AKILIMALI: Miaka 20 akizalisha ndizi, zina mapato ila Covid nusra imvuruge

Na SAMMY WAWERU

HANNAH Njoki amekuwa katika kilimo cha ndizi kwa zaidi ya miaka 20 na anakiri ni zao lenye mapato ya haraka.

Alikikumbatia ili kusaidia kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kismingi.

Njoki hata hivyo anasema aligeuza wazo hilo kuwa biashara, baada ya majirani na wanakijiji kuridhishwa na mazao yake, na kuomba wauziwe.

“Nilianza na kipande kidogo tu cha ardhi na baada ya kugundua ndizi zina soko, niliongeza hadi ekari mbili,” anasema.

Alitumia mtaji wa Sh10,000 pekee, uliogharamia mbolea na leba, mbegu akipanda migomba asilia.

Hata ingawa baadaye alipunguza hadi ekari moja, Njoki anaendeleza kilimo cha zao hilo katika kijiji cha Gachinga, Ikinu, Kaunti ya Kiambu.

Alichukua hatua hiyo ili kujumuisha mimea mingine, angalau kuona ana mseto wa mazao.

Huku wengi wa wakazi eneo hilo wakijishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ukulima wa mahindi na maharagwe, Njoki amepamba uga wake wa matunda kwa migomba.

Aidha, kuna inayochana maua, kutunda na mingine ndizi kukomaa, mama huyu akisema kila wiki hakosi kufanya mavuno.

“Mavuno yakichelewa sana labda ni kwa mwezi mmoja pekee,” aelezea, akisema ameratibu shamba lake kwa mpangilio.

Kulingana na masimulizi yake, tangu aingilie kilimo cha ndizi, kimekuwa kikimpa tabasamu, furaha ambayo imemrahisishia kusukuma gurudumu la maisha.

Mahangaiko ya kupata karo, ameyaangazia kwa kiwango kikubwa.

“Kimsingi, sijataabika vile kupata karo. Mtoto anapotumwa nyumbani, hufanya mauzo ya ndizi na kumrejesha,” asema mkulima huyu ambaye ni mama watoto wanne.

Ndizi zikiwa miongoni mwa matunda kipenzi cha wengi, Njoki anasema soko bora limekuwa la mazao mabichi.

Aidha, wanunuzi wake wanatoka masoko mbalimbali Kiambu.

Ni kilimo-biashara anachosema kilikuwa kimenoga hadi Kenya ilipokumbwa na janga la corona Machi 2020, mambo yakaanza kuenda mrama.

Njoki anaiambia Akilimali kwamba soko la ndizi limeyumbishwa, kiasi cha kuhofia mazao yake kuozea shambani.

“Kwa sasa nina zaidi ya vifungu 200 vilivyokomaa shambani. Nina wasiwasi visiive kabla sijapata wanunuzi,” anasema.

Bei ya kifungu kimoja, hutegemea udogo au ukubwa wake. Huchezea kati ya Sh200 – 1, 000.

Kinyume na awali, mkulima huyu anasema wateja wake na ambao ni wa kijumla hawanunui mazao kwa wingi, pengine kwa hofu ya kukadiria hasara.

Ugonjwa wa Covid-19, na ambao ni janga la kimaitaifa umeathiri karibu sekta zote, ile ya kilimo na biashara pia ikijumuishwa.

Licha ya serikali kudai soko la mazao mbichi ya kilimo, hasa matunda na maua, limenoga nje ya nchi kipindi hiki cha corona, wakulima wanasema hawahisi kauli hiyo.

“Bado tungali kwenye mataa. Ni muhimu serikali itangamane na wakulima nyanjani,” Njoki ahimiza.

Mkulima huyu hata hivyo anasisitiza hayupo radhi kuasi kilimo cha ndizi, akisema changamoto anazopitia ni za muda tu.

Kwa kuzingatia taratibu faafu kitaalamu, ekari moja ina uwezo kusitiri kati ya migomba 450 – 550.

“Upanzi, nafasi ya mita 2.5 hadi 5 kati ya miche ya migomba ndiyo bora,” ashauri Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya matunda na miti, na kuongeza kuwa mbolea ya mifugo ndiyo faafu na ichanganywe na udongo na fatalaiza.

“Kilimo cha matunda kinafanikishwa na uwepo wa maji ya kutosha,” asisitiza, akielezea haja ya kukumbatia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji.

“Mataifa kama vile Misri na Israili, yameibuka kuwa bora katika uzalishaji wa matunda kwa sababu ya mfumo wa kuvuna maji licha ya kuwa jangwa. Kenya tuna hali bora ya anga na maji ya kutosha, muhimu ni kuweka mikakati kabambe kuyavuna ili kufanya kilimo,” Mwenda anafafanua.

Hannah Njoki anasema hutegemea maji ya mvua, ombi lake kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu na pia ya kitaifa likiwa kuzindua miradi ya maji ili aendeleze azma yake katika ukuzaji wa ndizi.

Mwanazaraa huyu anaendelea kutathmini suala la uongezaji mazao yake thamani, hasa kuyaivisha ili kuwahi soko bora.

Mbali na ukuzaji wa ndizi, Njoki pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi na kuku, mbolea ya mifugo hao akiitumia kuboresha migomba.

LISHE: Ndizi na viazi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MATOKE ni chakula chenye asili ya kiganda.

Hata hivyo, wanavyopika raia wa Uganda na tunavyopika sisi Wakenya ni tofauti. Raia wa Uganda wana mazoea ya kuyapika kwa mvuke tu ilhali Wakenya mpaka tuyapambe kwa viungo tofauti tofauti.

Aidha zipo njia nyingi sana za kupika ndizi hizi mbichi. Unaweza ukakaanga, kuchemsha na kuziponda ndizi.

Matoke ni rahisi sana kupika na ni chakula kitamu na pia kinapatikana kwa bei ambayo kwamba wengi wanaweza kuimudu.

Pamoja na ladha yake muruwa, matoke vile vile yana faida aina aina za kiafya. Kwanza yanasaidia kupunguza uzito kwa kudhibiti upataji wa kalori.

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa mapishi: Dakika 40

Walaji: 4

Ndizi na viazi kabla kupikwa. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

 • matoke (ndizi mbichi) 12 kubwa
 • viazi kilo 1 ½
 • nyama kilo 1
 • nyanya 4 zilizokatwa katwa au kusagwa
 • karoti 1 iliyokatwa katwa
 • dhania 1
 • pilipili mboga 1 iliyokatwakatwa
 • nyanya ya kopo
 • kitunguu saumu kilichosagwa kijiko 1
 • pilipili manga kijiko 1
 • curry powder vijiko 2
 • chumvi kiasi
 • mafuta ya kupikia/ uto vijiko 2 vya mezani

Maelekezo

Bandika sufuria mekoni kisha ueke mafuta ya kupikia na yakishika moto, weka kitunguu maji.

Kitunguu kikikaribia kuwa hudhurungi, weka pilipili manga, curry powder na kitunguu saumu na uendelee kupika kwa dakika mbili. Sasa weka karoti, pilipili mboga na dhania pia uzipike kwa dakika mbili.

Weka nyanya, nyanya ya kopo pamoja na chumvi ukipenda, kisha ufunike upike kwa dakika tano au mpaka nyanya ziive na zikauke maji.

Weka nyama na supu yake pamoja na matoke na viazi. Kama nyama yako imelainika sana, unaweza ukaiacha uitie matoke na viazi vitakapoiva.

Pia, weka matoke na viazi kwa wakati mmoja kwa sababu vinachukua muda sawa kuiva. Kisha weka maji kiasi ili yasaidie matoke kuiva.

Funika matoke yako uyaache kwa dakika 25 (mpaka matoke na viazi vilainike).

Matoke yapo tayari. Unaweza ukayaacha na maji mengi kiasi kama unataka yawe na rojo ili ufurahie utamu au ukayaacha yawe makavu. Pia unaweza ukaweka Royco na kuyaacha yatokote kwa dakika mbili.

Pakua na ufurahie.

ULIMBWENDE: Ndizi na urembo

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MBALI na kuliwa, ndizi zina manufaa mengine, hasa katika urembo wa ngozi.

Ndizi zina virutubisho muhimu vinavyoboresha ngozi.

Ndizi pia zina aina tatu za sukari zinazojulikana kama ‘sucrose’, ‘fructose’ na ‘glucose’.

Hakikisha unanawa uso wako mara mbili kwa siku. Unapofanya hivyo, unaondoa uchafu.

Ndizi husaidia kuzuia chunusi.

Hakikisha unanawa uso kwa sabuni ambayo inaendana na ngozi yako. Ikiwa ngozi yako ni ya mafuta, hakikisha unatumia sabuni ambayo itakuacha ukiwa mkavu na kama ngozi yako ina ukavu, jioshe na sabuni itakayokufanya uwe na unyevu.

Kulainisha ngozi

Changanya asali na ndizi kipande kimoja cha ndizi iliyopondwa na upake kwenye uso na shingo.

Nawa uso kwa maji fufutende baada ya muda wa nusu saa. Fanya hivi angalau mara moja kwa wiki.

Kung’arisha uso

Ndizi huwa na Vitamini C ambayo husaidia kuiweka ngozi kuonekana iking’aa. Kwenye ndizi iliyopondwa, ongeza vijiko viwili vidogo vya juisi ya limau na upake kwa uso na shingo. Osha kwa maji fufutende baada ya dakika 20.

Ni vizuri kupaka mchanganyiko huu wakati unataka kuenda kulala.

Kuzuia mikunjo

Ponda parachichi na ndizi pamoja. Paka kwa uso na uoshe baada ya muda. Mchanganyiko huu hulainisha ngozi ya uso na kuwa laini lakini pia hupunguza ukubwa wa matundu ya ngozi ya uso wako.

Kusugulia uso (Scrubing)

Changanya ndizi na sukari kijiko kimoja, kisha paka usoni na usugue taratibu. Ndizi hulainisha ngozi kavu na sukari huondoa seli zilizokufa kwenye ngozi.

Saga ndizi moja na Oats vijiko vitatu kisha changanya na asali na maziwa. Paka usoni kwa dakika 15 kisha sugua. Baada ya dakika 15 osha.

