JAMVI: Mirindimo mipya ya Tangatanga baada ya BBI kuzikwa

Na WANDERI KAMAU

MRENGO wa ‘Tangatanga’ umepata msisimko mpya wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya na Bonde la Ufa, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kufutilia mbali mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Mara tu baada ya uamuzi huo, Naibu Rais William Ruto alitoa ujumbe “kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipenda Kenya.”Dkt Ruto alisema huu ni wakati nchi iheshimu maamuzi yanayotolewa na taasisi huru.

Sherehe hizo zilitanda katika maeneo ya Kati, hasa Kaunti za Muranga, Nyeri na Nyandarua, viongozi wa mrengo huo wakiwaongoza wafuasi wao “kusherehekea” ushindi.Wabunge wanaoegemea mrengo huo walisema hatimaye mahakama imedhihirisha kuwa wao ndio “watetezi halisi” wa wananchi.

“Huu ni uamuzi unaooyesha wazi sisi ndio watetezi halisi wa wananchi. BBI ni njama na mpango wa watu wachache kujitengeneze nyadhifa za uongozi. Kama ambavyo tumekuwa tukishikilia, huu ni wakati kwa viongozi na serikali kuangazia masuala ya maendeleo na kufufua uchumi wa nchi. Mageuzi ya kikatiba ni jambo tunaloweza kushughulikia baadaye,” akasema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) ambaye ni miongoni mwa washirika wakuu wa karibu wa Dkt Ruto.

Kauli kama hizo zilitolewa na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Faith Gitau (Nyandarua), Milicent Omanga (Seneta Maalum) kati ya wengine ambao walikuwa miongonu mwa wale waliopiga kura ya ‘La.’

Katika kaunti za Baringo, Uasin Gishu na maeneo mengine ambayo ni ngome za kisiasa za Dkt Ruto, wananchi pia walijumuika pamoja kushabikia uamuzi huo.

Bunge la Kaunti ya Baringo lilikuwa miongoni mwa yale yalipiga kura kupinga mswada huo.Licha ya msisimko huo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa ingawa huenda hilo likaonekana kama “ushindi” kwa wakati huu, bado ni mapema kwa mrengo huo kuanza kusherehekea.

Wanasema ingali mapema kudhani mchakato huo umevurugika kabisa, kwani bado kuna nafasi kwa wale wanaouendesha kuakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

“Huu ni mchakato wa kisiasa na kisheria kwa wakati mmoja. Kwa wale wanaounga mkono BBI, wana nafasi kukata rufaa mahakamani. Kisiasa, huu ni mradi wa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga. Ingawa kwa wakati huu wanaonekana kupata pigo kisiasa, wao ni wanasiasa, hivyo huenda wakabuni njia mbadala kutimiza malengo yao,” Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mnamo Ijumaa, mwenyekiti-mwenza wa Sekretariati inayoendesha mchakato huo, Bw Junet Mohamed, alisema wanaandaa kundi la mawakili ambao watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wiki ijayo.

Bw Mohamed, ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki, alitaja uamuzi huo kama “mapinduzi ya kisheria” yanayoendeshwa na majaji wanaolenga “kulipiza kisasi” dhidi ya Rais Kenyatta.

“Uamuzi huu ni ushirikiano fiche uliopo kati ya baadhi ya maafisa wa Idara ya Mahakama na wanaharakati ili kuilemaza serikali na utendakazi wake. Ni njama zinazoendeshwa kwa ushirikiano na wanasiasa wanaoipinga serikali na juhudi za kuiunganisha nchi ambazo zinazoendelezwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Mohamed.

Hata hivyo, wadadisi wanaeleza kuwa licha ya baadhi ya viongozi wanaounga mchakato huo kupuuza maamuzi ya mahakama, ni hatua ambayo inaonekana kumjenga kisiasa Dkt Ruto na viongozi ambao walijitokeza wazi kuipinga BBI.

Baadhi yao ni kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua na Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni.Mdadisi wa siasa Godfrey Sang’ anasema taswira ambayo imewekwa na uamuzi huo nyoyoni mwa Wakenya wengi ni kuwa Dkt Ruto ni “mtetezi wa wananchi” hata ingawa huenda hilo lisiwe kweli.

Anaeleza kuwa ingawa Dkt Ruto hakuwa amejitokeza moja kwa moja kuupinga mpango huo, kauli zake kuwa kuna masuala muhimu yanayopaswa kushughulikiwa kwanza ndiyo yanaonekana kuwateka wengi.

“Ujenzi wa dhana ni muhimu sana katika siasa. Hilo ndilo huwavutia ama kutowavutia wananchi. Ilivyo sasa, Dkt Ruto na washirika wake wanaonekana kuwa washindi kutokana na uamuzi huo, ikizingatiwa wengi wao wameadhibiwa kutokana na misimamo yao kisiasa,” akasema Dkt Sang.

Baadhi ya washirika wake waliopoteza nyadhifa zao ni Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) kama Kiongozi wa Wengi Kwenye Seneti, Seneta Susan Kihika (Nakuru) kama Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) kama Kiranja wa Wengi kati ya wengine.

“Ni wazi wanasiasa hao wataonekana kama ‘mashujaa’ miongoni mwa wafuasi wao kwani wataanza kujipigia debe kwa misingi ya masaibu ya kisiasa ambayo wamekuwa wakipitia. Ni mbinu ambayo Dkt Ruto amekuwa akitumia pia, hasa kwa kutengwa serikalini na Rais Kenyatta. Bila shaka, huu ni wakati mwafaka kwao kujijenga kisiasa,” asema Dkt Sang.

Hata hivyo, wadadisi wanasema bado ni mapema, kwani hatima kamili ya uamuzi huo bado haifahamiki.“Ingawa hii ni nafasi yao kujijenga, itabidi wangoje hadi mwelekeo kamili wa mchakato huo ufahamike,” akasema.

Tangatanga wapinga vikali mswada wa BBI

WINNIE A ONYANDO na CHARLES WASONGA

MJADALA kuhusu Mswada wa Mageuzi ya Katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI), jana uliendelea katika Bunge la Kitaifa na Seneti huku wabunge wa tangatanga wakdhalilisha shughuli hiyo wakisema sio ya dharura wakati huu.

Lakini wabunge wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walishabikia kupitishwa kwa mswada huo, jinsi ulivyo, wakisema mapendekezo yaliyomo yanashughulikia changamoto kadha zinazoikumba nchi.

Wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Aisha Jumwa (Malindi), Glady Shollei (Uasin Gishu), Cecily Mbarire (Mbunge Maalum) miongoni mwa wengine walisema, bunge lilipaswa kujadili changamoto zinazowakumba Wakenya kama vile janga la Covid-19, baa la njaa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Wabunge hao, ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, pia walidai mswada huo utawaongezea Wakenya gharama kupitia kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi na idadi ya maeneo bunge kutoka 290 hadi 360.

“Mswada huu hauna maana kwa Wakenya wakati huu. Lingekuwa jambo la busara ikiwa kikao kama hiki kingeitishwa kujadili jinsi Wakenya watapata chanjo, chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Aliye na njaa ni mwenye hasira,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo pia alionya kuwa, wakazi wa Nyeri watapinga mswada huo wa BBI kwa sababu kaunti hiyo iliachwa nje katika ugavi wa maeneo bunge 70 mapya yanayopendekezwa.

Bw Gachagua alitaja hatua hiyo kama ubaguzi ambao unalenga kuwafukarisha watu wa Nyeri.

“Wale ninaowawakilisha hawana sababu ya kuunga mkono mswada huu kwa sababu umewabagua na hivyo kuwasukimia umasikini zaidi. Rasilimali za kitaifa hugawanywa kwa misingi ya maeneo bunge lakini hatujaongezewa eneo bunge lolote,” akasema Bw Gachagua.

Kwa upande wake, Bi Mbarire alisema mswada huo ni hatari kwa sababu unadhoofisha uhuru wa Idara ya Mahakama kupitia uteuzi wa afisi ya kupokea malalamishi kuhusu majaji, maarufu kama “ombudsman”.

“Ikiwa mswada huo utapitishwa, majaji watakuwa watumwa wa afisi ya rais ambayo ndio itateua afisa wa kupokea malalamishi dhidi yao. Hii itaathiri shughuli za utoaji wa haki mahakamani,” akaeleza.

Awali, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) Muturi Kigano alipuuzilia mbali wabunge waliotaka mswada huo ufanyiwe marekebisho akisema, madai yao hayana mashiko kikatiba.

Wengine waliounga mkono mswada huo ni wabunge Opiyo Wandayi (Ugunja), Jeremiah Kioni (Ndaragua), Chris Wamalwa (Kimimini), Zulekha Hassan (Mbunge mwakilishi wa Kwale), miongoni mwa wengine.

Katika Seneti, wajumbe waligawanyika kuhusu mswada huo huku wale wa mrengo wa tangatanga wakishiniza ufanyiwe mabadiliko huku wenzao wa kieleweke wakishinikiza upitishwe ulivyo.

Sawa na wenzao wa bunge la kitaifa, maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho), na Mithika Linturi (Meru) walisema kuna vipengele hatari katika mswada huo ambavyo vinapaswa kurekebishwa.

Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, wabunge na maseneta hawakuwa wamepiga kura kuhusu mswada huo. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alidokeza kuwa huenda mjadala huo ukaendelea Jumanne wiki ijayo.

Tangatanga walia kuteswa na wandani wa Uhuru

Na MWANGI MUIRURI

VIONGOZI wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya, wamedai kuhangaishwa wanapojiandaa kwa chaguzi ndogo zinazopangiwa kufanyika mwezi ujao eneo hilo.

Seneta wa Kaunti ya Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, amedai kuwa wanasiasa wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wamezindua njama zisizofaa kuvuruga nafasi ya Tangatanga kutwaa nyadhifa za maeneo-bunge ya Juja na Kiambaa pamoja na Wadi ya Muguga katika chaguzi ndogo zijazo.

Alidai kuwa, nia iliyopo ni kuhakikisha Dkt Ruto na wenzake hawatamwaibisha Rais katika ngome yake ya Kaunti ya Kiambu.

“Tulipewa kidokezo kuwa baada ya Mbunge wa Juja, Bw Francis Munyua kuaga na kisha diwani wa Muguga, Bw Eliud Ngugi akamfuata, kuliandaliwa mkutano wa dharura katika mkahawa mmoja ulio katika barabara ya kutoka Ruiru Kimbo hadi Nembu na ambapo iliazimiwa kuwa chaguzi hizo ndogo kwa vyovyote vile zisitawaliwe na Tangatanga,” akadai.

Kulingana naye, mambo hayo ndiyo yaliyomfanya Dkt Ruto kujitenga na chaguzi hizo ili asionekane kama anayetaka kukabiliana na Rais Kenyatta moja kwa moja ngomeni kwake.Aliwataka wapinzani wao wazingatie haki za demokrasia na kuwapa wananchi nafasi ya kujiamulia mkondo wanaotaka kufuata kisiasa bila shinikizo za vitisho na kuhangaishwa.

Hata hivyo, wafuasi wa Rais Kenyatta katika eneo hilo wamekuwa wakipuuzilia mbali lalama za wapinzani wao wakitaka wafuate sheria ikiwa hawataki kukamatwa na kushtakiwa kwa makosa waliyowahi kuyafanya.

