Amri ya kubomoa jengo la gavana yakoroga seneta

Na DENNIS LUBANGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi, Bw Kiprotich Cherargei, ametishia kushtaki Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) baada ya kuagiza kubomolewa kwa afisi ya gavana kwa msingi kuwa jengo hilo si salama.

Bw Cherargei aliikashifu NCA kwa kutaka jengo hilo libomolewe ilhali mamlaka hiyo ndiyo iliidhinisha ujenzi wake.

“Nilidhani kuwa katika uhandisi, kila awamu ya ujenzi huidhinishwa na mhandisi pamoja na mwanakandarasi. Katika hali hii ni NCA iliyoidhinisha ujenzi wa jengo hilo na sasa inataka libomolewe. Nitawashtaki kama watachukua hatua hiyo ya ubomoaji,” akasema Bw Cherargei.

Kwenye ripoti ya mapema iliyoandikwa Machi 23, 2018, NCA ilitilia shaka uthabiti na usalama wa muundo uliotumiwa kwa ujenzi huo.

Ripoti hiyo inasema usanifu ujenzi wa awali wa jengo hilo ulibadilishwa wakati ujenzi ukiendelea ili kuongeza orofa zaidi, na hivyo basi msingi wa jengo uko hatarini kuwa hafifu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumapili, seneta huyo alimkashifu pia Gavana Stephen Sang, kwa kukubaliana na msimamo wa NCA.

“Hili jengo lilitumia zaidi ya Sh150 milioni za mlipa ushuru. Ubomoaji wake utatumia karibu Sh20 milioni au zaidi,” akasema.

Alidai uamuzi wa NCA umechochewa kisiasa ili kunufaisha watu ambao watapewa kandarasi ya ujenzi upya, akasisitiza uamuzi kama huo lazima ufanywe kwa kushirikisha maoni ya wananchi.

Aliomba utawala wa Bw Sang ujishughulishe na ujenzi wa nyumba ya gavana badala ya kujiingiza kwa mipango ya kubomoa afisi yake.

“Tuko katika awamu ya mwisho ya kupeana fedha za kaunti ambazo zilitengwa katika mwaka wa kifedha uliopita kwa hivyo inafaa tujihadhari kuhusu jinsi tunavyotumia pesa za kaunti. Sitakubali jengo hilo libomolewe. Linahitaji tu kuimarishwa zaidi,” akasema.

Waziri wa miundomsingi katika kaunti, Bw Hillary Koech, alisema serikali ya kaunti iliwaalika maafisa wa NCA kuthibitisha uthabiti wa jengo hilo wakati lilipopata nyufa.

Kaunti ilikuwa imetumia Sh124 milioni kwa ujenzi wake, na Sh10 milioni zingine zimepangiwa kutumiwa kulikamilisha.

Bw Cherargei alikanusha madai kuwa pingamizi lake linatokana na sababu za kibinafsi dhidi ya gavana akasema hana nia ya kuwania ugavana bali anataka utumizi bora wa pesa za umma.

Majumba 1,437 jijini Nairobi ni hatari kuishi – NCA

Na BERNARDINE MUTANU

Katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita, Mamlaka ya Kusimamia Ujenzi nchini )(NCA) imebaini kuwa majumba 1,437 ni hatari kuishi Jijini Nairobi.

Hii ni baada ya utafiti kufanywa na mamlaka hiyo alisema soroveya mkuu Moses Nyakiongora.

Tangu Janauri, familia kadhaa zimepoteza makao baada ya majumba walimokuwa wakiishi kubomoka Pipeline na Kariobangi kusini.

Kutokana na hilo, serikali inalenga kubomoa majumba yaliyothibitishwa kuwa hatari katika mitaa ya Imara Daima, Zimmerman na Huruma.

Kulingana na mhandisi wa serikali Bw Samuel Charagu majumba mawili yatabomolewa Zimmermna na sita Huruma.

Majumba mengi yaliyolengwa kwa ubomoaji huo hayajafikia kiwango cha ubora kilichowekwa.

Kulingana na utafiti huo, majumba 650 ni hatari sana na mengine 826 yanaaminika kutokuwa salama.

Majumba 4,879 yamechunguzwa na mengine 651 yanahitaji kuchunguzwa mara moja. Majumba 185 yamewekwa katika ramani eneo la Pipeline.

Kufikia sasa majumba 34 yamebomolewa na mengine 40 yalipatikana kuwa na hitilafu ambazo haziwezi kurekebishwa, kumaanisha kuwa yatabomolewa. Baadhi ya wamiliki wa majumba wamepewa muda wa makataa kurekebisha majumba yao.

Mnamo Jumamosi asubuhi, jumba lingine la orofa nne lilibomoka eneo la Ruai.