• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mwathethe astaafu kumpisha Kibochi wadhifa wa mkuu wa majeshi

Mwathethe astaafu kumpisha Kibochi wadhifa wa mkuu wa majeshi

Na SAMMY WAWERU

MEJA Jenerali Robert Kariuki Kibochi amepokezwa mikoba na mtangulizi wake Samson Mwathethe kuwa mkuu mpya wa wanajeshi wa Kenya (KDF).

Mkuu huyo mpya wa majeshi amemrithi Mwathethe aliyemkabidhi zana za uongozi wa kikosi hicho katika hafla iliyoandaliwa Ijumaa katika makao makuu ya KDF – DoD – jijini Nairobi.

Katika hafla ya aina yake, na iliyohudhuriwa na Waziri wa Ulinzi Dkt Monicah Juma pamoja na wakuu wa KDF, Mwathethe alimkabidhi rasmi Kibochi bendera ya Kenya na cheti cha kikosi cha wanajeshi.

Mkuu huyo – Mwathethe – ambaye kwa sasa ni mstaafu, alikagua gwaride la heshima la wanajeshi kwa mara ya mwisho.

Meja Jenerali mpya Kibochi pia alikagua gwaride la heshima, kufungua jamvi la uongozi.

Hafla hiyo iliyopambwa na wanajeshi, walimuaga Jenerali Mwathethe ambaye alihudumu kama mkuu wao tangu 2015, ambapo mizinga 17 ilifyatuliwa hewani na kikosi cha wanajeshi wa majini, kama ishara ya kutambua mchango wake katika kikosi hicho na taifa kwa jumla.

Ni baada yake kuhudumu katika wadhifa huo kwa muda wa miaka mitano.

“Ni fursa ya kipekee kuhudumu kama Mkuu wa Majeshi,” Mwathethe akasema katika hotuba yake, huku akimpongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kumteua kuhudumu wadhifa huo.

Kwa upande wake Bw Kibochi, alieleza kufurahishwa kwake kwa uteuzi huo, akiahidi kuendeleza mikakati ya mtangulizi wake na kuimarisha kikosi cha KDF.

“Kwa hakika wadhifa huu ni heshima kuu kupokezwa, kuongoza maafisa wote wa kijeshi, wa kike na kiume. Ninaahidi kuendeleza mikakati ya mtangulizi wangu na kuimarisha kikosi hiki,” Jenerali Kibochi akasema.

Mwathethe alijiunga na kikosi cha wanajeshi mnamo 1978.

Gari rasmi lililovutwa na wanajeshi wa ngazi ya brigedia na meja jenerali, lilielekezwa nje ya makao makuu ya KDF, Bw Mwathethe akaingia katika gari lake binafsi ishara kuwa sasa ni raia.

Mkuu mpya wa Majeshi, Meja Jenerali Kibochi ataapishwa mnamo Jumatatu.

Atahudumu kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

  • Tags

You can share this post!

Serikali imeweka zuio kwa manufaa yenu, Supkem yaambia...

Watu wanne wasombwa na maji eneo la Ngoliba

adminleo