Barasa: Waliozua fujo Kabuchai wangali huru, tunaonewa kama wandani wa Ruto

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kimilili Bw Didmus Barasa amedai wandani wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto wanahangaishwa kwa sababu ya msimamo wao kisiasa.

Bw Barasa alisema Ijumaa waliozua rabsha mnamo Alhamisi wakati wa uchaguzi mdogo eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma hawakutiwa nguvuni.

Mbunge huyo alisema wanasiasa waliokamatwa kwa madai ya kuwa na silaha hatari kwenye magari yao, zinazosemakana zilipangiwa kutumika kuzua fujo wanaandamwa kwa sababu ya ajili ya kuegemea upande wa Dkt Ruto.

“Hatujawahi kupiga yeyote wala kutishia. Waliozua vurugu wangali huru hawakukamatwa,” akalalamik mbunge huyo.

Bw Barasa ni miongoni mwa wabunge wanne wa Tangatanga waliotiwa nguvuni.

Wanajumuisha Mabw Barasa (Kimilili), Nelson Koech Belgut), Wilson Logo (Chesumei) na seneta wa Nandi, Samson Cherargei.

Wanne hao wamefikishwa mahakamani Bungoma.

Uchaguzi mdogo wa Kabuchai ulizua ushindani mkali kati ya Joseph Majimbo Kalasinga wa chama cha Ford-Kenya, kinachoongozwa na seneta wa Bungoma Bw Moses Wetangula, na mgombea wa UDA, Evans Kakai.

Bw Kalasinga aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 19, 274 akifuatwa na Kakai 6, 455. Chama cha UDA kinahusishwa na Dkt Ruto.

Kiti cha Kabuchai kilisalia wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Bw James Mukwe Lusweti, Desemba 2020.

Wabunge 4 wa Tangatanga wakamatwa kwa kuhonga wapigakura

 JARED NYATAYA na CHARLES WASONGA

WABUNGE wanne wa mrengo wa Tangatanga wangali wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma baada ya kukamatwa kwa madai ya kuwahonga wapiga kura katika uchaguzi mdogo unaoendelea eneo bunge la Kabuchai.

Didmus Barasa (Kimilili), Nelson Koech (Belgut), Wilson Kogo (Chesumei) na seneta wa Nandi Samson Cherargei walikamatwa Alhamisi asubuhi katika eneo la Masese, Kaunti ya Bungoma. Eneo hilo liko karibu na barabara ya kutoka mjini Chwele- Bungoma.

“Hatujaachiliwa. Bado tumezuiliwa hapo na bila kuambia makosa yetu. Inaonekana kuwa serikali inapanga kuendeleza wizi wa kura kwa sababu sisi ni maajenti wa mgombeaji wetu. Hakuna ushahidi kuwa tulikuwa tukiwahonga wapiga kura, inavyodaiwa,” Bw Barasa akaambia Taifa Leo kupitia ujumbe mfupi.

Sasa chache kabla ya shughuli ya kupiga kura kuanza viongozi wa Ford Kenya wakiongozwa na kinara wao Moses Wetang’ula na mgombeaji wa chama hicho Joseph Majimbo, walilalamika kuwa wandani hao wa Naibu Rais William Ruto walikuwa wakiwahonga wapiga kura.

Bw Majimbo pia alielekeza kidole cha lawama kwa wabunge wengine wa Tangatanga John Waluke (Sirisia) na Fred Kapondi (Mt Elgon) kwa kutoa vishawishi vya fedha kwa wananchi ili wampigie kura mgombeaji wa United Democratic Alliance (UDA) Evan Kakai.

“Tunataka maafisa wa polisi na wale wa IEBC kufanya uchunguzi wa kina kuhusu visa hivi vya utoaji hongo kwa wapiga kura. Uamuzi wa wananchi unapasa kuheshimiwa katika uchaguzi huu,” Bw Wetang’ula akawaambia wanahabari.

Hata hivyo Bw Kakai alikana madai hayo na badala yake akaisuta Ford Kenya kubuni madai hayo na kuchochea fujo.

“Wameamua kushiriki fujo na propaganda zisizo na maana yoyote. Hii inaonyesha kuwa Ford Kenya wameingiwa woga,” mgombeaji huyo wa UDA akasema baada ya kupiga kuta katika Shule ya Msingi ya Pongola.

Pigo kwa Jumwa na Tangatanga wakizimwa Kadu

Na CHARLES LWANGA

WANASIASA wa pwani wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wamepata pigo kuu, baada ya juhudi zao za kuzindua upya chama cha Kadu Asili kugonga mwamba.

Kiongozi wa Kadu Asili, Bw Gerald Thoya, amemtaka msajili wa vyama vya kisiasa kuingilia kati akidai chama chake “kimeingiliwa kinyume cha sheria” na watu anaoamini wanataka “kusababisha mgogoro wa kisiasa na kiusimamizi katika chama.”

Wabunge Aisha Jumwa (Malindi) na Owen Baya (Kilifi Kaskazini), walioasi ODM, ndio wataathirika zaidi kwani walikuwa mstari wa mbele kupigia debe uzinduzi upya wa Kadu Asili kama chama cha kisiasa cha Pwani.

Uzinduzi huo ulitazamiwa kufanyika mwezi Machi baada yao kukibadilisha jina ili wakitumie kama chombo chao katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi wengine wa Pwani wanaoegemea mrengo wa Tangatanga, unaohusishwa na Dkt Ruto, ni pamoja na Mohamed Ali (Nyali), Khatib Mwashetani (Lungalunga), Sharif Ali (Lamu Mashariki), Jones Mlolwe (Voi), Paul Katana (Kaloleni), Ali Wario (Bura), Benjamin Tayari (Kinango) na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar.

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Alhamisi, kiongozi wa Kadu Asili, Bw Thoya, alisema kuwa alistaajabishwa na hatua ya “wanasiasa fulani wa Pwani” kujitosa chamani bila uongozi kufahamishwa, kiasi cha kubadilisha katiba ya chama ili kukidhi maslahi yao.

“Nilimwandikia barua Msajili wa Vyama vya Kisiasa baada ya kujua kuwa baadhi ya watu walikuwa wamevamia chama chetu, kiasi cha kubadilisha katiba, ishara, rangi na kauli mbiu pasipo uongozi kufahamishwa.

“Hatutakubali hilo kwa sababu Kadu Asili ni chama cha kitaifa kinachojisimamia vyema, chenye uongozi thabiti unaoendeshwa kwa mujibu wa Sheria za Vyama vya Kisiasa na Katiba ya Kenya,” alisisitiza Bw Thoya.

Kadu Asili ni miongoni mwa vyama vya kisiasa vinavyosubiriwa kwa hamu mno kutumiwa na wanasiasa katika uchaguzi wa 2022.

Baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga eneo la Pwani walidhamiria kukibadilisha jina na kukifanya maarufu eneo hilo ili kukitumia kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye kura ijayo.

Bi Jumwa ametangaza nia yake ya kutema chama cha ODM, kinachoongozwa na kinara Raila Odinga, na kugombea kiti cha ugavana cha Kilifi 2022 kwa tiketi ya Kadu Asili; huku akiunga mkono azma ya urais ya Dkt Ruto ya 2022.

Alikuwa ameanza kupigia debe vilivyo chama cha Kadu ili kuvutia wanachama wapya na kupata ufadhili kutoka kwa Dkt Ruto.

Wiki mbili ilizopita, mbunge huyo wa Malindi alianzisha kampeni kali kupeperusha Kadu Asili na kusajili wanachama wapya, katika mkutano ulioandaliwa nyumbani kwake Kakuyuni, Malindi.

Hata hivyo, mwenzake wa Kilifi Kaskazini, Bw Baya, alisusia mkutano huo licha ya kuwa miongoni mwa wageni wa heshima walioalikwa kuhudhuria.

Tangatanga watimua wahubiri na kuteka mazishi ya diwani

Na WAIKWA MAINA

MAZISHI ya diwani Mburu Githinji wa wadi ya Rurii, Kaunti ya Nyandarua, Jumanne yaligeuka kuwa uwanja wa fujo baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto kuvuruga ratiba na kuanza kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta.

Wanasiasa hao walitwaa ratiba na uendeshaji wa mazishi hayo kutoka kwa viongozi wa makanisa kwa nguvu, ambapo waliendeleza harakati za kuipinga ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), huku pia wakizindua kampeni za kuwapigia debe watu wanaopanga kuwania nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kizaazaa kilianza wakati Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti hiyo, Bi Faith Gitau (pichani juu), alipoalikwa kuwahutubia waombolezaji. Kwenye hotuba yake, Bi Gitau alisisitiza lazima wanasiasa alioandamana nao wapewe nafasi kuhutubu pia.

Mapema wiki hii, wahubiri katika kaunti hiyo walikuwa wametangaza kuwa wanasiasa hawataruhusiwa tena kuhutubu katika hafla zinazoongozwa na kanisa.

Juhudi za viongozi wa kanisa kumrai Bi Gitau kuzingatia mpangilio wa ratiba hazikuzaa matunda baada ya mbunge huyo kusisitiza kuwa lazima wageni pia wahutubu.

Katika kile kilionekana kuwa njama iliyopangwa awali, vijana walevi walielekea kwenye jukwaa na kuanza kuwapigia kelele viongozi wa dini huku wakitishia kuvuruga mazishi hayo.

Polisi walikuwa na wakati mgumu kuwakabili vijana hao, ambao walifanikiwa kwenda kwenye jukwaa na kuanza kuondoa vipaza sauti.

Katika ishara nyingine iliyoonyesha kisa hicho kilikuwa kimepangwa, mbunge wa Olkalou, David Kiaraho alinyakua kipaza sauti kimoja na kusimamia hafla.

Bw Kiaraho alianza kuwaita wanasiasa waliokuwepo kuhutubu huku vijana wakishangilia. Vijana hao wanadaiwa kusafirishwa kutoka miji ya Kinangop, Naivasha na Ol Kalou.

Wanasiasa waliohutubu walimuunga mkono aliyekuwa mbunge wa Embakasi ya Kati, John Ndirangu kuwania ubunge katika eneo hilo.

Kwa pamoja, wanasiasa kutoka mirengo yote miwili walimuunga mkono mwanawe marehemu, Bi Mary Githinji kumrithi babake kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika.

Wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Gathiru Mwangi (Embakasi ya Kati) na Bw Kipkirui Chepkwony kutoka Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF) walimpigia debe Dkt Ruto.

huku wakimkashifu Rais Kenyatta, handisheki na BBI.

“Tunaambiwa nchi itakumbwa na mapigano ikiwa tutajadili na kupigia debe siasa za ‘wilbaro’, kupinga BBI au kuzungumza kuhusu njama za mabwanyenye na maslahi ya watu maskini. Hatutatishwa! Tunahitaji kueleza ukweli, BBI si suala muhimu katika eneo la Kati na nchi nzima kwa jumla,” akasema Bw Gachagua.

Sibabaishwi na matusi yenu, Uhuru awaambia Tangatanga

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu amevunja kimya chake kuhusu tetesi za kundi la Tangatanga linalokosoa matamshi yake ‘mamlaka ya urais yanafaa kuwa mikononi mwa jamii tofauti na zile mbili ambazo zimeongoza tangu Kenya ilipopata uhuru’.

