mwenza mwanamke kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Mwanamke huyo ni Martha Karua kwa sababu nyingi. Karua ni mwanamke mwerevu anayetosha kuwa rais na pia anaweza kupata kura nyingi za wanawake sio tu eneo la Mlima Kenya pekee bali kote nchini kwa kuwa watachukua kuwa watawakilishwa katika uongozi wa nchi,” asema mchanganuzi wa siasa Sam Omwenga.

Kulingana na mdadisi wa siasa, Dkt Amukowa Anangwe, tiketi ya Raila na Karua ina nguvu kuliko ya viongozi wengine kutoka eneo la Mlima Kenya.

Wengine ambao wamekuwa wakitwa kwamba wanaweza kuwa wagombea wenza wa Bw Odinga ni Justin Muturi (Spika wa Bunge la Kitaifa), Peter Kenneth (mbunge wa zamani wa Gatanga), Mutahi Kagwe (Waziri wa Afya) na Anne Waiguru (Gavana wa Kirinyaga).

Washauri wa karibu wa Rais Kenyatta pia wamekuwa wakipigia debe ushirikiano wa Bw Odinga na Bi Karua, wakisema wakiungana wanaweza kumshinda Dkt Ruto kwa kura nyingi.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Mutahi Ngunyi, ambaye ni mshauri wa karibu wa Rais Kenyatta, Bi Karua anahitaji kuungwa mkono na Rais Kenyatta ashirikiane na Bw Odinga.

Duru za kisiasa zinasema kuwa kizingiti kikubwa kwa ushirikiano wa Bw Odinga na Bi Karua ni tofauti zao kuhusu BBI.

Huku Rais Kenyatta na Bw Odinga wakiunga mkono mchakato huo, Bi Karua alikuwa mmoja wa walioupinga kortini na anaamini Katiba ya 2010 inafaa kulindwa na kutekelezwa kikamilifu.

Kulingana na mdadisi wa siasa Geff Kamwanah, kizingiti hicho kinaweza kuondolewa kabla ya kongamano la Limuru 3 ambalo ni wazo la Bi Karua na MUF, na limekumbatiwa na mabwanyenye eneo hilo walio na ushawishi mkubwa.

“Bi Karua ni kiongozi mwenye msimamo, lakini sidhani atakataa uamuzi wa jamii ikimtaka aiwakilishe katika serikali ya kitaifa,” asema Bw Kamwanah.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa Narc Kenya anaamini kwamba umoja wa eneo la Mlima Kenya ni muhimu kwa maslahi ya wakazi.

“Tumejitolea kuunganisha Mlima Kenya na masuala tunayozungumzia yanahusu usalama wa watu na vyama, usawa katika uwakilishi na usawa katika ugavi wa raslimali na maendeleo,” alisema Bi Karua.

Mlima Kenya ‘kuwatahini’ wawaniaji wa urais 2022

Na MACHARIA MWANGI

VIONGOZI wa Mlima Kenya wataandaa orodha ya maswali watakayotumia kuwapiga msasa wawaniaji wa urais kabla ya kutangaza msimamo kuhusu watakayemuunga mkono mwaka 2022.

Viongozi hao wa vuguvugu la Mt Kenya Unity Forum, wakiongozwa na kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua, Jumatatu walisema maswali hayo yanaangazia masuala manne makuu ambayo ni muhimu kwa ustawi wa eneo la Mlima Kenya.

Bi Karua alisema kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto tele huku akitoa mfano wa Kaunti ya Laikipia ambayo inakumbwa na tatizo la ukosefu wa usalama.

“Usalama pia ni suala muhimu ambalo tunahitaji lishughulikiwe haraka na serikali,” akasema Bi Karua.

Alishikilia kwamba suala la ugavi wa rasilimali kwa usawa na uwakilishi linahitaji kushughulikiwa.

Alisema vuguvugu hilo pia linatetea demokrasia ya vyama vingi nchini.

Bi Karua ameteuliwa kuwa msemaji wa vuguvugu hilo linalojumuisha viongozi ambao wamekwama kisiasa katikati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto.

“Lengo letu kuu ni kuunganisha eneo la Mlima Kenya hata baada ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema waziri huyo wa zamani wa Haki.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo alisema kuwa hawatalegeza kamba katika juhudi zao za kutaka kuunganisha eneo la Mlima Kenya.

“Masilahi ya eneo la Mlima Kenya ndio tunatetea. Tunakaribisha kila mtu kujiunga na vuguvugu hili,” akasema Bw Kabogo.

Aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye pia ni kiongozi wa The Service Party, alisema viongozi wa Mlima Kenya wako huru kujadili masuala nyeti yanayoathiri watu wa eneo hilo bila uwoga.

Mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Mwere alisema kuwa viongozi hao wameungana kuhakikisha kuwa jamii za Mlima Kenya zinazungumza kwa sauti moja.

Karua aongoza Mlima kujipanga

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua na wenzake wa Chama cha Kazi Moses Kuria na Mwangi Kiunjuri wa The Service Party of Kenya (TSP), wamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kupuuza eneo la Mlima Kenya katika mipango ya siasa za urithi uchaguzi mkuu unapokaribia.

Walisema kwamba Rais Kenyatta hakualika viongozi wa eneo la Mlima Kenya kwenye mkutano wake na vinara wa vyama vya kisiasa katika Ikulu ya Mombasa, Jumanne wiki hii.

Kwenye mkutano huo, Rais Kenyatta alikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula wa Ford Kenya, Gideon Moi wa Kanu na Wycliffe Oparanya ambaye ni naibu kiongozi wa ODM.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta aliwataka viongozi hao kuungana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ili kumshinda Naibu Rais William Ruto.

“Katika mkutano wa majuzi Mombasa, ni eneo la Mlima Kenya pekee ambalo halikuwakilishwa ilhali kuna eneo ambalo liliwakilishwa na viongozi watatu. Hii ni moja ya sababu zetu kuamua kuunda kundi la kuleta pamoja Mlima Kenya kuchukua mwelekeo wa pamoja,” walisema.

Hisia za viongozi hao ni kwamba Rais Kenyatta ataondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu ujao na eneo hilo linafaa kuwa na kiongozi atakayewakilisha maslahi ya eneo la Mlima Kenya kwenye serikali ijayo.

Viongozi hao walisema kwamba nia yao ni kuunganisha eneo la Mlima Kenya kwa lengo la kuhakikisha maslahi yao yatawakilishwa kwenye serikali ijayo.

Kwa kufanya hivi, viongozi hao walisema wanalenga kongamano la tatu eneo la Limuru ambako eneo la Mlima Kenya litaamua mwelekeo wa kisiasa litakaochukua kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Jamii za Mlima Kenya chini ya mwavuli wa muungano wa Gema unaoleta pamoja Wagikuyu, Waembu na Wameru huwa zinakutana Limuru kuweka mikakati ya kisiasa na kuamua msemaji wao eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu.

“Tunatangaza kwamba Narc Kenya, The Service Party na Chama cha Kazi vimeunda kundi kwa lengo la kuhakikisha masuala na maslahi ya eneo la Mlima Kenya yatashughulikiwa. Tutapanua kundi hili kuhusisha wote walio na nia sawa,” walisema kwenye taarifa fupi iliyosomwa na Bi Karua jijini Nairobi.

Viongozi hao walisema kwamba wanatarajia kongamano la tatu la Limuru ndani ya miezi mitatu ijayo.

Kulingana na viongozi hao, mchakato ambao wameanzisha hautajumuisha wanasaisa pekee mbali utahusisha viongozi wengine wenye ushawishi wakiwemo viongozi wa kidini.

“Tunatambua kwamba maeneo mengine yanaendelea kuungana kwa lengo la kujipanga uchaguzi mkuu unapokaribia lakini sisi katika Mlima Kenya tumebaki nyuma,” alisema Bw Kiunjuri.

Wanasiasa hao walisema kwamba hawana nia ya kuvunja vyama vyao kuunda kimoja kuwasikilisha eneo hilo.

Vile Vile, Bw Kuria na Bw Kiunjuri walisema kwamba hawataunganisha vyama vyao na chama cha United Democratic Alliance cha Naibu Rais William Ruto inavyodaiwa na baadhi ya viongozi.

“Vyama vyote vilivyosajiliwa na msajili wa vyama ni vya kitaifa na kwamba hivyo vyetu sio vya kisiasa. Hatuna nia ya kuvunja vyama vyetu au kutaka vingine vivunjwe kwa kuwa kila kimoja kina malengo yake,” walisema.

Mbunge wa Kieni, Kanini Kega alikaribisha juhudi za wanasiasa hao akisema eneo la Mlima Kenya linahitaji kuungana kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

BBI: Karua adai Uhuru alinyakua mamlaka ya raia

Na RICHARD MUNGUTI

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, na wakili mashuhuri John Khaminwa, Ijumaa waliongoza mawakili 10 kumkosoa Rais Uhuru Kenyatta, kwa kuasisi mchakato wa kubadilisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano ­(BBI).

Bi Karua na Bw Khaminwa waliambia Mahakama ya Rufaa kwamba Rais Kenyatta alinyakua mamlaka ya Wakenya alipoasisi mchakato huo.

Hivyo, mawakili hao waliomba Mahakama ya Rufaa isivuruge uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu, walioamua kwamba mwananchi wa kawaida ndiye mwenye mamlaka ya kuanzisha marekebisho ya Katiba wala sio maafisa wakuu serikalini.

