• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Polio: Wazazi wahimizwa kuwapeleka watoto wao kwa chanjo

Polio: Wazazi wahimizwa kuwapeleka watoto wao kwa chanjo

Na KENYA NEWS AGENCY

WAZAZI wameombwa wapeleke watoto wao kwa awamu ya pili ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio.

Zoezi hilo, linalonalenga zaidi ya watoto 3.4 milioni walio chini ya miaka mitano, lilizinduliwa awamu ya kwanza katika kaunti 13.Awamu ya pili ilianza Jumamosi iliyopita na itaendelea hadi kesho kutwa Jumatano.

Kaunti zinazoshiriki ni Kajiado, Garissa, Wajir, Mandera, Isiolo, Mombasa, Kilifi, Kitui, Machakos, Kiambu, Tana River, Lamu na Nairobi.Akizungumza baada ya kuzindua zoezi hilo Kajiado, Afisa Msimamizi wa Huduma za Matibabu, Bw Jacob Sampeke, alisema chanjo hiyo inatolewa baada ya visa sita vya virusi vya polio kuthibitishwa katika kaunti za Garissa na Mombasa.

Bw Sampeke alieleza kuwa polio ni hatari sana na huleta ulemavu wa kudumu, hivyo hakuna mtoto anayefaa kutiwa hatarini kwa kukosa kuchanjwa. “Polio ni ugonjwa mbaya sana unaosababisha sehemu za mwili kupooza.

Kaunti 13 ziko katika hatari zaidi na ndizo zinalengwa. Naomba wazazi wote kutoa watoto wao wachanjwe,” alisema.Aliyekuwa Seneta Maalum Harold Kipchumba, ambaye ni balozi wa kampeni ya hamasisho kuhusu polio, alisema kuna baadhi ya makundi ya kidini ambayo ilikuwa vigumu kufikia wakati wa awamu ya kwanza.

Aliyahimiza kuweka kipaumbele afya ya watoto wao kwa kuwapeleka kwa chanjo kwenye awamu hii ya pili.Bw Kipchumba alitaja madhehebu kama vile Kabonokia ambayo yamewapa maafisa wa afya wakati mgumu kwa kukataa watoto wao kupewa chanjo.

Alisisitiza kuwa ni haki ya kila mtoto kupata chanjo, na wanaoficha watoto watakamatwa na kushtakiwa.

  • Tags

You can share this post!

Walimu hawana budi kusubiri miaka 2 bila nyongeza

Kocha aliyechagua kufunza uwanjani badala ya darasani