Kundi hilo linalohusishwa na Naibu wa Rais, William Ruto limetaja matamshi hayo kama yanayoendeleza ukabila nchini.

Dkt Ruto pia amenukuliwa hadharani akiyakosoa, pamoja na salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga na Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inayopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

Akiwasuta wanasiasa wa kundi la Tangatanga, Rais Kenyatta alisema hababaishwi na matamshi mazito wanayomrushia.

Kwenye mahojiano ya pamoja na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Agikuyu, kiongozi wa nchi Jumatatu alisema kwa sasa haja yake kuu ni kuona amefanyia wananchi maendeleo na kuhakikisha ameafikia sera zake.

“Wanadhani wakinitusi nitawatumia askari washikwe? Kama wameona matusi kwa rais ni bora endeleeni, mimi niko hapa kazi hadi nitakapoikamilisha,” akasema.

Akicharura kundi la Tangatanga, Rais Kenyatta alilionya kutojaribu kusimamisha utendakazi wake wala kuzua fujo nchini.

“Hata kabla hawajaongea na kunitukana, huanza kwa kueleza maendeleo yaliyofanywa. Unadhani hiyo kazi hujifanya? Hufanywa na serikali ambayo ninaiongoza,” Rais akasema.

Akieleza kushangazwa kwake na tetesi za wakosoaji wake, Rais alisema hana shida na yeyote, lengo lake likiwa kuafikia ahadi zake kwa Wakenya kabla kukamilisha hatamu yake ya uongozi 2022.

“Lazima nifanye kazi niliyoahidi wananchi na niikamilishe…kauli yangu kuhusu jamii zingine zipokezwe mamlaka hakuna mahali nimesema ni vita ya 2022, haja yangu ni amani, utulivu na maendeleo ya Kenya,” Rais Kenyatta akafafanua, akiridhia salamu za maridhiano kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Handisheki, kwa kile alitaja kama “hatua iliyochangia kuleta amani nchini”.

Rais pia aliendelea kuhimiza Wakenya kukumbatia Ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI, akisema itasaidia kuangazia tofauti zinazojiri kila miaka ya chaguzi, ikiwa ni pamoja na kuleta maendeleo.

BBI inapendekeza kufanyiwa marekebisho ya Katiba, suala ambalo limeonekana kupingwa na Dkt Ruto na wandani wake.

Naibu wa Rais pia amekuwa akikosoa uhalisia wa Handisheki, akihoji inalenga kuzima ndoto zake kuingia Ikulu 2022.

Tangatanga wamzomea Uhuru kwa matamshi

Na WANDERI KAMAU

WANASIASA wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wamkashifu vikali Rais Uhuru Kenyatta wakidai matamshi yake Jumamosi, kwamba wakati umewadia kwa jamii zingine kuongoza nchi, ni kuchochea ukabila.

Rais Kenyatta alitoa matamshi hayo kwenye mazishi ya mamake kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, Kaunti ya Vihiga.

Ni kauli ambayo ilionekana kumlenga Naibu Rais William Ruto, ambaye amekuwa akiendesha kampeni kuwa sasa ni wakati wa watu wa tabaka la chini maarufu kama “Hustler Nation” kuchukua uongozi wa nchi.Lakini jana, wabunge zaidi ya 20 wa mrengo huo walikosoa matamshi ya Rais Kenyatta, wakisema yeye binafsi hakuchaguliwa kama rais kwa msingi wa kabila lake.

“Rais Kenyatta lazima afahamu alichaguliwa na Wakenya 2013 na mara mbili mnamo 2017 kutokana na sera alizokuwa nazo kuiendesha nchi wala si kutokana na kabila lake,” akasema Seneta Kipchumba Murkomen wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Viongozi hao walikuwa wamehudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa la House of Hope, eneo la Kayole, eneo bunge la Embakasi ya Kati, Nairobi, wakiandamana na Dkt Ruto.

Mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) alisema ni makosa kwa Rais Kenyatta kuirejesha nchi kwenye mwelekeo huo, ikizingatiwa kesi zilizowakabili pamoja na Dkt Ruto katika Mahakama ya Kitaifa ya Uhalifu (ICC) nchini Uholanzi zilitokana na mapigano ya kikabila mnamo 2007.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alisisitiza kuwa Wakenya hawatakubali kurejeshwa katika mijadala ya kikabila, kwani wameona athari zake kwenye chaguzi za awali.

Wazee wakemea matamshi ya chuki

Na Oscar Kakai

BARAZA la wazee wa jamii ya Kalenjin (Myoot) limetadharisha wanasiasa wa mirengo ya Kieleweke na Tangatanga dhidi ya kutoa matamshi ya chuki yanayoweza kutumbukiza nchi katika ghasia.

Wazee hao wametaka malumbano ya siasa za urithi wa urais mwaka 2022 yakome.

Mwenyekiti Bw James Lukwo alisema wanahofia kuhusu viongozi ambao wanatoa semi za chuki kiholela na kuendeleza ukabila ambao huenda ukaligawanya taifa.

Akiongea na wanahabari mjini Kapenguria, Bw Lukwo alisema wameshuhudia mambo yanayoweza kuibua uhasama kati ya jamii wakati wa uchaguzi.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa makini matamshi ya wanasiasa. Tunataka yafike kikomo baada ya Rais kukutana na naibu wake wiki jana,” akasema, akigusia maombi ya kitaifa yaliyofanyika Ikulu ya Nairobi juzi.

 

‘Tangatanga’ sasa wamtaka Uhuru kuvunja Bunge

Na Brian Ojamaa

WABUNGE wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuvunja Bunge la Kitaifa kama alivyoshauriwa na Jaji Mkuu David Maraga.

Wabunge hao walisema jana kuwa Rais anapaswa kuzingatia Katiba kama alivyoahidi alipokula kiapo cha kuapishwa kuhudumu kwa muhula wa pili.

Walisema anapaswa kuvunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya.

Wabunge hao, ambao walikuwa wameandamana na Dkt Ruto kwenye hafla ya kuchangisha pesa kwa makanisa kadhaa katika eneobunge la Bumula, Kaunti ya Bungoma, walisema kuwa wako tayari kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Mbunge wa Kuria Magharibi, Bw Mathias Robi, alisema kuwa Rais Kenyatta hana lingine ila kuvunja Bunge kama alivyoshauriwa ili kudhihirisha kwamba anatii Katiba.

“Jaji Mkuu alisema kuwa Bunge limeshindwa kupitisha Sheria kuhusu Usawa wa Jinsia. Hivyo, tunapaswa kwenda nyumbani na kushiriki upya kwenye uchaguzi. Rais hana lingine ila kufanya hivyo.”

 

Maswali 10 ya ‘Tangatanga’

Na WANDERI KAMAU

MRENGO wa ‘Tangatanga’ Jumamosi uliitaka serikali kujibu maswali 10 kuhusu mpango wa kuwasajili upya Wakenya kupitia mfumo wa ‘Huduma Namba’, ukidai uwepo wa njama za wizi wa kura na uporaji wa fedha za umma.

Serikali ilieleza kuhusu mpango wa kuwasajili Wakenya ambao hawakusajiliwa kwenye awamu ya kwanza ya shughuli hiyo kufikia Desemba mwaka huu.

Lakini Jumamosi, karibu wabunge 10 wa mrengo huo, ambao humuunga mkono Naibu Rais William Ruto, waliitaka Serikali kueleza kuhusu dharura ya kurejelea usajili huo, wakidai unaendeshwa kwa njia ya siri.

Wabunge hao walijumuisha Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu), John Kiarie (Dagoretti Kusini), Nixon Korir (Lang’ata) miongoni mwa wengine.

Kwenye kikao na wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi, wabunge hao walishangaa sababu ya kutoa zabuni ghali ya mpango huo “kwa njia fiche”.

“Mbona mchakato wa utoaji tenda kuhusu mchakato unaendeshwa kisiri badala ya njia ya wazi kama ilivyo kwenye Katiba? Mbona idara husika hazijashirikishwa?” wakadai viongozi hao, katika taarifa iliyosomwa na Bw Kiarie.

Vilevile, waliitaka serikali kueleza sababu ambapo kampuni moja ya kigeni imelipwa Sh7 bilioni kuendesha mpango huo. Walidai serikali imeiteua kampuni ya Muhlbauer High Tech International (au Muhlbauer ID Services GmbH) kuendesha mchakato huo.

Walidai kuwa watu wawili, waliowataja kama Matthias Karl Kohler na H Karashani wamekuwa wakifanya vikao na baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS).

Walisema wawili hao wamekuwa wakikaa katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi kwa wiki moja iliyopita, huku wakizuru makao makuu ya NIS kwa muda huo wote.

Waliwataja wawili hao kuwa mamluki huku wakitaka ufafanuzi kuhusu aliyelipa gharama za kuwasafirisha nchini, ulinzi wanaopewa na aliyegharimia malipo yao kwenye hoteli waliokaa walipowasili nchini.

“Ili kuonyesha umuhimu kuhusu mpango huu, wawili hao walipewa ulinzi mkali kutoka kwa vikosi maalum vya usalama kwa siku tano walizokaa nchini,” akadai Bw Kiarie.

Dai lingine walilotaka majibu ni kuhusu kujumuishwa kwa afisa waliyemtaja kama Dkt Mativo kutoka NIS kama Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa Usajili wa Huduma Namba.

Aidha, waliitaka Serikali kueleza yaliyojadiliwa kwenye mikutano waliyodai ilifanyika mnamo Septemba 11 na 14 mtawalia.

Wabunge hao pia walishangaa kuhusu hatua ya mradi huo kuondolewa kutoka Wizara ya Usalama wa Ndani hadi chini ya usimamizi wa NIS.

“Ikizingatiwa wizara hiyo imesema kampuni zote zitakazohusika kwenye mpango huo ni za hapa nchini, mbona isitueleze asili ya kampuni ya Muhlbauer High Tech International?” akaeleza.

Walisema kuwa kwa mchakato huo kuendelea, lazima serikali itoe maelezo yote kuhusu Wakenya waliosajiliwa kwenye awamu ya kwanza ya mchakato huo.

Hata hivyo, chama cha ODM kiliyapuuza madai hayo, kikiyataja kama yasiyo na msingi, kwani Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu serikalini waliojitokeza kusajiliwa kwenye awamu ya kwanza mwaka uliopita.

Kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna, chama hicho kiliyataja madai hayo kama dalili ya kuogopa kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa 2022.

‘Tangatanga’ wasihi Uhuru azungumze na Ruto

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamemsihi Rais Uhuru Kenyatta afanye mazungumzo na naibu wake ili kumaliza uhasama uliopo baina ya viongozi hao.

Viongozi hao wamemtaka Rais Kenyatta na Dkt Ruto wapatane ili kumaliza tofauti baina yao ambazo zimesababisha chama cha Jubilee kugawanyika.

Akizungumza katika eneo la Kamukunji, Eldoret, katika Kaunti ya Uasin Gishu, Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany alimtaka Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto wapatane ili kutuliza joto la kisiasa ambalo limeanza kushuhudiwa humu nchini.

