• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Mitandao iwe ya kupeana habari na sio kushambuliana, wanahabari na wanaharakati waambiwa

Mitandao iwe ya kupeana habari na sio kushambuliana, wanahabari na wanaharakati waambiwa

NA FARHIYA HUSSEIN

WANAHABARI wa kike pamoja na wenzao kutoka mashirika ya kutetea haki za binadamu wamepata mafunzo ya kupambana na udakuzi wa mtandaoni, lakini muhimu zaidi wakiambiwa watumie jukwaa hilo kupeana habari muhimu badala ya kupapurana wenyewe kwa wenyewe.

Wanawake hao ambao walikutana Kaunti ya Mombasa walielezwa umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kwa njia inayofaa.

Baadhi walilaumiwa kwa kutumia mitandao ya kijamii kuendeleza chuki badala ya kujiinua kimaisha na kibiashara.

Bi Topister Juma kutoka shirika la Muslims for Human Rights (MUHURI) aliwarai wanawake kuongozana wenyewe kwa wenyewe namna ya kutumia mitandao ya kijamii kwa njia sahihi.

“Tutumie mitandao kwa njia bora kujinufaisha sisi wanawake kama wafanyabiashara, kwa kutafuta elimu itakayotusaidia sisi na sio kutumia mitandao vibaya kwa kutoa matusi na kuharibiana jina na sifa kwani kufanya hivyo ni kushusha hadhi zetu kama wanawake,” alisema Bi Juma.

Wanawake na wanahabari waliohudhuria mafunzo hayo, walielezea changamoto zao ikiwa pamoja na baadhi kupokea vitisho mtandaoni kutokana na kazi zao.

Baadhi ya wanawake katika tasnia ya uanahabari na uanaharakati wakipokezwa mafunzo ya namna ya kujikinga mtandaoni. Warsha ilifanyika jijini Mombasa. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Wengi wao walitaja kutengwa na jamii kwa sababu ambayo yanazungumziwa mtandaoni kuwahusu.

Bi Naima Omar ambaye anafanya kazi kwa karibu na madaktari na wauguzi katika sekta ya afya, alielezea matumaini kuelekea mbele katika kulinda habari zake mtandaoni.

“Hapo awali, nilikuwa sizingati masuala muhimu kama nenosiri na umuhimu wake ila kupitia mafunzo haya nimeelewa ni muhimu kueka nenosiri tofauti kwa kila ukurasa wa mtandao wa kijamii kwani hii itafanya iwe vigumu kwa wadukuzi kuingia kwa akaunti yangu,” alieleza Bi Omar.

Mwanahabari Ruth Aura alieleza matumaini yake akiwarai wanahabari wenzake kuangazia masuala ya mitandao ya kijamii na changamoto zake kusaidia jamii kuelewa kwa uwazi hatari zilizoko.

Pia, walielezwa vifaa vilivyoko katika mtandao wa kijamii (tools) na jinsi wanavyoweza kuvitumia kujikinga dhidi ya wadukuzi.

Bi Maryline Laini kutoka Shirika la Nkoko Injuu Africa, alieleza umuhimu wa wanawake waliopata fursa hiyo kujitolea kufunza wengine kwenye jamii masuala walioelezwa.

Baadhi ya wanawake katika tasnia ya uanahabari na uanaharakati wakipokezwa mafunzo ya namna ya kujikinga mtandaoni. Warsha ilifanyika jijini Mombasa. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Mkurugenzi Mkuu kutoka Shirika la AMWIK, Bi Patience Nyange alisema wanahabari kuwa katika hatari kubwa ya mashambulio mtandaoni.

“Mimi binafsi nimeweza kujifunza mengi kutokana na mafunzo ya leo na naahidi nitaweza kuwafunza wenzangu ambao hawakupata fursa ya kujiunga na sisi leo. Mashambulio ya mtandaoni huathiri wanahabari,” alisema Bi Nyange.

Aidha, walionywa dhidi ya kuweka masuala yanayohusu maisha yao kibinafsi au familia zao kwenye mtandao, wakielezwa busara aina hiyo itasaidia kulinda habari muhimu kuhusu maisha yao.

Mafunzo hayo yaliongozwa na Shirika la Paradigm Initiative likishirikiana na MUHURI, Article-19 miongoni mwa mashirika mengine.

Baadhi ya wanawake katika tasnia ya uanahabari na uanaharakati wakipokezwa mafunzo ya namna ya kujikinga mtandaoni. Warsha ilifanyika jijini Mombasa. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

  • Tags

You can share this post!

Hofu wanaougua ukoma wakiendea wapiga ramli kwa kuamini ni...

AMINI USIAMINI: Kasuku kwa jina Kea hula kondoo

T L