• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Ndege iliyobeba abiria 40 yatua ghafla

Ndege iliyobeba abiria 40 yatua ghafla

Na MANASE OTSIALO

NDEGE ya shirika la Skyward Express iliyokua imebeba abiria wapatao 40 ilitua ghafla jana kwenye mkondo wa ndege unaojengwa mjini Burahache, nchini Somalia.

Bado haijabainika ni vipi ndege hiyo aina ya Fokker50 yenye nambari ya usajili 5Y GRS ilivyoishia Burahache, mji ulio karibu na Elwak, Mandera Kusini.Kwa kawaida, ndege hiyo huendesha safari zake kwenye maeneo baina ya Nairobi- Elwak- Mandera lakini iliripotiwa kukosa mkondo wa ndege wa Elwak na kuishia Burahache.

Akithibitisha kisa hicho, Kamishna wa Kaunti ya Mandera Onesmus Kyatha alisema abiria wote waliokuwamo ndani ya ndege hiyo walipatikana.“Kulikuwa na kisa cha ndege kutua ghafla katika mji wa Somalia ulio karibu na Kenya lakini hakuna majeruhi au wahasiriwa walioripotiwa.

Abiria wote waliokuwemo wapo salama na katika mipaka yetu,”alisema.Bw Kyatha alisema habari za kina zitafuata kuhusu ni vipi ndege hiyo ilikosa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Elwak zitasambazwa baada ya rubani na wenzake kuandikisha taarifa.

“Tutaweza kujua ni vipi ndege hiyo iliishia kutua Burahache badala ya Elwak kutoka kwa rubani na timu yake,” alisema.Ndege hiyo ilitua kwenye uwanja huo ambao bado haujakamilika kujengwa na kulazimika kujisukumiza kwenye mkondo huo ambapo vijisehemu vyake viliharibiwa.

Bi Nasra Bashir Ali, Msemaji wa Waziri Mkuu wa Somalia alisema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa “ndege iliyokuwa imebeba watu 45 ilipoteza mwelekeo kwenye mondo wa Elwak jana. Hakuna aliyejeruhiwa katika kisa hicho.”

Idadi kubwa ya abiria walikuwa wanaelekea kuhudhuria mazishi katika eneo la Borehole 11, Mandera Kusini ya Mandera, ya Bw Suraw Issack, ambaye ni baba yake Bw Mohamed Suraw, aliyewahi kuhudmu kama meya wa Nakuru..

“Tuna wanajeshi wa vikosi vya Amisom katika eneo hilo waliofanya haraka kuokoa ndege hiyo na abiria na wahudumu wote ambao kufikia sasa wamesafirishwa katika mji wa Elwak,” alisema Bw Kyatha.Umbali kati ya Elwak na Burahache ni karibu kilomita kumi.

Juhudi za kuwasiliana na Skyward Express, kampuni inayomiliki ndege iliyoathiriwa, ziliambulia patupu huku simu kadhaa zilizopigiwa usimamizi wa shirika hilo zikikosa kujibiwa.

  • Tags

You can share this post!

Tiketi ya ODM yavutia wengi wanaotaka kurithi Ojaamong

Tuchukue mkopo kufungua nchi – Raila