Polisi kizimbani kwa kumumunya mamilioni ya NSSF

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wakuu wawili wa polisi akiwamo naibu wa afisa msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Narok (OCS) walishtakiwa Jumatatu kwa kulaghai Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) Sh3.4 milioni.

Bw Milton Odhiambo Barasa, aliye naibu wa OCS na James Thuo Njuguna, wa kitengo cha kupiga picha walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku.

Walikanusha shtaka la kula njama za kumumunya hela za malipo ya uzeeni ya kikosi cha polisi Sh3,482,451 kwa kuidhinisha hati feki za Samuel Kiprotich Bett.

Washtakiwa hao walidaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya 2017 na 2018 katika makao makuu ya polisi jijini Nairobi.

Shtaka la pili lilisema hawakuchukua tahadhari iwapasavyo kuzuia kutoweka kwa pesa hizo..

Washtakiwa waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakifichua wamehudumia kikosi cha polisi kwa zaidi ya miaka 27 kila mmoja na “ wanaendelea kutekeleza majukumu yao.”

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walipigiwa simu kutoka stesheni wanakohudumu kufika katika makao makuu ya uchunguzi (DCI) kuhojiwa.

“Washtakiwa walizuiliwa tangu Ijumaa hadi leo walipofikishwa kortini,” hakimu alielezwa.

“Huduma za washtakiwa zingali zahitajiwa hasa wakati huu wa kupambana na ugonjwa wa Corona na visa vingine vya uhalifu,” Bi Mutuku alielezwa na wakili anayewatetea washtakiwa hao.

Hakimu aliwaamuru washtakiwa hao walipe kila mmoja dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Pia aliwataka wafike kortini tena Julai 20, 2020 kutengewa siku ya kusikizwa kwa kesi inayowakabili.

Karangi atolewa kijasho wanachama wa bodi ya NSSF kukwepa kikao na PIC bungeni

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa Bodi ya wasimamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na Mafao (NSSF) Julius Karangi alikabiliwa na wakati mgumu Jumanne kuelezea ni kwa nini wanachama wa bodi yake walikaidi mwaliko wa kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu uwekezaji (PIC).

Kutofika kwa wanachama wengine saba wa bodi hiyo kulisababisha wanachama wa PIC kuahirisha mkutano wao na Jenerali (Mstaafu) na wenzake na kuwaagiza warejee Jumatatu, Novemba 25, 2019.

Kati ya wanachama 10 wa bodi hiyo, ni wawili pekee, kando na mwenyekiti Jenerali (Mstaafu) Karangi, walioitikia mwaliko wa kufikia mbele ya kamati hiyo kujibu maswali kadhaa kuhusu masuala mbalimbali kuhusiana na usimamizi wa asasi hiyo. Vilevile, alikuwepo kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Bw Anthony Omerikwa.

Wanachama wengine waliofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir ni aliyekuwa mbunge wa Laisamis John Lekuton na Profesa Dulacho Galgalo Barako.

Wale ambao hawakufika mbele ya kamati hiyo ya PIC ni pamoja na Katibu wa Wizara ya Leba Peter Tumm, Damaris Muhika, Marion Mutungi, Mark J. Obuya, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu-K) Francis Atwoli na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE).

“Kwa sababu ni wanachama watatu pekee waliofika, sheria haituruhusu kuendelea na kikao hiki. Kwa hivyo, Bw Mwenyekiti itabidi mrudi na muwashawishi wenzenu kuandamana nanyi Jumatatu, Novemba 25,” akasema Bw Nassir.

Naye mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa alisema kutofika kwa wanachama hao wa bodi kunadhihirisha jinsi ambavyo hawachukulii kwa uzito wajibu wao katika NSSF.

Jeneralai Karangi aliwaambia wabunge hao kwamba ni wanachama wawili pekee wa bodi yake waliompigia simu wakiomba radhi kwamba hawangehudhuria.

“Na Katibu Mkuu Francis Atwoli amesafiri nje ya nchi katika ziara ya kikazi nchini Nigeria,” akasema Jenerali Karangi.

