Maandamano dhidi ya Gavana Sang yatibuka

Na TOM MATOKE

MAANDAMANO yaliyopangwa kufanyika Ijumaa dhidi ya seneta wa Nandi, Stephen Sang yalitibuka dakika ya mwisho baada ya mmoja wa waandalizi kutoweka na kibali cha polisi na vifaa vilivyopaswa kutumiwa katika shughuli hiyo.

Bw Shadrack Kemei ambaye alikuwa na leseni hiyo na vifaa vingine kama firimbi na mabango hakuweza kupatikana Ijumaa asubuhi.

Baadhi ya waandamanaji waliwasili mjini Kapsabet saa kumi na mbili asubuhi na kusubiri viongozi wao kwa saa kadhaa ili waanze maandamano dhidi ya Gavana Sang.

Hata hivyo, walitawanyika mwendo wa saa sita adhuhuri walipokosa kumpata Bw Kemei na kuapa kwamba watapanga siku nyingine ya kufanya maandamano.

Maandamano hayo yaliitishwa na Seneta wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei na mwenyekiti wa chama cha Jubilee katika kaunti hiyo Sammy Biwott kulalamikia madai ya ufisadi katika serikali ya Gavana Sang.

Ijumaa, Bw Biwott alisema hawakuweza kumpata Bw Kemei au kupata vifaa walivyonuia kutumia kwenye maandamano.

Alisema waliahirisha maandamano hadi siku nyingine na kwamba hawatamwamini mtu mmoja kuwawekea vifaa hivyo.

“Watu wa Nandi walimchagua Gavana Sang kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 alipoahidi kubadilisha kaunti yao na kuleta mageuzi lakini ufisadi umeongezeka tangu alipoingia ofisini,” alidai Bw Biwott.

Kulikuwa na maafisa wengi wa polisi mjini kabla ya maandamano hayo kufutiliwa mbali.

Jaramogi ahusishwa na mzozo wa mpakani

TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG

MZOZO wa mpaka kati ya Kaunti za Nandi na Kisumu ulichukua mwelekeo mpya Jumatatu baada ya jina la aliyekuwa makamu wa rais Jaramogi Oginga Odinga kutajwa.

Viongozi kutoka Kaunti ya Nandi walisema kaunti hizo mbili zilibuniwa Jaramogi alipokuwa makamu wa rais wa rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

Viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa lililokuwa baraza la mji wa Nandi Charles Tanui walidai kwamba Jaramogi alimuomba Mzee Kenyatta kuruhusu watu wa jamii ya Waluo waliokuwa wakiishi Kisumu kuhama na kuishi maeneo ya milimani ya Nandi msimu wa mvua kubwa ili wasisombwe na mafuriko.

Walisema Mzee Kenyatta alikubali ombi hilo na mamia ya watu kutoka Nyanza waliruhusiwa kuishi Nandi karibu na mpaka kwa muda hadi mvua ipungue.

“Wakati Jaramogi aliacha kazi ya makamu wa rais, wenzetu kutoka Kisumu waliendelea kuishi katika ardhi ndani ya Kaunti ya Nandi hadi Mzee Kenyatta alipokufa 1978,” alisema Bw Tanui.

Viongozi wa Kaunti ya Nandi wameunga mipango ya Gavana Stephen Sang mpaka huo uchunguzwe upya. Bw Sang na viongozi hao wanataka maeneobunge ya Muhoroni na Kisumu Mashariki wakisema yalitwaliwa wakati wa ujenzi wa reli.

Wanadai kwamba Waingereza waliwafukuza Wanandi kwa sababu ya kupinga ujenzi wa reli. Bw Sang aliongoza mkutano wa viongozi wa Nandi miezi mitatu iliyopita kabla ya Tume ya Ardhi kuzuru eneo hilo.

Mkutano huo ulipitisha azimio la kuhakikisha maeneo yanayozozaniwa yamerejeshwa Kaunti ya Nandi. Walitaja maeneo hayo kama miji ya Miwani, Kibos, Kibigori, Kopere, Chemelil, Fort Tenan na Muhoroni. Hatua hiyo ilizua taharuki kwenye mpaka wa kaunti hizo mbili na kuathiri uwekezaji katika kilimo.

Maafisa wa kaunti waingia mafichoni kuhepa kukamatwa na EACC

TOM MATOKE NA BARNABAS BII

 

MAAFISA wakuu katika Serikali ya Kaunti ya Nandi wamekimbilia mafichoni kuhepa maafisa wa Tume ya Ufisadi (EACC) wanaofanya uchunguzi wa sakata ya ubadhirifu wa mabilioni ya pesa katika muda wa miaka mitano iliyopita.

