Mama asimulia mahangaiko ya bintiye aliyenajisiwa na mhudumu wa bodaboda

Na LAWRENCE ONGARO

FAMILIA moja eneo la Juja Farm, kaunti ya Kiambu,  inataka haki itendeke baada ya binti wao aliyenajisiwa kubaki na upweke.
Ilidaiwa muda wa miezi mitatu ambayo imepita binti hiyo amejaribu kujitoa uhai mara mbili bila mafanikio.
Ukweli wa mambo ni kwamba mnamo mwezi Desemba 2018, binti huyo aliabiri bodaboda mwendo wa saa mbili za usiku lakini mhudumu huyo wa bodaboda, alimpeleka kichakani na kumnajisi  kwa zaidi ya muda wa saa nne, kabla ya kumpeleka alikotarajia.
Baadaye alimuarifu mamake kuhusu tukio hilo.
Hatua ya haraka ilichukuliwa kwa kupiga ripoti kituo cha polisi cha Juja Farm.
Taarifa iliandikwa na akakubaliwa kwenda hospitalini ambapo ilithibitishwa kweli alinajisiwa.
Hata hivyo mamake msichana anasema hadi wa leo mshukiwa yuko mafichoni lakini anaonekana nyakati zingine.
“Mimi jambo linaloniudhi sana ni kwamba polisi wanaostahili kunisaidia wanaonekana wanamkinga mshukiwa. Ni jambo linalofanya kesi hiyo kuonekana kuwa ngumu kuendesha,” alisema mama huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe hadharani.
Anasema bintiye anasomea shule moja ya upili katika kidato cha tatu.
“Msichana wangu amesongwa na mawazo mengi ajabu ambapo kwa muda wa miezi miwili mitatu hivi iliyopita amejaribu kujitoa uhai mara mbili; jambo ambalo limepunguza bidii yake masomoni. Tafadhali ninaomba haki kutoka kwa serikali,” alijitetea mama huyo.
Uchunguzi
Naye naibu wa afisa mkuu wa polisi OCPD, kituo cha Juja, Bw Justine Njeru, alisema tayari wameanzisha uchunguzi wa kina ili kuona ya kwamba haki inatendeka.
“Tayari maafisa wangu wanaendelea kufanya uchunguzi ili kunasa mshukiwa ambaye inadaiwa yuko mafichoni,” alisema Bw Njeru.
Mama wa msichana anasema msichana wake alirudi kwa likizo fupi kutoka shuleni siku tatu zilizopita na mwanaye huyo amekuwa amejifungia kwenye nyumba akihofia kukejeliwa na wananchi.
Anazidi kueleza kuwa msichana huyo ameshindwa hata kula chakula kama kawaida.
Mama huyo amelazimika kuketi karibu na mwanaye kila Mara akimliwaza kwa kumpa ushauri.
“Hata mimi huhofia akiwa shuleni anaweza kufanya kitando kibaya akibaki pekee yake bila rafiki,” alisikitika mama huyo.
Mzazi hiyo anataka hatua ichukuliwe dhidi ya maafisa kadha wa polisi ambao anadai wanajaribu kumkinga mshukiwa ambaye angekuwa amefunguliwa mashtaka kwa sasa.

Wazazi watakiwa kuripoti visa vya watoto kunajisiwa na watu wa familia

NA KALUME KAZUNGU

IDADI ya visa vya watoto wadogo wanaonajisiwa kwa kubakwa na kulawitiwa katika kaunti ya Lamu inaibua maswali mengi.

Kwa mujibu wa Shirika la Kutetea Haki za Waislamu (MUHURI) tawi la Lamu, zaidi ya watoto 10 hudhulumiwa kingono kila mwezi bila ya waathiriwa kupata haki.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Jumatatu, maafisa wa MUHURI walisema cha kusikitisha zaidi ni kwamba watoto wengi wanaopitia madhila hayo huishia kufichwa na wazazi badala ya visa hivyo kuangaziwa ili waadhiriwa wapate haki.

Afisa Mkuu wa MUHURI eneo hilo, Bi Ummulkher Salim, alisema aghalabu wanaotekeleza vitendo hivyo kwa watoto husika ni wale wa uhusiano wa karibu, ikiwemo wajomba, mabinamu na pia akina baba wa watoto hao.

Alitaja sehemu za Tchundwa, Kiunga, na mji wa kale wa Lamu kuwa miongoni mwa maeneo ambapo visa vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo vinaendelezwa kisiri.

Mwenyekiti wa CIPK tawi la Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe. Amelaani vikali ubakaji na ulawiti wa watoto eneo la Lamu, akisema vitendo hivyo ni kinyume cha dini. Ataka wahalifu kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Picha/ Kalume Kazungu

Kwa mujibu wa Bi Salim, wazazi wamekuwa wakichangia pakubwa kukithiri kwa vitendo hivyo kutokana na kwamba wengi wao hukimbilia kutatua uhalifu huo kijamii badala ya kuwaripoti wahalifu ili wakabiliwe na mkono wa sheria.

“Ni masikitiko makuu kwamba watoto wengi hapa Lamu wamekuwa wakibakwa na kulawitiwa. Cha ajabu ni kwamba watu wa ukoo ndio mara nyingi hutekeleza vitendo hivyo. Hii ndiyo sababu wazazi wanakimbilia kutatua matatizo hayo kijamii badala ya kuhakikisha wahalifu wamekabiliwa na mkono wa sheria,” akasema Bi Salim.

Naye Naibu Afisa wa MUHURI eneo la Lamu, Bw Ali Habib, alisema shirika hilo tayari limeanzisha mpango wa kufadhili kesi kwa waathiriwa wa vitendo hivyo.

Kulingana na Bw Habib, wazazi wa waathiriwa au waathiriwa wenyewe wanahimizwa kuripoti visa hivyo kwa ofisi ya MUHURI ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka dhidi ya wanaotekeleza vitendo hivyo.

Naibu Afisa wa MUHURI tawi la Lamu, Ali Habib wakati wa mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake. Picha/ Kalume Kazungu

Wazazi wapige ripoti 

“Lengo letu kama MUHURI ni kuhakikisha haki imepatikana kwa watoto wanaofanyiwa unyama huo. Tunawahimiza  wazazi wa watoto husika kupiga ripoti kwa ofisi yetu.

Kama shirika, tutachukua malalamishi yao kisiri bila ya kumtaja yeyote atakayeripoti kwetu. Tuko tayari kudhamini kesi kama hizo na kuona kwamba haki imepatikana na visa hivyo vinakomeshwa kabisa eneo la Lamu,” akasema Bw Habib.

Wakati huo huo, Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) tawi la Lamu limelaani vikali vitendo hivyo dhidi ya watoto eneo hilo.

Mwenyekiti wa CIPK tawi la Lamu, Ustadh Abubakar Shekuwe aidha alipinga vikali madai kwamba kutoripotiwa kwa visa kama hivyo kunatokana na utamaduni wa kale pamoja na misingi ya dini ya kiislamu kwa wakazi wa Lamu.

Aliwashauri wazazi kutowaficha majumbani watoto wao punde wanapodhulumiwa.

“Kubakwa au kulawitiwa kwa watoto ni kinyume kabisa cha dini. Wanaotekeleza uhalifu huo sharti waandamwe kisheria. Dini inakataza zinaa na kufanywa kwa vitendo kama hivyo kwafaa adhabu kali,” akasema Ustadh Shekuwe.