Thuluthi mbili

Kulingana na sheria ya NSSF, angalau thuluthi mbili ya wanachama wa bodi yake ya usimamizi ndiyo wanahitajika katika vikao vyake ili viwe halali. Kwa hivyo, wakati wa mkutano na kamati ya PIC katika majengo ya Bunge Jumanne bodi hiyo ilipasa kuwakilishwa na angalau wanachama saba.

Hii ndiyo sababu iliyofanya wabunge kudinda kuendelea na mkutano na kuwaamuru waondoke na warejee wakiwa idadi hitajika kwa mujibu wa sheria za hazina hiyo.

Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba wanachama wa bodi hiyo walifeli kufika mbele ya wabunge “kimakusudi kwa sababu walijua suala la uteuzi wa Afisa Mkuu Mtendaji lingeibuliwa.”

“Mambo ni magumu katika NSSF kwa sababu wanachama wa bodi wako tu lakini wanakwepa kufika mbele ya kamati,” akasema meneja mmoja wa cheo cha juu ambaye aliomba tusichapishe jina lake.

“Hawatizami NSSF kama taasisi. Haja yao kuu ni kuhakikisha kuwa mtu wanayempendelea ndiye anashikilia wadhifa wa afisa mkuu mtendaji,” akasema.

Kumekuwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wanachama wa bodi hiyo kwa muda wa zaidi ya miaka mitano hali iliyofanya kufeli kuteuliwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kudumu.

Ni kutokana na mvutano ambapo Bw Omerikwa amekuwa akishikilia wadhifa huo kama kaimu kwa zaidi ya miaka mitano tangu mtangulizi wake Richard Langat afutwe kazi kwa tuhuma za ufisadi.

Isitoshe, wengi wa wasimamizi wengine wa hazina hiyo pia wanashikilia nyadhifa zao kama makaimu.

Mapema 2019 shughuli ya mahojiano ya kusaka atakayeshikilia wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji ilifanyika katika hoteli ya Windsor Golf ambapo ilidaiwa kuwa Bw Omerikwa aliibuka bora.

Aghalabu nchini Kenya wengi wana mazoea ya kuita NSSF kuwa ni Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni.

Cotu kusukuma kuteuliwa kwa mkuu wa NSSF

Na MAGDALENE WANJA

MUUNGANO wa kitaifa wa vyama vya wafanyakazi Kenya (COTU-K) umetishia kwenda mahakamani kusukuma kuteuliwa kwa Afisa Mkuu katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na Mafao (NSSF).

Kulingana na katibu wa Cotu Bw Francis Atwoli, juhudi za kumteua msimamizi zimekuwa zikigonga mwamba na kupingwa na baadhi ya watu wenye maslahi binafsi.

Afisa mkuu wa sasa na baadhi ya wakurugenzi wakuu katika shirika hilo wako katika nafasi za ukaimu.

“Haya ni baadhi ya maswala ambayo yanachangia katika kuzembea kwa utendakazi katika shirika hilo. Cotu itaenda mahakamani kusukuma hatua ya kuchaguliwa kwa msimamizi haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Atwoli katika taarifa.

Atwoli alipeana mfano wa hivi punde ambapo bodi ya NSSF ilifanya mkutano ambao ulihudhuriwa na wanachama wa muungano wa Cotu ambapo Bw Anthony Omerikwa aliibuka mshindi katika uteuzi.

Alimlaumu mwenyekiti wa bodi Jenerali (Mstaafu) Dkt Julius Karangi na Waziri wa Leba Ukur Yatani kwa kutotilia maanani suala hilo linalowaathiri mamilioni ya wafanyakazi.

Msimamizi anapoteuliwa, mwenyekiti wa bodi huwasilisha jina lake kwa Waziri wa Leba kwa uchunguzi unaohusu msasa.

Bw Atwoli alisema kuwa licha ya kuandika barua kwa Dkt Karangi kuhusu swala hilo miezi miwili iliyopita, hawajapokea jibu lolote.

“Kutokana na kimya cha wawili hao, Cotu inajiandaa kuelekea mahakamani juma lijalo,” aliongeza.

Nafasi hiyo ya kazi ilichapishwa mnamo Aprili 2019.

