Matatizo ya akili yazidi kutokana na sheria kali za coronavirus

Na WAANDISHI WETU

WATAALAMU wa afya ya akili wameitaka serikali kuweka mipango ya kupunguzia Wakenya msongo wa mawazo, inapopambana na virusi vya corona.

Hii ni kutokana na ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai wakilalamikia hali ngumu ya maisha, kuongezeka kwa mizozo ya kinyumbani na wengi kulewa chakari nyumbani wakijaribu kujiondolea mawazo.

Mtaalamu wa saikolojia Prof Halimu Shauri, ameonya kwamba matukio aina hii yataendelea kushuhudiwa kama serikali haitajali kuhusu afya ya kiakili ya wananchi ikiwemo wanaowekwa karantini.

Alisema masharti makali kama yanayohitaji watu kutokongamana wala kukaribiana, kujifungua nyumbani, pamoja na hali ngumu za maisha ni sababu tosha za kufanya binadamu kutatizika kiakili, ingawa ni masharti muhimu kupambana na ueneaji wa virusi vya corona.

“Tumeathirika kihisia, kiuchumi na unapoambiwa ukae karantini, mara msikaribiane…unakosa ule usaidizi uliozoea kutoka kwa wengine. Hatuna marafiki wa kuzungumza nao tena,” akaeleza Prof Shauri.

Aliongeza kuwa watu wanapoachwa pweke huwa wanawaza sana kuhusu matatizo yanayowakumba kimaisha na kuchukua hatua zinazowadhuru.

Anusurika kifo

Mnamo Jumamosi mchana, mwanamume mwenye umri wa makamu alinusurika kifo katika Kaunti ya Nakuru baada ya kujirusha kutoka kwenye daraja la wapita njia katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Nairobi.

Marafiki wake walisema jamaa huyo alikuwa ni mhudumu wa hoteli mjini Nakuru na alishikwa na msongo wa mawazo aliposimamishwa kazi wakati biashara zilipoathirika na masharti ya kupambana na Covid-19.

Kisa hiki kilijiri siku chache baada ya kingine katika kijiji cha Wuoth Ogik, Kaunti ya Migori, ambapo mwanamke alimrusha mtoto wake mtoni kisha akajaribu kujitoa uhai.

Kulingana na walioshuhudia, mwanamke huyo alikuwa amelalamikia hali ngumu ya kiuchumi kutokana na janga la corona.

Katika Kaunti ya Nyandarua, mwanamume aliacha watu midomo wazi alipovaa gunia na kuandamana na binti yake mdogo hadi katika Hospitali ya JM Memorial akitaka mkewe atolewe hospitalini.

Alidai maadui wa kibiashara wa mkewe waliwadanganya polisi kuwa alisafiri Tanzania majuzi ndipo akawekwa karantini.

 

Ripoti za Samuel Baya, Waikwa Maina, Valentine Obara na Ian Byron

Msongo wa mawazo na ulevi kupindukia ni hatari

Na SAMMY WAWERU

TATIZO la nafasi finyu za ajira nchini Kenya hasa kwa vijana ni suala ambalo limeendelea kusalia kitendawili.

Maelfu ya vijana kila mwaka hufuzu kwa vyeti mbalimbali vya masomo kutoka taasisi za juu za elimu.

Wengi wameishia kufanya kilimo, biashara na wengine kutafuta kazi ughaibuni kwa ajili uhaba wa nafasi za ajira, angaa kuzimbua riziki.

Baada ya kuhitimu Stashahada ya Habari na Teknolojia (IT) kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta, (JKUAT) 2006, Kenneth Kimathi alijiunga na orodha ya vijana wanaosaka ajira.

Bw Kenneth Kimathi, katika hafla uwanjani Ndumberi iliyowaleta watu 5,200 waathiriwa wa pombe pamoja na wakafuzu kutoka mafunzo ya utaratibu wa kujisuka upya na kuasi ulevi kupindukia. Picha/ Sammy Waweru

Alihangaika miaka kadhaa na kwa neema ya Mungu barobaro huyu alipata kazi katika kambi moja ya kijeshi, nchini Afghanistan.

“Nilikuwa nikituma maombi ya kazi katika kampuni na mashirika tofauti kitengo cha kozi niliyofanya japo hakuna mwaliko niliopata. Mwanzoni mwa mwaka 2011 nilipata nafasi ya kazi katika kambi moja ya kijeshi Afghanistan,” anasema Kimathi.

Anasimulia kwamba alifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, kiasi fulani cha mshahara akikituma nyumbani, Kenya, kwa mmoja wa familia yake kama akiba.

Kuchapa gange bila kuweka akiba, kumewaacha wengi maskini hohehahe wanapostaafu.

Akiba kufujwa

Bw Kimathi anasema maafikiano yake na mwanafamilia aliyepokea pesa ilikuwa amnunulie kipande cha ardhi na kujenga vyumba vya kukodisha.