“Jinsi tulivyokuwa tukipanga mwaka wa 2013 kuhusu ni nani alifaa kuwa Rais na naibu, kisha wawili hao wakakubali kukaa pamoja, ndivyo wanavyofaa wazungumze kisha watupe mwelekeo kama wafuasi wa Jubilee ili tukomeshe haya mambo tunayoshuhudia,” akasema Bw Kositany.

Alikuwa ameandamana na Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri ambaye alimwondolea lawama Dkt Ruto kutokana na matamshi yaliyotolewa na Bw Ng’eno na Bw Sudi.

Lakini kwa mujibu wa mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri ambaye anaegemea mrengo wa Rais Kenyatta, Dkt Ruto anafaa kujilaumu kwa kusababisha uhasama wa kisiasa baina yake na kiongozi wa nchi.

Bw Ngunjiri alisema kuwa Rais Kenyatta alikuwa ameahidi Dkt Ruto kwamba angempigia debe katika kinyang’anyiro cha urais 2022 iwapo asingefanya kampeni za mapema.

Bw Ngunjiri alisema kuwa kitumbua cha Naibu Rais kiliingia mchanga alipopinga Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao Rais Kenyatta anataka kutumia kuacha taifa likuwa limeungana atakapostaafu 2022.

“Rais aliweka wazi kuwa hataweza kufanikisha ndoto yake ya kuunganisha taifa hili iwapo kutakuwa na kampeni za mapema. Kampeni hugawanya watu na hiyo ndiyo maana Rais amekuwa akipinga siasa za mapema,”

“Inashangaza kuwa Naibu wa Rais alianza mchakato wa kutaka kumrithi Rais Kenyatta mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 uliokuwa umegawanya taifa hili,” akasema Bw Wambugu.

Akaunti za ‘Tangatanga’ zanyemelewa

Na ONYANGO K’ONYANGO

BAADA ya kupokonywa nyadhifa za uongozi katika chama cha Jubilee, washirika wa Naibu Rais William Ruto sasa wameingiwa na wasiwasi kwa vile akaunti zao za kibinafsi zachunguzwa kubainisha chanzo cha mapato yao.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, wabunge wanaoegemea upande wa Dkt Ruto ulio maarufu kama kikundi cha ‘Tangatanga’ walisema wanashuku hatua hizo ni miongoni mwa juhudi za kutaka kuwazima ili wasimpigie debe anapojiandaa kuwania urais ifikapo mwaka wa 2022.

Mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi ambaye ni mtetezi sugu wa Dkt Ruto alidai kwamba serikali imeunda kikosi maalumu cha wapelelezi kinachoshirikisha maafisa wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS) na Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kuwatisha wandani wa Naibu Rais.

Bw Sudi alidai kwamba kikosi hicho kinaendelea kuchunguza chanzo cha mali yake kibinafsi na shughuli zake.

“Tunatishwa kwa msimamo wetu. Walitaka kuchunguza biashara ninazofanya na kwa kuwa sifanyi biashara yoyote na serikali, kuna shamba nililouza zamani. Sasa wananichunguza na ninasubiri waje kunikamata,” alisema.

Mbunge wa Keiyo Kusini, Bw Daniel Rono, ambaye ni mshirika mwingine wa Dkt Ruto aliambia Taifa Jumapili kwamba mapema Agosti alizimwa kutoa pesa katika mojawapo ya akaunti zake za benki hadi aeleze zilitoka wapi.

“Mimi nimeathiriwa na vitisho vya serikali. Baada ya kuchunguza jinsi miradi ya hazina ya maeneobunge (NG-CDF) inavyotekelezwa katika eneobunge langu na kukosa doa lolote, wameanza kuchunguza mapato yangu ya fedha. Haieleweki kwa nini kuchunguza nilivyopata Sh300,000 pekee… Ingeeleweka kama zingekuwa zaidi ya Sh1 milioni,” alisema Bw Rono.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua alijipata katika hali sawa serikali ilipomzuia kutoa zaidi ya Sh200 milioni katika akaunti zake za benki.

Bw Gachagua ni mmoja wa washirika wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya.

Jumamosi, Dkt Ruto aliendelea kuwahimiza washirika wake wasiogope vitisho vya kila mara. Alitoa wito kama huo mapema wiki hii akisema kwamba watatishwa kwa kila namna wabadilishe msimamo.

“Tusirudi katika mbinu zilizopitwa na wakati za kisiasa. Tunaweka nchi katika hatari ya ghasia,” alisema.

Washirika wengine wa Dkt Ruto wanaomulikwa na serikali ni seneta Susan Kihika (Nakuru), wabunge Kimani Ngunjiri (Bahati), Kimani Ichungwah (Kikuyu) miongoni mwa wengine.

Lakini viongozi wanaomuunga Rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata walipuuza madai ya washirika wa Dkt Ruto wakisema wanaeneza uongo ili wahurumiwe na umma.

“Serikali haitishi yeyote, inaamini katika Uhuru wa kujieleza na makundi ya kisiasa. Italinda haki hizi kila wakati hata wakati uhuru huo unatumiwa kukosoa serikali, hata hivyo uhuru huo sio leseni ya kutenda uhalifu,” alisema Bw Kang’ata.

Jana, akiwa Mombasa, Dkt Ruto aliendelea kuwashambulia mahasimu wake walio katika Chama cha Jubilee akiwataka wahame kwa vile wameonyesha nia ya kuunga mkono azimio la Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga. Msimamo kwamba Jubilee itamuunga mkono Bw Odinga ulikuwa umetolewa na Naibu Mwenyekiti wa chama hicho, Bw David Murathe.

‘Tangatanga’ wawekea DCI na EACC presha

Na MISHI GONGO

KUNDI la wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ limemtaka mkurugenzi wa idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) na maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kukoma kuwahangaisha wafuasi wa Naibu Rais William Ruto na badala kuwakamata waliyohusika katika sakata ya pesa za corona.

Wakizungumza katika shule ya msingi ya Kongowea mjini Mombasa katika hafla ya kuwakabidhi wazee kadi za bima ya afya, ambayo ilihudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, viongozi hao wamesema japo majina ya walioshiriki katika wizi huo yametolewa parawanja, maafisa hao hawajawachukulia hatua yoyote.

Wakiongozwa na mbunge wa Nyali Mohammed Ali, wamesema serikali imekuwa ikiwaandama wafuasi wa Dkt Ruto kama njia ya kuwaadhibu kwa msimamo wao.

“DCI na EACC waache kuwaandama kina Aisha Jumwa na wengineo. Tunataka bilioni zilizoibiwa katika sakata ya corona zirudishwe,” akasema mbunge huyo.

Mohammed Ali aliyekuwa amevaa maski akiingia kwa mkutano huo amesema hatovaa maski hadi pale pesa zilizoibwa zitakaporudishwa.

Naibu Rais William Ruto akihutubia umati. Picha/ Mishi Gongo

Aidha wameutia dosari mpango wa maridhiano (BBI) wakisema kuwa ni njama ya aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta ‘kujinufaisha’.

“Hii ni kutaka kuleta ukabila katika serikali. Wanataka kupata vyeo hata ikitokea wameangushwa debeni na kuwafanya walipa ushuru kugharimia umero wao,” akasema.

Mbunge huyo alisema hata baada ya mageuzi yaliyoleta Katiba Mpya mwaka 2010 eneo la Pwani bado limesalia nyuma kimaendeleo.

Alisema kufikia sasa Wapwani wengi bado wanaishi kama maskwota kwa kukosa hatimiliki za vipande vya ardhi.

‘Tangatanga’ wakiri fimbo ya Uhuru yatisha

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto, wamekiri kuwa fimbo kali ya Rais Uhuru Kenyatta iliwalazimu kuenda chini ya maji.

Kwa miezi kadhaa sasa, wafuasi hao wa kikundi hiki maarufu kama Tangatanga wamepunguza shughuli zao za kisiasa baada ya msururu wa adhabu kutoka kwa wakuu wa Chama cha Jubilee wanaomtii Rais Kenyatta.

Miongoni mwa adhabu walizopewa ni kupokonywa nyadhifa muhimu bungeni, huku wengine wakidai kuandamwa na asasi za usalama serikalini.

“Ukiamua kufanya jambo ambalo linakinzana na Rais, unatishwa kwamba watakupeleka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza vile unavyotumia Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF),” akasema Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Caleb Kositany, aliye mwandani mkubwa wa Dkt Ruto.

Majuzi, Dkt Ruto aliwarai viongozi wa makanisa kuwaombea washirika wake, akisema baadhi yao wanatishwa kufikishwa mahakamani ikiwa hawatafuata mielekeo fulani ya kisiasa.

Licha ya wengi wao kuamua kukaa kimya, Mbunge wa Keiyo Kusini, Daniel Rono, alisema baadhi yao hawafurahishwi na hali hiyo.

“Rais Kenyatta ana udhibiti kamili wa serikali, hivyo Dkt Ruto hawezi kumkabili jinsi baadhi yetu tunavyotaka. Vilevile, (Ruto) anamheshimu Rais, hivyo hawezi kufanya jambo lolote linaloonyesha wazi anamkosea heshima mkubwa wake,” akasema Bw Rono.

Wanachama wa Jubilee wanaoegemea upande wa Rais walisema wandani wa Dkt Ruto wako kwenye njiapanda, hivyo hawapaswi kudai Rais anawakandamiza.

Mbunge wa Cherangany, Bw Joshua Kuttuny, alisema kuwa ni dhahiri sasa washirika wa Dkt Ruto wamepoteza mwelekeo kisiasa kwani hawakutarajia mbinu ambazo Rais alitumia ‘kuilainisha’ Jubilee baada yao kumkosea heshima kwa muda mrefu.

“Wanapaswa tu kukubali kwamba wameshindwa,” akasema Bw Kutuny.

Kwa mujibu wa mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu, huenda ikawa Tangatanga wameshindwa katika mbio zao, na sasa wameamua kunyamaza kwa muda ili kujipanga upya.

Tangatanga yatumia sakata ya fedha za corona kutakasa Ruto

Na LEONARD ONYANGO

MADAI kuhusu wizi wa mamilioni ya fedha zilizotengwa kukabiliana na janga la virusi vya corona yamegeuka baraka kwa Naibu wa Rais William Ruto huku wandani wake wakiyatumia kumtakasa.

Kulingana na wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto, maarufu Tangatanga, sakata hiyo ya wizi wa fedha za corona, imedhihirisha kuwa madai ya ufisadi ambayo Naibu wa Rais amekuwa akilimbikiziwa ni porojo tu.

Rais Kenyatta amemtenga naibu wake Dkt Ruto katika juhudi za kukabiliana na janga la virusi vya corona. Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mwenzake wa Usalama Fred Matiang’i, ndio wamekuwa wakiongoza juhudi za kupambana na maradhi ya corona.

Naibu wa Rais Ruto hajakuwa akialikwa kuhudhuria vikao ambapo Rais Kenyatta amekuwa akihutubia taifa kila mwezi. Dkt Ruto, hata hivyo, amekuwa akishirikishwa kwenye mikutano ya Rais Kenyatta na magavana kujadili maandalizi yanayofaa kuwekwa na kaunti ili kukabiliana na idadi kubwa ya wagonjwa wa virusi vya corona.

