• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
TEKNOHAMA: App ya kukabiliana na homa ya Corona

TEKNOHAMA: App ya kukabiliana na homa ya Corona

Na LEONARD ONYANGO

HUKU Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema kuwa kinga dhidi ya homa ya Corona itapatikana ndani ya miezi 18 ijayo, serikali ya China sasa inatumia programu za simu (app) katika juhudi za kupunguza maambukizi ya maradhi hayo.

Tangu mkurupuko wa maradhi hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,500 kutokea miezi miwili iliyopita, mamia ya app zimetengenezwa kutoa taarifa kuhusu virusi hivi

Serikali ya China, wiki iliyopita, ilizindua app ya simu inayoeleza watu ikiwa wako kwenye hatari ya kupatwa na maambukizi ya virusi vya homa hiyo au la.

App hiyo inayofahamika kama Close Contact Detector pia inaonya watu dhidi ya kugusana ili kuepuka kupatwa na virusi hivyo.

App hiyo imetengenezwa na taasisi tatu za serikali ya China, kulingana na shirika la habari la Xinhua.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa hiyo itasaidia pakubwa kupunguza maambukizi huku ulimwengu ukiendelea kungojea kinga ya virusi hivyo.

App hiyo inakueleza unapokaribiana na watu wanaoshukiwa kuwa waathiriwa wa maambukizi ya virusi hivyo.

Ukiketi karibu na mtu ambaye alikuwa akihudumia mwathiriwa kwa mfano, app hiyo inakufahamisha kujitenga nao ili usiambukizwe.

Unapotaka kuabiri matatu iliyo na msongamano wa watu, hukushauri usipande.

Hata hivyo, China haijaelezea namna app hiyo inabaini watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya Corona.

Kulingana na Xinhua, app hiyo imeidhinishwa na Wizara ya Uchukuzi na Safari za Ndege.

Wiki mbili zilizopita, China pia iliwataka wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa na homa hiyo kujipima joto na kutuma kwa vituo vya afya kila asubuhi.

Serikali iliwataka kutuma vipimo vya joto kwa kutumia app kama vile WhatsApp. Joto linapokuwa la juu kupita kiasi, serikali itatuma maafisa wa afya kumshughulikia mwathiriwa.

Ongezeko la joto mwilini ni miongoni mwa dalili za homa ya Corona.

Chuo Kikuu cha Tokyo pia kimetengeza kifaa kinachoweza kutambua waathiriwa wa homa hiyo ambayo sasa imepewa jina jipya la COVID-19.

Shirika la WHO wiki iliyopita lilitangaza kuwa kinga ya kwanza ya kuzuia maambukizi huenda ikapatikana katikati mwa mwaka ujao.

“Kinga ya kwanza ya kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Corona huenda ikawa tayari ndani ya miezi 18 ijayo. Lakini kwa sasa tuendelee kutumia silaha zilizopo kukabili maradhi hayo,” akasema Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Alitangaza maradhi hayo kuwa tishio kwa ulimwengu japo kufikia sasa yameua mtu mmoja pekee nje ya China.

“Asilimia 99 ya maambukizi hayo yameathiri Wachina. Lakini katika siku za hivi karibuni yamekuwa yakisambaa kwa kasi katika nchi nyinginezo kote ulimwenguni,” akasema Tedros.

Aidha alisema kuwa wanasayansi wangali wanachunguza vigezo mbalimbali kabla ya kutengeneza kinga.

“Inashangaza kwamba ugonjwa ambao umeangamiza zaidi ya watu 1,000 ndani ya miezi miwili haukujulikana hapo awali. Ili kushinda maradhi haya, wanasayansi ni sharti wapate majibu yote kuhusiana na kiini chake na jinsi unavyosambazwa,” akasema.

Watafiti kutoka katika nchi mbalimbali wanaendelea na utafiti wa kisayansi ili kubaini kinga ya kukabili maradhi haya.

Kwa mfano, nchini Uingereza, Taasisi ya Kukabili Maradhi ya Kuambukizwa nchini humo, inasema kuwa itaanza majaribio ya kwanza ya kinga Aprili, mwaka huu.

Homa ya Corona imeua idadi kubwa zaidi ya watu kuliko maradhi ya Homa ya Mfumo wa Kupumua (SARS) iliyokurupuka nchini China mnamo 2003 na kuua watu 774. Jumla ya watu 8,000 waliambukizwa homa ya SARS.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Tatizo la mwasho wa ngozi na matibabu

MAZINGIRA NA SAYANSI: Mafuriko husababisha msongo wa mawazo

adminleo