“Niliporejea nchini 2012 kwa likizo, nilipata hakuna kilichofanyika; kwa maana pesa nilizotuma zilifujwa,” afichua.

Pigo hilo lilifungua sura nyingine ya maisha ambapo alijitosa katika unywaji wa pombe kwa sababu ya msongo wa mawazo.

Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, kijana huyu alifuja karibu Sh500,000 kupitia unywaji wa chang’aa.

Kimathi ambaye ni mzaliwa Meru, ingawa anaishi eneo la Kahawa Wendani, Kiambu, anaendelea kueleza kuwa likizo ilipokamilika alirudi Afghanistan na ndipo masaibu yake yalizidi.

“Kwa kawaida wanaofanya kazi nchini humo kutoka mataifa ya kigeni hupitia ukaguzi wa kimatibabu, nilipatikana na ugonjwa wa Kisukari. Sikuruhusiwa kufanya kazi tena, nikalazimika kurejea Kenya,” afichua.

Ugonjwa wa Kisukari kwa ajili ya pombe

Unywaji wa pombe kupindukia husababisha upungufu au ukosefu wa chembechembe za Insulin mwilini.

Kulingana na MaryAnn Njeri, mtaalamu wa masuala afya katika Hospitali ya Guru Nanak jijini Nairobi anasema upungufu ama ukosefu wa Insulin mwilini husababisha ugonjwa wa Kisukari.

“Dhana kuwa utumiaji wa sukari husababisha ugonjwa huu si kweli, ingawa sukari nyingi si bora kiafya. Unywaji wa pombe kupita kiasi ni mojawapo ya kiini cha Kisukari,” anafafanua, akiongeza kusema kuwa pia kuna visa vinavyotokana na urithi wa ugonjwa huu.

Aghalabu Kisukari huathiri kongosho na akirejela suala la Kimathi, mdau huyu anasema huenda alionekana hali yake kiafya haitamuwezesha kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za kampuni ama shirika aliloajiriwa.

“Visa vya aina hii hushuhudiwa. Ni muhimu kukumbusha kuwa unywaji wa pombe kupindukia husababisha Saratani,” aeleza Bi Njeri.

Kuna visababishi kadha wa kadha kwa mtu kujipata katika hali ya kunywa pombe. Mtaalamu huyu anaorodhesha presha ya marafiki waraibu wa vileo na mzongo wa mawazo, kama viini vikuu.

“Wale wa mzongo wa mawazo wanapaswa kupata ushauri wa kina,” ahimiza.

Ni kufuatia akiba yake kufujwa na kumwaga unga, Bw Kimathi alizidiwa na mawazo, akakumbatia ‘suluhu’ ya kuwa mteja wa mama pima kila siku. Machi 2018 gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alianzisha mpango wa Kaa Sober, uliolenga kunasua waathiriwa wa pombe.

Aidha, walihusishwa katika kufanya vibarua vya kufagia barabara, kufyeka na kusafisha mitaro ya majitaka Kiambu, ambapo serikali ya kaunti hiyo ilikuwa ikiwalipa Sh400 kwa siku.

Zaidi ya vijana 6,000 ndio walisajiliwa Kimathi akiwa mmoja wao. Mbali na kushirikishwa katika shughuli za kuwataka ‘wasahau’ kunywa pombe, waathiriwa walipokea mafunzo ya kozi fupifupi za mikono na kiufundi kama useremala, ushonaji, uashi, mapishi na ususi, bila malipo katika taasisi za elimu ya juu 37 Kiambu kwa muda wa miezi mitatu.

Walipokea vyeti vya kufuzu mnamo Februari 26, 2019, gavana akiwapiga jeki kwa Sh20,000 kila mmoja.

“Zitawasaidia kuweka biashara ili mjiimarishe kimaisha. Ukosefu wa kazi kwa vijana Kiambu ni changamoto inayowashinikiza kunywa pombe, itatatuliwa wakipata ajira. Wakati wa kampeni 2017 niliwaahidi kutatua suala hili na lazima tupate mwafaka,” alisema Bw Waititu katika hafla ya kufuzu kwa waathiriwa wapatao 5,200 uwanja wa Ndumberi.

Kimathi. 34, ameishi kwa mahangaiko matamanio yake yakiwa kupata msamaria mwema atakayemtunuku kazi.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo alisema tangu pigo la akiba kupunjwa hajaweza kurejelea hali yake ya kawaida.

“Ndio kwa sasa sinywi pombe, lakini kurudi daraja nililokuwa imekuwa vigumu,” akasema.

Pili, aliodhania ni marafiki wake wa karibu walimtoroka alipofilisika. Mpango wa Kaa Sober ulimuwezesha kupokea mafunzo ya upishi, na kupokea cheti.