• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Treni kufufua uchumi Mlima Kenya

Treni kufufua uchumi Mlima Kenya

JAMES MURIMI na NICHOLAS KOMU

SEKTA ya utalii na uchumi wa mji wa Nanyuki unatarajiwa kustawi baada ya kuanza tena kwa safari za reli kati ya Nairobi na Nanyuki.

Treni ilianza safari zake kati ya Nairobi na Nanyuki mnamo Desemba 12, mwaka huu, baada ya kusitishwa kwa karibu miongo miwili.

Safari za treni hiyo zingali katika awamu ya majaribio, lakini maafisa wa Shirika la Reli nchini na serikali ya Kaunti ya Laikipia wanasema wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa abiria wanatumia treni.

Treni hiyo ilipoanza safari zake ilitumiwa na idadi ndogo ya abiria lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wasafiri. Treni hiyo huenda Nairobi na kurudi mara moja kwa wiki lakini Shirika la Reli nchini linasema safari hizo zitaongezeka katika siku za usoni.

Treni hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1,600, hutoka Nairobi Ijumaa saa mbili asubuhi na hupitia na kusimama katika vituo vya Thika, Mitubiri, Makuyu, Maragua, Murang’a, Sagana, Karatina, Kiganjo na Naromoru.

Treni hiyo huondoka Nanyuki Jumapili saa mbili asubuhi kuelekea jijini Nairobi.Abiria wanaosafiri kutoka Nairobi kuelekea Nanyuki hulipa nauli ya Sh1,000 kutumia behewa la hadhi ya juu na Sh200 kutumia mabehewa ya hadhi ya wastani.

Wanaoabiri treni njiani hulipa nauli ya kati ya Sh50 na Sh100.Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini Philip Mainga alisema kuwa hivi karibuni shirika hilo litaongeza idadi ya vituo kuhakikisha kuwa abiria wengi wananufaika na huduma za treni hiyo.

Treni hiyo huchukua kati ya saa saba na tisa kusafiri kutoka Nairobi hadi Nanyuki ilhali basi au matatu hutumia chini ya saa nne kusafiri umbali sawa.Baadhi ya abiria wamekuwa wakipendelea kutumia usafiri wa barabara badala ya treni ili wafike haraka.

Shirika la Reli pia linalenga watalii ambao watakuwa wakizuru maeneo ya Nanyuki kujionea vivutio mbalimbali.Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi alisema kuwa treni hiyo itafufua shughuli za utalii katika maeneo ya Mlima Kenya na kupiga jeki uchumi wa Nanyuki.

Gavana Muriithi aliambia Taifa Leo jana kwamba Wakenya na watalii wanaotaka kufurahia mandhari ya mji wa Nanyuki wikendi wanaweza kutumia treni hiyo.

You can share this post!

Wakenya wakerwa na Gavana Kimemia kutumia Sh12 milioni...

Wagonjwa wa kansa wageukia mitishamba