Vijana wamekataa kuwekeza kwa hazina ya uzeeni – Ripoti

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya vijana nchini hawawekezi katika hazina za malipo ya uzeeni, ripoti imefichua.

Kulingana na ripoti ya utafiti wa Infotrak idadi ya Wakenya wanaowekeza katika hazina za pensheni za uzeeni imepungua hadi asilimia 10.

Utafiti huo, ulibaini kuwa badala ya kuwekeza katika hazina ya malipo ya uzeeni, baadhi ya Wakenya sasa wameamua wawe wanawekeza katika mali kama vile mashamba na biashara nyinginezo zitakazowawezesha kujipatia hela uzeeni wakati watakapostaafu.

Akizungumza wakati wa kutolewa kwa ripoti ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hazina ya Pensheni ya Kaunti (CPF) Hosea Kili, alisema kuna hatari ya Wakenya wengi kuteseka baada ya kustaafu kutokana na ukosefu wa malipo ya pensheni.

“Idadi kubwa ya vijana wanaofanya kazi hawawekezi katika hazina za malipo ya uzeeni. Hiyo inamaanisha kwamba watapata taabu watakapostaafu kwani hawataweza kujikimu kimaisha,” akasema Bw Kili.

Ripoti hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwa Hazina ya Pensheni ya Serikali za Mitaa (Laptrust) jijini Nairobi.

“Inasikitisha kwamba asilimia 90 ya Wakenya hawawekezi katika hazina zitakazowafaa baada ya kustaafu,” akasema Bw Kili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Infotrak, Angela Ambitho, alisema utafiti huo ulifadhiliwa na CPF na ulifanywa kati ya kaya 1,500 kote nchini.

Bi Ambitho alisema kuwa kupungua kwa idadi ya watu wanaowekeza katika hazina za malipo ya uzeeni ni ishara kwamba vijana wanahitji elimu kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baada ya kustaafu.

Hazina ya ilianzishwa mnamo 1929 kwa ajili ya kuwalipa pensheni wafanyakazi waliohudumu katika serikali ya mkoloni.

Jumla ya wafanyakazi 20,074 wa serikali ya kitaifa na kaunti zote 47 wanawekeza katika hazina ya Laptrust na watu 7,098 wanapokea malipo ya uzeeni.

Waliostaafu kuhesabiwa tena kuondoa wale bandia

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali inatarajiwa kuhesabu watu waliostaafu kutoka huduma ya umma kwa lengo la kuondoa maelfu ya wastaafu bandia ambao wanadhaniwa kupora serikali mamilioni ya fedha kila mwezi.

Kulingana na Hazina ya Kitaifa, wafanyikazi wa serikali waliostaafu 300,000 watatarajiwa kujiwasilisha katika vituo vya Huduma.

Serikali imechukua hatua hiyo kwa lengo la kudhibiti kiwango kikubwa cha pesa zinazotumiwa na serikali kila mwezi.

Pesa zinazolipwa waliostaafu zinatarajiwa kuzidi Sh100 bilioni mwaka ujao.  Idara ya Pensheni inakisia kulipa pensheni jamaa wa walioaga dunia, hali ambayo imekuzwa na mfumo wa kupata fedha za pensheni kielektroniki.

Shughuli hiyo itaanza Februari 11 ambapo waliostaafu watakuwa na mwezi mmoja kujiwasilisha vituoni humo wakiwa wamebeba vitambulisho na stakabadhi ya benki katika Kituo cha Huduma kilichoko karibu.

Hazina ya Fedha inalenga kusimamisha kuweka pesa za pensheni moja kwa moja katika akaunti za wastaafu ambao hawatafika kutambulishwa.

“Watakaokataa kufika watadhaniwa kuaga dunia na malipo kwa akaunti zao za benki yatasimamishwa,” alisema afisa wa KRA anayeelewa kuhusiana na suala hilo.

Kinara wa NSSF taabani kujitaja mmiliki wa shamba la ekari 134

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA meneja mkuu hazina ya malipo ya uzeeni (NSSF) Josphert Konzolo alijipata taabani kwa kudai ndiye mmiliki wa shamba la ekari 134 lenye thamani ya Sh8bilioni.