Huku wakiwaomba majaji wa rufaa kukubali uamuzi wa wenzao watano wa Mahakama Kuu – uliosimamisha mchakato huo wa BBI – Dkt Khaminwa na Bi Karua walisema Rais aliteka haki ya mwananchi wa kawaida kwa kuasisi marekebisho hayo kupitia BBI.

Dkt Khaminwa alisema rufaa aliyowasilisha Rais Kenyatta yapasa kutupiliwa mbali; kwa sababu huwa hatii maagizo ya mahakama, na hukiuka mara kwa mara Katiba.

Alitoa mfano wa Rais kukataa kuwaapisha majaji 41 walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

“Waandalizi wa Katiba ambayo ndiyo sheria kuu ya nchi hawakuruhusu viongozi waliochaguliwa kuasisi marekebisho ya katiba,” alisema.

Bi Karua aliomba mahakama kutumia uwezo iliyopewa na Katiba kuwaadhibu wanasiasa wanaotaka kutumia ushawishi wao kukiuka sheria hiyo kuu yaa nchi.

Kinara huyo wa Narc Kenya aliongeza kwamba Mahakama ya Rufaa ina nguvu sawa na zile za viongozi wa Serikali ya Kitaifa, na kwamba mihimili yote ya serikali inapata nguvu kutoka kwa wananchi.

“Nguvu za mahakama hii sio duni kuliko za Serikali Kuu; mihimili yote ya serikali hutoa nguvu zao kwa raia, na mahakama hii ina uamuzi wa mwisho wa kutafsiri Katiba,” alikariri Karua.

Alihoji kuwa wanasiasa wakuu nchini wanataka kubadilisha Katiba kwa nia ya kuendelea kuwa mamlakani.

“Katiba huwekwa ili kuzima matumizi mabaya ya mamlaka na inaoenekana hii haieleweki kwa viongozi wa serikali ya Kenya,” akasema.

Bi Karua aliomba korti hiyo ya rufaa kuagiza maafisa wa serikali ambao wamekuwa wakitumia pesa za umma katika mchakato huo haramu, wazilipe.

Zaidi, anataka mahakama kutupilia mbali rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliozima BBI.

“Ni kupitia uamuzi wa mahakama hii, bila woga au mapendeleo, ambapo nchi hii itaafikia mageuzi yaliyotazamiwa wakati Katiba ya 2010 ilipitishwa,” aliongeza.

Rais wa Mahakama ya Rufaa, Daniel Musinga, majaji Roselyn Nambuye, Hannah Okwengu, Patrick Kiage, Kairu Gatembu, Fatuma Sichale na Francis Tuiyot wanasikiliza rufaa iliyowasilishwa na Rais Kenyatta, Ofisi ya BBI, Mwanasheria Mkuu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mawakili Dudley Ochiel, Ian Mathenge, Edga Busiega , Christian Adole, Evans Ogada, Elisha Ongoya na Muthoni Nyaguto waliomba majaji hao wasihofu bali watupe nje rufaa hiyo.

Bw Adole aliomba mahakama iamuru Rais Kenyatta awarudishie umma pesa zilizotumiwa na kamati ya BBI, aliyoiteua kuzunguka nchini kupokea maoni ya wananchi.

Vigogo wapigania Karua kuunda muungano naye

Na BENSON MATHEKA

MSIMAMO imara wa kisiasa wa kiongozi wa chama cha NARC- Kenya, Martha Karua, umevutia baadhi ya wagombea urais wanaopanga kumrushia chambo wakitaka kumshawishi aungane nao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Tajiriba yake katika siasa na ujasiri wake katika masuala yenye umuhimu wa kitaifa, umefanya jina lake kutajwa na wanamikakati wa wanasiasa wanaopanga miungano ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa Bi Karua hakujibu tulipotaka kupata kauli yake, wadadisi wanasema kutokana na misimamo yake mikali, wengi wanachukua muda kabla ya kumweleza nia yao na wanatumia kila mbinu kumvutia upande wao.

Wadadisi wanasema kwamba, Bi Karua ndiye anayeweza kuwa mgombea bora mwenza wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Naibu Rais William Ruto amepenya eneo la kati ambapo kampeni yake ya hasla imepata umaarufu mkubwa na baadhi ya duru zinasema kwamba, wanamikakati wake pia wametaja jina la Bi Karua.

Bw Odinga hajatangaza azima ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, lakini kulingana na wandani wake wa karibu, waziri mkuu huyo wa zamani ndiye chaguo la chama cha ODM.

Bi Karua ni mmoja wa wanaopinga Mswada wa Kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), uliosimamishwa na Mahakama Kuu na ambao Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wanaunga.