Wanasiasa wa Tangatanga wakiongozwa na mbunge wa Soy Caleb Kositany, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, sasa wanataka wizara ya Afya kuelezea namna imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha zilizotengwa kupambana na virusi vya corona.

Hii ni baada ya ripoti kufichua kuwa kandarasi za kuleta vifaa vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya kupatwa na virusi vya corona, maarufu PPEs, zilipewa jamaa na marafiki wa viongozi wakuu serikalini na chama cha Jubilee.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, wafanyabiashara hao walaghai waliuzia serikali vifaa hivyo kwa bei maradufu ikilinganishwa na bei ya sokoni.

Watu wenye ushawishi serikalini, kulingana na ripoti, waliiba hata msaada wa kupima virusi vya corona uliotolewa na bwanyenye wa China, Jack Ma.

Bw Kositany alidai kuwa wizara ya Afya imetumia mamilioni ya fedha kupatia Idara ya Ujasusi (NIS) kutafuta watu wanaotangamana na waathiriwa wa virusi vya corona.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, jana aliambia Taifa Jumapili kuwa sakata hiyo ya wizi wa fedha za corona, imemwondolea lawama Dkt Ruto ambaye amekuwa ‘akipakwa tope’ na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini kwamba ni mfisadi.

Dkt Ruto amekuwa akisema kuwa madai ya ufisadi ambayo amekuwa akihusishwa nayo hayana msingi na yanalenga kumchafulia jina ili kuzima azma yake ya kuwania urais 2022.

“Ruto hajahusishwa katika masuala ya kupambana na janga la virusi vya corona, sasa tunataka tuambiwe aliyeiba Sh30 milioni za corona. Wakenya sasa wanajua mwizi ni nani,” anasema Bw Sudi.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni mmoja wa nguzo muhimu za Dkt Ruto katika eneo la Magharibi, sasa anataka Naibu wa Rais Ruto kupewa usimamizi wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na janga la virusi vya corona.

“Mheshimiwa Rais, ili kuboresha utendakazi wa kamati ya kukabiliana na virusi vya corona, Naibu wa Rais anafaa kupewa usimamizi wake,” akasema Bw Khalwale kupitia akaunti yake ya Twitter.

Mkurugenzi wa shirika la kijamii Internnational Centre for Policy and Conflict (ICPC) Ndung’u Wainaina, anataka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwajibika kwa ujiuzulu kufuatia madai ya ubadhirifu wa fedha za kupambana na virusi vya corona.

“Inashangaza kwamba serikali inatuma wakaguzi wa hesabu katika kaunti kuchunguza namna zimetumia mamilioni ya fedha zilizotengewa vita dhidi ya corona. Ukweli ni kwamba, wizara ya Afya ndiyo inafaa kuchunguzwa kwanza,”anasema Bw Wainaina.

Naye wakili Ahamednasir Abdullahi, anamtaka Rais Kenyatta kujitokeza na kuwaadhibu waliohusika na ubadhirifu wa fedha za corona. Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando, anasema kuwa sakata hiyo ya fedha za corona imemtakasa Dkt Ruto.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa kwamba Naibu wa Rais ni fisadi lakini sasa madai hayo yameanza kukosa mashiko,” akasema Bw Kabando ambaye hivi karibuni alidai kuwa serikali ya Rais Kenyatta imeanza kuyumba.

Ruto aona mwanya wa kuanza kutangatanga tena

NAIBU Rais, Dkt William Ruto Alhamisi alidokeza kuwa ataanza ziara zake sehemu mbalimbali nchini hivi karibuni kufuatia kulegezwa kwa marufuku ya usafiri kutokana na janga la corona.

Ziara nyingi za Dkt Ruto na wafuasi wake mashinani, almaarufu kama Tangatanga, zilizimwa tangu janga la corona lilipoingia nchini.

Kwa wiki kadhaa sasa, Naibu Rais amelazimika kukutana na viongozi wa kijamii, wanasiasa, viongozi wa kidini na vijana nyumbani kwake Karen, Kaunti ya Nairobi au Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alipozungumza jana akitoa misaada ya vifaa mbalimbali kwa makundi ya vijana na wanawake katika makazi yake Karen jana, Dkt Ruto alisema amefikia uamuzi wa kujiandaa kurudi mashinani kwa vile ameombwa kufanya hivyo na vijana.

“Kwa sasa mambo ya corona yamelegezwa kidogo. Nitawatembelea alivyoomba huyu mungwana hapa ili nijionee biashara na shughuli zingine mnazofanya kujipatia riziki,” akasema Dkt Ruto.Licha ya kuwa Rais Uhuru Kenyatta alilegeza baadhi ya kanuni za kuzuia uenezaji virusi vya corona, marufuku ya mikutano ya kisiasa ingali ipo.

Kila wiki, Naibu Rais hutoa misaada kama vile mitambo ya kuosha magari, mashine ya ususi, mitambo ya kushona nguo, miongoni mwa vifaa vinginevyo, kwa makundi ya vijana kutoka maeneo bunge kadhaa ya Nairobi.

Ijapokuwa yeye husema misaada hiyo ni ya kuinua vijana kiriziki, wadadisi wanaamini anaandaa ‘jeshi’ la kuvumisha sifa zake mashinani anapojiandaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.’Huu si wakati wa siasa, huo wakati utafika baadaye,’ alisema jana.

Alikuwa ameandamana na Seneta Maalum Millicent Omanga na wabunge Nixon Korir (Langata), George Theuri (Embakasi Magharibi) na James Gathiru (Embakasi Mashariki).

Wakati huo huo, mwandani wake sasa wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta aharakishe kutoa ripoti ya Mpango wa Maridhiano.Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany jana alidai kuna njama ya kisiasa inayozuia kutolewa kwa ripoti hiyo.

Alisema wanachama wa kundi la Tangatanga wako tayari kwa mapendekezo yoyote ya jopokazi hilo lililoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji.

“Tunataka watutolee ripoti ya BBI badala ya kujaribu kuitumia kucheza siasa. Tunajua wanatafuta wale ambao wataipinga; wailete tu hamna atakayeipinga,” akasema Bw Kositany ambaye amegeuka msemaji wa mrengo huo wa Dkt Ruto.

Wiki iliyopita, Seneta Haji alisema wamekamilisha kazi ya kuandaa ripoti hiyo na kwamba wataiwasilisha kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga, “wakati ambapo wawili hao watakuwa tayari.”

Imedaiwa kuwa shughuli hiyo imecheleweshwa kutokana na hali kwamba Bw Odinga yuko Dubai ambako anaendelea kupata afueni baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hii ina maana kuwa Wakenya watasubiri hadi arejee nchini kabla ya ripoti hiyo kutolewa. Wiki jana Bw Odinga aliahidi kurejea shughuli zake za kisiasa “hivi karibuni.”

Lakini Mbunge wa Keiyo Kusni Daniel jana aliambia Taifa Leo kwamba huenda Rais na Bw Odinga wameingiwa na wasiwasi kutoka na ufichuzi wao kwamba wanaunga mkono wazo la kuanzishwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi kwani utawafaa kubuni ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema wakereketwa wa BBI wamekuwa wakiendeleza propaganda kwamba Dkt Ruto anapinga juhudi za kuunganisha taifa, kupitia ripoti ya BBI.

“Kwa kuwa sasa wamegundua kuwa Naibu Rais anaunga mkono wazo hilo, sasa wanasaka kisingio kingine kabla ya kutolewa kwa ripoti hiyo,” akasema Bw Rono.

Aidha, Mbunge huyo anabashiri kuwa huenda Rais Kenyatta na Bw Odinga wametofautiana kuhusu baadhi ya mapendekezo kwenye ripoti hiyo na sasa wanaichelewesha ili kutoa nafasi ya wao kukubaliana.

Tangatanga walia kutengwa katika miradi ya maendeleo

Na MWANGI MUIRURI

WABUNGE wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, wamelalamika wakidai maafisa serikalini wanatumia miradi ya umma kuweka uhasama wa kisiasa.

Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro na Bi Alice Wahome kutoka Kandara wamedai kuna njama ya kutumia miradi hiyo ya maendeleo kushawishi wakazi maeneo ya Kati wamwepuke Dkt Ruto.

Hayo yametokea siku moja tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaagiza mawaziri, manaibu wao na makatibu wa wizara waanze kuzuru kila eneo nchini kukagua miradi ili ikamilike kwa muda ufaao.

Wakiongea na Taifa Leo jana, wawili hao walisema hawatakubali miradi ya maendeleo kutumiwa kuendeleza siasa za kuwagawanya wananchi kwani huduma za kiserikali ni haki ya umma.

Waliteta kuwa kamati kuu ya utekelezaji miradi ya kiserikali ikiongozwa na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i huwa haiwaaliki wafuasi wa Dkt Ruto katika mikutano ya kuratibu maendeleo.

‘Ijumaa iliyopita, kamati hiyo iliwaalika wabunge wa Murang’a katika mkutano Nairobi kujadili miradi ya maendeleo ya kaunti hiyo. Lakini mimi na mwenzangu wa Kandara hatukualikwa,’ akasema Bw Nyoro.

Mikutano sawa na hii iliandaliwa na viongozi wa Magharibi ambao wanaonekana kuegemea upande wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, huku wakosoaji wao wakiachwa nje.

Bw Nyoro alidai kamati hiyo inataka kuhadaa wenyeji wa Murang’a kuwa hawana haki ya kutekelezewa maendeleo ikiwa wao ni wafuasi wa Dkt Ruto.

‘Sisi kama watu wa Murang’a ni walipa ushuru na kutekelezewa maendeleo ni haki ya kimsingi wala sio ya kisiasa. Tunafaa tukatae utapeli huo wa kubaguliwa kwa msingi wa imani yetu ya kisiasa,’ akasema.

Kwa upande mwingine, Bi Wahome alisema Rais alichaguliwa sambamba na Dkt Ruto na ndio wakuu wa serikali kwa pamoja.

‘Imekuwaje tunaambiwa tumtenge Dkt Ruto ilhali kisheria wawili hao ndio serikali? Na itakuwaje tena sasa iwe wafuasi wa Dkt Ruto watanyimwa maendeleo ilihali hata wao hutozwa ushuru sawa na hao wengine?’ akahoji Bi Wahome.

Wawili hao walisema kuwa hawatabanduka kutoka ufuasi wa Dkt Ruto wakisisitiza kuwa wengi wa wapiga kura wa Murang’a wamewaagiza wasalie papo hapo.

Walishikilia kuwa kamati ya Dkt Matiangi kuhusu maendeleo inahadaa wapiga kura mashionani kuwa ndiyo inagawa miradio ya kimaendeleo.

Mivutano ya UhuRaila, Tangatanga kuwanyima haki watu wa Kirinyaga

Na CHARLES WASONGA

MCHAKATO wa kuchunguza madai yaliyotolewa dhidi ya Gavana Anne Waiguru na madiwani wa Kirinyaga wanaotaka abanduke tayari umetekwa na mvutano wa siasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Hali hii inatarajiwa kuvuruga haki katika mchakato huo.

Wadidisi wanasema inasikitisha kuwa madai ya ufisadi dhidi ya Bi Waiguru sasa yamegubikwa na siasa za ubabe kati ya mirengo ya ‘handisheki’ na ‘tangatanga’ ilivyodhihiri katika Seneti mnamo Jumanne wakati wa kubuniwa kwa kamati ya kusikiza madai dhidi ya Bi Waiguru.