Bw Konzolo aliyemweleza Jaji Elijah Obaga kuwa aliinunua shamba hilo kwa bei ya Sh96milioni alijikuta katika hali ya suinto fahamu.

Bw Konzolo alisema aliuziwa shamba hilo na Bw John Mugo Kamau kati ya 1998 na 2011.

“Nilinunua shamba hili kutoka kwa muwekezaji Bw Kamau kwa bei ya Sh96milioni kisha akanipa hati ya umiliki, “ Bw Konzolo alisema

Aliongeza alisaidiwa na mkewe marehemu Noel kulipia pesa hizo kupitia kwa kampuni ya mawakili ya Bw Macmillan Mutinda Mutiso.

Bw Konzolo alisema baada ya kununua shamba hilo liliandikishwa kwa jina la kampuni yao Telesource .Com Limited

Kinara huyo wa zamani wa NSSF alihojiwa kwa undani zaidi jinsi alivyonunua shamba  hilo na wakili Cecil Miller anayewakilisha kampuni ya Muchanga Investments Limited ambayo wamiliki wake ni mfanyabiashara mwendazake  Horatius Da Gama Rose na aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori.

Wakili Cecil Miller akimhoji Konzolo. Picha/ Richard Munguti

“Ulikuwa kinara wa NSSF?” Bw Miller alimwuliza Konzolo

“ Ndio,” alijibu

“Hebu mweleze Jaji Obaga ikiwa ulishtakiwa kwa ufisadi ukiwa kinara wa NSSF,”  Bw Miller akasema.

“Ndio nilishtakiwa,” alijibu Konzolo na kumataka Bw Miller aeleze jinsi kesi ilivyokamilishwa.

“Hebu eleza korti kama nilifungwa ama kuachiliwa,” Konzolo akasema.

“Je ulishtakiwa kwa wizi wa Sh100 milioni kutoka kwa benki ya Barclays?” Miller akamuuliza.

“Ndio nilishtakiwa na nikaachiliwa. Kesi ilitokana na fitina tu za kikazi,”alijibu.

“Kisha nataka uieleza hii mahakama kwamba wewe na wakili wako Mutinda Mutiso mlishtakiwa kwa ulaghai wa shamba hilo pamoja na aliyekuwa waziri wa ardhi Charity Ngilu, “ Bw Miller alimwuliza tena.

Mlalamishiu huyo kwa gadhabu alimwuliza jaji amtetee kwa vile maswali anayoulizwa na Miller yanalenga kumharibia sifa

“Jibu maswali jinsi unavyoulizwa,” Jaji Obaga alimwamuru.

“Ndio nilishtakiwa pamoja na Bi Ngilu ambaye sasa ni Gavana wa kaunti ya Kitui,” akasema Konzolo

“Je unajua mliachiliwa na mahakama ya rufaa kwa vile tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC haikuwa na makamishna wa kutosha na sasa wapo na mnaweza kufunguliwa mashtaka tena,”alisema Bw Miller

Bw Konzolo alijibu na kusema maswali hayo yanalenga kushusja hadi yake katika jamii na kumfanya aonekane kama mtu mfisadi.

Bw Miller aliambia Mahakam kuwa ushahidi ulio na EACC na Mwanasheria mkuu unaonyesha kuwa nakala ya ufisadi aliyonayo Konzolo imepatikana kwa njia ya ufisadi. Kesi inaendelea

 

 

 

 

 

Waziri kujibu mashtaka kwa kumwondoa Atwoli NSSF

Na BERNARDINE MUTANU

Waziri wa Leba Ukur Yatani ana hadi Jumatano kujibu mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani na COTU kuhusiana na hatua yake ya kutomteua tena Francis Atwoli katika bodi ya Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Washtakiwa walitakuwa na Jaji Onesmus Makau Jumatatu kuwasilisha majibu kabla ya kusikizwa kwa kesi hiyo Jumatano.

Chama hicho cha wafanyikazi kinataka mahakama kusimamisha bodi ya NSSF kufanya mikutano yoyote kabla ya kuchapishwa jina la Atwoli katika gazeti rasmi la serikali.

