• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Sudi adai yeye ndiye ‘mpishi’ katika serikali ya Ruto

Sudi adai yeye ndiye ‘mpishi’ katika serikali ya Ruto

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kapseret, Oscar Sudi amepigia upatu uhusiano wake wa karibu na Rais William Ruto akisema yeye ni mmoja wa viongozi wanaoaminika kwenye duara la kiongozi wa nchi.

Bw Sudi, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, kwenye video amenukuliwa akidai kwamba yeye ni “mkarabati wa mambo katika Ikulu”.

Akijitaja kama mtu wa jikoni, mbunge huyo wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) amesema anaelewa mambo yanavyoendeshwa katika serikali ya Kenya Kwanza.

Video hiyo, Sudi anaskika akihutubia wakazi katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo hata ingawa kwa utani, alionekana kukerwa na mmoja wa madiwani (MCA) aliyelalamikia anachochea wananchi kuhusu ujenzi wa soko.

“Muwache kuchochea wananchi kuhusu hii soko…Kwani wewe ndiye ulitangaza mambo ya soko. Soko inakuja, tumeweka bajeti,” mbunge huyo akasema.

Akaendelea kueleza, “Njia bora kama kiongozi ni kuenda katika ofisi ya gavana umuulize kuihusu, au hata ungeniuliza (akimaanisha yeye mwenyewe – Oscar Sudi)…Hukuniuliza hata swali moja, na unajua mimi ni mkarabati na mimi ni mtu wa jikoni wa usiku Ikulu. Mimi ndo najua mambo yote vile yanaenda”.

Kulingana na mazungumzo yake, soko lililotajwa kwamba linapaswa kujengwa lilikuwa ahadi ya Rais Ruto.

Aidha, Bw Sudi alisuta MCA huyo akisema lengo lake lilikuwa kujipendekeza kwa umma.

Mbunge huyo mcheshi wa Kapseret alionya viongozi wa kisiasa Kaunti ya Uasin Gishu dhidi ya kuchochea uhasama baina ya umma.

“Unakuja kujitetea hapa ati ndio raia wakupigie makofi? Muwe viongozi waadilifu kwa kuja tuzungumze. Mchakato wa siasa za kitambo kuchochea watu wapigane, sitaukubali kaunti hii,” Bw Sudi alitangaza, akitoa onyo kwa wanasiasa.

  • Tags

You can share this post!

Del Monte yamulikwa walinzi wake wakihusishwa na mauaji ya...

Krimasi: Washukiwa 34 wa uhalifu wakamatwa Starehe

T L