Kiwanda cha kuongezea ndizi thamani Kisii

Na RICHARD MAOSI

UKIZURU Kaunti ya Kisii, utaona ni sehemu ambayo wakulima wengi wanajivunia zao la ndizi.

Baina ya milima na mito, kilomita tatu hivi kutoka mjini Kisii, tulielekezwa katika taasisi ya Kenya Induastrial Research and Development Institute(KIRDI), ambapo tulikumbana na Aska Nyakwara anayetumia ndizi kutengeneza bidhaa mbalimbali.

“Kutokana na ndizi ninaweza kutengeneza unga, mkate, chakula cha wanajeshi, mvinyo, siagi chakula cha watoto na vibanzi,”akasema.

Aska ambaye ni mama wa watoto watatu anasema alihitimu na stashahada ya Food Science kutoka Kisumu Polytechnic mnamo 2003.

Kulingana naye alitafuta mbinu ya kujiajiri mara tu alipogundua amekulia katika sehemu ambayo wakulima wengi wanapanda ndizi, ingawa bidhaa hii haikuwa na soko la uhakika.

Kuanzia hapo alijizatiti na kuungana na vijana wa mtaani wakaanza kupanda aina nyingine ya ndizi ambazo hazikuwa zikipandwa katika kaunti ya Kisii, huku akilenga kutafuta soko la nje.

Baina ya 2004-2008 Aska alijiunga n Kenya Agricultural Livestock and Research Organisation(KALRO) kufanya utafiti kuhusu aina ya ndizi ambazo zingefanya vyema katika milima ya Kisii na Nyamira mbali na zile za kiasili.

Aska Nyakwara akionyesha chombo kinachotumika kukata ndizi kabla ya kuongezewa thamani.
Anasema kutokana na ndizi anaweza kutengeneza bidhaa nyingi kama vile mvinyo, mkate, chakula cha watoto, chakula cha wanajeshi miongoni mwa lishe nyinginezo. Picha/ Richard Maosi

“Aidha nilitaka kujua ni bidhaa gani zinaweza kutengenezwa kutokana na ndizi,”alisema, , hii ni baada ya kugundua kwamba kulikuwa na aina nyingine ya ndizi kama vile williams, paces na cavedish.

Kuanzia hapo shirika la KALRO, lilimsaidia kupata teknolojia inayohitajika na masine za kuzalisha bidhaa zinazotokana na ndizi.

Anasema kutokana na ndizi mtu anaweza kutengeneza aina nyingi ya vyakula muradi awe na mtaji wa kutosha pamoja na ujuzi unaohitajika.

Aidha mjasiria mali atahitajika kudumisha usafi wa hali ya juu, mbali na kupata kibali kutoka kwa shirika la ubora wa bidhaa KEBS.

Anasema kiwanda chake kimesaidia kutoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana, kuanzia hatua ya kuvuna shambani, mpaka wakati wa kufikisha mazao katika karakana yake.

Kulingana na Aska ni dhahiri kwamba wakulima wanaweza kupata hela nyingi endapo wataongezea mazao yao thamani, badala la kuyauza moja kwa moja ambapo wakati mwingine mazao huharibika.

Kuongezea ndizi thamani kumesaidia kukabiliana na matapeli ambao wamejaa sokoni, ambao mara nyingi huwanunulia wakulima ndizi kwa bei nafuu na kuuza kwa bei ghali.

Chakula cha wanajeshi

Anasema kutokana na ndizi zilizoiva anatengeneza chakula cha wanajeshi ambacho ni ungaunga uliokausha na kusagwa.Hatimaye huchanganywa na madini muhimu ya protini na kabohaedreti.

Chakula hiki kina nguvu kwa sababu mchanganyiko wake vilevile umejaa maziwa na ndicho wanajeshi hutumia wakiwa vitani ili kuwarudishia nguvu.

Hatua ya kuandaa chakula cha wanajeshi ni pamoja na kuchanganya unga wa ndizi, njugu, maziwa na aina nyingine ya nafaka.Kisha hukandwa kwa maziwa.

Mbali na kuongeza nguvu mwilini, husaidia kuimarisha uwezo wa macho kuona mbali na kukinga mwili dhidi ya mkurupuko wa maradhi.

Vibanzi

Aska anasema ameajiri vijana wengi ambao humsaidia kutembeza bidhaa kutokana na ndizi sokoni mojawapo ikiwa ni vibanzi.

Vibanzi hivi huwa vimepakiwa katika gramu mbalimbali, kuanzia gramu 50 ambayo huuzwa Sh 30 hadi gramu 100 ambayo huuzwa Sh55.

Anasema kutokana na mkungu mmoja wa ndizi anaweza kutengeneza vibanzi vyenye thamani ya Sh 2200 ambapo mkungu mmoja huuzwa Sh 700.

Akifanya hesabu yake anaweza kutengeneza faida ya Sh1,500 zaidi ya mara tatu bei ya kawaida ya mkungu wa ndizi.

Anasema ndizi hununuliwa kutoka kwa wakulima , ambao husafirisha bidhaa zao katika maeneo ambayo yametengwa ili kupima kwanza.

Aska anasema husambaza vibanzi katika maduka ya kijumla mjini Kisii, Kisumu, Bomet na Narok.

Bidhaa nyingine anazouza kupitia mtandao wa kijamii ni mvinyo huku lita moja ikiuzwa kwa Sh800.

Kulingana na Aska anasema mtandao wa kijamii ni mojawapo ya njia bora kwa muuzaji kusambaza bidhaa zake kwa wauzaji ambapo wateja wengi wamekuwa wakiitisha bidhaa hasa wakati huu wa makali ya Covid-19.

Chakula cha watoto

Hiki ni chakula cha watoto kuanzia miezi sita hivi, ambapo ni unga unaoweza kuchanganywa na maji au maziwa kisha ukapewa watoto.

Anasema kuwa unga huu utakuwa sokoni hivi karibuni ikizingatiwa kuwa manufaa yake kwa watoto wanaokuwa ni makubwa.

Aska anaomba serikali ya kitaifa kuwekeza katika nguvu kazi za vijana wasiokuwa na ajira, kutoa mikopo bila riba ili vijana waweze kujiajiri.

Pili anawashauri vijana kujiunga na taasisi kama vile Kalro ili kujifunza teknolojia mbalimbali za kuongezea mazao ya shambani thamani.

VINYWAJI: Jinsi ya kuandaa ‘smoothie’ ya papai na ndizi

Na DIANA MUTHEU

dmutheu@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 5

Vinavyohitajika

 1. Papai ½
 2. Ndizi 1
 3. Maziwa glasi 1
 4. Blenda
Viungo vinavyohitajika kutengeneza ‘smoothie’ ya papai na ndizi. Picha/ Diana Mutheu

Jinsi ya kuandaa

Toa maganda ya matunda yako kisha yakatekate vipande vidogovidogo ukivitia ndani ya blenda yako.

Ongeza maziwa katika mchanganyo huo wa matunda kisha hakikisha unasaga katika blenda hadi ‘smoothie’ yako ilainike vizuri.

Viungo ndani ya blenda. Picha/ Diana Mutheu

Koroga na umimine katika kikombe chako. Burudika.

LISHE: Ndizi

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji: 2

Vinavyohitajika

 • ndizi mbivu
 • nyama kilo 1 (iliyopikwa)
 • vitunguu maji 2
 • giligilani kijiko 1
 • Garam masala kijiko 1
 • nazi 1
 • nyanya 4 zilizoiva
 • kitunguu saumu 1
 • nyanya ya kopo kijiko 1
 • tangawizi
 • chumvi
 • karoti 1
 • pilipili mboga 1
 • Curry powder kijiko 1

Maelekezo

Kwenye sufuria mekoni, weka mafuta ya kupikia.

Mafuta yakiwa tayari, weka vitunguu maji kisha pika kwa muda wa dakika mbili.

Weka kitunguu saumu, tangawizi, garam masala, giligilani na curry powder; pika kwa dakika moja kisha weka nyanya.

Pika nyanya ziive mpaka zitengane na mafuta, kisha weka nyanya ya kopo iache kwa dakika moja.

Weka ndizi, chumvi na nyama pika kwa dakika 10 kwa moto ya wastani mpaka nyanya zichanganyike na ndizi.

Weka tui ya nazi pika kwa dakika 5, kisha weka tui zito acha mpaka tui lipungue, katia pilipili hoho na karoti pika kwa dakika 10.

Pakua na chochote ukipendacho.

AKILIMALI: Ndizi ni uwekezaji wa maana, panda kwa wingi

Na JOHN NJOROGE

njorogejunior@gmail.com

Kwa safari ya kilomita 10 kutoka kituo cha magari cha Cheponde katika barabara ya Molo- Nakuru, tunapitia kwa njia nyembamba ambayo ni mbovu, inayopitia katikati ya shamba la Cheponde mjini Elburgon na kutufikisha nyumbani kwake Timothy Gachie na kumpata akiwa kazini katika shamba lake lililoko Keriko eneo la Rongai katika kaunti ya Nakuru.

Huku amevalia shati ya kahawia, suruali ya kijivu na viatu vya kazi, Gachie alikuwa akiangalia na kuzunguka kwa miti ya ndizi yake iliyoharibika.

Kando kidogo, wake wawili wa mzee Gachie walikuwa wanakata nyasi na matawi ya viazi vitamu kwa ng’ombe wao wa maziwa.

Gachie ni dereva mstaafu wa malori ambaye kwa sasa hujihusisha na ukulima wa kikuu kwa shamba lake la ekari nane ambazo amezigawanya kwa sehemu tofauti. Kati ya hizo ekari nane, nusu ekari ameitenga kwa upanzi wa ndizi ambayo anakuza kwa wingi.

“Nilipokuwa nafanya kazi katika nchi ya Uganda, nilitambua kuwa mwajiri wangu alikuwa na shamba kubwa ambalo alipanda ndizi nyingi. Akiwa shambani la mwajiri wake, aligundua kuwa hakuwa na kazi nyingi aliyoifanyia kwa shamba lake la ndizi,’’ akasema Gachie.

Alisema bosi wake alihakikisha ndizi zake hupata maji ya kutosha na pia kukata matawi ya shina yaliyokua kupita kiasi.

Wakati Gachie alistaafu miaka sita iliyopita, alianza ukulima wa ndizi na kwa vile shamba lake ni kubwa, alitenga sehemu na kupanda miti ama shina ya ndizi aliyoitoa nchi ya Uganda.

