• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Mkahawa Solutions: Programu inayorahisisha biashara zinazohusu mikahawa

Mkahawa Solutions: Programu inayorahisisha biashara zinazohusu mikahawa

NA MAGDALENE WANJA

JANGA la Covid-19 lilikuwa na mazuri yake kwa sababu kwa kiwango kikubwa liliamsha ari ya watu mbalimbali kukuna vichwa na kuibuka na ubunifu mkubwa kiteknolojia.

Kwa mfano kuna programu inayofahamika kama Mkahawa Solutions ambayo waanzilishi wake walikuwa na nia kwamba iweze kurahisisha biashara zote zinazohusiana na mikahawa.

Hii ni pamoja na kuuza bidhaa, kupata wafanyakazi, kutafuta huduma za mkahawa, ama kuuza mkahawa wenyewe.

Alipokuwa akisomea somo la Ethnobotany katika Chuo Kikuu cha Eldoret (UoE), Edwin Mghanga alijihusisha na biashara ya kuuza nyama ya mishikaki.

Edwin Mghanga (kushoto), na Charles Mwakio, ambao ni waanzilishi wa programu ya Mkahawa Solutions. PICHA | MAGDALENE WANJA

Hii ilimpa ujuzi katika sekta ya upishi na baada ya muda mfupi, alikuwa akifinya biashara ya mapishi katika sherehe mbali mbali katika kaunti ya Uasin Gishu.

Kwa upande mwingine, Charles Mwakio alikua akisaidia katika uendeshaji wa biashara ya familia jijini Mombasa. Alipenda sana kujihusisha na biashara ya kuwaridhisha wateja na akawa akitumia sehemu fulani ya muda wake kuwafunza wafanyakazi jinsi ya kuwapa wateja huduma bora.

Hii iliwaleta pamoja binamu hao mnamo mwezi Julai 2020 na wakaanza kuunda programu hiyo.

“Serikali ilipoweka sheria na masharti makali kwa biashara za mikahawa wakati wa janga la Covid-19, wengi wa wamiliki wa biashara hizi, walitaka usaidizi ili kijifahamisha na sheria mpya, na hivyo tuliweza kutoa huduma mbalimbali kwao,” anasema Mwakio.

Biashara hii inategemea teknolojia kwa kiwango kikubwa ili kufanikiwa.

“Tuna uwezo wa kuwahudumia kati ya wateja 15 na 40 ambao hutafuta huduma mbalimbali,” anaongeza.

Ndoto yao ni kupanua biashara yao na kufikia hatua ambapo wataweza kutoa huduma zaidi katika nchi nyingine.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Jinsi wazo la kutatua changamoto ya kiafya...

Dkt Neema Lema atumia teknolojia kutibu watoto kwa kuwapa...

T L