Wazazi wa watoto waliouawa wakiri walijua Masten Wanjala

Na MARY WAMBUI

WAZAZI wa watoto waliotekwa nyara na kunyonywa damu na Masten Wanjala, 20, jana walikiri kuwa walimfahamu vyema mshukiwa kabla ya kugeuka kuwa muuaji wa watoto wao.

Wazazi hao waliofika katika mochari ya City jijini Nairobi, wakati wa shughuli ya upasuaji kubaini kilichosababisha vifo vya watoto hao, walisema kwamba, hawakudhani kwamba Masten waliyemfahamu angedhuru watoto wao.

Masten anadaiwa kuua watoto 13 baada ya kuwanyonya damu katika maeneo mbalimbali nchini.Wazazi waliogubikwa na majonzi waliketi nje ya chumba cha upasuaji ambapo Afisa Mkuu wa Upasuaji wa Serikali Dkt Johansen Oduor aliongoza kikosi cha maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) katika juhudi za kubaini kilichosababisha vifo vya watoto hao.

Miili miwili iliharibika kiasi cha kutotambuliwa. Moja kati ya miili hiyo ilisalia mifupa tu.Wazazi wa Junior Mutuku Musyoka, 12, na Charles Were Opindo, 13, baadaye walitambua miili ya wana wao.

Wavulana hao walitoweka kijijini Kitui katika mtaa wa mabanda wa Majengo walipokuwa wakicheza kati ya Juni 7 na Juni 30, mwaka huu.

Baadaye, miili yao ilipatikana ikiwa imetupwa vichakani katika eneo la Kabete.Jana, Dkt Oduor alisema wavulana hao wawili walikufa baada ya kunyongwa na walikuwa na majeraha kichwani.

Huku familia hizo zikijiandaa kwa ajili ya mazishi ya wanao, familia ya Brian Omondi aliyetoweka kijijini hapo mnamo Juni 10, mwaka huu, bado haijafanikiwa kupata mwili wake.

Wanashuku kuwa huenda mwili wake ni miongoni mwa maiti mbili ambazo hazijatambuliwa.

Mama yake, Grace Adhiambo alisema kuwa, walifika mochari kutafuta mwili wa mwanawe lakini hawakuupata. “Mshukiwa alipokamatwa, nilipeleka picha ya mwanangu kwa maafisa wa DCI ili wamwonyeshe mshukiwa ikiwa atamtambua,” akasema Bi Adhiambo.

Alisema kuwa maafisa wa DCI walipomwonyesha picha alisema: “Aah ni Brian, huyu nilimuua na nikatupa mwili kwa maji.”

“Hicho ndicho kilitufanya kuamini kwamba mwili wa mwanangu ni miongoni mwa maiti zilizopatikana.”

Moja ya miili ambayo haijatambuliwa ni mvulana na mwingine ambao umesalia mifupa ni msichana.Familia nyingine ambayo haijapata mwili wa binti yao ni ya Halyma Hassan aliyetoweka Februari mwaka huu.

Baba ya Halyma, Hassan Suleiman, 40, alisema kuwa bintiye wa umri wa miaka minane, alitoweka katika hali ya kutatanisha.

Nilianza kuua nikiwa na umri wa miaka 16 – Masten

Na MARY WAMBUI

UCHUNGUZI umefichua kwamba Masten Milimu Wanjala, 20 anayeshukiwa kuteka nyara watoto, aliwaua waathiriwa wake 13 peke yake kwa kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, Alhamisi wapelelezi walisimamisha utafutaji wa miili zaidi, baadhi ambayo inahitaji matingatinga kufikia ilikotupwa.

“Baadhi ya familia zilizohuzunishwa na kupotea kwa watoto wao hazikujua kwamba walikuwa wameuawa na hayawani huyo na miili yao kutupwa vichakani eneo la Lower Kabete. Wengine walitumbukizwa kwenye mitaro ya maji-taka jijini na kuachwa kuoza,” Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) George Kinoti aliandika kwenye Twitter.

