Wanafunzi wengi wakosa kuripoti shuleni baada ya daraja la Ngoliba kubomoka

Na LAWRENCE ONGARO

DARAJA lililobomoka eneo la Ngoliba miezi mitatu iliyopita lilisababisha wanafunzi wengi kukosa kurejea shuleni mapema wiki hii.

Daraja hilo huunganisha kaunti za Kiambu na Murang’a.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Ngoliba iliyoko Thika Mashariki, Bi Esther Kamau alithibitisha kuwa wanafunzi wengi walikosa kufika shuleni huku wakihofia kuvuka hadi upande mwingine hapo kwa mashua kwa sababu mto Thika ulikuwa umevunja kingo zake.

“Wazazi wengi wamesema ni hatari kwa watoto kuvuka kwa sababu mto umefurika na kuna viboko hatari wanaopatikana hapo,” alisema Bi Kamau.

Alisema wanafunzi na wakazi wa maeneo hayo hulipa ada ya kati ya Sh50 na 20 kuvushwa kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Chifu wa eneo hilo la Ngoliba Bi Alice Njoki amewashauri wakazi wa pande zote mbili wawe makini sana wanapopitia kwenye daraja hilo.

Alieleza ya kwamba wakazi wa maeneo hayo wanakadiria hasara kubwa kwa sababu kwa miezi hiyo michache biashara zao zimeyumba.

Alisema licha ya wakazi hao kutoa malalamiko yao kuhusu daraja hilo bado hakuna lolote la maana limefanyika.

“Kuna hatari kubwa ya wanafunzi kupitia daraja hilo kwa kutumia mashua kwa sababu mto Thika umefurika kwa sasa kutokana na mvua kubwa inayonyesha,” alisema chifu huyo.

Alieleza ya kwamba iwapo mvua kubwa inayonyesha itaendelea kwa wiki kadhaa, bila shaka biashara na masomo yatakwama kwa muda.

Alitoa wito kwa afisi ya ustawi wa eneobunge la Thika – NG-CDF – kufanya juhudi kuona ya kwamba daraja hilo linajengwa haraka iwezekanavyo.

Wahudumu wa bodaboda wamepata hasara kubwa kwa sababu hawawezi kusafiri hadi ng’ambo ya pili kubeba abiria. Bw George Mutisya anasema biashara ya uchukuzi imeyumba kwa sababu “hatuna kazi ya kufanya kwa wakati huu.”

“Tunataka viongozi wanaohusika na urekebishaji wa daraja hilo wafanye hima kuona ya kwamba kazi inaendeshwa mara moja ili shughuli zirejee kama kawaida,” alifafanua Bw Mutisya.

Chifu ajengewa ofisi mpya Ngoliba

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ngoliba, Thika Mashariki sasa wanaweza kupata huduma za chifu wao katika ofisi mpya.

Kabla ya kujengwa kwa hii mpya, walikuwa wanapata huduma zao kwenye ofisi ya matope kukiwa na changamoto tele.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema kwa zaidi ya miaka 15 hakuna ukarabati wowote uliofanyika katika ofisi hizo za awali.

“Ofisi hiyo imegharimu Sh1.5 milioni na imejengwa kisasa kupitia fedha za mgao wa serikali wa ustawi wa maeneobunge NG-CDF,” alisema Bw Wainaina.

Alisema kutokana na janga la corona linaloendelea kutikisa ulimwengu, machifu mashinani wana jukumu la kuwahamasisha wananchi.

Chifu wa eneo hilo Bi Alice Njoki Kago, alisema ofisi hiyo mpya tayari imeleta mwamko mpya sehemu ya Ngoliba na vitongoji vyake.

“Hapo awali kulikuwa na idadi chache ya watu waliofika ofisini kuleta malalamiko. Lakini tangu ofisi hii mpya ifunguliwe, watu ni wengi wanaofika hapa kuwasilisha malalamishi,” alisema Bi Kago.

Alisema wakati huu wa janga la corona wamechukua jukumu kuona ya kwamba wananchi wanahamasishwa kunawa mikono, kuvalia barakoa, na kujiepusha na mikusanyiko.

Muhimu zaidi aliwashauri wakazi wawe makini na wana wao hasa wakati huu ambapo wako nyumbani kwa likizo ndefu kutokana na janga la maradhi.

Alisema huu pia ni wakati wa wazazi kuwapa watoto wao majukumu mengine muhimu ya kijamii kama kufua nguo, kupika chakula, kuandaa nyumba, na pia kuwahamasisha kuhusu maisha yao ya baadaye.

Alisema wao – machifu – ndio jicho la serikali na watazidi kuchukua jukumu hilo la kuhamasisha wananchi kuhusu corona.

Kampuni ya Wachina ya Sinohydro yawapa chakula wakazi wa Thika Mashariki

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwajali watu wanaohitaji chakula hasa wakati huu taifa na ulimwengu mzima unaposhuhudia janga la Covid-19.