“Ukulima wa ndizi ndio rahisi kwa mkulima yeyote. Maji na mbolea pekee ndiyo huhitajika katika msimu wa kupanda,’’ akasema Gachie.

Kwa muda wa mwaka mmoja, mkulima huyu alisema miti ya ndizi huanza kuibuka na rangi ya zambarau huanza kuonekana katika sehemu ambayo ndizi huchipukia.

Hata hivyo, Gachie alisema maji na mbolea nyingi husabambisha miti ya ndizi kumea na kukua kwa upesi.

“Kwa wakati huu, mkulima hustahili kutoa matawi ama sehemu za miti ya ndizi (suckers) zilizokua kupita kiasi,’’ akasema na kuongeza kuwa aliendelea kunyunyizia mbolea kwa miti ya ndizi ilipokuwa ikikua.

Wakati wa matayarisho ya shamba, wakulima wa ndizi huagizwa kulima shamba wakati wa kiangazi ili kutokomeza magugu na kupata wasaa mzuri wa kupanda wakati mvua ndefu inapoanza.

Kulingana na idara ya kilimo, ukubwa wa mashimo unapopanda wakati wa kiangazi hufaa kuwa 90 kwa 90 kwa 90 cm na 60 kwa 60 kwa 60 cm katika sehemu zilizoko na mvua.

Afisa mmoja ambaye ni mtaalamu wa wadudu na magonjwa na ambaye aliomba tulibane jina lake alisema kuwa wadudu kama vile Banana Weevil, Nematodes na Banana Silvering Thrips ndio huvamia ndizi mara nyingi.

“Wadudu kama vile Banana Weevils hutegwa kwa kutumia vipande vya shina vilivyozeeka nazo Banana Silver Thrips hunyunyiziwa dawa ya wadudu,’’ akasema.

Alisema kuwa magonjwa yanayo athiri ndizi ni kama vile Cigar, End Rot, Panama, Sigatoka Leaf Spot, Bacterial Xanthomas Wilt, Black leaf Streak, Bunchy Top na Anthracnose baadhi ya magonjwa mengine.

Gachie amepanda migomba mia nne (400) katika shamba lake lakini mia mbili (200) kati ya hayo yaliharibika wakati mvua ya mafuriko ilinyesha hivi majuzi.

“Nilipata hasara zaidi ya laki mbili wakati wa mafuriko hayo ambapo nilitarajia kupata zaidi ya milioni mbili baada ya mauzo katika mwisho wa mwaka huu,’’ akasema huku akionyesha baadhi ya ndizi zilizoharibiwa.

Gachie alifichua kuwa yeye huuza ndizi zake ndani ya nchi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwa shilingi elfu moja na kumlipa mfanyi kazi wake anayewatunza na kuyafanya kazi kwa shilingi mia mbili kwa siku.

Kulingana naye ndizi hazina msimu wa kuvuna hasaa zikiwa zimepata mbolea ya kutosha.

Mkulima huyu anakumbuka siku moja ambapo alipata elfu hamsini (50,000) kwa mauzo ya ndizi ambazo alisema kuwa ndio kiwango cha juu sana kwa mkulima wa ndizi kupata kwa siku moja.

“Serikali kuu na zile za kaunti hufaa kutengeneza na kutafuta soko kwa wakulima wa ndizi ilikuuza mazao yao kwa bei nafuu,’’ akasema.

Gachie amechiba bwawa ndogo ambapo yeye hutumia magomba anaponyunyizia maji.

Gachie amewekeza pakubwa kwa ukulima wake wa ndizi ambapo aliongeza kuwa aliacha ukulima wa mahidi ili kujishughulisha na ukulima wa ndizi.

“Mahindi yana kazi nyingi kabla ya muda wa kuvuna kufika. Afadhali nipande vyakula vya miezi michache kuliko nipande mahidi,’’ akasema.

Alikiri kuwa hata ingawa ana shamba kubwa ambalo angelitumia kufuga mifugo, aliacha ufugaji wa ng’ombe za maziwa na kuingia kwa kilimo.

Gachie pia hupanda vitunguu, mboga, pilipili, dania baadhi ya zingine.

Wakulima wengi katika maeneo ya Elburgon na Molo wameacha kilimo cha mahidi ambacho huchukua muda mrefu kabla mavuno na kujiingiza na kilimo biashara.

Katika ukulima huu, mkulima hupanda vyakula vyake katika sehemu ndogo ambayo humpa mapato mazuri.

AKILIMALI: Vijana wabuni ajira kwa kusaga unga wa ndizi

Na PETER CHANGTOEK

CHINI ya umbali wa kilomita moja kutoka katika soko la Muthinga, katika wadi ya AguthiGaaki, kwenye uga wa chuo cha mafunzo anuwai cha Gathinga, mjini Nyeri, ndipo lilipo kundi la vijana lijulikanalo kama G-STAR.

Kundi hili lilituzwa kwa tuzo ya ‘mkulima bora’ katika maonyesho ya mwaka huu mjini Nyeri. Wanachama wa kundi hilo huzikagua, kupima uzani wa ndizi na kuzinunua kutoka kwa wakulima wanaoyawasilisha mazao hayo katika eneo hilo.

“Sisi huzinunua ndizi kutoka kwa wakulima kwa Sh12 kwa kilo moja, na kuzisaga kuwa unga,’’ adokeza Charles Wachira, 37, ambaye ni mwenyekiti wa kundi hilo, huku akitukaribisha kwa moyo mkunjufu.

Mnamo mwaka 2013, kundi hilo liligundua kuwa kulikuwako na uharibifu wa mazao ya ndizi baada ya kuvunwa katika eneo hilo, na wakaja na wazo la kuzuia kutokea kwa uharibifu huo. Hivyo basi, wakaamua kuboresha thamani ya ndizi kwa kuzikausha na kuzisaga kuwa unga, na hivyo kuzibuni nafasi za ajira.

Pindi tu ndizi zinaponunuliwa nao, husafishwa, na maganda huambuliwa na kukatwakatwa kuwa vipande vidogo na kusafishwa tena, kisha, ndizi hizo huwekwa kwenye kikausho cha sola. Kabla ndizi hizo hazijasagwa, kifaa fulani cha kupima hali ya unyevu hutumiwa kupima iwapo zimekauka ipasavyo.

Licha ya mafanikio ambayo kundi hilo limeyapata, hayakupatikana kwa urahisi.

Kundi lenyewe lilianzishwa na wanachama wanane tu, mnamo mwaka 2013, na mwaka mmoja baadaye, likaanza kuzitafuta hela za kuliwezesha kundi kuziendesha shughuli zake.

Baadhi ya wanachama wa kundi la G-ST wakipakia bidhaa wanazozitengeneza kwa kutumia ndizi, katika chuo cha anuwai cha Gathinga, mjini Nyeri. Picha/ Peter Changtoek

Mnamo mwaka 2015, lilipokea fulusi kutoka kwa mashirika matatu yasiyokuwa ya serikali. Lilipokea Sh50,000 kutoka kwa Uwezo Fund, Sh100,000 kutoka kwa Hazina ya vijana, Sh90,000 kutoka kwa shirika la USAID kupitia kwa mradi ujulikanao kama ‘Yes Youth Can Program’ na mnamo mwaka 2018, vilevile, likapokea Sh1.775 milioni kutoka kwa mradi wa Upper Tana.

Aidha, kundi hilo likapata mafunzo kutoka kwa asasi tofauti tofauti; mathalani Wambugu Farm, na chuo kikuu cha JKUAT kuhusiana na utengenezaji wa chakula.

Hata hivyo, changamoto kuu ikawa ni kutokuwa na shamba la kuendeshea shughuli zao, kwa sababu wanachama walipoomba fedha, mashirika yasingekubali kutoa fedha kwa mradi ambao ungeanzishwa katika shamba la mtu binafsi.

Jitihada za kulitafuta shamba zikaanza, na ikawachukua takribani miaka mitatu ili kulipata. Kwa wakati uo huo, wanachama sita wakaondoka kutoka kwenye kundi, na wawili tu ndio wakasalia. Jambo hilo likawashurutisha wawili hao kuwasajili wanachama wengine ili wapate ufadhili wa kifedha, la sivyo wangeambulia patupu.

Kundi hilo lilipewa kipande cha ardhi na serikali ya kaunti, katika chuo anuwai cha vijana cha Gathinga na shughuli za ujenzi wa kiwanda zikang’oa nanga.

Kwa sasa, kiwanda hicho kina vikausho vitatu vya sola, ambavyo hukausha kilo 400 kwa wiki moja.

Baada ya ndizi kusagwa, huchanganywa na unga wa mtama na mahindi kwa vipimo vya 1:1:2 (mtama, mahindi na ndizi mtwawalia). Unga uo huo uliochanganywa, hupakiwa na kuuzwa katika kaunti mbalimbali, kama vile; Nairobi, Nyeri na viunga vyake.

Kupunguza uharibifu

Agnes Muchiri, ambaye ni afisa aliyestaafu kutoka kwa Wizara ya Kilimo, katika kaunti ya Nyeri, anasema kuwa utengenezaji wa unga wa ndizi ni mojawapo ya mbinu za kupunguza uharibifu wa mazao baada ya kuvunwa shambani, huku virutubisho vilivyomo kwa ndizi mbichi vikisalia kwa unga huo.

“Unga huo una uwanga ambao husaidia utumbo kuwa na afya,’’ afichua mtaalamu huyo.

Ndizi zina manufaa mengi katika mwili wa binadamu. Zina madini aina ya ‘Potassium’, ambayo husaidia moyo kufanya kazi vyema, na pia husaidia mwili kutekeleza shughuli ya mmeng’enyo wa chakula (digestion) vizuri.

Pia, ndizi zina madini aina ya ‘Magnesium’, ambayo husaidia misuli na husaidia kuboresha usingizi kwa waja.

Isitoshe, zina madini ya zinki (Zinc), ambayo huimarisha kinga dhidi ya maradhi katika mwili wa mwanadamu.

Vilevile, ndizi huwa na madini aina ya fosforasi (Phosphorous), ambayo husaidia moyo kufanya kazi vyema mwilini.

AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni chenye manufaa tele

Na SAMMY WAWERU

KATIKA shamba la Lucy Muriithi, tunakaribishwa na rangi ya kijani cha migomba. Kuna inayozalisha ndizi, mingine inachana maua na mingine ingali midogo.

Mama huyu anatazama kifungu cha ndizi kilichoning’inia mgombani, pengine kukagua ikiwa kimetosha kuvunwa.

“Baada ya wiki kadhaa kutoka sasa nitavuna ndizi zilizokomaa,” anadokeza Bi Muriithi.

Kijiji cha Karii, Kangai Kaunti ya Kirinyaga anakokuza ndizi, shughuli mbalimbali za biashara na kilimo zimeshika kasi, angaa kujizimbulia riziki.

Wakazi waliojituma wanaonekana kujishughulisha katika kilimo cha nyanya, mboga za aina mbalimbali, mahindi, matunda na maharagwe.

Katika ekari moja ya Lucy, ameipamba kwa matunda aina ya ndizi.

Alianza kilimo cha matunda haya 2014 baada ya kuchoshwa na maharagwe ya Kifaransa maarufu kama French beans, na miaka mitano baadaye hajutii kamwe mkondo aliochukua.

“Soko la maharagwe hayo lilidorora, nikakosa kampuni za kuuzia kwa sababu yanakuzwa kupitia kandarasi. Yaliishia kuharibikia shambani,” aeleza.

Mbali na kukumbwa na masaibu tele kupata soko, anasema gharama ya kukuza French beans ni ya juu mno. Hata hivyo, moyo wa Lucy sasa unatabasamu kwani umetulizwa na kilimo cha ndizi.

Zaraa ya ndizi haina mkuno wa nywele wala akili, kwani gharama ya leba, pembejeo na mtaji ni nafuu ikilinganishwa na mimea mingine. Isitoshe, soko la mazao si kikwazo kwa sababu matunda haya yana walaji wengi. Ndizi ni zao la nne bora duniani baada ya mchele, ngano na mahindi.

Mkulima Lucy Muriithi hupanda ndizi za migomba iliyoimarishwa kitaalamu, almaarufu ‘tissue culture bananas’.

“Nilianza na robo ekari na ilinigharimu Sh25, 000 pekee,” anafichua.

Mkulima huyu anasema kilimo cha ndizi hakihitaji mwalimu. Shamba likilimwa, mashimo yenye kimo cha urefu wa futi mbili yanaandaliwa. “Shimo linapaswa kuwa na kipenyo cha futi tatu, na nafasi ya mita tatu kwa tatu mraba – kutoka shimo moja hadi nyingine,” akaelezea.

Yanawekwa mbolea, karibu mageleni au madoo mawili kila shimo na mkulima huyo huichanganya na fatalaiza yenye madini ya Ammonia, Phosphorous na Nitrogen. Pia, hutia dawa dhidi ya wadudu.

“Nikishapanda, hurejesha udongo hadi kimo cha futi moja. Nafasi iliyosalia ni ya kutunza migomba kwa maji na mbolea,” asema. Ekari moja inasitiri takriban mbegu 1, 600 moja ikigharimu kati ya Sh70 – 100.

Bw James Macharia, mtaalamu, anasema ili kupata mazao bora, mengi na ya kuridhisha, machipukizi yanayotoka kandokando mwa mgomba mama uliopandwa yanapaswa kupogolewa na kusalia na manne pekee.

“Machipukizi mengi huleta ushindani wa lishe; maji na mbolea. Ni heri kusalia na machache yatakayotoa mazao ya kuridhisha,” anasema Bw Macharia.

Baadhi ya wakulima wangali wanaendelea kukuza ndizi kupitia mfumo wa zamani, ambapo machipukizi yanayojitokeza kandokando mwa migomba mama hutolewa na kutumika kama mbegu. Inatumika kwa msingi kuwa inapunguza gharama, pamoja na kupandwa moja kwa moja.

Akiwahimiza kukumbatia tissue culture bananas, Bw Macharia anasema mfumo wa zamani una changamoto zake kwani migomba na mazao huathiriwa upesi na wadudu na magonjwa kama Fusarium wilt, Sigatoka na Bacterial wilt.

Magonjwa ya virusi kama banana streak na bunchy top, yanasambazwa na machipukizi hayo. Fukusi na Nematodes, ni wadudu wanaoshuhudiwa mara kwa mara kwa migomba iliyopandwa kutoka kwa machipukizi. Mbali na kuwa na mazao duni, mtaalamu huyu anasema mfumo wa zamani unachukua muda mrefu kuzalisha.

“Ndizi zilizoimarishwa kitaalamu zinakidhi vigezo vya uhitaji wa soko pamoja na kusaidia kuongeza mapato kwa wakulima, wafanyabiashara husika na kunufaisha taifa kwa jumla,” anafafanua.

Ekari moja iliyotunzwa vyema ina uwezo kuzalisha zaidi ya tani 25, sawa na kilo 25, 000.

Hapa nchini ndizi hununuliwa kwa vifungu, na kulingana na Lucy Muriithi kimoja ni kati ya Sh400 – 800. Wateja wake hutoka Kagio na wengine masoko ya Nairobi.

AKILIMALI: Alienda Mombasa kusaka ajira lakini akageuka mkulima mahiri wa ndizi

Na HASSAN POJJO na LUDOVICK MBOGHOLI

HAMISI Bakari, 41, ni mzaliwa wa Matungu katika kijiji cha Namasanda huko Mumias, eneo la Magharibi mwa Kenya, aliyeajiriwa kazi ya kuuza vitambaa kwenye duka la Mhindi lililoko katikati mwa jiji la Mombasa.

Kwa sasa bwana Hamisi Bakari ni mkulima wa kujitegemea anayekuza zao la ndizi eneo la Chaani.

“Nilitoka kwetu nikiwa mkulima, nikaja Mombasa kuajiriwa. Lakini kazi niliyoipata ni ya kuuza vitambaa vya nguo na leso kwenye duka la Mhindi,” Bakari aambia Akilimali kwenye mahojiano.

Anasema alijitahidi sana.

“Kuuza kwa Mhindi kunahitaji moyo kwani nilishindwa kuendelea na kazi, ndipo nilipoamua kuanza shughuli za ukulima. Niliona ardhi ya Chaani hapa Changamwe ni yenye rutuba. Na kwa kuwa nilizoea ukulima huko nyumbani, nilihisi nianze rasmi kuitumia ardhi hii kwa kilimo,” Bakari afichua.

Anaongeza: “Ni sehemu ndogo sana niliyoianzishia ukulima kama hatua muhimu ya kunitoshelezea mahitaji ya kifamilia.”

Kulingana na mahojiano yake na Akilimali, uhaba wa mashamba mjini Mombasa haukumfanya akose kutimiza ndoto yake.

‘Nakubali hapa mjini kuna uhaba wa ardhi kwa ukulima, lakini haijalishi kwani uzoefu wangu umenipa maamuzi mapya ya kuwa mkulima stadi wa ndizi. Nilipania kuwa mkulima wa mashinani na hivyo badala ya kung’ang’ania kazi ya kuajiriwa, nikaanza kutafuta kazi mbadala ambayo ndiyo hii,” mkulima huyu adokezea zaidi Akilimali.

Hata hivyo Akilimali imegundua hamu kubwa ya Hamisi Bakari ni kujishugulisha na kilimo mseto, mbali na ukuzaji wa zao la ndizi.

Kama tulivyosema awali, Hamisi Bakari aliingia mjini Mombasa kutoka Mumias miaka 24 iliyopita, ambapo alitafuta kazi za kuajiriwa kabla ya kufanikiwa kazi kwenye duka moja linalomilikiwa na mfanyabiashara wa kihindi katika eneo la Mwembe kuku (biashara street).

Kazi aliyokuwa akiifanya ni kuuza vitambaa vya nguo na vipande vya Leso, lakini baadaye aliiona kazi hiyo haimfai, akaanza shughuli za ukulima wa mboga za kila sampuli sawa na ukuzaji wa zao la ndizi.

“Nilianza ukulima wa mboga za sukumawiki, mchicha, kunde na mabenda miongoni mwa mazao mengineyo,” asema Hamisi Bakari.

Anaendelea kutoa ufafanuzi.

“Hata hivyo sasa nashughulikia ukuzaji wa zao la ndizi, ambao nahisi unanikidhia mno mahitaji yangu. Hapa situmii mbolea maana udongo ni mzuri zaidi. Miongoni mwa sampuli za zao la ndizi ninazokuza zinatoka huko kwetu Mumias. Aina hizo ni mbokoya, shikhuthi, nashirembe na likomia (mkono wa tembo),” aarifu Akilimali.

Kutokana na juhudi zake tangu aanze shughuli za ukulima, tayari bwana Hamisi Bakari amenufaika pakubwa si haba.

‘Kwa kweli naona mafanikio makubwa mno kwenye shughuli hizi za ukulima. Miaka 4 iliyopita (mwaka wa 2015) nilianza kupata mafanikio makubwa ya ukulima, ndipo nilipoamua kuwa mkulima kamili kwa kuanzisha ukulima mseto’ asisitizia Akilimali.

‘Niliagiza aina tofauti za mbegu za ndizi (migomba) kutoka kwetu Mumias, nikazipanda na sasa naona mafanikio na faida yake’ asema mkulima huyu.

Aidha, Akilimali imegundua kuwa Bakari Hamisi ndiye mkulima wa pekee katika eneo ambalo anaishi.

‘Ni kweli, hapa ni mjini na hakuna wakulima. Mimi pekee ndiye niliyeamua kutumia ardhi hii kwa ukulima, hasa baada ya kugundua ina rutuba nyingi na muda mrefu imekuwa akikaa bure bila kutumiwa,” aelezea zaidi.

Kuhusu ushauri wake kwa wakazi wa Mombasa, mkulima Hamisi Bakari anasisitiza umuhimu wa kujituma kimaisha.

“Kama unaishi hapa Mombasa, usikae bure ukitafuta kazi ambazo hazipatikani. Kama hakuna kazi ya kufanya, tafuta kipande cha ardhi isiyotumika na uanze kushughulikia ukulima,” adai Bakari.

‘Wengi hudhania mjini hakufai kulimwa mazao, mbona mimi nimelima ndizi na najipatia faida?’ aliuliza mkulima huyu wa mjini.