Inasemekana Bw Odinga anatafuta kiongozi wa kuungana naye kutoka eneo la kati ambapo jina la Bi Karua limetajwa na wanamikakati wake kama njia moja ya kumtaka abadilishe nia ya kuunga mchakato huo.

“Pingamizi kubwa ni msimamo wa Bi Karua kuhusu BBI. Hii imefanya wanamikakati wa Bw Odinga kusita japo wanaamini anaweza kuongeza thamani katika kambi yao ikizingatiwa hana rekodi ya ufisadi,” alisema mbunge mmoja wa ODM aliyeomba tusitaje jina lake asiadhibiwe kwa kufichua mikakati ya chama.

Bi Karua na Bw Odinga wamekuwa wakiunga mirengo tofauti ya kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa 2007. Kwenye uchaguzi huo, Bi Karua alikuwa akiunga chama cha Party of National Unity dhidi ya ODM cha Raila Odinga.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Mutahi Ngunyi, Bw Odinga akiungana na Bi Karua, watahitaji asilimia 6 pekee ya kura za eneo la Mlima Kenya kushinda urais.

“Kwenye uchaguzi wa 2007, 2013, na 2017, Raila alikuwa na asilimia 44 ya kura. Kwa hivyo, Uhuru akichagua Karua, unafikiri anaweza kukosa kuvutia asilimia 6 ya kura za Mlima Kenya?” ahoji Ngunyi.

Lakini mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo anasema kwamba, japo Bi Karua ni mwanasheria mkakamavu na mwanaharakati mtajika ambaye msimamo wake unavutia wengi, muungano unaoweza kuvutia ni akiwa na Gavana Ann Waiguru na Peter Kenneth upande mmoja.

Anasema sio rahisi kwa Bi Karua kuyumbishwa na mawimbi ya siasa na kubadilisha msimamo wake.

Duru katika chama cha United Democratic Alliance ambacho Dkt Ruto ananuia kutumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, zinasema kwamba, wanamikakati wa naibu rais walianza kumchangamkia Bi Karua kwa kupinga mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI.

“Tatizo limekuwa ni mbinu ya kumshawishi,” alisema afisa huyo na kukata simu.

Vuguvugu la Linda Katiba halitachoka kunusuru nchi – Karua

Na SAMMY WAWERU

SIEGEMEI upande wowote wa kisiasa katika mchakato wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), amesema Bi Martha Karua.

Kiongozi huyo wa Narc-Kenya amesema mrengo anaoegemea ni ule wa kuokoa Katiba ya Kenya, chini ya vuguvugu la Linda Katiba analoongoza.

“Mirengo kadha imechipuka, kuna inayounga mkono, mingine kupinga kwa sababu za ushawishi wa kisiasa. Mimi ninasimama na mrengo unaofuata sheria kuokoa Katiba – Linda Katiba,” Bi Karua akasema.

Licha ya mahakama kuu kuharamisha BBI, mswada maarufu unaopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga na ambao ni waasisi, wamekata rufaa uamuzi huo.

Mahakama ya rufaa jana ilitangaza kuwa kesi hiyo itasikilizwa kati ya Juni 29 na Julai 2, 2021.

Aidha, itasikilizwa na jopo la majaji saba, wakiongozwa na jaji mkuu wa mahakama ya rufaa, Bw Daniel Musinga.

Wakati ikifutilia mbali, mahakama kuu ilitaja BBI kama mswada haramu, na ambao haukuzingatia sheria za Katiba kuuanzisha.

Mengi ya mabunge ya kaunti, la kitaifa na pia seneti, yaliuidhinisha.

Mahakama kuu ilisisitiza marekebisho ya Katiba yanapaswa kuanzishwa na Mkenya binafsi au kundi la Wakenya binafsi, ila si asasi ya serikali.

“Sheria imeweka wazi kuhusu mchakato wa marekebisho ya Katiba. Linda Katiba itaendelea kusimamia ukweli,” Karua ambaye pia ni wakili akasisitiza.

Bi Karua pia anapendekeza fedha ambazo zitatumika kukata rufaa, zielekezwe kukabili virusi vya corona na kukwamua uchumi.

Karua apendekeza wakati wa uchaguzi kuwe na maafisa maalum

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amesema mvutano unaoshuhudiwa mara kwa mara wakati wa chaguzi kuu nchini, utasuluhishwa endapo kutakuwa na maafisa maalum watakaokuwa wakifuatilia shughuli zote bila ushawishi wowote.

Bi Karua amesema maafisa hao hawapaswi kutoka katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wala kuhusishwa na siasa.