Naibu kamishna wa Thika Mashariki, Bw Thomas Sankei, ametoa wito kwa mashirika yaliyo na uwezo yawajali watu walioathirika na ambao hawana chakula.

Alisema hayo wakati akiipongeza kampuni ya Sinohydro Corporation ambayo ilijitokeza wazi na kuwapa chakula wakazi zaidi ya 300 katika eneo la Kilimambogo ambako kumetundikwa kizuizi kinachowazuia wasafiri kuelekea kaunti za Machakos na Murang’a.

Kamishna wa Thika Mashariki Thomas Sankei akisambaza barakoa kwa wakazi wa eneo la Ngoliba. Picha/ Lawrence Ongaro

Mnamo Jumamosi kampuni hiyo ya Wachina ya kusaga kokoto na mawe, ilitoa chakula ambapo wakazi hao walipokea unga wa ugali, mafuta ya kupikia na hata sabuni ya kuogea.

“Naishukuru sana kampuni hiyo kwa kazi nzuri wameonyesha ya kuwajali wakazi wa Kilimambogo eneo la Ngoliba kwa kuwapa chakula,” alisema Bw Sankei.

Kizuizi kilichowekwa, walisema, kimewazuia wakazi wengi kutembea kwenda maeneo mengine kwa shughuli za kujitafutia chakula.

Baadhi walisema kinachowapa afueni kidogo ni kwamba walibakisha chakula kidogo walichovuna msimu uliopita.

Wakazi hao wametoa mwito kwa wahisani popote walipo wafanye juhudi ili kuwapa chakula haraka iwezekanavyo.

Wakazi wengi katika eneo hilo wanafanya kazi za mashamba na katika kampuni ya uchimbaji mawe iliyoko hapo karibu.

Bw Sankei alisema wakazi hao wanaishi katika maisha ya kipato cha chini na kwa hivyo wanahitaji misaada kwa wingi.

“Mimi kama afisa wa serikali eneo hili natoa mwito kwa wahisani hasa wafanyabiashara wengi walio Thika Magharibi, wajitokeze na kusaidia watu wangu wa upande huu wa Mashariki ambako mara nyingi huwa kukavu,” akasema afisa huyo.

Watu wanne wasombwa na maji eneo la Ngoliba

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya wakazi wanne kusombwa na maji katika mto Athi, eneo la Ngoliba Thika Mashabiki, wakazi wanaiomba Kaunti ya Kiambu usaidizi.

Mnamo Jumatano wakazi wanne wa kijiji cha Ngoliba walisombwa na maji walipokuwa wakivuka Mto Athi wakiwa kwenye boti.

Wakazi wa eneo hilo walisema ya kwamba walikuwa watu sita katika mashua hiyo lakini wawili miongoni mwao walijinusuru na wakaogelea hadi upande wa pili.

Mnamo Jumatano naibu gavana wa Kiambu Bi Joyce Ngugi alizuru kijiji hicho ambapo aliwahakikishia wakazi kuwa kaunti hiyo itajenga daraja la kuvukia upande wa pili.

Chakula kwa wakazi

Alisema serikali ya kaunti inapanga kusambaza chakula kwa wakazi wa eneo hilo.

Bi Ngugi aliwashauri viongozi waache kuingiza siasa katika shughuli hiyo ya kusambaza chakula.

“Sisi kama viongozi tunastahili kuugana na kusaidia wananchi bila kuegemea upande wowote,” alisema Bi Ngugi.

Alisema kaunti ya Kiambu itafanya juhudi kuona ya kwamba kila mwanachi anapata chakula bila kubaguliwa.

Aliwashauri madiwani, machifu na wazee wa vijiji kuketi pamoja na kupanga vizuri jinsi wananchi wanavyostahili kupewa chakula.

Bi Judy Nyaguthii Wang’ombe, alisema mwanaye wa kiume alisombwa na maji alipoungana wa wenzake watano kwenda kuvua samaki.

Hata hivyo, alisema ilidaiwa mawimbi mazito ndiyo yalisababisha sita hao kusombwa na maji.

Licha ya kikosi cha uokozi kufika eneo hilo kwa juhudi za kuokoa watu hao bado walishindwa kuwapata.

Lakini watu wawili pekee ndio walifanikiwa kujinusuru kutoka kwa mto huo ambao unavuma kwa kasi kubwa.

Alisema kwa muda wa siku tatu mfululizo mvua kubwa imenyesha katika eneo hilo.

Bi Wang’ombe alitoa mwito kwa serikali kuwatafutia ajira vijana wengi ambao hawana kazi ya kufanya.

“Kijana yangu alikuwa ana ujuzi wa kurekebisha umeme, lakini hajafanikiwa kupata kazi,” alisema Bi Wang’ ombe.

Wakazi wa kijiji hicho wanaiomba serikali iingilie kati mara moja kuona ya kwamba daraja la kisasa linajengwa ili watu waweze kuvuka kwa urahisi hadi upande wa pili.