Anadai maeneo ya mjini yana mapande ya ardhi yanayokaa bure ambayo yanaweza kutumiwa kwa ukulima.

‘Matajiri wanaomiliki ardhi kubwa ambazo hazitumiki, wawape wanaotaka kuzistawisha kwa ukulima ili wajipatie riziki. Sio vizuri ardhi hizo zikae miaka mingi na hazistawishwi’ ashauri bwana Hamisi Bakari kwenye mahojiano na Akilimali.

AKILIMALI: Alifanya hesabu; ndizi zamlipa kuliko mahindi

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA jamii nyingi Magharibi mwa Kenya, ndizi ni mojawapo ya mimea muhimu ambapo ni nadra kuingia katika boma la yeyote na kukosa.

Hii ni mojawapo ya sababu zilizomsukuma Mzee Musamula Patrick Deans, 61, mkazi wa kijiji cha Busaina, Mbihi, Kaunti ya Vihiga kujitosa katika aina hii ya kilimo.

Kwa Bw Musamula, udogo wa shamba lake haujamzuia kujihusisha na kilimo hiki ambapo huu ukiwa mwaka wake wa tatu tangu ajishughulishe vilivyo katika kilimo hiki, anazidi kufurahia mazao.

Licha ya kwamba shamba lake ni la ukubwa wa ekari 0.9 pekee, kwa sasa ana mimea 32 ya ndizi mbapo anashughulikia aina tatu ya mmea huu; fhia 17, valery na grand Nain.

“Nina mimea minane ya fhia- 17 na mimea mingine 25 ni mchanganyiko wa ndizi aina za valery na grand nain,” anasema.

Kulingana na Musamula, wazo la kujihusisha na kilimo hiki lilimjia baada ya kufanya utafiti na kugundua kwamba angepata mazao mengi kutokana na mmea huu ikilinganishwa na mahindi ambayo yanapandwa kwa wingi katika sehemu hii.

“Kwa mfano, niligundua kwamba shamba la ukubwa wa mita 7m x12m lingetoa gunia moja la kilo 90 la mahindi lenye thamani ya Sh4,000. Kwa upande mwingine, kwenye nafasi hiyo hiyo ningepanda mimea sita ya ndizi na baada ya mavuno ya kwanza, kila mmoja ungenipa migomba mitano ya ndizi, ikiuzwa kwa Sh800 inaleta Sh24,000,” aongeza.

Mbali na masuala ya kitamaduni, ari yake ya upanzi wa ndizi ilitokana na faida zinazotokana na mmea huu.

“Awali nilikuwa nahusika na kilimo cha mahindi, ambapo mazao hayakuwa na faida sana, tulikuwa tunatumia tu kwa lishe. Baadaye niligundua kwamba ndizi zingeniletea faida kubwa hasa ikizingatiwa kwamba bei yake sio mbaya sokoni,” aeleza.

Tangu aanze kulima amevuna zaidi ya migomba 60 ya ndizi, suala ambalo limempa matumaini mengi. Lakini haijakuwa rahisi kwa Musamula kwani kilimo hiki kina gharama zake.

“Nilikuwa na mashimo 32 ambapo kila moja lilikuwa likijazwa na toroli moja ya mbolea ya kawaida. Sokoni, bidhaa hii inanunuliwa kwa Sh80 kwa kila kilo. Aidha, shimo hilo lazima lijazwe kwa gramu 240 za mbolea ya DAT inayonunuliwa kwa Sh50 kwa kilo. Pia, uchimbaji mashimo haya una gharama kwani kila moja inagharimu Sh150. Mbali na hayo, lazima uwe tayari kuondoa magugu, shughuli inayofanywa mara moja kwa mwaka,” aongeza.

Fedha bado kidogo

Anasema kwamba bado hajaanza kunufaika vilivyo kifedha kutokana na kilimo hiki, lakini ufanisi wake katika matumizi ya kipande kidogo cha ardhi kuzalisha mazao mengi umekuwa kivutio cha wakulima wengine eneo hili.

Sasa penzi lake limeenda hatua zaidi ambapo ameanzisha mradi wa kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusiana na kilimo cha ndizi.

“Mafunzo haya yanahusisha kuwafunza kuhusu jinsi ya kupanda mmea huu, vilevile thamani ya ndizi badala ya kujihusisha na upanzi wa mahindi pekee. Kwa wanaoishi katika eneo hili, hawahitaji kusafiri mwendo mrefu ili kujijulia kuhusiana na kilimo cha ndizi,” asema.

Kampeni zake zimempeleka vijijini na hata katika shule eneo hili huku zikiwavutia wakulima katika eneo hili na mbali.

“Kijijini, tayari nimepata watu wanne wanaotaka kujihusisha vilivyo na kilimo cha ndizi. Kwa upande mwingine, nimekuwa nikipokea mialiko ya kutoa mafunzo katika maeneo ya Kakamega na Eldoret,” aongeza na kusisitiza kwamba nia yake ni kueneza ufahamu wake kwa watu wengine na hasa vizazi vijavyo.

Anasema kwamba nia yake pia ni kuelimisha wakulima wa eneo hili na kuwapa ujuzi na mbinu za kujiimarisha kupitia kilimo tofauti, badala ya kujihusisha na upanzi wa mahindi na maharagwe pekee.

Penzi lake katika masuala ya kilimo lilianza mwaka wa 1981, ambapo wakati huo alikuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa misitu eneo la Kitui.

“Nilikuwa nimehudhuria chuo cha mafunzo ya juu ambapo nilisomea uchumi wa elimu misitu (forest economics),” asema.

Lakini penzi lake kwa upanzi wa ndizi lilitokana na tatizo la ardhi ambalo kwa miaka limekuwa likiwakumba wakazi wa eneo la Vihiga.

“Hapa, kwa kawaida tuna vipande vidogo vya ardhi, na hivyo niligundua kwamba mahindi ambayo yalipandwa kwa wingi hayakuwa na manufaa mengi kwa jamii yetu,” asema.

Kwa hivyo kama mtaalamu wa misitu anasema kwamba alifanya utafiti kuhusu mmea ambao ungemletea thamani kubwa kwa kipande kidogo cha ardhi.

“Tayari watu katika eneo hili walikuwa wanajihusisha na kilimo cha ndizi, lakini tatizo ni kwamba hawakuwa wanafanya hivyo ili kuwaletea faida,” aeleza.

Na hivyo Februari 2016 alikata shauri ya kujitosa katika ukulima wa ndizi baada ya kupokea ufadhili kutoka kwa mradi wa ustawishaji uchumi (economic stimulus program), kwa ufadhili wa Serikali ya Kaunti ya Vihiga na ushirikiano na Wizara ya Kilimo.

Licha ya kuzama katika kilimo cha ndizi, hajaacha taaluma yake ya awali kama mtaalamu wa misitu. Amekuwa akishughulika katika upanzi wa miche na kuuza katika sehemu zingine humu nchini na mbali.

Lakini kwa sasa anazidi kuimarisha ujuzi wake kama mkulima wa ndizi na anasema kwamba yuko tayari kupeleka mafunzo yake katika sehemu zingine nchini.

USHAURI: Kuwa makini unaponunua ndizi ili kuepuka zilizoivishwa kwa kemikali

Na SAMMY WAWERU

ILI kuwa mwenye siha bora, wataalamu wa afya wanahimiza kula chakula chenye madini kamilifu.

Madini muhimu kwenye mwili wa binadamu na ambayo hayapaswi kukosa ni Protini, Vitamini na Wanga. Mengine ni Calcium kwa minajili ya kuimarisha mifupa na Iron.

Katika orodha ya Vitamini, mbali na mboga, matunda yamesheheni madini hii. Kuna matunda tofauti kama vile machungwa, karakara, matufaha, maembe, mapapai, ndizi, zabibu, haya yakiwa machache tu kuorodhesha.

Wakulima wamekuwa wakihimizwa kukumbatia mfumo wa kilimohai.

Huu ni mfumo ambapo mimea inakuzwa bila kutumia kemikali, hasa mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa.

Magonjwa kama Saratani yanadaiwa kuchangiwa na lishe, hasa mazao yaliyozalishwa kwa pembejeo zenye kemikali. Wadau husika katika sekta ya kilimo hususan wataalamu wamekuwa wakihamasisha haja ya kufanya kilimohai ili kuepuka masaibu hayo.

Hata ingawa kuna wakulima wanaofuata ushauri huo, baadhi ya matunda yaliyokomaa na kuvunwa yanasemekana kuivishwa na kemikali.

Juliet Wanga afisa na mtaalamu wa masuala ya afya anasema mnunuzi anapaswa kuwa makini anaponunua ndizi, anazotaja zimeathirika pakubwa. “Ndizi zinapokomaa huvunwa na kusubiriwa ziive, baadhi ya wafanyabiashara wameibuka na mbinu mbadala – kutumia dawa zenye kemikali kuziivisha haraka. Hii ni hatari katika afya ya binadamu,” aonya Bi Wanga.

Ingawa ndizi zikiachiliwa kuivia shambani zinapokomaa huwa katika hatari ya kushambuliwa na wadudu, wakulima huzivuna na kuzihifadhi katika maghala. Aidha, kiwango cha joto kinachopendekezwa kufanikisha hilo ni nyuzi kati ya 14 na 16 katika kipimo cha sentigredi.

Wakulima wengi hufunika ndizi kwa majani au maganda ya migomba.

“Huyafunika kwa kuyazungushia maganda kisha ninayatia kwenye gunia na kulifunika. Huiva baada ya siku kadhaa,” asema Stephen Macheru, mkulima kutoka Nyeri.

Mtaalamu Juliet Wanga anatahadharisha kuwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wanatumia njia za mkato kuivisha matunda haya.

“Kwa kawaida, ndizi zinapaswa kuiva kati ya siku tatu hadi nne. Zinapovunwa zikiwa kijani, halafu siku inayofuata zinakuwa zimeiva unafaa kuwa na wasiwasi. Kuna wanaotumia mkato kwa kuziivisha kwa kemikali,” afafanua.

Ndizi zilizoiva ni za rangi ya manjano na zingine kijani.

“Sehemu zingine za maganda husalia na michirizi ya kijani. Ndizi yote ikiwa ya manjano una haki kuitilia shaka. Dawa inapotumika kuivisha huibadilisha rangi usione ya kijani,” anaonya.

