Watu 500 wameuawa katika mashambulio nchini Syria – UN

Na AFP

UMOJA WA MATAIFA

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema kwamba watu 500 wakiwemo watoto 120, wameuawa katika muda wa wiki moja katika mashambulio ya ndege mashariki ya Ghouta nchini Syria na kutaja hali hiyo kama jehanamu ulimwenguni.

Bw Guterres alisema hayo wakati ambao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiungwa na Urusi, lilipitisha kwa kauli moja amri ya kusitishwa kwa vita nchini Syria kwa siku 30 kuruhusu misaada ya kibinadamu na dawa kufikia waathiriwa.

Azimio la kusitisha mapigano hayo mara moja lilipitishwa wakati wanajeshi wa serikali ya Syria walipokuwa wakiendelea kuponda ngome za waasi eneo la Mashariki ya Ghouta, ambapo mamia ya watu wameuawa katika mashambulio ya wiki moja.

“Tumechelewa kukabiliana na mzozo huu, tumechelewa sana,” Balozi wa Amerika aliambia baraza baada ya kura na kulaumu Urusi kwa kuwa kikwazo kwa kura hiyo.

Azimio hilo linataka kusitishwa kwa vita mara moja kote Syria ili kuruhusu misaada kuwafikia wagonjwa na waliojeruhiwa bila kutatizwa.
Ili Urusi iweze kuunga mkono azimio hilo, ilibidi lugha iliyotumiwa ibadilishwe kufafanua kuwa lingetekelezwa bila kuchelewa badala ya kuwa lingeanza kutekelezwa saa 72 baada ya kupitishwa.

Mabalozi walisema walikuwa na hakika kwamba hatua hii isingefungua milango ya kuahirisha kusitishwa kwa vita, kwa sababu wanachama wa baraza walikuwa wameweka wazi kwenye majadiliano kwamba amri ingetekelezwa haraka.

Mabalozi hao walisema kwamba Guterres ataarifu baraza kuhusu hali ya utekelezaji wa azimio hilo katika muda wa siku 15.

Inasemekana Russia ilikubali kuunga azimio hilo baada ya kuthibitishiwa kuwa halitaathiri mashambulio dhidi ya kundi la kigaidi la Islamic State au Al-Qaeda, pamoja na watu, makundi na mashirika yanayohusishwa na vitendo vya kigaidi.

Hatua hii itaruhusu serikali ya Syria kuendelea kushambulia magaidi wanaoshirikiana na Al-Qaeda eneo la Idlib, mkoa wa mwisho unaodhibitiwa na magaidi nchini Syria.

Kulingana na azimio hilo, mashambulio yatakomeshwa maeneo ya Ghouta Mashariki, Yarmouk, Foua na Kefraya.

Ufaransa yaahidi kusaidia Iraq kujijenga upya

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian. Picha/ Hisani

Na MASHIRIKA

WAZIRI wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian Jumatatu aliizuru Iraq ili kuangazia mikakati ya ujenzi mpya wa taifa hilo baada ya kukumbwa na mapigano kwa muda mrefu.

Hayo yanajiri baada ya serikali ya Iraq kutangaza kulishinda kundi la kigaidi la Islamic State (IS) ambalo limekuwa likiisumbua katika sehemu mbalimbali nchini humo.

“Nimekuja ili kueleza kujitolea kwa Ufaransa katika juhudi safari ya kuijenga mpya (Iraq). Daima tutakuwa pamoja nanyi. Tumekuwa hapa katika harakati za kuleta amani, na tukakuwepo mnapoanza kurejesha uthabiti wa nchi,” akasema Bw Le Drian.

Ufaransa ilikuwa mojawapo ya nchi ambazo zilishirikiana na Iraq kwenye operesheni yake dhidi ya kundi la IS, baada ya kundi hilo kuteka maeneo mengi ya mpaka kati yake na Syria mnamo 2014.