Tume hiyo ya EACC imekita kambi katika kaunti hiyo katika muda wa siku tatu zilizopita huku ikiwasaka maafisa wa sasa na waliokuwepo, wanaohusishwa na pesa hizo kwa kutoa kandarasi za ujenzi wa barabara na pia zabuni bila kufuata utaratibu unaostahili.

Wapelelezi wa tume walifanya misako katika nyumba za maafisa hao katika kaunti za Nandi, Uasin Gishu, Trans Nzoia na Vihiga ambapo walichukua stakabadhi muhimu ambazo ni pamoja na hati miliki za ardhi, mashine za kielektroniki, stakabadhi za zabuni na uagizaji miongoni mwa nyingine.

Afisa mkuu wa polisi eneo la Nandi, Bw Patrick Wambani alithibitisha kuwa kundi la maafisa wa EACC liliomba usaidizi wake kuwasaka baadhi ya waliohusishwa na ubadhirifu wa pesa za umma.

Pia walizuru makao ya aliyekuwa gavana Cleophas Lagat ambapo kaunti wakati wa kipindi chake inashukiwa kupoteza mabilioni kati ya 2014 hadi sasa.

Jumatatu, wapelelezi waliwakamata washukiwa zaidi ya 10 waliohusishwa na uporaji wa pesa za umma miongoni mwao wakiwa ni katibu wa kaunti, Bw Francis ominde na aliyekuwa afisa mwandamizi wa fedha, Bw Emmanuel Wanjala na kuchukua stakabadhi za ardhi na nyingine za zabuni.

Taarifa nyingine zilieleza kuwa maafisa hao walipata kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa afisa wa ngazi za juu baada ya kuvamia nyumbani kwake.

Miongoni mwa waliokamatwa na kuandikisha taarifa katika msako wa EACC ni afisa wa fedha katika kaunti, Bi Helen Katam na aliyekuwa mkuu wa fedha, Bw Charles Muge.

Amri ya kubomoa jengo la gavana yakoroga seneta

Na DENNIS LUBANGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi, Bw Kiprotich Cherargei, ametishia kushtaki Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) baada ya kuagiza kubomolewa kwa afisi ya gavana kwa msingi kuwa jengo hilo si salama.

Bw Cherargei aliikashifu NCA kwa kutaka jengo hilo libomolewe ilhali mamlaka hiyo ndiyo iliidhinisha ujenzi wake.

“Nilidhani kuwa katika uhandisi, kila awamu ya ujenzi huidhinishwa na mhandisi pamoja na mwanakandarasi. Katika hali hii ni NCA iliyoidhinisha ujenzi wa jengo hilo na sasa inataka libomolewe. Nitawashtaki kama watachukua hatua hiyo ya ubomoaji,” akasema Bw Cherargei.

Kwenye ripoti ya mapema iliyoandikwa Machi 23, 2018, NCA ilitilia shaka uthabiti na usalama wa muundo uliotumiwa kwa ujenzi huo.

Ripoti hiyo inasema usanifu ujenzi wa awali wa jengo hilo ulibadilishwa wakati ujenzi ukiendelea ili kuongeza orofa zaidi, na hivyo basi msingi wa jengo uko hatarini kuwa hafifu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumapili, seneta huyo alimkashifu pia Gavana Stephen Sang, kwa kukubaliana na msimamo wa NCA.

“Hili jengo lilitumia zaidi ya Sh150 milioni za mlipa ushuru. Ubomoaji wake utatumia karibu Sh20 milioni au zaidi,” akasema.

Alidai uamuzi wa NCA umechochewa kisiasa ili kunufaisha watu ambao watapewa kandarasi ya ujenzi upya, akasisitiza uamuzi kama huo lazima ufanywe kwa kushirikisha maoni ya wananchi.

Aliomba utawala wa Bw Sang ujishughulishe na ujenzi wa nyumba ya gavana badala ya kujiingiza kwa mipango ya kubomoa afisi yake.

“Tuko katika awamu ya mwisho ya kupeana fedha za kaunti ambazo zilitengwa katika mwaka wa kifedha uliopita kwa hivyo inafaa tujihadhari kuhusu jinsi tunavyotumia pesa za kaunti. Sitakubali jengo hilo libomolewe. Linahitaji tu kuimarishwa zaidi,” akasema.

Waziri wa miundomsingi katika kaunti, Bw Hillary Koech, alisema serikali ya kaunti iliwaalika maafisa wa NCA kuthibitisha uthabiti wa jengo hilo wakati lilipopata nyufa.

Kaunti ilikuwa imetumia Sh124 milioni kwa ujenzi wake, na Sh10 milioni zingine zimepangiwa kutumiwa kulikamilisha.

Bw Cherargei alikanusha madai kuwa pingamizi lake linatokana na sababu za kibinafsi dhidi ya gavana akasema hana nia ya kuwania ugavana bali anataka utumizi bora wa pesa za umma.