Mdau huyu anahimiza wanunuzi kuwa makini wanapochagua matunda haya sokoni. Pia, anashauri haja ya kurejelea mfumo asilia – utumizi wa majani na maganda ya migomba kuivisha ndizi.

Mbali na kuyahifadhi katika maghala, matunda haya ukiyanunua yakiwa mabichi na uyaweke sakafuni yataanza kuiva baada ya siku tatu au nne.

MAPISHI: Jinsi ya kupika ndizi na samaki wa kukaanga

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji: 2

Ndizi. Picha/ Margaret Maina

Vinavyohitajika

 • Ndizi 6
 • Mafuta ya kupikia
 • Samaki 2
 • Kitunguu saumu
 • Chumvi kijiko 1
 • Limau au ndimu 1
 • Pilipili manga
 • Tangawizi 1
 • Vitunguu maji 2
 • Nyanya 2

Maelekezo

Menya na kisha kata ndizi mzuzu vipande vidogovidogo.

Weka kikaangio mekoni, mimina mafuta kwenye kikaangio chenyewe na usubiri yapate moto.

Weka ndizi zikiwa kwenye chombo mekoni, kisha acha kwa muda ziive. Hakikisha unazigeuza ili ziive vizuri pande zote. Weka ndizi zinazotosha ili ziive vizuri.

Ndizi zikiiva, epua na weka kwenye chombo safi kando. Rudia kwa vipande vilivyobaki hadi umalize.

Andaa samaki. Nyunyizia juisi ya limau vizuri juu ya samaki – nje na ndani – kwa uwiano ulio sawa ili samaki apate ladha nzuri. Nyunyiza chumvi vizuri nje na ndani ya samaki.

Ponda kitunguu saumu (au kama una kitunguu saumu cha unga) kisha paka juu ya samaki vizuri, nje na ndani vilevile. Nyunyizia pilipili manga ya unga juu yake na mpake kwa ndani pia. Hakikisha unaweka kiungo hiki tu endapo unakula pilipili kwa sababu kama hutumii pilipili hii hatua si lazima.

Weka tangawizi kwenye samaki. Paka vizuri kwa nje na ndani.

Kata vitunguu maji; weka kwenye kikaangio chenye mafuta ya kupikia. Kaanga hadi viwe vya rangi ya kahawia. Sasa weka nyanya huku ukikoroga.

Zikiiva, weka samaki juu ya vitunguu ili iwe rahisi majimaji yakichuja yanaangukia kwenye vitunguu.

Funika na kwenye moto wa wastani acha chakula chako kipikike kwa dakika 10.

Epua, pakua na ufurahie.

KILIMO: Manufaa ya mbegu za ndizi zilizoimarishwa ’tissue culture banana’

Na SAMMY WAWERU

HADI kufikia sasa baadhi ya wakulima wanaendelea kukuza ndizi kupitia mfumo wa machipukizi (suckers). Huu ni mkondo wa zamani ambapo migomba michanga inayojitokeza kandokando mwa migomba mama hutolewa na kutumika kama mbegu. Inatumika kwa msingi kuwa inapunguza gharama, ikiwa ni pamoja na kupandwa moja kwa moja.

Baadhi ya wadau wa masuala ya kilimo wanasema kwamba mfumo huo una changamoto zake kwani migomba na mazao huathiriwa upesi na wadudu na magonjwa kama Fusarium wilt, Sigatoka na Bacterial wilt.

Magonjwa ya virusi kama banana streak na bunchy top, yanasambazwa na machipukizi.

Fukusi na Nematodes, ni wadudu wanaoshuhudiwa mara kwa mara kwa migomba iliyopandwa kutoka kwa machipukizi.

Migomba inayoepuka na kustahimili changamoto hizo, huchukua muda mrefu kukomaa.

“Mazao ya mbegu za aina hiyo, machipukizi, huwa haba,” anasema James Macharia, mtaalamu kutoka Green Oasis Plants Centre, Murang’a.

Ukuaji wa teknolojia, pia umekuwa wenye tija chungu nzima katika sekta ya kilimo. Uzalishaji wa ndizi ni mojawapo ya inayojivunia kwa hatua hii.

Kujiri kwa mbegu zilizoimarika, maarufu kama ‘tissue culture bananas’ kumekuwa kwa manufaa kwa wakulima wa ndizi nchini.

Ni mfumo mpya, uliotafitiwa na kuidhinishwa, ambapo changamoto zinazoshuhudiwa kutokana na upanzi wa machipukizi kama mbegu zimetatuliwa.

Aidha, watafiti wameweza kuibuka na uzalishaji wa mbegu za hadhi ya juu na zinazowiana na uwezo wa ‘mmea mzazi’ au mother plant.

Kuwa salama

Kupitia mfumo huu mpya, Bw Macharia anasema miche mingi inazalishwa kwa wakati mfupi na huwa salama dhidi ya wadudu na magonjwa.

Migomba michanga hupelekwa katika maabara ili kuzalishwa mbegu-miche, kupitia taratibu zilizowekwa.

Baadaye huhamishiwa katika kifungulio, greenhouse, ili kutunzwa kwa wiki kadhaa kabla kupandwa.

Ndizi hukua vyema maeneo yanayopokea kiwango cha mvua zaidi ya milimita 1,000 kwa mwaka. Yasiyoafikia kigezo hiki, wakulima wanahimizwa kutumia mfumo wa kunyunyuzia maji mashamba kwa mifereji.

Mtaalamu James Macharia anasema udongo unapaswa kuwa wenye rutuba.

“Usiwe unatuamisha maji,” anashauri Bw Macharia.

Mtaalamu wa masuala ya kilimo, Bw James Macharia aonesha mazao ya ndizi zilizoimarishwa, tissue culture banana. Picha/ Sammy Waweru

Maji mengi husababisha mimea na mazao kuoza.

Miche ya ndizi hupandwa kwenye mashimo, moja likipendekezwa kuwa na upana-diameter, wa futi 3 na urefu wa futi 2 kuenda chini.

“Kipimo cha nafasi kati ya mashimo kiwe mita 3 mraba,” asema Bi Lucy Muriithi, mkuzaji wa ndizi zilizoimarishwa kaunti ya Kirinyaga.

Kulingana na mkulima huyu udongo wa juu huchanganywa na mbolea ya mifugo na ya kisasa pamoja na dawa dhidi ya wadudu.

Mchanganyiko huo hurejeshwa shimoni, linamwagiliwa maji kisha mche unapandwa kimo cha karibu sentimita 40.

Mtaalamu Macharia anashauri wakulima kupanda miche iliyoidhinishwa na taasisi husika za kilimo nchini kama vile Karlo.

Chuo Kikuu cha Masuala ya Kilimo na Teknolojia (JKUAT) pia huzalisha tissue culture bananas.

Baada ya upanzi, unahimizwa kutumia nyasi za boji-mulching, zilizokauka ili kuzuia uvukuzi wa maji.

“Maji ni kiungo muhimu katika kilimo cha ndizi. Mazao bora na mengi yanapatikana ukiwa na chanzo cha maji ya kutosha,” anaeleza mkulima Lucy, akidokeza kwamba hutegemea maji ya Mto Thiba ambapo ameelekeza mtaro shambani mwake.

Ndizi zilizoimarishwa huanza kuzalisha baada ya mwaka mmoja na miezi mitatu, kinyume na machipukizi yanayoanza baada ya miaka miwili.

Ekari moja ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 25 sawa na kilo 25,000.

Hata hivyo Lucy anasema ndizi huuzwa kwa vifungu vinavyozalishwa ambapo kimoja hugharimu kati ya Sh400 na Sh800.

MAPISHI: Jinsi ya kupika matoke

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa kupika: Dakika 30

Walaji: 2

Vinavyohitajika

 • Ndizi mbivu
 • Nyama kilo 1 iliyopikwa
 • Vitunguu maji 2
 • Giligilani kijiko 1
 • Garam masala kijiko 1 cha
 • Nazi 1
 • Nyanya 4 zilizoiva
 • Kitunguu saumu 1
 • Nyanya ya kopo kijiko 1
 • Tangawizi
 • Chumvi
 • Karoti 1
 • Pilipili mboga 1
 • Curry powder kijiko 1

Maelekezo

Kwenye sufuria safi, mimina mafuta ya kupikia kisha bandika mekoni.

Mafuta yakisha chemka, weka vitunguu maji kisha pika kwa dakika mbili.

Weka kitunguu saumu, tangawizi, garam masala, giligilani na curry powder halafu pika kwa dakika moja kabla ya kuongeza nyanya.

Pika nyanya ziive na mpaka nyanya zitengane na mafuta. Sasa mimina nyanya ya kopo na uiache kwa dakika moja.

Weka ndizi, chumvi na nyama na upike kwa dakika 10 kwa moto wa wastani mpaka nyanya zigande kwenye ndizi.

Tia tui ya nazi, pika kwa dakika saba, kisha weka tui nzito na uache mpaka tui ipungue, katia pilipili mboga na karoti na uache chakula kiendelee kuiva.

Pakua na chochote ukipendacho.

AKILIMALI: Kilimo cha ndizi ni rahisi, mapato ni mazuri

Na SAMMY WAWERU

MAENEO mengi nchini Kenya yana uwezo wa kuzalisha ndizi kwa sababu ya hali yake bora ya hewa na udongo.

Meru, Kisii, Nyeri, Nyamira, Kirinyaga, Kakamega, Embu, Bungoma na Murang’a ndizo kaunti tajika katika ukuzaji wa ndizi.

Maeneo mengine yanayotambulika ni Kerio Valley, Kericho, Makueni na Baringo.

Kulingana na wataalamu wa kilimo, zao hili linastawi katika maeneo yenye joto la wastani na kupokea mvua ya kutosha. James Macharia, mtaalamu wa kilimo Murang’a na ambaye pia ni mkuzaji wa zao hili, anasema ndizi hunawiri maeneo yanayopokea kiwango cha mvua milimita 2,500 au zaidi, kila mwaka.

“Kiwango cha joto kinapaswa kuwa nyuzi 27 sentigredi,” anasema Bw Macharia. Aidha, maeneo hayo yawe yenye urefu wa kati ya mita 0 hadi mita 1800, juu ya ufuo wa bahari (altitude).