“Wawe maafisa wa kipekee watakaokuwa wakishirikiana na IEBC wakati wa uchaguzi. Kazi yao iwe kufuatilia zoezi zima, upigaji kura unapoendelea, wakati wa kuhesabu wawe ange na kujiri na matokeo yao,” wakili Karua akapendekeza.

Alisema wanapaswa kuwa huru, na wasioripoti kwa asasi yoyote ile. “Mfumo huu ukitekelezwa, hakuna atakayelalamikia udanganyifu na wizi wa kura. Matokeo yao baadaye yatalinganishwa na ya IEBC,” Waziri huyo wa zamani wa Masuala ya Haki na Katiba akafafanua.

Bi Karua alisema kesi za uchaguzi zinazowasilishwa mahakamani huenda zikapungua au hata zikawa historia.

Kila mwaka wa uchaguzi mkuu, idara ya mahakama hupokea malalamishi ya udanganyifu kusakatwa, hasa kutoka kwa wagombea waliobwagwa. Visa vya wizi wa kura vimekuwa vikiripotiwa.

Uhuru na Ruto wajiuzulu ikiwa hawawezi kushirikiana – Karua

Na Wanderi Kamau

KIONGOZI wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, amesema Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha mfano mbaya katika uzingatiaji wa Katiba kwa kumtenga Naibu Rais William Ruto katika uendeshaji wa serikali.

Kwenye mahojiano jana, Bi Karua alisema Rais Kenyatta amevunja sheria kwa kumtenga Dkt Ruto. Bi Karua alisema kuwa ijapokuwa wawili hao wameruhusiwa kutofautiana kuhusu masuala fulani, wanapaswa kubuni ushirikiano katika utendakazi wao kwa manufaa ya Wakenya.

Alisema ikiwa watafeli kufanya hivyo, basi wanapaswa kujiuzulu na kuwapa nafasi wananchi kuwachagua viongozi watakaofanya kazi kwa ushirikiano mzuri.

“Ikiwa watashindwa kushirikiana, basi wajiuzulu na kuwapa Wakenya nafasi kuwachagua viongozi wapya. Walichaguliwa pamoja, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano. Ikiwa rais anahisi hawezi kushirikiana na naibu wake, na ikiwa (rais) anahisi naibu amefanya kitendo kinachokiuka Katiba, basi anapaswa kubuni mchakato wa kumwondoa mamlakani au ashirikiane naye,” akasema.

Uhusiano wa wawili hao ulianza kudorora Machi 2018, baada ya Rais Kenyatta kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

 

Karua na kundi la Tangatanga walivyoungana kushambulia BBI

Na Wanderi Kamau

LICHA ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kupigia debe Mpango wa Maridhiano (BBI), kuna viongozi na wanaharakati waliojitokeza wazi kuupinga mchakato huo.

Miongoni mwao ni kiongozi wa chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua, mwanaharakati David Ndii, John Githongo, Gavana Kivutha Kibwana (Makueni), chama cha Thirdway Alliance, mrengo wa Tangatanga (ambao humuunga mkono Naibu Rais Dkt William Ruto) kati ya wengine.

Bi Karua aliwakosoa vikali Rais Kenyatta na Bw Odinga, akisema wanapaswa kutekeleza Katiba ya sasa badala ya kuanza mchakato wa kuifanyia marekebisho ili “kujifaidi wao wenyewe”.

“Ni makosa kwa wawili hao kuiteka Katiba ya nchi na kuifanya kama mali yao. Rais anapaswa kutekeleza Katiba ya 2010. Hatuhitaji mageuzi yoyote ya kisheria kwani Kenya haina mgogoro wowote wa kikatiba. Changamoto kuu tulizo nazo ni mtindo wa serikali kukwepa utekelezaji wa maagizo ya mahakama,” akasema Bi Karua.

Mwanasiasa huyo aliungana na wanaharakati wengine kutoka Kituo cha Sheria kuwasilisha kesi kortini kupinga mchakato huo.

Mrengo wa ‘Tangatanga’ ulitoa kauli kama hizo, ukisema kuna masuala mengi muhimu yanayopaswa kushughulikiwa nchini badala ya mpango huo.Miongoni mwa viongozi wa mrengo huo waliopiga kura ya ‘La’ kuipinga ripoti ni wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Rigathi Gachagua (Mathira) kati ya wengine.

Karua aonya kuhusu njama ya kuahirisha kura

Na MARY WANGARI

KIONGOZI wa Narc Kenya, Bi Martha Karua amepuuzilia mbali uwezekano wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2022 kutokana na janga la Covid-19.

Alisisitiza kwamba Katiba hairuhusu serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, kuongeza muda wa utawala wake.“Hairuhusiwi kikatiba. Serikali haiwezi kutumia janga kuendeleza utawala wake. Ni sawa na kuongeza muda wa mateso kwa Wakenya na kutumia fedha za umma kujitajirisha.”

