AKILIMALI: Mkulima anavyochuma kutokana na matundadamu

Na PETER CHANGTOEK

MATUNDADAMU yenye rangi nyekundu yananing’inia kwa mimea katika shamba moja lililoko katika eneo la Ainabkoi, katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Mja anapoingia katika shamba hilo, huvutiwa na matunda hayo yanayomfanya yeyote kutokwa na mate mdomoni, anapoyatazama.

Elisha Onzilu, 40, ni mwenye mimea hiyo iliyonawiri. Isitoshe, ana shamba jingine katika eneo la Nyaru – takriban kilomita 47 kutoka mjini Eldoret – katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, na jingine eneo la Kipkabus, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kwa jumla, Onzilu ana mimea ya matundadamu katika ekari tano anakochuma kati ya kilo 700 hadi 1,000 za matunda hayo kila baada ya wiki mbili kwa kila ekari.

Onzilu alipokuwa shuleni walikuza matundadamu shambani mwao, ila yalikuwa machache tu ya kuliwa.

Pindi alipokamilisha kidato cha nne mnamo 2,000 alijipa shughuli ya kukuza miche ya mivinje, mikalatusi na mingineyo kabla kujitosa katika matundadamu

Aliuza miche hiyo kwa taasisi kadha za serikali. Hata hivyo, kiangazi kilipozidi 2010, soko la miche likanyauka akalazimika kugeukia aina nyingine ya kilimo ambayo ingempa fedha.

“Nikafanya utafiti kuhusu matundadamu, ambapo pia nilielekea Nairobi kuchambua soko,” asema na kueleza kuwa alianza na suala la soko kabla kuzamia shughuli hasa ya ukuzaji mimea hiyo.

Mnamo 2011, akawa anayanunua matundadamu kutoka kwa wakulima walioishi karibu naye na kuyauza.

“Nayanunua na kutumia wateja Nairobi. Nilipoona soko limepanuka niliomba wazazi nusu ekari ili nianze kukuza matunda yangu mwenyewe,” alihoji mkulima huyo.

Kilimo hicho alikichangamkia 2012, na muda si muda akaanza kuhesabu faida.

“Yalipoiva 2013 nikapata kampuni ya Fresh & Juice mjini Limuru, iliyokuwa imepewa tenda ya kuuzia duka la jumla la Nakumatt matundadamu.

“Mara moja nikaanza kuweka akiba na ilipofika 2016 nikanunua shamba la ekari moja kule Kipkabus kwa pesa hizo,” afichua na kusema alitumia mtaji wa Sh100,000 kuanzisha kilimo hicho.

Mbali na ya kwake Onzilu pia aliendelea kuyanunua ya wakulima wengine ili kuwaridhisha wateja wake, ambao sasa walikuwa wengi.

Ni hali iliyomfanya kuelekea Nairobi kutafuta nafasi ya kuwasilisha matundadamu kama mmoja wa saplaya wakubwa katika soko maarufu la matunda la Marikiti, na akafanikiwa.

Licha ya maduka ya Nakumatt kufungwa, hilo halikumwathiri kwani alikuwa ameshaanza kukita katika soko la Marikiti na pia lile la City Park, lililoko eneo la kifahari la Parklands mjini Nairobi.

Katika shamba lake la Kipkabus, mkulima huyu alichagua pia kukuza mikarakara. Hata hivyo, alipitia changamoto si haba.

“Mimea ilifagiliwa na magonjwa, faida ikaharibiwa na mfumkobei na kwa jumla ilinitoa jasho sana. Nikachuma tu miaka miwili 2017 na 2018,” aeleza baba huyu wa mtoto mmoja.

Mwaka 2018 alikodi shamba lingine la ekari mbili katika eneo hilo la Kipkabus, akalitumia kupanua kilimo chake cha matundadamu na sasa anaendelea kuyachuma.

“Kwa jumla, nina ekari tano za matundadamu; tatu katika Kaunti ya Uasin Gishu na mbili katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet,” asema.

Aina ya Giant Red Oratia ndiyo huzaa matunda mengi; mmea mmoja hutoa kilo mbili kila baada ya wiki mbili. Mkulima anaweza kuchuma kilo 2,000 kwa shamba la ekari moja la aina hiyo.

Onzilu hupanda miche 1,200 katika ekari moja.

“Wakati wa upanzi tunatumia mbolea debe moja. Unaacha nafasi ya mita mbili kati ya mimea,” adokeza mkulima huyo.