Kuna aina mbalimbali ya ndizi, za upishi; Ng’ombe, Nusu Ng’ombe na za kijani zenye asili ya Uganda Green. Zinazokua maeneo kame; William, Grand Naine, Giant Cavedish, Gros Michel maarufu kama Kampala na Apple kwa jina lingine Kasukari.

Ni muhimu kutaja kuwa ndizi pia zinaweza kukuzwa kwa kutumia mfumo wa kunyunyizia maji mashamba (irrigation).

Kulingana na wakulima waliofanikisha kilimo cha ndizi, ni kwamba maji, mbolea na kupogoa matawi yanayochipuka ndivyo vigezo muhimu. Migomba, ambayo ni mbegu, ipandwapo huchukua karibu siku 340 ili kuanza kuzalisha na kuvuna ndizi.

“Msimu wa kiangazi, migomba huhitaji kunyunyiziwa maji mara moja au mbili kwa wiki,” aeleza Bi Mary Wairimu, mkulima Kirinyaga.

Taratibu za kupanda

Miaka ya awali, wakulima walikuwa wakitumia mbegu asili yaani migomba katika uzalishaji. Hata hivyo, muda unavyozidi kusonga teknolojia inaendelea kukua na kuvumbua mbinu za kisasa kunogesha sekta ya kilimo.

Watafiti kupitia taasisi husika za kilimo na ufugaji nchini, wanahimiza wanazaraa kutumia mbegu za kisasa na zilizoimarika kuzalisha ndizi, maarufu kama ‘tissue culture bananas’. Ni mbegu zilizotafitiwa, na kubainika kuwa na uwezo wa kudhibiti athari za magonjwa na wadudu wanaoshambulia matunda.

Mkungu wa ndizi. Picha/ Sammy Waweru

Ekari moja inasitiri wastani wa mbegu 540, moja ikikadiriwa kugharimu Sh120.

Kitaalamu, mashimo ya kupanda yanapaswa kuwa na urefu wa kati ya futi 1.5 hadi futi 2 kuenda chini, kila moja. Upana uwe futi 1.5.

“Nafasi ya shimo moja hadi lingine iwe kati ya mita 2.5 hadi mita 3,” aeleza Bw James Macharia, ambaye ni mtaalamu wa kilimo.

Kulingana na mdau huyu ni kwamba mkulima anapaswa kutia mbolea kwenye mashimo, ikifuatwa na udongo, japo lisijazwe. Mbegu zipandwe, kisha zimwagiliwe maji.

Siri za kufanikisha kilimo cha ndizi ni maji, mbolea na kupogoa matawi. “Nafasi shimo iliyosalia juu ni ya kutunza migomba kwa mbolea ya mifugo au kuku, ambayo huongeza kiwango cha mazao,” asema Bw Macharia.

Mgomba unapotoa migomba midogo kandokando, unahimizwa kuipogoa isalia na kati ya mitatu hadi mitano. Bw Macharia anasema hatua hii huwezesha iliyosalia kuzalisha ndizi kubwa bora na zenye hadhi ya juu, kwa sababu haitakuwa na ushindani wa chakula ambacho ni maji na mbolea.

Palizi pia ni muhimu kwa sababu hudhibiti usambaaji wa wadudu. Makwekwe pia huleta ushindani wa chakula kwa migomba.

Wadudu wanaoshambulia ndizi ni; Nematode na Fukusi. Magonjwa kwa ndizi ni Sigatoka, Fusarium Wilt na Bacterial Wilt.

Virusi vya mimea pia husababisha magonjwa kama banana bunchy top na banana streak. Mkulima anahimizwa kutafuta ushauri kutoka kwa watalaamu wa kilimo au maduka ya kuuza dawa za mimea, ili kukabiliana na changamoto za wadudu na magonjwa.

Kifungu kimoja cha ndizi mbichi kilichovunwa hugharimu kati ya Sh300-350 bei ya kijumla. Maeneo ya mijini, bei hupanda hadi Sh500.

Migomba huzalisha ndizi karibu kipindi cha miaka 10 mfululizo, kabla ya kuing’oa ili kupanda mingine.

Ni muhimu wakulima kuwa na njia mbadala za kuongeza ubora katika mazao wanayozalisha (value addition) ili kuongeza mapato. Ndizi pia husagwa kuwa unga wa kupika uji na ugali. Zilizoiva, huunda sharubati kwa kuchanganya na matunda mengine.

AKILIMALI: Migomba 220 ya ndizi imekuwa mbinu thabiti ya kujikimu kwake

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA Kaunti ya Kirinyaga, tulikutana na mkulima wa ndizi ambaye amefanya kilimo hiki kwa miaka saba sasa.

Bw Samwel Muchiri ni baba wa mtoto mmoja na mkazi wa eneo la Nyangati katika Kaunti Ndogo ya Mwea.

Ingawa yeye hukuza pia mpunga, viazi vitamu na mahindi, mmea anaoukuza kwa zaidi katika shamba lake la nusu ekari ni ndizi.

“Nimeligawa shamba langu katika vijisehemu vingi ili nikuze mimea tofauti,” anatanguliza Muchiri kwa kukiri kwamba katika sehemu ambapo ametenga ili iwe mahsusi pa kukuzia ndizi, amepanda migomba 220.

Kulingana naye, upanzi wa migomba humhitaji mkulima kuchimba mashimo yenye upana wa takriban sentimita 90 kwa kila upande na kisha kupanda miche ya ndizi huku akifukia mashimo kwa mchanga mwepesi na mbolea nyingi ya kiasili.

Baada ya upanzi huu, huwa anaanza shughuli ya kunyunyizia maji kwa wingi akitumia mifereji ili kufanikisha ukuaji wa miche kwa haraka.

Maji haya huwa anayatoa kwenye mto unaopitisha mkondo wa maji karibu na shamba lake.

Ili kuwezesha mimea hii kunawiri zaidi kwa njia bora, yeye huwa anatoa mimea na magugu yasiyohitajika kwa kutumia dawa na kadri migomba inapopata majani makubwa, huwa inaweka kivuli kote shambani ambapo pia ni njia mojawapo ya kuzuia majani yenyewe kukua kwa wingi.

Anadokeza kuwa baada ya muda, huwa anaongeza mbolea za dukani ili kuimarisha kasi ya kukua kwa migomba na uzalishaji wa ndizi.

Kwa kawaida, mgomba huchukuwa muda wa hadi miezi tisa kukomaa na kisha kumchukua muda wa miezi miwili zaidi ya kuvuna.

Kuvuna huku huwa kunafanyika mara moja kwa wiki hadi miezi miwili iishe.

Kwa mujibu wa Muchiri, kilimo hiki cha ndizi kuwa kinampa riziki ya kila siku kwani kimemwezesha kujipa ajira pamoja na kuyakimu mengi ya mahitaji yake binafsi na ya mkewe.

Kwa kawaida, migomba haina shughuli nyingi baada ya kupandwa na baadhi ya mambo ambayo huwa anafanya ni kunyunyizia maji angalau mara moja kwa wiki.

Bw Samwel Muchiri akielezea jinsi anavyotunza na kukuza ndizi katika shamba analolimiliki katika eneo la Nyangati, Mwea, Kirinyaga. Picha/ Chris Adungo

Bw Muchiri anaelezea kuwa wateja wake ni wafanyabiashara wa kati ambao hujinunulia ndizi kwa bei nafuu kabla ya kuchuuza katika masoko mbalimbali ya Kirinyaga, Nyeri, Murang’a na Nairobi kwa bei nafuu zaidi.

Katika msimu mzuri, Bw Muchiri huwa anauza kilo moja ya ndizi kwa Sh20 lakini kwa msimu wenye ushindani mkubwa kuto kwa mazao mengine haswa maembe, kilo moja ya ndizi humgharimu mnunuzi Sh14.

Anafichua kwamba mkungu mmoja wa ndizi unapovunwa, huwa na uwezo wa kutoa kati ya kilo 40 na 50 za ndizi.

Ina maana kwamba yeye hutia mfukoni kati ya Sh800 na Sh1,000 kutokana na mkungu mmoja wa ndizi.

Hata hivyo, anaungama kuwa wafanyabiashara wa kati huwa ni changamoto kubwa kwake kwani kwa kawaida, wao hutaka wanunue mazao yake kwa bei ya chini ilhali sokoni wanauza kwa bei ya juu.

Aidha, wadudu huwa ni changamoto pia na dawa za kupigana nao ni ghali mno.

Hata hivyo, anasema kilimo cha ndizi kina manufa mengi kwani baada ya kuvuna, miche mingine huchomoza na kukua na hata kustawi kama migomba mingine.

Bw Muchiri ana matumaini mengi na katika siku zijazo, anatarajia kuwa akijipelekea mazao yake sokoni ili kuepukana na wafanyabiashara wa kati ambao kwa wakati mwingine, huwadhulumu wakulima.

Jambo ambalo angeomba lifikie mashirika ya serikali na hasa Wizara ya Kilimo, ni wajue namna ya kuyashughulikia maslahi ya wakulima kwa kuandaa semina za kuwaelimisha na kuwapa ujuzi wa kisasa wa kutunza mimea na pia kupata mbegu bora ili kufanikisha
kilimo hiki cha ndizi hata zaidi.

Kaunti

Bw Muchiri pia anasema kuwa serikali za kaunti zina jukumu la kuimarisha kilimo mashinani kwani sekta hii pia ni wajibu wa gatuzi.

“Serikali za kaunti zinapaswa pia kuwavutia wawekezaji kwa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za ndizi ili wakulima wafaidike zaidi.”

Katika kilimo cha ndizi, Bw Muchiri mwanzo huwa anatayarisha mbegu katika sinia ili kuwezesha kukua kwa miche hadi itoe majani.

Mbegu hizi huwa ni za aina mbili, Williams na Grand Nine na ambazo huwa anaziagiza kutoka nchi ya Israeli kupitia kwa kampuni ya Aberdare Technologies.

“Baada ya mwezi mmoja katika sinia hizi, huwa ninatoa miche hii na kuiweka katika vijikaratasi ili kuiwezesha mizizi yake kukua,” anaelza.

Kulingana naye, miche hii huwa katika mazingira yenye kivuli ili kudhibiti hali ya joto inayoweza kutokana na jua.