Maseneta waligawanyika kwa misingi ya mirengo hiyo miwili, ambapo Jubilee na Nasa walitetea kuundwa kwa kamati maalum ya kuchunguza madai dhidi ya Waiguru na ukaibuka mshindi kwa kura 45.

Nao upande uliotaka suala hilo lishughulikiwe katika kikao kizima cha Seneti ulijumuisha wandani wa Naibu Rais William Ruto, ambao walilemewa baada ya kupata kura 14 pekee.

Taswira iliyojitokeza ni kwamba Gavana Waiguru alipata ushindi wa kwanza kutokana na kuwa ni rahisi kwa wanachama 11 wa kamati hiyo “kushawishiwa” kwa urahisi kumtakasa Bi Waiguru.

Kimsingi, suala hilo sasa limechukua mwelekeo wa siasa za kitaifa, wala sio masuala yanayowahusu wakazi wa Kirinyaga, haliambayo itayeyusha masuala muhimu katika hoja hiyo.

Wakili na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa George Ogola, anaonya kuwa uwepo wa mivutano kuhusu suala hilo lenye uzito kwa wakazi wa Kirinyaga itawanyima haki.

“Inasikitisha kuwa tayari kuna madai kuwa makundi haya mawili yalifanya mikutano ya kujadili namna ya kufanikisha malengo yao. Mrengo wa handisheki ulisemekana kukutana kupanga namna ya kumnusuru Waiguru huku wapinzani wao wakipanga namna ya kumsulubisha,” anasema.

Siku chache kabla ya hoja hiyo kusomwa rasmi katika Seneti, Bw Odinga, na wandani wake, waliripotiwa kukutana na Gavana Waiguru katika mkahawa mmoja mtaani Karen kupanga mikakati ya kumwondolea lawama.

Ingawa Bw Odinga alikana ripoti hizo, mwandani wake wa karibu, Junet Mohammed, alitangaza hadharani kuwa chama cha ODM kimeamua “kusimama” na Bi Waiguru bila kujali madai dhidi yake.

Siku moja baada ya mkutano huo, Dkt Ruto naye aliongoza mkutano wa maseneta 16 katika makazi yake rasmi katika mtaa wa Karen, ambapo ajenda kuu ilikuwa na suala lilo hilo la hoja ya kumtimua Bi Waiguru afisini.

Duru kutoka mkutano huo zilisema kuwa Naibu Rais aliwataka maseneta hao, wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, kuhakikisha kuwa “Waiguru anaangushwa au kuokolewa kwa misingi ya namna atakavyojitetea dhidi ya makosa aliyodaiwa kutenda.”

Wanaodaiwa “kudhamini” msukumo wa kutimuliwa kwa Waiguru mashinani katika kaunti ya Kirinyaga ni pamoja na Naibu wake Peter Ndambiri, Mbunge Mwakilishi wa Wanwake Wangui Ngirici, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho.

Hata hivyo, Dkt Kibicho amekana madai hayo akisema yeye ni mtumishi wa umma na haruhusiwi kushiriki mieleka ya kisiasa.

HANDISHEKI KIZINGITI KWA UTAWALA BORA

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Javas Bigambo anakubaliana na kauli ya Wakili Ogola kwamba misimamo kinzani ya kisiasa ndiyo inatilia shaka uwezekano wa seneti kuishughulikia suala hilo kwa njia huru.

“Madai ya Seneta Orengo kwamba wale wanaotafuta kichwa cha Waiguru hawako katika bunge la kaunti ya Kirinyaga bali wako kwingineko, yalikuwa mazito mno,” anasema Bw Bigambo.

Madai ya Seneta huyo wa Siaya yamewatia hofu madiwani wa Kirinyaga, viongozi wa eneo hilo na mrengo wa Tangatanga ndani na nje ya seneti, kwamba mrengo Rais Kenyatta, Odinga na Kalonzo Musyoka utatumia ushawishi wake kumnusuru Gavana Waiguru.

Hii ndio maana madiwani 23 wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kamau Murango walisema hata kama Seneti itamwokoa Bi Waiguru watapambana naye mashinani.

“Tunaweza kuwasilisha hata hoja kumi za kumwondoa mamlakani; hatutachoka,” akasema.

Naye diwani wa wadi ya Mutira David Kinyua Wangui, aliyedhimini hoja hiyo akaongeza: “Ni wazi kwamba kuna njama ya kutupilia mbali uamuzi wetu kama bunge la Kirinyaga. Uhuru na Raila wanafaa kuelewa kuwa hata kama wakimwokoa Waiguru katika Seneti atarudi nyumbani na tutamfunza adabu”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Narc-Kenya Bi Martha Karua, anataja mipango ya kumnusuru Gavana Waiguru kama ithibati kuwa muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga hauna nia ya kusaidfia katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

“Sasa ni wazi kuwa wao ndio kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi,” anaongeza.

Huku wingu la siasa likigubika mchakato wa kusaka ukweli kuhusu madai dhidi ya Bi Waiguru kupitia Seneti, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeanza kumchunguza gavana huyo na bunge la kaunti ya Kirinyaga kuhusiana na sakata ya upeanaji zabuni na ulipaji marupurupu kinyume cha sheria.

Meneja wa tume hiyo katika eneo la Kati, Charles Rasugu wiki jana aliwaambia wanahabari kuwa malalamishi dhidi ya Bi Waiguru yanahusiana na utoaji wa zabuni ya thamani ya Sh50 milioni na kupokea malipo ya Sh10.6 milioni ya safari hewa ya kigeni.

Watu wa Kirinyaga sasa watasubiri matokeo ya uchunguzi huu wa EACC kupata ukweli kuhusu sakata hiyo kwani mchakato wa Seneti tayari umezamishwa ndani ya bahari ya siasa.

Joto lazidi kambi ya Ruto Duale akiandamwa

FARHIYA HUSSEIN na VALENTINE OBARA

MWANDANI mwingine wa Naibu Rais William Ruto, Aden Duale, yumo motoni baada ya polisi kuanzisha uchunguzi dhidi yake.

Kiongozi huyo wa wengi katika Bunge la Taifa anachunguzwa kwa madai ya kupeleka chakula kilichooza katika makao ya watoto mjini Garissa.

Hii imeibuka wiki moja baada ya mshirika wake mwingine, Rashid Echesa kukamatwa na kushtakiwa kuhusiana na kashfa ya utoaji wa zabuni feki ya ununuzi wa silaha za kijeshi za thamani ya Sh40 bilioni.

Kwenye uchunguzi huo dhidi ya Bw Duale, kikosi cha maafisa wa polisi, afya, Idara ya Ubora wa Bidhaa (KEBS) na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) walipekua afisi za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) Garissa Mjini kunakosimamiwa na mbunge huyo.

Imefichuka mbunge huyo, ambaye amekuwa mwandani wa Dkt Ruto kwa muda mrefu, aliagizwa mnamo Jumatano kufika katika ofisi za Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ili aeleze kuhusu malalamishi hayo ambayo ameyakanusha.

“Hakuna ukweli wowote katika suala hilo. Unaweza kwenda Garissa kujionea mwenyewe ukitaka. Nilizungumza na mkuu wa DCI kibinafsi akaniambia hakuna chochote hapo,” Bw Duale aliambia Taifa Leo kwa simu.

Licha yake kukana, Taifa Leo imethibitisha Bw Duale aliambiwa afike mbele ya Benedict Oyaro wa DCI.

Ripoti zilifichua Bw Duale alitembelea makao ya watoto ya Najah, eneo la Bulla Iftin mjini Garissa mnamo Jumatatu wiki hii na akatoa msaada wa vyakula.

“Tulipofungua magunia ya vyakula tuliona vitu vyeusi ndipo tukaingiwa na wasiwasi. Hapo ndipo tuligundua chakula kilikuwa tayari kimeoza,” akasema mmoja wa wahudumu katika kituo hicho.

Ilikuwa mara ya kwanza Bw Duale kutembelea makao hayo ya watoto tangu alipoanza kuwakilisha eneobunge hilo miaka 15 iliyopita.

Meneja wa kituo hicho, Bw Mohammed Noor, alithibitisha kulikuwa na vyakula vilivyopatikana vimeharibika ikiwemo mchele, unga na mahindi.

Imeibuka kuwa chakula hicho kilikuwa kimetolewa na jamii ya Wabohra, ambao walimwomba Bw Duale kuwasaidia kukisambaza kwa wenye mahitaji.

Baada ya kufichuka kwamba chakula kilikuwa kimeoza, maafisa wa jamii hiyo walimtumia ujumbe Bw Duale kuomba radhi wakisema hawakukagua vyakula hivyo kabla kutolewa katika stoo zao.

Kisa hiki kimewafanya wafuasi wa Dkt Ruto kusisitiza kuwa ndio tu wanaolengwa kwa kile wanasema ni kutaka aonekane kuwa mfisadi na pia kuwanyamazisha.

Mwezi uliopita walilalamika wakati Bw Mwangi Kiunjuri aliposimamishwa kazi ya Waziri wa Kilimo, na baada ya Bw Ferdinand Waititu kuvuliwa cheo chake cha ugavana Kiambu.

Jumapili, Bw Kiunjuri aliyendamana na viongozi wengine wa kikundi cha Tangatanga akiwemo Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria katika ibada Nanyuki, alimkashifu Rais Uhuru Kenyatta akidai anadhulumu wakosoaji wake.

“Leo hii Kiunjuri na Kuria wakisimama waseme barabara za Laikipia ni mbovu na zinapasa kutengenezwa, kesho yake watakujiwa na DCI, KRA na EACC,” akasema Bw Kiunjuri.

Bw Kuria pia anaandamwa na kashfa kadhaa ikiwemo madai ya kufuja pesa za Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF).

Viongozi wengine ambao wandani wa Naibu Rais wanaamini waliadhibiwa na serikali kuu ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich, ambaye alishtakiwa kwa uporaji wa fedha za miradi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer mwaka jana.

Naye Mbunge Kimani Ngunjiri (Bahati) alipokonywa silaha huku walinzi wa mwenzake Alice Wahome (Kandara) wakiondolewa, naye na Ndindi Nyoro (Kiharu) akakamatwa mwaka jana kwa madai ya kuzua rabsha kanisani.

Marufuku kwa wabunge wa Ruto kuhutubu kanisani

NA MWANDISHI WETU

WABUNGE 10 wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, Jumapili walikatazwa kuhutubu katika Kanisa Anglikana la St Thomas, Kerugoya, Kaunti ya Kirinyaga.

Wabunge hao wa mrengo wa Tangatanga walikuwa wameandamana na Dkt Ruto kwa ibada, lakini Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Wangui Ngirici pekee ndiye alikubaliwa kuhutubu kando na Naibu Rais.

Hatua hiyo ilitokana na agizo la Askofu Mkuu wa ACK, Jackson ole Sapit kwamba siasa zisiruhusiwe kanisani. Bi Wangui alikubaliwa kuwataja wanasiasa waliokuwepo.

Wakati Dkt Ruto alipohutubu, alihakikishia wasimamizi wa kanisa kwamba watafuata maagizo yao.

