• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
PSG, Bayern na Juve zatamba Barca ikizidi kusuasua ligini

PSG, Bayern na Juve zatamba Barca ikizidi kusuasua ligini

Na MASHIRIKA

NEYMAR Jr alipachika wavuni mabao mawili na kusaidia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kufungua mwanya wa alama 10 kileleni mwa jedwali baada ya kupepeta Bordeaux 3-2 katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumamosi usiku ugani Matmut Atlantique.

Bao jingine la PSG lilijazwa kimiani na mshambuliaji chipukizi raia wa Ufaransa, Kylian Mbappe. Bordeaux walipata mabao yao kupitia Alberth Elis na M’Baye Niang.Ushindi huo wa PSG wanaonolewa na kocha Mauricio Pochettino uliwadumisha kileleni mwa jedwali kwa alama 34 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na Lens walioponda limbukeni Troyes 4-0.

PSG wamepoteza mechi moja, kuambulia sare mara moja na kushinda michuano 11 kati ya 13 iliyopita ligini. Matokeo hayo yanawaweka pazuri zaidi kurejesha kabatini kombe ambalo Lille waliwapokonya mnamo 2020-21.

Katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Barcelona walitupa uongozi wa mabao matatu kwa nunge dhidi ya Celta Vigo ugani Balaidos na kulazimishiwa sare ya 3-3. Mechi hiyo ilikuwa ya mwisho kwa kocha mshikilizi Sergi Barjuan kusimamia kambini mwa Barcelona.

Chini ya rais Joan Laporta, Barcelona watamtambulisha rasmi mkufunzi mpya Xavi Hernandez kwa mashabiki, usimamizi na wachezaji wao ugani Camp Nou hii leo. Wakicheza dhidi ya Celta, mabao ya mabingwa hao mara 26 wa La Liga yalifumwa wavuni kupitia Ansu Fati, Sergio Busquets na Memphis Depay huku wenyeji wakipata yao kupitia Nolito Duran na Iago Aspas aliyetikisa nyavu mara mbili.

Mambo yalizidi kuwa shwari kwa Bayern Munich katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya mabingwa hao mara 30 kukung’uta SC Freiburg 2-1 uwanjani Allianz Arena. Masogora hao wa kocha Julian Nagelsmann sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa pointi 28, nne kuliko nambari mbili Borussia Dortmund.

Nchini Italia, Juventus walirejea ndani ya orodha ya 10-bora kwenye msimamo wa jedwali la Serie A baada ya Juan Cuadrado kuwafungia bao la pekee na la ushindi dhidi ya Fiorentina.Masogora hao wa kocha Massimiliano Allegri sasa wamejizolea alama 18 kutokana na mechi 12 zilizopita ambazo zimewashuhudia wakishinda mara tano, kuambulia sare mara tatu na kupoteza mechi nne.

You can share this post!

Majagina wamtaka Mwendwa agure FKF

Kiunjuri avuna wawaniaji 20 wakiingia TSP

T L