Katika eneo hili, pia huwa anazuia kupatikana kwa wadudu na magonjwa.

Baada ya miezi miwili miche hii ikiwa katika karatasi hizi, huwa tayari kwa kuuzwa na kupandwa na wakulima wengine mbalimbali.

Wakati huu, huwa imefikisha urefu wa takriban sentimita 30 hivi.

AKILIMALI: Mkulima chipukizi wa ndizi anayevuma Rongai

Na FRANCIS MUREITHI

HUKU akiwa amevalia shati la samawati lenye mikono mifupi, kofia ya samawati na suruali ndefu ya rangi sawia, na viatu vya raba chapa gumboots, Patrick Kigen yuko kwenye shamba lake la ndizi katika eneo la Ol Rongai, kaunti ya Nakuru.

Hata bila ya kuinua kichwa chake juu Kigen ambaye ndio mwanzo umri wake unagonga miaka 28, anafyeka magugu na kuondosha matawi yaliyokauka kwenye ndizi wakati Akilimali ilipomtembelea hivi majuzi.

Mkulima huyu chipukizi amepanda migomba ya ndizi kwa shamba robo ekari na uchu wa ukulima wa ndizi aliupata kutoka kwa mamake Jane Tuigong ambaye alivuma zama zake kama mkulima shupavu wa ndizi katika eneo hili ambalo linapakana na mlima Menengai.

“Nilikuwa nafurahia kula ndizi tamu ambazo zilivunwa moja kwa moja kutoka shambani na mama mzazi. Hili lilinipa motisha kuwa hata na mimi siku moja nitabobea na kuwa mkulima mahiri wa ndizi,” anasema Kigen ambaye ni mtaalamu wa ulimwengu wa teknolojia ya taarifa na mawasiliano.

Na ili kufaulu katika kilimo cha upanzi wa ndizi aina ya FHIA 17, Grand naine na Williams, Kigen huchimba shimo la urefu wa kati ya futi moja unusu na futi mbili na upana sawia na huo.

Aidha anadokeza kuwa wakati mkulima anachimba shimo hilo ni sharti ahakikishe mchanga unaotoa kutoka juu ya ardhi na ule unaopatikana ndani ya shimo hauchanganywi.

“Miche ya ndizi yapaswa kutengana kwa kati ya mita tatu hadi mita nne ili kuipa miche hiyo nafasi ya kumea vizuri na kupata jua la kutosha. Kisha, mkulima anahitajika kuweka ndani ya shimo mbolea iliyokolea na kisha kuchanganya na mchanga mwororo alioutoa ndani ya shimo. Kisha kinachofuata ni kupanda miche na kuacha kibakuli cha maji na kuweka matawi yaliyokauka juu kuzuia unyevu na maji kuyeyuka wakati wa kiangazi,” anaelezea Kigen.

Ubora

Mbali na kuzuia unyevu na maji kuyeyuka, maganda yaliyokauka husaidia pakubwa kuchangia kuimarisha kiwango cha ubora wa udongo kwa kuzuia kukua kwa magugu haribifu.

Ili kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu, kama vile konokono na magonjwa mengine kama vile fusarium, yeye hunyunyuzia mimea yake dawa.

Ukulima wa ndizi una gharama zake hasa wakati wa kuanza kilimo hiki kwa vile mimea hushambuliwa na wadudu hatari ambao husababisha ugonjwa wa kupooza na ikiwa mkulima hatanyunyuzia madawa mapema huenda akapata hasara kubwa,” anasema Kigen.

Kigen huvuna kati ya mikungu mitano hadi 10 ya ndizi kila wiki na kisha kuiuza kati ya Sh200 na Sh800 kulingana na uzito na urefu wa mkungu.

“Wakati kilimo kimenawiri mimi huweka kibindoni kati ya Sh5,000 na sh10,000 kila wiki wakati nawasilisha ndizi zangu sokoni,” anasema Kigen.

Afisa wa kilimo cha matunda katika Kaunti ya Nakuru Joseph Gaturuku anasema kuwa ili wakulima wa ndizi wanufaike na jasho lao ni sharti wahakikishe wanafanyia udongo uchunguzi ili kubaini kama una magonjwa na endapo watafanya hivyo huenda wakapata mavuno kemkem.

“Uchunguzi wa udongo ni muhimu sana katika kilimo cha ndizi kwa vile mmea wa ndizi huchukua muda mrefu shambani na ni kupitia uchunguzi wa udongo ambapo mkulima atafahamu magonjwa yanayoweza kukwaza kilimo chake,” anasema Gaturuku.

Anatoa mwito kwa wakulima kumwagilia mimea yao maji kwa wingi.

AKILIMALI: Wanasayansi waibuka na aina ya ndizi isiyoathiriwa na magonjwa

NA FAUSTINE NGILA

HATIMAYE wanasayansi wamepata suluhu katika juhudi zao za kusaka aina bora zaidi ya ndizi inayoweza kustahimili ugonjwa hatari wa majani kunyauka unaosababishwa na bakteria.

Ugonjwa huo, ambao husababisha ndizi kuiva bila kukomaa, kuoza na hatimaye mmea kunyauka, umeathiri pakubwa uzalishaji wa ndizi katika maeneo ya milima katika kanda ya Afrika Mashariki na kuchangia uhaba wa chakula na riziki ya mamilioni ya wakulima.

Kabla ya uvumbuzi huu, iliaminika kuwa aina zote za ndizi katika kanda hii, isipokuwa aina ya Musa balbisiana, zilikuwa zinavamiwa na ugonjwa huu wenye chimbuko lake nchini Ethiopia ambao sasa umeenea hadi Afrika ya Kati.

Kundi la watafiti lililoongozwa na mkuu wa utafiri wa ndizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Tropiki (IITA) Prof Rony Swennen, mtaalamu wa mimea Dkt George Mahuku na mwenzake Dkt Valentine Nakato walitafiti aina 72 za miche ya ndizi za familia ya Musa.

Eneo la kati la jani changa zaidi la miche ya miezi mitatu lilitiwa kioevu aina ya Xcm ambamo bakteria za ugonjwa huo husafiria.

Dalili za matokeo zilifuatiliwa kila wiki kwa miezi minne, na matokeo ya mwisho kuthibitisha kuwa Musa balbisiana ni aina ya ndizi inayostahimili bakteria hizo zinazosababisha unyaukaji wa mimea.

Hata hivyo, utafiti huu ulikuwa na changamoto zake.

Ndizi za familia ya Musa balbisiana hazivutii watafiti wengi hasa katika uzalishaji wa mbegu mpya za kimseto, kwa kuwa ni za kundi la BB, ambalo lina aina ya ndizi zenye imani ya kishirikina za Tani, ambazo miche yake yenye ndizi zinazoweza kuliwa haiwezi kukuzwa shambani kwa kuwa haipatikani na hukuzwa kwa majani yake na kutengeneza lishe ya mifugo.

Kisayansi, ndizi zinazoweza kuliwa ni za kundi la A.

Ugonjwa wa mimea ya ndizi kunyauka husababishwa na bakteria ya Xcm na dalili zake ni pamoja na majani kugeuka manjano na kunyauka, kioevu cha manjano wakati mgomba umekatwa, kudidimia kwa kichipuko cha kiume, ndizi kuiva kabla ya kukomaa, rangi tofauti ndani ya ndizi na hatimaye kufa kwa mmea mzima.

Kuenea kwake ni haraka hasa kupitia kwa vifaa vyenye bakteria hii, wadudu wanaoruka na vifaa vya kupanda na kupalilia.

Ugonjwa huu hukabiliwa na wanasayansi kwa kuufuatilia kwenye mashamba, kung’olewa kwa mimea iliyoathirika na kutia dawa vifaa vyenye maambukizo.

“Uvumbuzi huu ni muhimu sana kwa mamilioni ya wakulima wa ndizi Afrika Mashariki, kwa kuwa mbinu bora ya kuzima ugonjwa ni kuunda aina ya mimea inayoustahimili,” akasema Dkt Nakato kutoka Uganda.

Maendeleo haya basi yanawapa watafiti nafasi kutumia jeni kutokana na mmea usioathirika lakini usioliwa, kuunda aina mpya ya ndizi zinazolika, kulingana na watafiti hao.

Nchini Uganda, ndizi huchangia asilimia 20 ya kalori zote zinazotumika na kila mtu.

Xcm, bakteria sugu inayoharibu mimea ya ndizi, inapatikana katika mataifa ya Burundi, DRC, Rwanda, Tanzania, Uganda na Kenya. Kwa jumla, mataifa haya huzalisha tani milioni 21 za ndizi zenye thamani ya Sh433 bilioni, huku ugonjwa huu sasa ukitishwa kufifisha mavuno.

Katika jitihada zao za kuzalisha aina zisizoathirika na ugonjwa huo, kundi hilo la watafiti lilitumia aina zote za ndizi katika kituo chao cha IITA nchini Uganda, na kuteua aina 13, zenye uwezo wa kustahimili ugonjwa huo, unaofanana na ule wa Musa balbisiana.

Dkt Nakato aliteua seli kutokana na aina Musa acuminata, aina nyingine ya ndizi za msituni ambazo tayari imo katika mpango wa IITA wa kuzalisha ndizi za maeneo ya milimani.

Hatua hizi, alisema, zitakuwa nguzo muhimu katika mchakato wa kuzalisha miche ya ndizi zinazoliwa na zisizoathirika na ugonjwa huo.

“Matokeo ya utafiti huu ni muhimu sana kwa jamii ya kilimo cha ndizi. Kupitia matokeo haya, tutazidisha juhudi zetu za kuzalisha aina za ndizi zinazostahimili makali ya ugonjwa huo,” akasema Profesa Swennen.

Mashirika hayo mawili yanajivunia kutafiti na kuzalisha miche ya ndizi zenye mavuno ya hali ya juu ya matoke kwa jina NARITA, iliyoundwa kwa mseto wa ndizi za milimani za Afrika Mashariki na aina ya Calcutta 4, kutokana na familia ya ndizi za Musa acuminata.

Aina ya NARITA, kulingana na watafiti hao, itapimwa kama ina bakteria za unyaukaji wa mimea na huenda ikatumika kwa mipango ya siku za usoni ya kuboresha mazao ya matoke kwa kuyapa nguvu za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.