Huchimba mashimo ya kina cha futi mbili na upana wa futi mbili, akachanganya mbolea asilia debe moja au mbili na mchanga uliotoka kwa mashimo hayo, akanyuyiza maji na kupanda miche.

Kila baada ya wiki mbili Onzilu huchuma matundadamu kati ya kilo 750 na 1,000 kutoka kwa ekari moja.

Mmea unapozaa matunda kwa mara ya kwanza, aghalabu, mavuno si mengi, lakini kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo kiwango cha mazao kinazidi kuongezeka.

Mkulima huyo, ambaye pia huikuza miche ya matundadamu na kuwauzia wakulima wenzake, anasema janga la Covid-19 limeathiri soko la matunda hayo.

Hapo awali, alikuwa na mteja ambaye alikuwa akimchukua tani nzima ya matundadamu; lakini kwa sasa hununua kati ya kilo 300 na 400 pekee.

Aidha, kwa sasa anayauza matundadamu kwa bei ya kati ya Sh70 na 80 kwa kilo moja. Hapo awali aliyauza Sh100 kwa kilo.

Anasema uaminifu baina ya mwuzaji na mteja ni muhimu sana katika biashara.

“Nina wateja zaidi ya 20 katika soko la Marikiti lakini hatujawahi kuonana. Mimi huwatumia tu matunda nao hunitumia pesa,” aeleza.

Ilivyo kawaida, yeye hunyunyiza dawa kuua wadudu wanaovamia mimea hiyo.

Aidha, magonjwa kama vile Tree Tomato Mosaic ni hatari kwa matunda hayo.

Yote tisa, Onzilu asisitiza kilimo cha matundadamu kina faida zaidi ikilinganishwa na mimea mingine. Anapania kuongeza thamani kwa matunda yake katika siku zijazo.

AKILIMALI: Mwanafunzi wa JKUAT avuna hela kwa kukuza matundadamu

Na SAMMY WAWERU

ZIARA aliyofanya Charity Kigera kwa mkulima mmoja wa matundadamu Nyandarua mapema 2019 ilichochea ari yake kuingilia kilimo cha matunda.

Msichana huyu ambaye yuko mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), anakosomea kozi ya Masuala ya Savei, anasema alikaribishwa na miti ya matundadamu maarufu kama tree tomato pia tamarillo iliyozaa matunda yaliyonawiri.

“Alinichumia tunda na nilipolikumbatia lilijaa kwenye kiganja cha mkono,” anasema Charity, 25, akielezea kwamba mkulima huyo alikuwa na miti mitano pekee.

Anafafanua, ilizaa matunda kiasi kwamba akihesabu kila tawi lilikuwa na matundadamu yasiyopungua 14. Taswira hiyo ilimshawishi, na huo ukawa mwanzo wa safari yake katika kilimo.

Charity anasema hakulila. Alienda nalo nyumbani akiwa na wazo, wazo atakavyokuwa mkulima wa matundadamu.

Ikizingatiwa kuwa ni mwanafunzi, alizungumza na babake ambaye pia ni mkulima ingawa wa viazi na mahindi, akamuarifu mipango yake chipuka. Hakusita kumpa kipande cha ardhi atimize matamanio yake.

“Nililikama, nikatoa mbegu zake, nikaziosha na kuzikausha kwenye kivuli kwa muda wa wiki moja na nusu hivi,” anaelezea, akisema utafiti aliofanya mitandaoni kupitia makala ya ukuzaji wa matundadamu ulimshauri asizikaushe kwenye jua.

Anasema miale ya jua huharibu machipukizi ya mbegu, kauli yake ikipigwa jeki na David Nderitu mkulima hodari wa matundadamu Nyeri.

“Miche ya matundadamu inatokana na mbegu za matunda makubwa yaliyokomaa, yakanawiri na ambayo mti mama umestawi na wenye afya,” Nderitu anasema, akiongeza kuwa gharama ya kununua miche inaweza kuondolewa kwa kujikuzia.

Tundadamu linakadiriwa kuwa na kati ya mbegu 200 – 400, Charity Kigera akieleza kwamba ilimchukua kipindi cha muda wa miezi mitano kuandaa miche.

“Uamuzi wa kuingilia kilimo ulienda sambamba na kipindi ambacho nilikuwa nimetumwa kufanya mazoezi ya kozi ninayosomea,” anadokeza mkulima huyu mchanga.

Charity anasema alikuwa ameandaa jumla ya miche 270, ila alipanda 200 kwenye robo ekari, iliyosalia akawapa majirani. Kwa kuzingatia taratibu faafu kitaalamu, ekari moja inaweza kusitiri karibu mitundadamu 1, 000.