“Tunahimiza raia waamke na kukomesha hila hiyo. Serikali hii ni sharti ifahamu kwamba Wakenya hawatavumilia usaliti mkuu ambao ni mapinduzi ya kikatiba. Kinachoendelea ni mapinduzi ya katiba na ni sharti tuyakomeshe,” alisema.

Alitaja serikali kama chanzo kikuu cha matatizo yanayowakumba Wakenya wakati huu wa mabadiliko ya hali ya anga na janga la Covid-19.

Kulingana naye, serikali inayotarajiwa kusuluhishia wananchi matatizo yao, sasa imegeuka kiini cha matatizo hayo wakati huu wa virusi vya corona na msimu wa mvua.

Aliwashutumu wahusika wakuu katika Kamati ya Kitaifa kuhusu Usalama na Kamati ya Kudhibiti Covid-19 kwa kuwaadhibu wakazi katika kaunti tano zilizofungwa, wanaohangaika kufika nyumbani jioni kufuatia kafyu ya mapema.

“Acheni kuwapiga vita Wakenya. Mikakati ya kurahisisha usafiri ibuniwe kwa kuzingatia changamoto za usafiri wa umma na ujenzi wa barabara unaoendelea jijini,” alisema.

Wakili huyo vilevile aliikosoa Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Dkt Fred Matiang’i kufuatia kisa cha hivi majuzi, ambapo wakazi kutoka kaunti hizo tano zilizofungwa walilazimika kukaa barabarani kwa saa kadhaa kwa kukiuka kafyu ya mapema.

Alisema kuwa maafisa wa polisi hawana mamlaka kisheria kuwaadhibu wanaokiuka saa za kafyu akisema ni mahakama tu inayoweza kutoa adhabu.

“Ingekuwa mimi ningesaidia watu kufika nyumbani hasa waliochelewa kwa dakika chache. Ningeelekeza maafisa wangu kuhakikisha hakuna msongamano wa magari kuanzia kituoni hadi barabarani.

“Kwa wanaoonekana kana kwamba walichelewa kimaksudi, ningewapa tiketi za kujiwasilisha kortini siku inayofuatia.Huwezi ukaweka watu barabarani hadi usiku. Hujaruhusiwa kisheria kutoa adhabu, ni korti tu inayoweza kuadhibu. Polisi ni sharti waache kutumia vibaya mamlaka yao ya kukamata watu na kugeuka wanaoshutumu, kutoa hukumu na kuadhibu watu,” alisema.

Bi Karua pia alitofautiana na hatua ya kuwafurusha wakazi katika ardhi za umma bila kuwapa notisi wala makao mbadala.Alifafanua kuwa, mbali na virusi hatari vya corona, wahasiriwa wanakabiliwa na tishio la kupata nimonia katika msimu huu wa mvua ya masika pamoja na matatizo mengine ya kiafya kutokana na msongo wa mawazo.

“Serikali inapaswa kuwapa notisi na kuwasaidia wahasiriwa kuhamia makazi mbadala. Hawawezi tu kutoweka. Serikali ilikuwepo watu hao walipokuwa wakijenga makao yao na haikuwakataza wakati huo. Serikali ina wajibu, ikiwa kweli ardhi hiyo ni ya umma inayohitajika sasa kuendelezwa,” akasema.

Karua: BBI ni hujuma kwa Katiba

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Narc-Kenya Bi Martha Karua ameendelea kupinga Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

BBI inapendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

Bi Karua amesema Jumatatu ahadi zinazotolewa na viongozi na wanasiasa wanaounga mkono BBI kuhusu kuimarishwa kwa Katiba ni hujuma kwa mwongozo huo wa sheria nchini.

Akitaja BBI kama jaribio la mageuzi haramu ya Katiba, alieleza kushangazwa na viongozi wanaosema wanataka Katiba iimarishwe ilhali ni wale wanaopuuza maagizo ya mahakama.

“Iwezekanaje viongozi wanaopuuza maagizo ya korti ndio wanadai kutaka kuiimarisha? BBI ni hujuma kwa Katiba,” akasema Waziri huyo wa zamani wa Sheria.

Karua alisema mchakato wa marekebisho ya Katiba unaoendeshwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga chini ya kundi la ‘Kieleweke’, unaenda kinyume na sheria na kukiuka matakwa ya Wakenya.

“Wakenya ndio wameipa afisi ya Rais, Bunge na Mahakama mamlaka, wanapaswa kuhusishwa katika maamuzi ya Katiba kukarabatiwa. Hawajui yaliyomo kwenye BBI,” akasema.

Karua alidai licha ya Wakenya kuhimizwa waunge mkono na kupitisha ripoti hiyo ya maridhiano, hawajui yaliyomo.