Kwa sasa, Iraq inatafuta wahisani kuisaidia kuijenga upya, kutokana na uharibifu mkubwa ambao ulisababishwa na mapigano hayo.

Aidha, mikakati hiyo ni pamoja na maandalizi ya kongamano la kuchanga fedha katika nchi jirani ya Kuwait, ambalo lilianza Jumatatu.

 

Israeli yashambulia kambi za jeshi la Iran na Syria ikidai waliichokoza

Wanajeshi wa Israeli kaskazini mwa taifa hilo eneo la Alonei Abba, Februari 11, 2018 wakikagua mabaki ya ndege waliyodungua. Picha/AFP

Na AFP

JERUSALEM, ISRAELI

ISRAELI Jumamosi ilishambulia vituo vya Iran nchini Syria baada ya ndege yake ya kivita kuangushwa na jeshi la angani la Syria. 

Kutokana na makabiliano kati ya mahasimu wa jadi Israeli na Iran tangu vita vianze Syria 2011, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliapa kuzuia Iran kuzua msukosuko wa kijeshi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mashambulio ya Israeli yalijiri baada ya kunasa ilichotaja kama ndege ya Iran isiyoendeshwa na rubani ikielekea Syria na kusema lilikuwa shambulio.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Israeli kutangaza hadharani kulenga inachotambua kama vituo vya Iran nchini Syria tangu mzozo huo ulipoanza.

Iran ilitaja madai ya Israeli kama uongo na kusema Syria ina haki ya kujilinda ikishambuliwa.

Aidha, Iran pamoja na mataifa mengine inayoshirikiana nayo nchini Syria – Urusi na kundi la Hezbollah lenye makao Lebanon-walikanusha madai ya Israeli kuhusu kunaswa kwa ndege.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Urusi ilitaka pande zote kuwa na uvumilivu na kusema haikubaliki kuzua vitisho kwa maisha na usalama wa wanajeshi wa Urusi walio Syria.

Msemaji wa jeshi la Israeli, Jonathan Conricus, alionya Syria na Iran kwamba zinacheza na moto, lakini akasisitiza kuwa nchi yake haitaki kuzidisha vita.

“Huu ndio ukiukaji wa hali ya juu wa utukufu wa Israeli kutendwa na Iran katika miaka ya hivi karibuni,” Conricus aliambia wanahabari.

Israeli ilisema ilitekeleza mashambulio makubwa dhidi ya vituo vya jeshi la angani la Syria na vituo vya kijeshi vya Iran.

Wanajeshi wawili wa ndege ya kivita aina ya F16 iliyoangushwa walikuwa hai ingawa mmoja wao alipata majeraha mabaya, jeshi lilisema. Walitua Israeli na kupelekwa hospitalini.

Israeli ilisema makabiliano yalianza baada ya ndege ya kivita isiyoendeshwa na rubani kuingia katika anga yake na kunaswa na helikopta.

Conricus alisema ilinaswa ikiwa ndani ya Israeli kaskazini ya jiji la  Beit Shean, karibu na mpaka wa Jordan.

Hata hivyo, hakueleza ikiwa ndege hiyo ilikuwa na silaha lakini akadai ilikuwa katika shughuli za kijeshi na ilitumwa na wanajeshi wa Iran kutoka kambi ya kijeshi ya Iran iliyoko eneo la Palmyra.

Alisema ndege nane za kivita za Israeli zililenga vituo vya kijeshi vya Iran vilivyoko Syria.

Shirika la haki za binadamu la Syrian Observatory for Human Rights, lenye makao Uingereza, lilisema Israeli ililenga vituo kadhaa vilivyoko mkoa wa kati wa Homs. Shirika hilo lilisema vituo hivyo hutumiwa na Iran na Urusi.

Msemaji wa mashauri ya nchi za kigeni wa Iran Bahram Ghasemi alilaumu Israeli kwa kudanganya akisema Iran haina wanajeshi Syria.