• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
MBOGA NA MATUNDA: Diwani ajitosa katika kilimo cha karakara huku akivuta majirani

MBOGA NA MATUNDA: Diwani ajitosa katika kilimo cha karakara huku akivuta majirani

Na DENNIS LUBANGA na WANDERI KAMAU

KAUNTI ndogo ya Moiben katika Kaunti ya Uasin Gishu inajulikana kwa kilimo cha mahindi na ngano.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Alice Rono, ambaye amejijengea jina kwa kilimo cha matunda ya karakara (passion) tangu 1997.

Amekuwa akiyauza matunda yake kwa kampuni ya Equatorial Horti Limited, ambayo huyasafirisha matunda hayo katika nchi kama Uganda, Ulaya kati ya masoko mengine duniani.

Rono, ambaye ni mjane na pia diwani maalum katika Bunge la Kaunti ya Kericho, ambaye huwakilisha masuala ya jinsia.

Alice Rono (kulia) akizungumza na baadhi ya watu waliomtembelea shambani mwake. Picha/ Dennis Lubanga

“Nilianza kilimo cha matunda ya karakara tangu 1997 katika shamba dogo baada ya kugundua faida yake. Hii ni kwa kuwa huwa yanachukua muda wa miezi minane pekee kukomaa,” anasema Alice kwenye mahojiano na Akilimali shambani mwake.

Mkulima huyo tayari amewaingiza majirani wake katika kilimo hicho. Ili kufanikisha mikakati ya kilimo chake, ameligawanya shamba lake la ekari sita katika maeneo kadhaa; ekari mbili huwa anakuza matunda hayo, kahawa katika ekari moja huku ardhi iliyobaki akipanda mazao ya kienyeji.

“Niliamua kuwafunza majirani zangu kilimo hiki ili kuwawezesha kuangazia ukuzaji wa mazao mengine yenye faida kando na mahindi. Bei za mahindi zimekuwa zikishuka mara kwa mara, hivyo kuwaathiri wengi wao kimapato,” akasema.

Diwani huyu huwa anatumia maji ya kisima kuendeshea kilimo chake.

Huwa anakuza karakara za manjano na zambarau.

“Mmea huu hauna gharama nyingi. Ninapovuna, huwa ninauza kilo moja kati ya Sh80 na Sh100, bei ambayo huniletea faida kubwa ikilinganishwa na mahindi,” asema.

Akaongeza: “Kwa kuwa huwa navuna karibu kila wiki moja, huwa ninapata karibu Sh100,000 ambazo hunisaidia sana kukidhi mahitaji yangu kama kulipia karo watoto wangu.”

Hata hivyo, anataja ukosefu wa maji ya kutosha kama baadhi ya changamoto ambayo imekuwa ikimkabili.

“Bila kuwa na maji ya kutosha, ni vigumu kupata matunda yatakayowaridhisha wateja. Huwa ninatumia karibu lita 20,000 za maji ambazo hunigharimu Sh15,000. Ninataka kujitosa katika mfumo wa unyunyizaji maji kwani nitapunguza gharama ninayotumia kwa sasa,” asema Rono.

Anawaomba wakulima wengine kuanza kujitosa katika kilimo cha mimea tofauti, badala ya kutegemea upanzi wa zao moja.

“Upanzi wa mimea kama mahindi na maharagwe ni mzuri lakini kuna haja ya kukuza mimea mingine tofauti. Mkulima anaweza kuligawanya shamba lake na kuanza kilimo cha mimea ya kibiashara,” anasema.

Ameirai serikali ya Kaunti hiyo kutathmini mpango wa kubuni kiwanda cha kuzalisha zao hilo, ili kuongeza ubora wake. Asema kuwa hilo litaongeza maradufu faida ambazo wakulima wanapata kutokanana uuzaji wake.

“Serikali ya kaunti inaweza kubuni kiwanda cha kutengeneza sharubati kwani huwa tunategemea viwanda kutoka Uganda,” anasema.

Kuongeza faida

Diwani wa wadi ya Ziwa Joseph Korir anamuunga mkono mwenzake, huku akiwaomba wakulima wengine kuanza kilimo cha mazao mbalimbali ili kuongeza faida wanazopata.

“Huu ndio wakati mwafaka wa kuwashinikiza wakulima wetu kutotegemea zao moja. Lazima waanze upanzi wa mazao ambayo yatakomaa kwa haraka na kuwapa faida. Hii ni hatua muhimu sana kwa kaunti yetu ambapo tuna furaha kubwa kuwa viongozi wetu wanawaongoza wakulima kwa vitendo. Tuna soko kubwa la karakara ndani na nje ya Kenya kwani bado haijajitosheleza,” anasema Bw Keitany.

Anasema kuwa zamani, walikuwa wakiuza kilo moja ya zao hilo kwa Sh30 pekee, lakini bei hiyo imeongezeka na kufikia Sh100.

You can share this post!

Kocha Migne ataja kikosi cha Harambee Stars tayari kwa AFCON

Imamu atandika muumini katika msikiti wakiomba

adminleo