• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Meno ya makinda wa Arsenal yapewa sifa

Meno ya makinda wa Arsenal yapewa sifa

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amesema kikosi chake cha wachezaji chipukizi kimedhihirisha uwezo mkubwa baada ya kushinda Portsmouth kwa mabao 2-0 ugani Fratton Park mnamo Jumatatu usiku na kufuzu kwa robo fainali ya FA Cup.

Arteta aliteremsha uwanjani kikosi kilichojumuisha wachezaji sita wasiozidi umri wa miaka 20, lakini kikashangaza kwa kucheza kwa kiwango cha juu, hasa katika kipindi cha pili, na kulaza Portsmouth ambayo ilikuwa haijashindwa katika mechi 19 za nyumbani, mbali na kuandikisha ushindi mara 10 katika mechi zake za majuzi.

Wenyeji walicheza vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini nguvu zao zikafifia kutokana na bao a Sokratis Papastathopoulos kufuatia krosi ya Reiss Nelson katika muda wa ziada kipindi cha kwanza.

Eddie Nketiah alimimina wavuni bao la pili dakika sita baada ya kipindi cha mapumziko baada ya kuandaliwa na Nelson.

“Nimeridhishwa na uchezaji wa makinda hawa,” Arteta aliwaambia waandishi.

Nafurahia kufanya nao kazi. Kwa kweli wanastahili nafasi kikosini. Daima si rahisi kubadilisha kikosi jinsi nilivyofanya, lakini wamethibitisha uwezo wao.”

“Walicheza katika mazingira magumu mbele ya mashabiki wa Portsmouth ambayo walipiga mayowe kila wakati. Lakini vijana wangu walijiamini na kucheza vizuri. Tulifunga mabao mawili na bado tulikuwa na nafasi ya kufunga mengine zaidi.”

Arsenal waliingia uwanjani baada ya majuzi kubanduliwa nje ya michuano ya Europa League na Olympiakos ya Ugiriki.

Katika kikosi chake, Arteta alifanya mabadiliko tisa, akijumuisha sajili mpya Pablo Mari aliyecheza kikosini kwa mara ya kwanza. Kwenye mechi hiyo, kiungo Lucas Torreira aliumia na kutolewa nje baada ya kugongana vibaya na James Bolton.

Makinda wengine waliovuma katika pambano hilo ni beki kushoto Bukayo Saka pamoja na Gabriel Martinelli.

Kutokana na ushindi huo, Arsenal inajivunia ushindi mara 22 dhidi ya Portsmouth tangu 1958.

Portsmouth wanashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ya Daraja ya Kwanza huku ikiwa na nafasi ya kurejea katika ligi kuu ya EPL.

Kikosi hicho cha kocha Kenny Jackett kilionyesha uwezo mkubwa, hasa ikizingatiwa kwamba kilianza bila washambuliaji matata Curtis, John Marquis na nahodha Tom Naylor.

Kikosi cha Arsenal

Emiliano Martinez, Sokratis Papastathopoulos, David Luiz, Pablo Mari, Bukayo Saka, Matteo Guendouzi, Lucas Torreira, Reiss Nelson, Joe Willock, Gabriel Martinelli, Eddie Nketiah; Benchi: Bernd Leno, Ainsley Maitland-Niles, Rob Holding, Granit Xhaka, Dani Ceballos, Nicolas Pepe, Alexandre Lacazette.

  • Tags

You can share this post!

FATAKI ZA FA: Manchester City mavizioni jicho sasa likiwa...

Harambee Starlets yatua Uturuki salama tayari kuvaana na...

adminleo