“Nina nakala kadha kutoka mitandaoni, sijui ipi ni halali na kaunti iliyoidhinisha mswada wa BBI ilitumia nakala gani? Wakenya hawajui yaliyomo, wawe makini kwa mageuzi hayo haramu wenyewe wajiokoe kwa kulinda Katiba,” Karua akaonya, akihimiza Wakenya kupinga BBI endapo kura ya maamuzi itaandaliwa.

Kaunti ya Siaya juma lililopita ilipitisha mswada huo, ikifungua jamvi la mabunge ya kaunti kujadili kupitisha au kuangusha ripoti hiyo ya maridhiano.

Kwenye ziara yake eneo la Mlima Kenya siku kadha zilizopita, Rais Kenyatta aliwarai madiwani kupitisha BBI, akiwaahidi kuwapa fedha kununua magari sawa na wanavyotunzwa wabunge.

Kulingana na Bi Karua, hatua ya Rais kuteka nyara madiwani kuunga mkono ripoti hiyo ni sawa na kuwahonga.

Alisema hayo wakati akihojiwa na runinga ya Citizen, ambapo alitaja madiwani kama viongozi wanaopaswa kulinda Katiba kwani walichaguliwa na wananchi kuwawakilisha katika serikali za ugatuzi.

“Wakati wakiapishwa kuingia ofisini waliapa kulinda Katiba, sasa tunaona wamehadaiwa,” akasema.

BBI ilibuniwa baada ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuzika tofauti zao za kisiasa mnamo Machi 2018, wakiapa kuunganisha taifa, hasa baada ya mgawanyiko wa kisiasa kushuhudiwa katika uchaguzi wa 2013 na 2017.

Naibu wa Rais Dkt William Ruto, kwa upande wake ameendelea kuongoza vuguvugu la ‘Tangatanga’ kuipinga BBI mtazamo wake ukionekana kuwiana na wa Bi Karua.

BBI: Karua atawezana?

Na MWANGI MUIRURI

KINARA wa Narc Kenya Martha Karua amejipata kona mbaya kutoka kwa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta katika serikali, baada ya kujitokeza kuongoza upinzani dhidi ya mpango wa BBI.

Siku moja tu baada ya kutoa tangazo hilo wakereketwa wa upande wa serikali wameanza kumpaka tope shujaa huyo wa kupigania mageuzi na utawala bora, wakimtaja kama anayetumiwa na Naibu Rais William Ruto kuongoza kampeni ya ‘La’ dhidi ya BBI.

“Bi Karua ni kivuli cha Ruto ambaye ndiye mkuu wa pingamizi dhidi ya BBI. Karua hana uwezo wowote wa kuongoza upinzani dhidi ya BBI lakini anapigwa jeki na waasi katika serikali,” Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe aliambia Taifa Leo jana.

Kombora hilo ni mwanzo tu wa vita vikali ambavyo Bi Karua anatarajiwa kukabiliana navyo kutokana na msimamo wake dhidi ya BBI yake Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wachanganuzi wa siasa wanasema mbunge huyo wa zamani wa Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga atakumbana na changamoto za kifedha kuendesha kampeni zake kote nchini, propaganda za kumvunja moyo na kumchafulia sifa pamoja na kutumiwa kwa taasisi kama vile polisi kuhujumu juhudi zake.

Serikali pia iko tayari kutumia kila mbinu kusukuma BBI, ambapo tayari imewaahidi MCA kuwapa Sh2 bilioni kila mmoja za kununua magari ili wapitishe BBI.

Changamoto nyingine inayomkabili mwanasiasa huyo ni kuwa anaoshirikiana nao kwenye juhudi zake hawana umaarufu wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa.

Tatizo ni kwamba licha ya Bi Karua kuwa mweledi wa kujadili masuala nyeti kwa ufasaha, atakuwa na wakati mgumu kuwashawishi wananchi kupigia BBI kura ya ‘La’, ikizingatiwa wengi wa Wakenya wamezoea kushabikia siasa duni za kikabila na kuhongwa na wanasiasa.

Lakini Bi Karua anashikilia kuwa hatarudi nyuma na hasukumwi na yeyote katika kupinga BBI: “Niko na haki ya kusimama kwa imani yangu ya kisiasa bila kushambuliwa kama anayesukumwa na wengine.

“Nilipambana kuokoa utawala wa Mzee Kibaki baada ya uchaguzi wa 2007. Wakati huo wote mimi sikuwa kivuli cha yeyote bali nilikuwa shujaa. Mbona leo naitwa kivuli?” akateta Bi Karua.

Mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi na aliyekuwa Mbunge wa Maragwa, Elias Mbau naa wanapuzilia mbali juhudi za Bi Karua wakidai kuwa anatafuta umaarufu wa kuwania ugavana wa Kaunti ya Kirinyaga mwaka ujao, wakisema hana makali ya kuzima BBI.

“Hatupingi BBI ili kujipatia umaarufu bali tunalenga kuhamasisha Wakenya wagutuke kuhusu njama inayoendelezwa na walio madarakani. Nikiwa na imani kuwa BBI haitufai kwa sasa na sio suala la dharura, nimeamua kujaza pengo la kuongoza walio na imani kuwa wanatapeliwa na kuhadaiwa kisiasa na Rais Kenyatta na Raila.”

Bi Karua anataja BBI kama njama ya viongozi wachache wenye ushawishi kisiasa kuendeleza maslahi yao ya ubinafsi, na kuwa haina mchango kwa maisha ya Wakenya walio wengi.

“Huwezi ukabomoa uchumi kupitia uharibifu wa biashara, kukopa fedha kiholela, kukosa kupambana na ufisadi na kuongeza raia ushuru wa juu kupindukia, kisha uje kutwambia makosa uliyofanya yatarekebishwa na BBI. Hata hauna heshima kwa Katiba tuliyo nayo kisha unaambia Wakenya kuwa inahitaji kurekebishwa! Huu ni unafiki!”

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata anamtetea Bi Karua akisema kuwa anaeleza tu maoni ya wengi na ana ukakamavu wa kutosha kufanikiwa.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua naye anasema wanaomkashifu Bi Karua ni wanasiasa wanaolenga kunufaika na BBI kibinafsi.

Bw Mark Bichachi, ambaye alihudumu kama mtaalamu wa mikakati ya siasa wa Bi Karua, anamtaja mwanasiasa huyo kuwa miongoni mwa watu wachache nchini walio na msimamo thabiti kuhusu imani yao. Alisema Bi Karua sio mgeni katika siasa za kutetea yaliyo ya haki kwa Wakenya.

Bw Bichachi anataka harakati za Bi Karua kusukumana na aliyekuwa Rais Daniel Moi katika vita vya ukombozi wa kidemokrasia.

Karua sasa amlaumu Uhuru

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amemsuta Rais Uhuru Kenyatta kwa kile anachodai ni kuwatelekeza watu wa Kirinyaga licha ya kuwepo kwa ushahidi kuwa kaunti hiyo inazongwa na usimamizi mbaya.

“Inaonekana kuwa Rais hajali kwamba Gavana Anne Waiguru na washirika wake wanapora mali ya Kirinyaga. Maseneta wa Jubilee walikuwa mstari wa mbele kumtakasa Waiguru licha ya ushahidi kuonyesha kuwa alihusika na ufisadi,” akasema.

Akihojiwa katika kituo cha runinga cha Citizen Jumatatu asubuhi, Bi Karua ameonya kuwa endapo Rais Kenyatta hataingilia kati suala hilo ambalo limeibua uhasama baina ya madiwani na Gavana Waiguru, wakazi wa Kirinyaga watakuwa katika masaibu tele.

Karua ambaye aligombea akashindwa na Waiguru katika kinyang’anyiro cha ugavana 2017 vilevile alidai kuwa wanachama wa kamati maalum iliyochunguza tuhuma dhidi ya Waiguru walipokea simu kutoka kwa watu fulani wakiwataka wasimhusishe gavana huyo na makosa hayo.

“Ningependa kusema wazi kwamba wanachama wa kamati hiyo walipokea simu. Tunafahamu kwamba kulikuwa na mikutano ya usiku; tunafahamu Spika alipigiwa siku na habari hizo tulipewa na maseneta ambao hawakutaka kutajwa,” akasema.

Akaongeza: “Kulikuwa na ushahidi tosha kwamba zabuni zilipeanwa kinyume cha sheria na maseneta pia walikiri watu wasiohitimu waliajiriwa. Kwa mtazamo wangu hayo ni makosa ambayo yana uzito wa kuwa msingi wa kuondolewa kwa gavana mamlakani,” Bi Karua akasema.

Mnamo Ijumaa, Kamati maalum ya Seneti iliyochunguza tuhuma kwenye hoja ya kumwondoa afisini Bi Waiguru ilimwondolea lawama.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Cleophas Malala (Seneta wa Kakamega) alisema Bunge la Kaunti ya Kirinyaga halikufafanua tuhuma za ukiukaji wa Katiba, matumizi mabaya ya afisi na ufisadi, ambazo gavana huyo alihusishwa nazo.

“Baada ya kamati hii kuchunguza suala hili, kulingana na sehemu ya 33 na sheria za seneti nambari 75 (2) imebainika kuwa mashtaka mawili dhidi ya gavana hayakufafanuliwa,” akasema Bw Malala.