COTU ilienda mahakamani wiki jana kwa kusema kukataa kuteuliwa kwa Atwoli ni kinyume cha Sheria ya NSSF, 2013.

Kulingana na COTU, ikiwa NSSF itafanya mkutano wowote, lazima wafanyikazi na waajiri wao wawakilishwe.

Kupitia kwa wakili wake Okweh Aichiando, COTU ilisema mkutano wowote wa NSSF bila COTU ni kinyume cha matakwa ya wafanyikazi, wachangiaji wakubwa zaidi wa hazina hiyo.

COTU yapinga uteuzi wa Karangi kusimamia NSSF

Na Wanderi Kamau

MUUNGANO wa Kitaifa wa Wafanyakazi (COTU) umepinga uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Mstaafu Julius Karangi kama mwenyekiti wa bodi ya Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Bw Karangi aliteuliwa wiki iliyopita na Waziri wa Leba Ukur Yattani kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, kuchukua nafasi ya Gideon Ndambuki baada ya kipindi chake kumalizika mnamo Februari.

Uteuzi wake tayari ushachapishwa katika gazeti rasmi la serikali, toleo la wiki iliyopita, huku ukitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Lakini Jumanne, COTU ilikosoa uteuzi huo, ikiutaja kuwa njama za serikali kuwaondoa Katibu wake Mkuu Francis Atwoli na Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waajiri Kenya (FKE) kama wanachama wa bodi ya hazina hiyo.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Naibu Katibu Mkuu wa Kwanza wa muungano huo, Earnest Nadome alisema kwamba wana habari kwamba kuna njama za kuwaondoa wawili hao “ili kuwanyang’anya udhibiti wa bodi hiyo.”

“Tuna habari kwamba lengo kuu la uteuzi wa Bw Karangi kama mwenyekiti wa hazina hii ni kuanza mchakato wa kutupokonya udhibiti wa uongozi wa hazina hii, licha ya Bw Atwoli na Bi Mugo kuwakilisha matakwa ya wafanyakazi kote nchini,” akasema Bw Nadome.

Mbali na hayo, Bw Nadome alisema kuwa watatumia njia zote kuhakikisha wawili hao wanabaki, kwani kuondolewa kwao ni sawa na “kuwanyamazisha wafanyakazi.”

“Hatuwezi kuketi kitako wakati serikali inapanga njama za kutunyamazisha kimakusudi,” akasema.

Uteuzi wa Bw Karangi unajiri huku hazina ikiandamwa na msururu wa sakata za rushwa zinazojumuisha kupotea kwa mabilioni ya fedha.

Mojawapo ya sakata hizo ni ununuzi tata wa hisa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) mnamo 2016, ambapo inahofiwa kwamba ilipoteza hadi Sh1.6 bilioni katika hali tatanishi.

Aidha, NSSF inadaiwa kutumia kampuni ya Discount Securities Limited (DSL) kununa hisa hizo, ila taratibu zilizofuatwa hazikuwa wazi.

Hilo lilipelekea baadhi ya maafisa wake wakuu kufunguliwa mashtaka, ila wamepinga madai hayo.

Hazina hiyo pia inakumbwa na mradi tata wa ujenzi wa Tassia, ambapo inadaiwa kwamba ilipoteza hadi Sh5 bilioni.

Hata hivyo, hazina imejitetea, ikidai kwamba kila taratibu zilifuatwa katika uendeshaji wa mradi huo.

Leba Dei ya malumbano kati ya COTU, NHIF na NSSF

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanaadhimisha siku ya wafanyakazi ulimwenguni Jumanne huku vyama vya wafanyakazi na serikali vikizozana kuhusu mabadiliko ya sheria yanayolenga kuondoa wawakilishi wao katika mashirika mawili yanayohifadhi mabilioni ya pesa zao.

Maafisa wa vyama vya wafanyakazi nchini wanapinga mabadiliko ya sheria yanayolenga kuondoa wawakilishi wa wafanyakazi katika bodi za Shirika la Taifa la Malipo ya Uzeeni (NSSF) na Shirika la Bima la Taifa la Afya (NHIF).

Wafanyakazi huchanga mabilioni ya pesa katika mashirika haya na muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu) huwakilisha maslahi yao katika bodi za kuyasimamia.