Mwathiriwa wake wa kwanza, Purity Maweu, 12, alitekwa nyara kutoka Kiima Kimwe, Kaunti ya Machakos mwaka wa 2015 na mshukiwa ambaye alifyonza damu yake hadi akafariki.

Mwili wa Maweu ulipatikana baadaye na jamaa yake na ukazikwa Machakos bila kilichosababisha kifo chake kubainika.

Wakati huo, mshukiwa huyo alikuwa na umri wa miaka 16. Mauaji ya Maweu yakawa mwanzo wa kutoweka kwa watoto wengine wengi na kupatikana wameuawa, jambo lililosababishia familia nyingi uchungu na mateso wakiwasaka watoto wao waliopotea, bila kuwapata.

Maelezo ya visa ambavyo mshukiwa huyo ametekeleza yanaonyesha jinsi kati ya 2015 na Julai 7 mwaka huu, watoto zaidi waliendelea kujipata katika unyama wake hadi Jumanne wiki hii wapelelezi waliokuwa wakifuatilia kutoweka kwa mtoto mmoja walipomfumania katika maficho yake mjini Kitengela.

Baada ya kukamatwa, Wanjala alikiri kwamba ameua zaidi ya watoto 10 ambao alitambua kama Aron, 13 ambaye alinyongwa eneo la Kamukuyo, Kimilili mwaka wa 2019 na Augustine Mukhisa, 13 ambaye mwili wake pia ulipatikana kwenye gunia katika choo karibu na nyumba ya baba yake eneo la Chwele, Bungoma mwaka 2020.

Hiki ndicho kijiji ambacho Wanjala anatoka na polisi wanashuku alitoroka baada ya kuua mtoto mwingine miaka kadhaa iliyopita.

Mnamo Disemba 2020, Wanjala alikiri kuwateka wavulana wawili wa kurandaranda mitaani kutoka mitaa ya Eastleigh na Mathare na kuwanyonga katika visa tofauti na kutupa miili yao.

Mnamo Juni 30 na Julai 7 mwaka huu, mshukiwa huyo pia aliteka nyara na kuwanyonga wavulana Charles Opindo Bala 13, na Junior Mutuku Musyoka, 12.

Mnamo Jumanne, alipeleka wapelezi katika eneo walikopata miili karibu na shule ya Kabete Approved School, Nairobi na mwingine kichakani karibu na Spring Valley, Westlands uliopatikana Jumatano.

Mwathiriwa mwingine alitambuliwa kama Austin, 12 kutoka Kitengela ambaye mshukiwa alikiri kwamba alimnyonga na kutupa mwili wake kwenye mitaro wa maji taka katika barabara ya General Waruinge, Nairobi. Mwili huo haujapatikana.

Pia kuna mvulana wa miaka 13 aliyemtaja kwa jina Josee aliyemtaka nyara kutoka Mlolongo na kutupa mwili wake katika mtaro wa maji taka kwenye barabara ya General Waruinge, Nairobi. Mwili wa mtoto huyo pia haujapatikana.

Mwathiriwa wake wa 10, Musa, alipatikana amenyongwa na mwili wake kuwekwa kwenye gunia lililotupwa katika mzunguko wa barabara ya Eastleigh 12th street, mtaani Eastleigh, Nairobi. Mwili huo ulipelekwa mochari na baadaye kuzikwa.

Bw Kinoti alisema mshukiwa alikuwa akiwalewesha waathiriwa kwa kutumia dawa ya unga au vinywaji vilivyowekwa dawa.

“Waathiriwa walikuwa wakilazimishwa kunywa, kunusa au kupuliziwa kitu kilichowalewesha kabla ya kutendewa ukatili. Pia, wapelelezi walipata kalenda iliyokuwa imeandikwa tarehe ambayo kila mauaji yalitendwa,” alisema Kinoti.