• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Suleiman Shahbal aahidi kuwatatulia wafanyabiashara kero katika bustani ya Mama Ngina

Suleiman Shahbal aahidi kuwatatulia wafanyabiashara kero katika bustani ya Mama Ngina

Na FARHIYA HUSSEIN

WAFANYABIASHARA waliozuiwa kuendesha biashara zao katika bustani ya Mama Ngina sasa wana matumaini baada ya mfanyabiahara na rafiki wa karibu wa Gavana wa Mombasa, Bw Suleiman Shahbal kuwaahidi kutatua suala hilo.

Wakizungumza katika mkutano na Bw Shahbal, wafanyabishara hao walifunguka na kuelezea mahangaiko wanayokumbana nayo.

“Tuko zaidi ya wafanyabiashara 350 hapa, lakini kila siku tunakosa riziki yetu kisa na sababu tumefungiwa nje ya mahali tulikuwa tukiendeleza biashara zetu. Tunaumia sana na tumejaribu kutoa wito mara kadhaa lakini hakuna anayetujali wala kutupa majibu,” akasema msimamizi wao Bw Salim Bawazir.

Bustani hiyo ya Mama Ngina ilifungwa mwezi wa Mei, pamoja na sehemu nyingine za nchi kutokana na juhudi za kupunguza kusambaa kwa Covid-19.

“Tunaona sehemu nyingine zishafunguliwa na wanaendeleza biashara zao. Lakini sisi tunashangaa mbona hapa mpaka sasa kumefungwa,” akalalamika.

Wafanyabiashara hao hujishughulisha na uuzaji wa vyakula, bidhaa na nguo za utamaduni.

“Watoto wamerudi nyumbani kwa likizo ndogo. Hatujui na hali hii ngumu tutawalisha vipi. Wakirudi shule watataka karo za shule. Tunaomba kama wananchi wa Kenya tuangaliwe na turuhusiwe kuendeleza biashara zetu,” akasema mfanyabiashara mwingine Asha Chengo.

Wafanyabiashara 350 walikuwa wamechaguliwa hapo awali kuwa ndio watakaoruhusiwa kuendeleza biashara zao katika bustani hiyo.

Aidha, Bw Shahbal amewaahidi wafanyabiashara hao kuzungumza na gavana Ali Joho na Waziri wa Utalii Najib Balala ili kusuluhisha mahangaiko yao.

“Nimesikitika kusikia haya ya leo. Nitaomba muda wa wiki moja na nitarudi na majibu. Nyinyi kama Wakenya mna uhuru wa kufanya biashara zenu,” akasema Bw Shahabal.

You can share this post!

Uhuru akaa ngumu majaji wakilia

Bayern Munich warefusha mkataba wa fowadi Maxim...