‘Tunaheshimu kanisa na hatutaingiza siasa zozote,’ akasema. Baadhi ya wabunge waliokuwepo ni Munene Wambugu (Kirinyaga Central), Gichimu Githinji (Gichugu), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Alice Wahome (Kandara).

Naibu Rais alitoa wito kwa wanasiasa wote nchini kuweka tofauti zao kando ili wamsaidie Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza ajenda zake za maendeleo.

Na George Munene

Wakati huo huo, alitoa wito kwa Wakenya kuombea familia ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi aliyefariki Jumanne iliyopita.

Vita vya Kieleweke na Tangatanga sasa vyaelekea Bungeni

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta anapanga kudhibiti bunge la kitaifa na lile la seneti ili kuendeleza agenda ya serikali bungeni litakaporejelea vikao vyake Jumatatu baada ya likizo ndefu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Anapanga kufanikisha udhibiti huo kwa kufanya mabadiliko katika uongozi wa Jubilee katika mabunge hayo mawili kwa kuwapokonya wandani wa Naibu Rais William Ruto nyadhifa zao ili kuzima uasi katika chama hicho.

Wadadisi wanasema hatua hiyo huenda ikadhoofisha zaidi uhasama ambao umekuwa ukitokota kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, haswa baada ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta amekasirishwa na baadhi ya viongozi wa Jubilee wanaoshikilia nyadhifa za uongozi bungeni, na kamati zake, ambao wamekuwa wakimkosoa hadharani tangu aliporidhiana kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 9, 2018.

Tangu wakati huo, wabunge wa Jubilee wamegawanyika kuwili. Kuna wafuasi wa kundi la Tangatanga, ambao wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 na wale wa kundi la Kieleweke, inayounga mkono maridhiano hayo, maarufu kama handisheki.

Katika bunge la Seneti, maseneta wanakabiliwa na hatari ya kupoteza nyadhifa zao ni pamoja na kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen na kiranja wa wengi Susan Kihika.

Kwa mfano, wawili hao mwezi jana waliowaongoza wenzao 10 kupambana kwa jino na ukucha kumwokoa aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu hoja ya kumwondoa mamlakani ilipojadiliwa katika seneti juzi.

Hata hivyo, juhudi zao ziligonga mwamba baada ya maseneta wa mrengo wa Kieleweke kuungana na wenzao wa upinzani kuidhinisha hoja hiyo.

Hoja hiyo ilipitishwa na bunge la kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 19, 2020.Hatua hiyo ilidaiwa kumkasirisha Rais Kenyatta ikizingatiwa kuwa baadhi ya mashtaka yaliyomkabili Bw Waititu yanahusiana na ufisadi, uovu ambao Rais Kenyatta amejitolea kupambana nao ili kuacha sifa bora atakapoondoka uongozini mnamo 2022.

Aidha, vita dhidi ya ufisadi ni mojawapo ya changamoto tisa ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga waliafikia kupambana nayo chini ya mpango wa maridhiano (BBI).

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ambaye ni mwanachama wa mrengo wa Kieleweke amethibitisha uwepo wa mpango wa Jubilee kufanya mabadiliko ya uongozi wake katika mabunge yote mawili.

“Ni kweli kabisa, mipango hiyo ipo na mabadiliko yatatekelezwa tutakaporejelea vikao baada ya likizo. Wenzetu wanaoshikilia nafasi za uongozi katika mabunge yote mawili waliteuliwa kuendeleza ajenda ya rais bunge ilivyoelezwa katika mkutano wa kwanza wa kundi la wabunge wa chama tawala mnamo Agosti 30, 2017.

“Wale ambao hawako tayari kutii ajenda hizo hawana sababu ya kuendelea kushikilia nafasi hizo,” akasema.

Akaongeza, “Hatutawaruhusu wale ambao wametwikwa jukumu la kuendeleza na kutetea ajenda ya serikali kuihujumu walivyofanya mwaka jana. Wale ambao wamekuwa wakimkosea heshima Rais na kuendelea kuhujumu ajenda yake ndani na nje ya bunge sharti wapokonywe afisi hizo mara moja.”

Naye Mbunge wa Tiaty William Kamket anasema Naibu Rais Dkt Ruto analindwa na Katiba na hawezi kufutwa, wandani wake wanaoshikilia nyadhifa kuu katika mabunge yote mawili wataandamwa.“Wakati ni huu, sio mwingine.

Wale ambao wamekuwa wakimkaidi Rais Kenyatta hawafai kuachiwa nafasi ya kutetea ajenda ya serikali bungeni kwa sababu wataihujumu kama ambavyo walifanya mwaka jana,” anasema mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Kanu.

Bw Kamket anasema wenzao wa Tangatanga ambao wanashikilia nyadhifa za uongozi wa kamati za bunge “wasubiri kuunda serikali yao iwape nafasi hizo wala sio serikali hii ya Rais Kenyatta ambayo wamekuwa wakiihujumu kila mara.”

Kando na Murkomen na Kihika, kunao Seneta wa Nandi Samson Cherargei ambaye ni mwenyekiti Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ua Kikatiba na mwenzake wa Bomet Christopher Lang’at ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu.Wawili hawa ni wandani sugu wa Naibu Rais ambao wamekuwa mstari wa mbele kukosoa baadhi ya maamuzi ya serikali wanayohisi yanahujumu nafasi ya Dkt Ruto kuingia Ikulu.

Katika bunge la kitaifa wanaokabiliwa na hatari ya kuangukiwa na shoka ni pamoja na Benjamin Washiali (kiranja wa wengi), naibu wake Cecily Mbarire, Kimani Ichung’wa (mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu Bajeti) miongoni mwa wandani wengine wa Dkt Ruto.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa kiongozi wa wengine Aden Duale atasazwa kwa sababu licha ya kuwa mwandani wa Dkt Ruto, “amekuwa mtetezi wa ajenda za serikali ndani na nje ya bunge.”

Kamati ya Bajeti, ambayo ndiyo ya kipekee yenye wanachama 51, ina usemi mkubwa katika mchakato wa utayarishaji bajeti ya kitaifa na ugavi wa fedha kwa wizara na idara mbalimbali za serikali.Jukumu la bunge katika utayarishaji wa bajeti hutekelezwa kupitia kwa uongozi wa kamati hii.

Vilevile, kamati hii ina uwezo wa kuchambua miswada yote ya serikali inayohusisha matumizi ya fedha za umma, hali inayoifanya kuwa wenye umuhimu mkubwa wa serikali ya kitaifa.

Ni kwa msingi huu, ambapo serikali inahisi kamati hiyo haiwezi kuongozwa na mtu “ambaye ametangaza vita dhidi ya Rais”.

Duru zinasema kuwa Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha katika utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, anapigiwa upatu kuchukua nafasi ya Bw Ichung’wa.

Ingawa utaratibu wa kumwondoa mwenyekiti wa kamati ya bunge ni rahisi, mchakato wa kuwaondoa wanaoshikilia nyadhifa za uongozi bungeni sharti uidhinishwe kwenye mkutano wa kundi la wabunge wa chama husika (PG).

Kwa mujibu wa sheria za bunge, ili mbunge apokonywe wadhifa wa mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa kamati, mmoja wa wanachama anahitajika kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye.

Na endapo hoja hiyo itaungwa mkono na wanachama wengi wa kamati hiyo, mwenyekiti huyo atakuwa amevuliwa wadhifa wake.Lakini kabla ya kuondolewa kwa Murkomen, Washiali, Kihika na Mbarire kutoka nyadhifa zao sharti uamuzi huo uidhinishwe katika mkutano wa PG ya Jubilee.

Na kumbukumbu za mkutano huo, pamoja na uamuzi wenyewe sharti ziwasilishwe kwa Spika wa Bunge la Kitaifa ndiposa majina yaondolewe kwenye orodha ya uongozi wa Jubilee Bungeni.

Ingawa mrengo wa Tangatanga umekuwa ukiitisha mkutano wa PG kujadili masuala yanayoibua migawanyiko ndani ya Jubilee, Rais Kenyatta amekuwa akipuuzilia mbali shinikizo hizo.

Sasa inasubiriwa kuonekana ikiwa Rais anapiga moyo konde na kuitisha mkutano huo ili kuifanikisha mabadiliko anayotaka bungeni.

Tangatanga sasa wakubali kueneza injili ya BBI kote nchini

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa Jubilee wanaounga mkono Naibu wa Rais William Ruto wametangaza kuwa wataanza kushiriki mikutano ya kuhamasisha Wakenya kuhusu ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen, zaidi ya wabunge 20 wa kundi la Tangatanga Jumanne walisema watahudhuria mkutano wa BBI utakaofanyika jijini Mombasa Jumamosi hii.

Viongozi hao walifanya kikao cha faragha kabla ya kutangaza kulegeza msimamo wao.

“Tutashiriki katika mikutano ya BBI itakayofanyika kote nchini. Wikendi hii tutakuwa jijini Mombasa na kikosi cha BBI. Tutahimiza wafuasi wetu katika maeneobunge yote 290 wajitokeze na watoe maoni yao,” akasema Bw Murkomen.

Viongozi hao walisema kuwa wanalenga kuhakikisha kwamba masuala wanayoambiwa Wakenya katika mikutano hiyo kuhusu ripoti ya BBI ni sahihi.

Hatua hii ni mabadiliko kwa kundi la Dkt Ruto, ambalo limekuwa likipinga vikali mikutano inayoendelea nchini wakisema kuwa haina haja kwani hakuna mtu anayepinga ripoti hiyo.

Kufikia sasa mikutano hiyo imefanyika katika maeneo ya Nyanza na Magharibi.

Msimamo wa awali wa kundi hilo ulikuwa kamba wanasiasa wasiruhusiwe kuandaa mikutano ya kuhamaisha Wakenya kuhusu BBI na badala yake jukumu hilo liachiwe jopokazi la watu 14 lililoandaa ripoti hiyo.

Wanasiasa wa Tangatanga pia walikuwa wakidai kuwa mikutano hiyo inatumiwa kufuja fedha za walipa ushuru.

Pia wamekuwa wakimshutumu Kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa madai ya kutumia mikutano hiyo kujipigia debe kwa ajili ya kinyang’anyiro cha urais 2022.

“Sasa tutashiriki kikamilifu katika mikutano ya BBI na ikibidi tutaiendesha sisi” akasema Bw Murkomen.

Juhudi za wanasiasa wa Tangatanga kutaka kuandaa mkutano sambamba na ule wa BBI uliofanyika uwanjani Bukhungu, Kaunti ya Kakamega, zilizimwa walipotawanywa na polisi.

Mikutano hiyo pia imekuwa ikitumiwa kushambuliwa mrengo wa Dkt Ruto.

UTEUZI: Tangatanga walia Uhuru alipendelea wandani wa Raila

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mrengo wa Tangatanga kutoka eneo la magharibi mwa Kenya wamelalamikia kile wanachotaja kama kupuuzwa kwa eneo hilo katika teuzi mpya ambazo Rais Uhuru Kenyatta alifanya serikalini Jumanne.

Walidai kwamba katika teuzi mpya ambazo kiongozi wa taifa alifanya, waliofaidi ni watu kutoka eneo la Nyanza ambao hawakumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2017 walivyofanya watu kutoka eneo hilo.