Amekumbatia mfumo wa kilimohai, na anaiambia Akilimali kwamba alitumia mbolea ya mifugo, hususan mbuzi katika shughuli za upanzi.

Badala ya kutumia fatalaiza kunawirisha mazao, Charity anasema kwenye mashina ya mitundadamu aliweka mbolea ya mbuzi ‘iliyoiva’ vizuri.

Magonjwa yanayoathiri tamarillo ni sawa na ya matunda mengine, ila kwa mkulima huyu anasema hakushuhudia ugonjwa wowote.

“Wadudu walioonekana japo niliwakabili kwa dawa ni vidukari,” anasema.

Matunzo mengine aliyofanya ni palizi dhidi ya kwekwe, kupogoa matawi ili kuondoa ushindani, na kunyunyizia maji hasa mitundadamu ikiwa michanga na ilipoanza kuchana maua na kutunda.

Charity Kigera mwanafunzi wa JKUAT ambaye anakuza matundadamu. Picha/ Sammy Waweru

“Kwetu tuna kisima chenye urefu wa futi 100, ambacho hutumia nguvu za umeme kupampu maji, hivyo basi mahangaiko ya maji hayapo,” anaelezea.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema ufanisi katika uzalishaji wa matunda unategemea kuwepo kwa maji ya kutosha.

“Kilimo chochote kile cha matunda kinafanikishwa na uwepo wa maji ya kutosha,” anasisitiza mtaalamu Daniel Mwenda, akihimiza wakulima kukumbatia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji.

Kulingana na Charity, changamoto kuu iliyomkumba ni matawi kuanguka, kwa kile anataja kama “matundadamu kuzaa ajabu”. Kibarua kikawa kuyasitiri kwa miti.

Kijiji cha Bahati, Gathanje, Kaunti ya Nyandarua, ni tajika katika ukuzaji wa viazi na mahindi, ila katika shamba la msichana huyu, taswira ni tofauti kabisa. Ni bustani ambalo linavutia kutokana na alivyolirembesha kwa matundadamu.

Alianza kufanya mavuno Novemba 2020, na kutokana na yalivyonawiri hofu yake ilikuwa moja tu; “Nitapata wanunuzi ilhali yamezaa kiasi cha kuangusha matawi?”

Ni wasiwasi uliomchochea kuyapiga picha na kuzipakia kwenye makundi yanayotoa huduma za kilimo mitandaoni.

Anasimulia kwamba majibu aliyopata, ya oda, yamemuacha kujutia ni heri angeyakuza kwenye ekari moja au hata zaidi.

“Wengi walikuwa wanunuzi wa kijumla wanaoagiza kilo zisizopungua 200, na kilichonishtua zaidi ni huyu mkulima aliyeniuliza ikiwa mazao niliyonayo yanaweza kujaa gari aina ya Probox,” anafafanua.

Ni gapu ya uhaba wa matundadamu aliyotambua Charity, kuanzia mwaka huu wa 2021 akipanga kuyalima kwenye ekari moja. Kutokana na oda alizopata, anakiri kiwango cha uzalishaji wa matundadamu Kenya ni cha chini sana, kikilinganishwa na walaji.

Ingawa yaliyoiva shambani yameisha, anasema kufikia sasa ameuza zaidi ya kilo 200, kila kilo ikinunuliwa Sh70.

“Cha kustaajabisha, miti inaendelea kuchana maua na kutunda,” anaeleza. Akifanya hesabu, anasema gharama aliyotumia kufikia sasa haizidi Sh5,000.

Huku akisubiri kufuzu kozi anayosomea JKUAT, licha ya mkurupuko wa janga la Covid-19 mwaka uliopita wa 2020 kuathiri kalenda ya masomo nchini, Charity anasema hatua aliyochukua kuingilia kilimo ni maandalizi ya jukwaa kujiajiri kupitia zaraa.

“Ndoto zangu zimekuwa kufanya kilimo cha matunda kama gange ya ziada, hata nikipata ajira nitakapohitimu chuoni. Nafasi za kazi za ofisi Kenya ni finyu mno, maelfu ya vijana waliofuzu kwa taaluma mbalimbali wakiendelea kuhangaika kwa kukosa ajira,” anasema, akishauri vijana kuthamini kilimo.

Anafichua, kwa sasa amejituma kufanya utafiti namna ya kuongeza matundadamu thamani, kutengeneza bidhaa zitokanazo nayo.