• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
STARS HOI: Senegal yaipiga Kenya magoli 3-0

STARS HOI: Senegal yaipiga Kenya magoli 3-0

Na MASHIRIKA

CAIRO, MISRI

SADIO Mane alifunga mabao mawili muhimu katika ushindi wa 3-0 katika mechi baina ya Senegal na Kenya mnamo Jumatatu usiku katika kabiliano la mwisho la Kundi C kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Misri.

Matokeo hayo yaliiacha Kenya kutegemea matokeo ya Kundi E na F ambapo iliomba Benin na Angola kushindwa na Tunisia na Mali mtawalia kwenye mechi za Jumanne usiku ndipo ifuzu. Mali iliipiga Angola 1-0 kupitia bao lakeĀ Amadou Haidara katika dakika ya 37, huku nayo Tunisia na Mauritania zikitoka sare tasa.

Fowadi huyo wa Liverpool, 27, alishuhudia mkwaju wake wa kwanza wa penalti katika kipindi cha kwanza ukinyakwa na kipa Patrick Matasi wa Harambee Stars ya Kenya.

Baada ya kuambulia sare tasa kufikia mwisho wa dakika 45 za kwanza, Senegal walirejelea kampeni za kipindi cha pili kwa matao ya juu huku wakiwekwa kifua mbele na Ismaila Sarr wa Rennes, Ufaransa kunako dakika ya 63. Mane alikiyumbisha kabisa chombo cha Kenya katika dakika ya 71, muda mfupi kabla ya kufunga penalti ya pili.

Goli la tatu la Senegal lilitokana na makosa ya beki Philemon Otieno wa Gor Mahia ambaye alimchezea Sarr visivyo ndani ya kisanduku. Mbali na Senegal kuzawidiwa penalti, Otieno alionyeshwa kadi ya pili ya manjano na hivyo kuweka Kenya katika ulazima wa kusalia na wachezaji 10 pekee uwanjani hadi mwishoni mwa mechi hiyo.

Senegal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Uganda katika mechi ya hatua ya 16-bora itakayosakatwa mnamo Julai 5.

Uganda walifuzu kwa awamu ya mwondoano baada ya kumaliza kampeni zao za Kundi A katika nafasi ya pili kwa alama nne, tano zaidi nyuma ya wenyeji Misri ambao walijivunia ushindi katika michuano yao yote mitatu.

Matokeo ya mechi zote nne zilizopigwa mnamo Jumatatu yaliwapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uhakika wa kusonga mbele zaidi katika fainali za AFCON mwaka huu kutokana na wingi wa mabao yao.

DR Congo walifunga kampeni zao za Kundi A katika nafasi ya tatu kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Zimbabwe ambao walisajili sare ya 1-1 katika mchuano wao wa pili dhidi ya Uganda mnamo Juni 26.

Vikosi vitakavyokamilisha kampeni zao za makundi katika nafasi mbili za kwanza kileleni vitafuzu kwa hatua ya 16-bora. Vikosi vingine vinne vitakuwa vile vitakavyosajili matokeo bora zaidi yatakayoviweka katika nafasi za tatu makundini.

Kenya, Guinea na Afrika Kusini zilikuwa miongoni mwa timu nne zilizokuwa zikisubiri sana matokeo ya hapo jana ya mechi za Kundi E na F ili kufahamu mustakabali wao kwenye fainali za mwaka huu.

Benin walivaana Jumanne na Cameroon huku Guinea-Bissau wakipimana ubabe na Ghana katika mechi za Kundi E. Kwa upande wa Kundi F, Angola walichuana na Mali huku Mauritania wakimenyana na mabingwa wa 2004, Tunisia.

Makali yafifia

Licha ya kutawala mchezo kwa dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza, makali ya Kenya yalizimwa ghafla katika kipindi cha pili, tukio ambalo kocha Sebastien Migne alikiri kwamba lilichangiwa na kutomakinika kwa baadhi ya masogora wake.

Licha ya kuwa kikosi kinachoorodheshwa na FIFA katika nafasi ya kwanza barani Afrika, Senegal ambao wanapigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa AFCON mwaka huu, watalazimika kuimarisha zaidi mchezo wao katika mechi zao zijazo.

Uwepo wa nyota Idrissa Gueye wa Everton katika safu ya kati ya Senegal uliwawezesha kuzima mashambulizi yote ya Kenya ambao walikosa kumwajibisha kabisa kipa wa Senegal.

Kwingineko, Algeria waliwapepeta Tanzania 3-0 katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi C. Chini ya unahodha wa kiungo Riyad Mahrez wa Manchester City, Algeria walikifanyia kikosi chao kilichokutana na Tanzania mabadiliko 11 kutoka kwa kile kilichowanyoa Senegal 1-0 mnamo Juni 27.

Algeria kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi kwa alama tisa, tatu zaidi ya Senegal. Kenya wanajivunia alama tatu huku Tanzania wakikokota nanga mkiani baada ya kupoteza michuano yao yote mitatu. Kikosi hicho kilikuwa kikishiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Benki: Kelele za mlango katu haziniasi...

Migne aahidi kuisuka upya Harambee Stars

adminleo