“Japo watu wetu walipigia Jubilee kura kwa wingi kuliko wale wa Nyanza, tunasikitika kuwa Rais Kenyatta hajateua mtu kutoka jamii yetu ya magharibi katika orodha aliyosoma akiwa Mombasa. Ni watu wa Raila ndio wameteuliwa hawakumpigia kura uchaguzi uliopita,” Mbunge Sirisia John Waluke akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi,

Aliandama na wenzake Didmus Barasa (Kimilili), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Malulu Injendi (Malava) na kiranja wa wengi bunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki).

Katika mabadiliko ambayo Rais Kenyatta alitangaza Jumanne katika mawaziri, mawaziri wasaidizi na makatibu wa wizara, aliyekuwa Mbunge wa Nyakach Peter Odoyo aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi wa Ulinzi huku Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi wa Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) Dkt Jwan Ouma akiteuliwa kuwa Katibu wa Wizara anayesimamia Mafunzo ya Kiufundi.

Bw Barasa alidai kuwa wawili hawa na watu wengine kutoka Nyanza, miongoni mwa wengine, waliteuliwa kwa sababu na ushawishi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais baada ya wawili hao kuridhiani kisiasa mnamo Machi 9, 2018.

“Hii handisheki kati ya Raila na Uhuru ndio sasa imepelekea watu wetu kukosa viti katika serikali hii ambayo tuliipigania kwa nguvu zetu zote. Rais hafai kutusahau ilihali ni sisi tulimsaidia wakati Raila na watu wake walisusia marudio ya uchaguzi Oktoba 26, 2017,” akasema.

Hata hivyo, Bw Washiali alikataa kuzungumzia suala hilo akisema Rais ana mamlaka ya kufanya mabadiliko na teuzi katika serikali yake anavyotaka.

“Nadhani Rais Kenyatta aliongozwa na busara katika mabadilika na teuzi aliyofanya leo (jana). Naamini walioteuliwa wataendeleza ajenda ya maendeleo ya Jubilee. Siwezi kumkosoa Rais kwa sababu ni bosi wangu,” akasema.

Wakati huo huo, wabunge hao wamekariri kuwa mkutano sambasamba ambao wamepanga kufanya mjini Mumias Januari 18 kujadili masuala ya ufufuzi wa sekta ya miwa utaendelea ulivyopangwa.

“Nimesikia watu fulani wakisema kuwa Mkutano wa BBI utakaofanyika mjini Kakamega siku hiyo ndio wa kipekee. Nawaambia kuwa sisi kama viongozi wanaojali masilahi ya wakulima wetu wa miwa tutakuwa mjini Mumiaa kujadili mustabali wao,” akasema Bw Washiali.

Kasisi motoni kwa kualika Tangatanga kwa harambee

Na KNA

KASISI wa Kanisa Katoliki mjini Bondo, Kaunti ya Siaya amejipata mashakani baada ya kualika wandani wa Naibu Rais William Ruto katika harambee ambayo haikuhudhuriwa na mwanasiasa yeyote wa Chama cha ODM kilicho na ufuasi mkubwa eneo hilo.

Uvumi sasa umeanza kuenea kwamba viongozi wa Kanisa Katoliki la St Andrews eneo la Bondo, ni wanachama wa vuguvugu la Tangatanga.

Waumini wa kanisa hilo wanaamini kwamba, uvumi huo unaenezwa na wanachama wa ODM waliokasirika wakubwa wao walipokosa kualikwa katika harambee iliyofanyika Parokia hiyo majuzi.

Viongozi walianza kurushiana lawama punde tu baada ya msaidizi wa Naibu Rais William Ruto- Bw Farouk Kibet, kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa mgombeaji wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra Macdonald Mariga- walipohudhuria harambee katika kanisa hilo mapema mwezi huu.

Kuhudhuria kwa watatu hao wanaochukuliwa kuwa “wageni” na kukosekana kwa viongozi wa eneo hilo katika harambee hiyo kulimweka pabaya Kasisi Collins Odiero huku ripoti zikienea kuwa aliwapuuza makusudi viongozi wa ODM na kuwaalika wale wa Jubilee.

Uvumi huo ungali unaendelea tangu Desemba 1 wakati harambee ilifanyika na Sh6.5 milioni kukusanywa kujenga afisi za Parokia.

Baadhi ya wakazi wanadai kuwa, viongozi wa kanisa wangewaalika viongozi wa vyama vyote huku baadhi wakimuunga Padre Odiero wakisema aliwaalika waliokuwa tayari kuchanga pesa.

“Tuna wandani wa viongozi wa ODM miongoni mwa waumini. Tafadhali komeni kutupiga vita kutoka ndani mliposhindwa kutujulisha kwa wakubwa wenu tulipowahitaji,” Padre Odiero alisema kwenye ibada Jumapili.

Alisema kamati iliyoandaa harambee ilijaribu kuwafikia viongozi wakuu wa ODM eneo hilo kwa miezi minne kupitia wandani wao na hata kwa kuwapigia simu lakini hakuna aliyekubali.

“Siku chache kabla ya harambee, tuligundua hawangefika,” alisema Padre Odiero.

Alisema yeye binafsi alimuita diwani ambaye pia ni mshirika wa kanisa lakini hakujitolea kuwaalika na hata mwenyewe hakuhudhuria.

Kwa vile muda ulikuwa unayoyoma, kamati iliamua kuwasiliana na msaidizi wa Dkt Ruto, ambaye ni Bw Kibet, na akakubali mara moja kuwa mgeni wa heshima.

“Kusema ukweli, sikufahamu kwamba Bw Kibet angeandamana na Murkomen na Mariga lakini walituchangia zaidi ya Sh800,000 kusaidia kujenga kanisa na hakuna shida yoyote. Sisi sio wanasiasa na hatuhusiki na siasa,” alisema Padre Odiero.

Aliwataka wafuasi wa ODM wanaoabudu katika kanisa hilo kukoma kueneza uvumi kwa nia mbaya ili kumchafulia jina kama msimamizi wa Parokia.

Lakini afisa wa ODM Peter Mbeka, ambaye kanisa lilisema lilimtumia kuwasiliana na Seneta Orengo amekanusha kueneza uvumi na kugawanya kanisa.

Alikiri kwamba alitwikwa jukumu la kuwasiliana na Bw Orengo lakini kamati ilipotakiwa kuandika barua ilikataa.

Alifichua kuwa wakati wa harambee aliwasiliana na mbunge wa eneo hilo Dkt Gideon Ochanda ambaye alituma mchango wake kupitia Bw Kibet.

Gavana anukuu Biblia huku akigura kundi la Ruto

Na NDUNGU GACHANE

VUGUVUGU la kisiasa linalomuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto, maarufu kama ‘Tangatanga’ limepata pigo kubwa la kisiasa baada ya Gavana Mutahi Kahiga wa Kaunti ya Nyeri kutangaza kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kahiga alisema ni Mungu pekee anayejua yule ataiongoza nchi baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022.

Gavana huyo amekuwa mshirika wa karibu wa Dkt Ruto kwani amekuwa akihudhuria hafla zake mbalimbali katika eneo hilo.

Lakini akinukuu Biblia, Bw Kahiga alimwambia Dkt Ruto kusubiri wakati huo ufike, huku akiwarai viongozi wa Mlima Kenya kukomesha kampeni za mapema.Alisema badala yake, wanapaswa kumuunga mkono Rais Kenyatta kutimiza ajenda zake za maendeleo.

“Zaburi 75: 6 inasema kwamba msijisifu, kwani Mungu ndiye humwinua mwanadamu amtakaye. Ndiye mwenye uwezo wa kumwinua ama kumshusha mwanadamu. Tunaweza kutumia muktadha huo kurejelea uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Kahiga.

Hatutaki siasa katika eneo la Mlima Kenya. Lazima tutafute njia ya kuzima malumbano yaliyopo. Hatupaswi kupigana kwa sababu ya mwanamume anayemtafutia riziki mke na watoto wake, lakini si kuangazia maslahi yetu.

Tuna jukumu la kukamilisha kazi ambayo Rais anatutaka tumalize. Tunaweza kulifaidi eneo hili sana kwa miaka mitatu iliyobaki ikiwa tutaacha siasa na kumuunga Rais Kenyatta mkono,” akasema.

Gavana huyo alikuwa ameandamana na mwenzake Anne Waiguru wa Kirinyaga kwenye hafla maalum ya kumtawaza Askofu Francis Kariuki wa kanisa la AIPCA Dayosisi ya Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Bi Waiguru pia amewahi kuonekana kama mwandani wa Ruto kabla kubadili msimamo wake kushabikia handsheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bw Kahiga alisema kuwa eneo hilo halipaswi kukubali kugawanywa kisiasa.Kauli yake inajiri huku serikali ikizidisha vita dhidi ya ufisadi.

Kufikia sasa, magavana watatu wamezuiwa na mahakama kuingia katika afisi zao hadi kesi dhidi yao kuhusu ufisadi zisikizwe na kuamuliwa.

Zima kiburi, Tangatanga wamfokea Matiang’i

WYCLIFF KIPSANG na TOM MATOKE

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto kutoka Bonde la Ufa wametoa masharti makali ndiposa washiriki katika utekelezaji wa ripoti ya BBI.

Viongozi hao kutoka Kaunti ya Nandi wakiongozwa na Seneta Samson Cherargei na wabunge Julius Meli (Tindiret), Cornelius Serem (Aldai) na Wilson Kogo (Chesumei) wanataka Rais Uhuru Kenyatta kuagiza mawaziri kukoma kujihusisha na ripoti ya BBI.

Huku wakionekana kulenga Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, wanasiasa hao walisema mawaziri hao wanasababisha mgawanyiko ndani ya chama cha Jubilee.

Seneta Cherargei alisema Rais Kenyatta na Dkt Ruto walipounda serikali baada ya uchaguzi wa 2013 na 2017 waliagiza mawaziri kujiepusha na siasa.

“Mgawanyiko uliomo ndani ya chama cha Jubilee hautaisha hivi karibuni endapo Rais Kenyatta hatatimua maafisa wakuu serikalini wanaojihusisha na siasa,” akasema Bw Cherargei.

“Mgawanyiko baina ya Rais Kenyatta na naibu wake unachochewa na mawaziri ambao wanataka kuhakikisha kuwa Dkt Ruto haingii ikulu 2022,” akasema Bw Serem.

Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen pia walimtaka Dkt Matiang’i kuheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi.

“Matiang’i ni lazima aheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi. Hatuwezi kuruhusu watumishi wa umma kama vile Matiang’i kuwa na ubaguzi katika kuwatumikia Wakenya,” akasema Bw Mandago.

Viongozi hao walishikilia kwamba masuala mengi yaliyomo ndani ya ripoti ya BBI yanaweza kutekelezwa kupitia bunge bila kura ya maamuzi.

Bw Murkomen alisema shughuli za serikali zinafaa kuendelea bila kutatizwa na kampeni za kutaka kufanyika kwa kura ya maamuzi inayoendeshwa wanasiasa wanaounga handisheki baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga..

“BBI ina mapendekezo mazuri ya kuboresha maisha ya Wakenya. Matiang’i aliteuliwa waziri kwa hisani ya chama cha Jubilee hivyo afanye kazi ya kuhudumia Wakenya,” akasema Mbunge wa Soy Caleb Kositany.