Hata hivyo, Wizara ya Leba inapendekeza sheria ibadilishwe ili wawakilishi wa wafanyakazi waondolewe katika bodi hizo. Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli na Katibu Mkuu wa chama cha walimu nchini Wilson Sossion wamepinga mapendekezo hayo wakisema mabadiliko hayo siyo ya kikatiba.

“Tuko tayari kupinga mabadiliko yaliyopendekezwa kortini kwa sababu yote yanaonekana kulenga haki za kikatiba za wafanyakazi. Baadhi ya watu wanataka kutumia sheria kunyima Wakenya haki zao za kikatiba,” alieleza Bw Sossion.

Miongoni mwa mabadiliko yanayopendekezwa ni wafanyakazi wanaonuia kugoma kutoa notisi ya siku 21 badala ya saba ilivyo kwa wakati huu.

Yakipitishwa na bunge, wafanyakazi hawatakuwa wakipeleka mizozo mahakamani moja kwa moja kabla ya kujaribu mbinu tofauti za upatanishi. Kulingana na waziri wa Leba Ukur Yattani, pendekezo hili linalenga kutatua mizozo ya wafanyakazi kabla ya kufika kortini na kulemaza huduma.

Vyama vya wafanyakazi vinahisi kwamba serikali inataka kuwa na idadi kubwa ya wawakilishi katika bodi ya NSSF ili kuwa na usemi mkubwa kuhusu pesa za wafanyakazi. “NSSF ni shirika la wafanyakazi na hawawezi kunyimwa nafasi ya kuwa na usemi kuhusu mali yao,” asema Bw Atwoli.

Lakini Bw Yattani anatofautiana nao akisema wameshindwa kuhakikisha shirika hilo linasimamiwa vyema.

“Kuna mipango duni ya uwekezaji katika NSS, usimamizi mbaya na ufisadi wa hali ya juu. Dhana kwamba washikadau ndio wasimamizi bora ni la kupotosha lau sivyo, NSSF lingekuwa limesimamiwa vyema kwa sababu Cotu na Shirikisho la Waajiri (FKE) zimewakilishwa,” alisema waziri Yattani.

 

COTU na FKE zatisha kujiondoa NSSF

Na BERNARDINE MUTANU

MUUNGANO wa Vyama vya Wafanyikazi (COTU-K) na lile la waajiri (FKE) limetishia kujiondoa katika Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Hii ni baada ya kugundua kuwa baadhi ya maafisa wa NSSF walikuwa wakilenga kubadilisha Sheria ya NSSF 2013, hata kabla ya utekelezaji wake kuanza.

Kulingana na taarifa iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli, mashirika hayo mawili, ambayo ni washirika wakuu wa NSSF hayajahusishwa katika mpango huo.

“COTU-K inapinga mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya NSSF 2013. Ni kinyume cha Katiba kufanyia marekebisho sheria ya NSSF bila kuhusisha COTU na Shirikisho la Waajiri (FKE),” ikasema taarifa hiyo.

Kulingana na Bw Atwoli, pesa zilizoko NSSF zimetoka kwa wafanyikazi na waajiri wao, na haiwezi kuwa wahusika wanaweza kuunda sheria bila kushirikisha COTU na FKE.

“Mpango huo ni kumaanisha kuwa wafanyikazi na waajiri hawana maana. Ikiwa wanachanga au la haijalishi kwa sababu kuna mtu anayefanya uamuzi kuhusiana na matumizi ya hazina hiyo bila idhini ya wafanyikazi na waajiri,” alisema Bw Atwoli.

Kulingana naye, haelewi ni vipi marekebishoo hayo kufanywa licha ya kuwa sheria hiyo haijaanza kutekelezwa.

“Bado sheria hiyo imo mahakamani kwa sababu ya maazimio ya watu wachache wanaotaka kuirekebisha tena,” alisema katika taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari.

COTU inataka kushauriwa kabla ya marekebisho yoyote kufanyiwa sheria hiyo la sivyo pamoja na FKE iunde mradi wa pensheni wa pamoja ambao utasimamiwa na vyama hivyo.